Kipima Joto cha Mwigulu Nchemba urais 2015

Hussein Massanza

JF-Expert Member
Dec 26, 2012
918
1,994
Kabla ya Januari 2014, kwa tathmini yenye mzani wenye usawa, Mwigulu Nchemba alikuwa mwanasiasa mpenda fujo, mkereketwa sana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mwenye kipaumbele kikubwa kwenye chama kuliko utaifa.

Katika majukwaa ya siasa, Mwigulu alisifika kwa kutema maneno ya shombo dhidi ya wapinzani. Bungeni ‘alikinukisha'. Hoja zake mara kadhaa zilisababisha vikao vya bunge kusimama, pale wapinzani waliposimama na kutaka muongozo wa kiti juu ya maneno au matamshi yake.

Kila uchaguzi mdogo ulipofanyika tangu baada ya Uchaguzi Mkuu 2010, Mwigulu aliingia kwenye rekodi ya kuhusika na vurugu ama kwa yeye mwenyewe na matamshi yake jukwaani au kutajwa kuunda vikundi vilivyohusika kufanya mashambulizi dhidi ya wapinzani.

Akiwa mratibu wa uchaguzi katika chama chake, Mwigulu hawezi kujiweka mbali na matukio ya vurugu yaliyotokea kwenye Uchaguzi Mdogo wa Igunga mwaka 2011, yupo aliripotiwa kuuawa, mwingine kumwagiwa tindikali. Ni matokeo ya ufanyaji wa siasa za chuki.

Lugha za mashambulizi, kauli za Mwigulu kushambulia viongozi wa Chadema ziliamsha shari na chuki kubwa ya kisiasa. Kiongozi lazima ujue kuchuja maneno. Vem atambue kuwa vyama vina wafuasi ambao kila mmoja ana kiwango chake cha akili, ustaarabu, uvumilivu, uungwana na ukatili.

Kiongozi wa chama cha siasa anaposimama jukwaani na kueleza kuna ukatili umefanywa, moja kwa moja akatuhumu aina fulani ya watu kuhusika, halafu akawaaminisha wafuasi wa chama chake kuwa aliyetendewa unyama ni mwenzao na alishambuliwa kwa sababu ya uanachama wake. Hiyo ni hatari kupita kiasi.

Hiyo ni kauli inayojenga chuki na hasira. Kiongozi wa kisiasa anaweza kudhani maneno yake ni mtaji tu wa kutengeneza huruma ya watu waweze kukipigia kura chama chake, anashindwa kuwaza hao aliowaambia kila mmoja ana kichwa chake.

Hakuna mtaa wa CCM, Cuf, Chadema, NCCR-Mageuzi, ACT, NLD, TLP, UDP, DP au wa chama kingine chochote, kwa maana hiyo wafuasi wa vyama hivyo wanachangia maeneo, mitaa, vitongoji, vijiji na mpaka nyumba za kuishi.

Kwa maana hiyo, kiongozi wa kisiasa anapohubiri chuki, maana yake anawaambia watu wanaoishi pamoja wachukiane. Chuki ni mwanzo wa ugomvi, hivyo basi mwanasiasa mchonganishi hawezi kujivua lawama pale wafuasi wa vyama wanapogombana.

Ndiyo maana Mwigulu siwezi kuacha kumtaja kuwa sababu ya matukio mabaya yaliyojiri Igunga kwa sababu hotuba zake jukwaani zilijenga chuki. Ni rahisi kuamini kwamba ndizo ziliibua hasira kwa wafuasi wa CCM kuwawinda wale wa vyama vya upinzani.

Ni ukweli kwamba wapinzani, hususan Chadema nao walikuwa wanarusha maneno ya vijembe na chuki ndiyo maana Mwigulu na timu yake walikuwa wanajibu. Mantiki hapa ni kwamba wote ni kundi moja. Ni wafanya siasa mbaya. Ila hapa tunamjadili Mwigulu.

Mfano; kuna hotuba Mwigulu aliwaambia wananchi wa Igunga kwamba kijana aliyemwagiwa tindikali ni mfuasi wa CCM na sababu ya kushambuliwa ni u-CCM wake, akawataja waliomshambulia kuwa Chadema.

Naamini Mwigulu alilenga kuwaambia wananchi wa Igunga waichukie Chadema kwa maana ya menejimenti yake. Hakujua kuwa wafuasi wa CCM waliosikiliza hotuba yake, kila mmoja aliondoka na lake. Mwingine anaamini Chadema ni mpangaji mwenzake, ni jirani yake.

