elivina shambuni
JF-Expert Member
- May 31, 2018
- 461
- 295
WAKATI wakazi wa mji wa Kisarawe mkoani Pwani, wakitarajia kuanzia leo kupata majisafi ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa), wakazi wa Ukonga, Ukonga Magereza, Gongo la Mboto, Pugu na Banana wilayani Ilala, watapata majisafi ifi kapo Aprili mwakani.
Hayo yamebainishwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Cyprian Luhemeja wakati akieleza maendeleo ya mradi mkubwa wa maji wa Kisarawe kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Dawasa, Jenerali Davis Mwamunyange, jana.
Mwamunyange aliipongeza Dawasa kwa kutekeleza mradi huo mkubwa kwa kutumia fedha zao za ndani, wakati kwenye miradi mingine mingi wamekuwa wakipewa fedha za serikali. Alisema mradi huo ni wa kihistoria na wa mfano kwa mamlaka zingine za maji nchini. “Kazi kubwa imefanyika Kisarawe. Mradi umekamilika kwa asilimia 99, zimebaki kazi ndogo ndogo, leo ilikuwa niwashe pampu ya maji kwenye tangi kubwa la Kisarawe, lakini bado kazi ndogo sana za kukamilisha” alisema Mwamunyange.
Aliwaeleza wakazi wa Kisarawe kuwa Dawasa imetekeleza kikamilifu na kwa haraka agizo lililotolewa na Rais John Magufuli la kuondoa kero ya maji katika mji huo. Luhemeja alifafanua kuwa Dawasa imetekeleza mradi huo wa Kisarawe, kwa kutumia fedha za ndani na umegharimu zaidi ya Sh bilioni 10. Alisema mradi huo utahudumia wananchi zaidi ya 25,000.
Luhemeja alisema tangi kubwa lililojengwa Kisarawe, litahifadhi maji mengi kuliko mahitaji ya mji wa Kisarawe, hivyo Dawasa imeamua kuongeza mtandao wa maji katika maeneo mengine ya jirani, yatakayohudumiwa na tangi hilo kubwa. Alisema wameanza kujenga tangi dogo eneo la Pugu, litakalorahisisha usambazaji maji ya Dawasa maeneo ya Pugu, Ukonga, Ukonga Magereza, Gongo la Mboto na Banana wilayani Ilala.