Kiswahili kutumika rasmi serikalini | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kiswahili kutumika rasmi serikalini

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by kilimasera, Apr 20, 2010.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Apr 20, 2010
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  SERIKALI imeagiza kutumika kwa Kiswahili katika usaili kwa watu wanaoomba kazi kwenye Wizara na Idara za Serikali na pia imetaka matangazo yote ya kazi za idara za umma yatolewe kwa lugha hiyo badala ya lugha ya kigeni kama inavyofanyika sasa hivi.

  Katika agizo hilo, pia serikali ambalo lilitolewa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika bungeni, imeagizwa dhifa mbalimbali za kitaifa, hotuba za viongozi, warsha, semina na mikutano ya kitaifa iendeshwe kwa Kiswahili.


  Pia alisema maofisa wa serikali na mashirika ya umma watumie Kiswahili katika shughuli zote kama vikao vya Bodi na mawasiliano ya kiofisi pia yaendeshwe kwa lugha hiyo ya taifa pamoja na kuandika madokezo.


  Pia aliagiza sheria zote ziandikwe kwa Kiswahili ikiwa ni pamoja na kutafsiri zile zilizoandikwa kwa lugha za kigeni. Alisema jitihada za makusudi zifanyike ili shughuli za Mahakama katika ngazi zote ziendeshwe kwa Kiswahili pia.


  Mijadala inayohusu shughuli za umma iendeshwe kwa Kiswahili na kumbukumbu zote zihifadhiwe kwa lugha ikiwa ni pamoja na nyaraka zilizotumika katika mijadala kuandikwa kwa Kiswahili. Waziri pia aliagiza majina ya barabara, mitaa na mabango yaandikwe kwa Kiswahili.


  Serikali imetoa kauli hiyo baada ya Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein katika kikao cha Baraza la Mawaziri Februari mwaka huu, aliagiza na kusisitiza suala la matumizi ya Kiswahili katika shughuli za serikali na kuwakumbusha watendaji serikalini kuzingatia Waraka wa Makamu wa Kwanza wa Rais, Rashidi Kawawa wa mwaka 1967.


  Mkuchika pia alisema mwaka 2005, Serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), William Lukuvi aliagiza taarifa za mikutano, semina na warsha nchini zitolewe kwa Kiswahili kwa manufaa ya wananchi.


  Alisema taarifa za miradi inayohusu wananchi ni lazima zitolewe kwa Kiswahili ikiwa ni pamoja na vipeperushi na nyaraka zinazohusu miradi hiyo.


  Mwaka 1974, aliyekuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (Utumishi), J. Mganga alitoa waraka alioelezea kuhusu matumizi ya Kiswahili katika ofisi za serikali ambao ulisisitiza barua kati ya Wizara na Idara ziwe za Kiswahili isipokuwa kama anayeandikiwa ni raia wa kigeni.


  Pia aliagiza vibao vyote vya majina ya ofisi au wizara na matangazo kama ya mahafali, sikukuu mbalimbali yaandikwe kwa Kiswahili, madokezo baina ya maofisa maofisini yawe ni kwa lugha ya Kiswahili, fomu zote za kujazwa ziwe za Kiswahili.


  Waziri huyo alirejea Waraka wa Kawawa ambaye ulimtaka kila ofisa wa Serikali na viongozi wote wawe mfano mwema katika kutumia lugha ya Kiswahili na kusiwe na kuchanganya changanya lugha na mfano mzuri katika mijadala ndani ya Bunge na watu wote waone fahari katika Kiswahili.


  “Kwa kuzingatia matamko haya na umuhimu wa lugha ya Kiswahili ikiwa sasa ni lugha ya kimataifa inayotumiwa mathalani kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika, Serikali inasisitiza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika shughuli za serikali na kutoa kauli kuwa pamoja na vipengele vilivyosisitizwa awali,” alisema Mkuchika.
   
 2. MIUNDOMBINU

  MIUNDOMBINU JF-Expert Member

  #2
  Apr 20, 2010
  Joined: Apr 14, 2010
  Messages: 452
  Likes Received: 24
  Trophy Points: 35
  Wazo zuri tatizo ni J e wataweza kulitekeleza kwa sasa, km wameshindwa tangu miaka ya 70 leo hii wataweza kweli?.Mie nina tia shaka.kwa sababu Lugha yetu hatuipendi kivitendo.
   
 3. A

  Akili Kichwani JF-Expert Member

  #3
  Apr 20, 2010
  Joined: Jan 7, 2010
  Messages: 1,504
  Likes Received: 22
  Trophy Points: 135
  nawapongeza sana tena sana japo kwa kutoa tamkp hili kwa ujasiri............. niseme wazi kuwa hii ni hatua ya kwanza ya ujasiri niliyoshuhudia ikichukuliwa na kuchika tangu ateuliwe kushika wadhifa alionao............. na ni credit isiyotiliwa shaka kwa utawala huu wa awamu ya nne.............. haongera sana .............

  wasiwasi wangu ni kuwa mfano katika usaili wa nafasi za kazi............. mwanafunzi aliyesooma kwa kiingereza kisha akaulizwa swali atoe jibu kwa kiswahili............. ataweza kutoa tafsiri sahihi ya jibu la swali aliloulizwana bila kukosea?......... mfano jibu lake likiwa "lifting up the veil of incorporation" wangapi wa wahitimu wetu wanaweza kulitafsiri hili kwa kiswahili fasaha bila kuzua mabishano juu ya tafsiri husika?.............. hata hivyo ni mwanzo mzuri............. hongera sana JK na timu yako kwa hili "tamko".............
   