Utashangaa nini ukisikia siku mbili baadaye kuna mwananchi anayesemekana ni mfuasi wa Chadema amekutwa ameuawa na kutupwa porini? Ipo wazi kwamba kwa sababu walioambiwa mwenzao amemwagiwa tindikali kila mmoja ana akili zake, inashindikana nini kulipa kisasi?

Mwigulu ni mwasisi wa siasa za kuitana magaidi. Kwa mara ya kwanza tukasikia Igunga kwamba kuna kambi za mafunzo ya ugaidi. CCM wakiwaita Chadema magaidi, vivyo hivyo Chadema nao walitoa matamko yao kuwa CCM ndiyo wamiliki wa chuo cha ugaidi, kwamba kiliingiza timu ya magaidi kutoka nje ya nchi.

Hayo ni matokeo ya siasa za kushambuliana bila hoja. Matokeo yake ni kuhamasisha chuki katika jamii, wafuasi wa vyama pinzani kuchukiana. Vilevile kuwafanya wananchi waishi kwa hofu, maana ukiwaambia wananchi kuna magaidi, unategemea wataishi kwa uhuru?

Kumbukumbu ya matukio ya Mwigulu kufanya siasa za bila hoja na kushambulia wapinzani hususan Chadema ni ndefu sana. Hii inatosha kuonesha ni mwanasiasa wa aina gani. Anaamini katika mashambulizi, siasa za "ukimwaga mboga namwaga ugali", siasa mbovumbovu (gutter politics) au ‘mbofumbofu' kama msemo wa Mwana-Hip Hop wa Kimasai, marehemu Mr. Ebbo.

Wakati fulani mwaka juzi (2013), Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, alizungumza bungeni akiwataka mawaziri wafanye kazi, wasijibu vijembe vya wapinzani kwa sababu yeye (Livingstone) na Mwigulu peke yake wanatosha. Wakati huo Mwigulu hajateuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha.

Kauli hiyo ya Livingstone, ilitoa jawabu kuwa yeye na Mwigulu ndiyo wataalamu wa siasa za kushambuliana, kujibizana na kuchafuana. Wengine ni watendaji, ila wao jukumu lao ni kutengeneza vijembe vya kurushiana na wapinzani.

Maendeleo ya nchi yeyote yanatokana na aina bora ya siasa zake. Siasa za ukweli, zinazoendeshwa kwa hoja zenye kujenga kwa kutawaliwa na ustaarabu, zimefanikisha maendeleo ya mataifa mengi.

CCM wanatekeleza ajenda zao, wapinzani wanapoona kuna kasoro wanakosoa, wanaokosolewa wanasikiliza, wakibaini kuna ukweli wanafuata, wakiona wakosoaji hoja zao hazina faida, wanazipinga kwa hoja. Siasa zisizo na hoja ndizo zinaiyumbisha nchi.

Tunapoelekea Uchaguzi Mkuu 2015 na kwa vile Mwigulu anatajwa kama mmoja wa vijana ambao wanatamani kuteuliwa na chama chake (CCM), kuwa mgombea Urais, kwa mtindo huo wa siasa unadhani anaweza kufaa? Anaweza kweli kuvaa viatu vya kuliongoza taifa la Tanzania lenye mikikimikiki ya kila aina?

Je, kwa kupitia kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwamba maendeleo ya nchi yanategemea vitu vinne, Ardhi, Watu, Viongozi Bora na Siasa Safi, Mwigulu anaweza kutosha kweli kumrithi Rais Jakaya Mrisho Kikwete?

Kama siasa safi ndiyo zao la viongozi bora. Na kama tumeshamuona Mwigulu aina yake ya siasa za vijembe na kushambuliana badala ya ujenzi wa hoja, anaweza kweli akawa kiongozi mwenye ajenda nzuri za kulifanya taifa liendelee kiuchumi na vilevile libaki na amani pamoja na utulivu wake?

Kama Mwigulu ameshajipambanua kuwa aina ya siasa zake ndiyo hizo, anawezaje kuifanya nchi hii kuwa na siasa safi ikiwa mwenyewe ni muumini wa siasa zisizofuata utaratibu (rough-and-tumble politics)? Au atajifunza siasa makini akiwa Ikulu? Nawaza tu!