 4. m

  mndebile Senior Member

  #4
  Apr 20, 2010
  Joined: Sep 4, 2009
  Messages: 149
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 35
  Hilo ni tamko zuri sana ila inatakiwa pia lugha zingine za kigeni zitiliwe maanani huko mashuleni ili tuwe na vijana wanaojua lugha zaidi ya moja kwa ufasaha, pia kwenye usaili nadhani kungekuwa na hiari ya msailiwa kutumia kiswahili au kiingereza, kwani itasumbua sana kutumia kiswahili pekee yake.
   
 5. M

  Mavunja Member

  #5
  Apr 20, 2010
  Joined: Feb 18, 2009
  Messages: 14
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 3
  Wazo zuri sana lakini ni lazima wahusika waandae mkakati wa utekelezaji. Baadhi ya mbinu za utekelezaji ni kwa kushirikiana na BAKITA. Kwanza makamusi ya Kiswahili Sanifu yazambazwe maofisini. Pia, BAKITA ianzishe tovuti yake na iweke kamusi rasmi ya Kiswahili yenye istalahi zote za kitaalamu ambayo inaendelea kuboreshwa wakati wote. Kamusi rasmi ya kwenye mtandao itakuwa rasilimali nzuri ya kusaidia kueneza matumizi ya lugha yetu. Bila kufanya hivyo wengi tutapambana na vikwazo katika kutumia lugha hii.

  Pia, huu ungekuwa wakati muafaka kupanga mkakati wa kuanza kutumia lugha ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia katika elimu ya sekodari na kuendelea.
   
 6. Edson

  Edson JF-Expert Member

  #6
  Apr 20, 2010
  Joined: Mar 7, 2009
  Messages: 9,202
  Likes Received: 722
  Trophy Points: 280
  tatizo linakuja kwenye kutekeleza hayo maagizo kama toka mwaka 1967
  zwalishindwa kutumia kiswahili leo sijui kama wataweza maana nchii yangu hii usanii mwingi sana
   
 7. Regia Mtema

  Regia Mtema R I P

  #7
  Apr 20, 2010
  Joined: Nov 21, 2009
  Messages: 2,974
  Likes Received: 19
  Trophy Points: 0
  Mmh patakuwa hapotoshi..Madessa yote yapo in English..Kazi kweli kweli.
   
 8. Kiroroma

  Kiroroma JF-Expert Member

  #8
  Apr 20, 2010
  Joined: Feb 6, 2009
  Messages: 368
  Likes Received: 30
  Trophy Points: 45
  Huku ni kukorogana kwa kwenda mbele
   
 9. kilemi

  kilemi JF-Expert Member

  #9
  Apr 20, 2010
  Joined: Mar 13, 2009
  Messages: 520
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 35
  Seminar papers za wanataaluma zitaandikwa na kujadiliwa kwa Lugha gani?
   
 10. manenge

  manenge JF-Expert Member

  #10
  Apr 20, 2010
  Joined: Apr 30, 2008
  Messages: 280
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 0
  NI jambo zuri sana japo limechelewa. Nilikuwa ninapata kichefuchefu kwenye mikutano/warsha za watu/ waswahili 200 na mzungu mmoja lakini mkutano huo unaendeshwa kiingereza kisa mzungu aweze kuelewa. kumbe ingekuwa rahisi mkutano huo ukaendeshwa kiswahili halafu akatafutwa mkalimani mmoja akamsaidia huyo mzungu. akili za kawaida tu ingeweza kungamua hilo. Lakini haina maana tukipuuze kingereza
   
 11. FirstLady1

  FirstLady1 JF-Expert Member

  #11
  Apr 20, 2010
  Joined: Jul 29, 2009
  Messages: 16,575
  Likes Received: 543
  Trophy Points: 280
  Hapa sijui itakuwaje ?
   
 12. Ndibalema

  Ndibalema JF-Expert Member

  #12
  Apr 20, 2010
  Joined: Apr 26, 2008
  Messages: 10,916
  Likes Received: 132
  Trophy Points: 160
  Kili na wana JF wote wala msiwasikilize hao wanasiasa wa bongo.
  hizo ni siasa tu hakuna lolote.
  Miaka yote walikuwa wapi hadi karibia na uchaguzi ndio wanakikumbuka kiswahili.
  Kwenda zao kule!!
   
 13. Zak Malang

  Zak Malang JF-Expert Member

  #13
  Apr 21, 2010
  Joined: Dec 30, 2008
  Messages: 5,410
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 0
  * Shughuli zote kuendeshwa kwa Kiswahili


  Serikali imeagiza matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika shughuli zake rasmi na pia majina ya mitaa na mabango kuandikwa kwa lugha hiyo ili kukienzi Kiswahili kama lugha ya taifa.

  Pia, zimetakiwa jitihada za makusudi zifanyike ili shughuli za mahakama katika ngazi zote ziendeshwe kwa lugha ya Kiswahili.

  Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika, alipokuwa akisoma kauli ya serikali kuhusu matumizi ya Kiswahili katika shughuli rasmi za serikali, bungeni mjini hapa jana.

  Katika agizo hilo, Mkuchika alisema dhifa mbalimbali za kitaifa, hotuba, warsha, semina na mikutano ya kitaifa, ziendeshwe kwa lugha ya Kiswahili na kuwataka maofisa wa serikali na mashirika ya umma kutumia lugha hiyo katika shughuli zao zote, kama vile vikao vya bodi, mawasiliano ya kiofisi, matangazo ya nafasi za kazi na mahojiano.

  Mkuchika pia alitaka mbao za matangazo na nyaraka zinazobandikwa za taifa na sheria zote ziandikwe kwa lugha ya Kiswahili, ikiwa ni pamoja na kutafsiri zile zilizoandikwa kwa lugha ya kigeni.

  Vilevile alitaka mijadala inayohusu shughuli za umma iendeshwe kwa Kiswahili, pia kumbukumbu zote zihifadhiwe kwa lugha ya Kiswahili, ikiwa ni pamoja na nyaraka zilizotumika katika mijadala kuandikwa kwa lugha hiyo.

  Katika agizo hilo, serikali imevitaka vyombo vya habari vinavyotumia lugha ya Kiswahili kuhakikisha vinatumia Kiswahili sanifu na mwanana na kuzingatia kwa dhati sarufi ya Kiswahili.

  Mkuchika alisema agizo hilo la serikali linazingatia matamko mbalimbali ya viongozi wa serikali wa awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu na umuhimu wa lugha ya Kiswahili, ikiwa sasa pia ni lugha ya kimataifa inayotumiwa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na yaliyotolewa na viongozi wa serikali kuhusu matumizi ya lugha hiyo.

  Alisema Kiswahili ndiyo lugha pekee, ambayo huzungumza na kueleweka na idadi kubwa zaidi ya Watanzania nchini kote, pia ni chombo muhimu ambacho kimewaunganisha Watanzania wakati wa kupigania uhuru na ni kielelezo thabiti cha utamaduni wa Mtanzania na kitambulisho kikuu cha taifa.

  “Hivyo, hatuna budi kukikuza na kukiimarisha. Haikuwa kwa bahati nasibu kwamba Kiswahili kilitangazwa kuwa lugha ya taifa la Tanzania mwaka 1962,” alisema Mkuchika na kuongeza:

  “Kwa kuzingatia matamko haya na umuhimu wa lugha ya Kiswahili, ikiwa sasa pia ni lugha ya Kimataifa inayotumiwa mathalan kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika, serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, inasisitiza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika shughuli za serikali na kutoa kauli kuzingatia vipengele vilivyosisitizwa awali.”

  Alisema matamko hayo ya viongozi wa serikali, yalianza kutolewa baada ya Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kulihutubia Bunge kwa mara ya kwanza kwa lugha hiyo Desemba 12, 1962.

  Alisema baada ya hapo, mwaka 1967, aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais, Hayati Rashid Kawawa, alitoa waraka wa matumizi ya lugha hiyo kwa mawaziri, naibu mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya, walimu wote na watumishi wa serikali wote.

  Mkuchika alisema pia mwaka 1974 aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi katika Rais, Utumishi, alitoa waraka wa utumishi namba moja wa mwaka 1974 ulioeleza kuhusu matumizi ya lugha ya Kiswahili katika ofisi za serikali.

  Alisema vilevile, Mei 2005, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), William Lukuvi, aliagiza taarifa za mikutano, semina na warsha nchini zitolewe kwa Kiswahili kwa manufaa ya wananchi, pia taarifa za miradi inayohusu wananchi ni lazima zitolewe kwa lugha hiyo ikiwa ni pamoja na vipeperushi na nyaraka zinazohusu miradi hiyo.

  Mkuchika alisema katika kikao cha Baraza la Mawaziri cha Februari 18, mwaka huu, Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, alisisitiza suala la matumizi ya lugha ya Kiswahili katika shughuli za serikali na kuwakumbusha watendaji serikalini kuzingatia waraka wa Hayati Mzee Kawawa alioutoa alipokuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais.

  ---Tangu Tanzania ilipopata uhuru mwaka 1961 kutoka Uingereza, serikali imekuwa ikiendesha shughuli nyingi kwa lugha ya Kiingereza.

  Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, zimekuwa zikitolewa kauli na viongozi mbalimbali wa serikali kutaka Kiswahili iwe lugha rasmi, ikiwemo kufundishia kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu.  CHANZO: Nipashe
   
Loading...