Labda ujana wake umechangia. Ugeni wake kwenye majukwaa ya kitaifa kisiasa umemponza, maana nyota ya Mwigulu ni kati ya mwaka 2010 na 2015. Kama ndivyo, basi vema atumie muda wa sasa kuzifanyia masahihisho siasa zake, pengine miaka ijayo akafaa. Natafakari tu!

Kwa wanaoamini kwamba Mwigulu ni bora, waje na majibu haya kama Mwarabu anaweza kuwa Mhindi mzuri. Yaani mwanasiasa mwenye mrengo wa siasa majitaka (gutter politician) anaweza kweli kuwa mwanasiasa safi (wise politician).

Mwigulu katika siasa zake, ameonesha yeye ni mzalendo sana wa chama chake kuliko nchi. Amejipambanua kuwa shabaha namba moja ya siasa zake ni kuwakabili wapinzani kuliko masuala mazito yanayoikabili nchi.

Katika siasa za kisasa, tunahitaji kuona wanasiasa wanabishana na kuungana pamoja katika masuala nyeti ya kitaifa, ni utoto wanasiasa kuanza kushambuliana maisha binafsi au mambo madogomadogo ambayo hayamsaidii mwananchi maskini.

Siasa za kujali chama (collective interest) kuliko utaifa ni aina nyingine ya ubinafsi. Mwanasiasa anapaswa kuweka mbele manufaa mapana ya kitaifa (interest of state) kwa siasa za ndani na za kimataifa lazima apiganie maslahi ya taifa (national interest).

Wanasiasa wenye mitazamo ya aina hiyo, ndiyo ambao hujikuta wanaungana pamoja bila kujali tofauti ya vyama vyao. Mfano hai ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahman Kinana, mara nyingi amekuwa na hoja moja inayoshabihiana na wapinzani kuhusu uwajibikaji wa viongozi kwa sababu ni ajenda nzuri kwa maslahi ya kitaifa.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka na Dk. Hamis Kigwangala (Nzega) wote CCM, mwanzoni kabisa hoja ya Tegeta Escrow ilipoanza, waliungana na wabunge wa upinzani, Zitto Kabwe, David Kafulila na John Mnyika, kusisitiza kuna wizi ulifanyika na lazima wahusika wawajibike.

Sendeka na Kigwangala, walijua kabisa kwamba misimamo yao ilikuwa inaivua nguo serikali inayoongozwa na chama chao lakini hawakurudi nyuma. Hawakujali vitisho wala kumuonea mtu haya. Hiyo ndiyo inaitwa kuiweka nchi mbele halafu chama baadaye.

MWIGULU NI KIGEUGEU;

Talking past each other ni msemo wa Kiingereza wenye maana ya watu kuzungumza vitu tofauti na kwa malengo yanayosigana lakini wao wanakuwa wanadhani wanazungumza jambo moja kwa madhumuni yanayofanana. Hii niliibaini katika sakata Tegeta Escrow.

Watu wengi walimsifia Mwigulu kwa mchango wake bungeni wakati akichangia ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kwamba alizungumza vizuri sana. Najua wapi aliwateka watu mpaka wakamwagia sifa kemkemu.

Msisitizo wa Mwigulu kuwa serikali haiwezi kukimbizana na akina mama barabarani wanaofanya biashara ndogondogo kukusanya kodi, ikaacha fedha nyingi za kodi shilingi bilioni 31 zipotee, ni hapo ndipo aliwakamata watu. Alionesha kujali wananchi maskini.

Il ukweli wa mchango wa Mwigulu ni kuwa alijikita kwenye kipengele cha kodi ambayo tayari ilikuwa imeshabainishwa kuwa haijalipwa kutokana na uchotwaji wa fedha za Tegeta Escrow bila kufuata utaratibu.

Hoja ya kodi haikuwa mpya, ilishaelezwa na kamati, ila Mwigulu aliipazia sauti na kwa sababu yeye ni sehemu ya serikali, akaonekana ametetea sana lakini ukweli ni kuwa hoja yake ilisigana na waliotaka uwajibikaji.

Kwa kuuchambua mchango wa Mwigulu ni kwamba aliwasafisha waliogawiwa fedha kwa kutangaza kuwa wanatakiwa walipe kodi kwa kila mmoja kulingana na kiasi alichoingiziwa kwenye akaunti yake.

Kama Naibu Waziri wa Fedha, kauli ile ilimaanisha tamko la mamlaka ya ukusanyaji kodi. Na kwa mujibu wa sheria, fedha inayolipishwa kodi maana yake ni fedha halali. Hivyo, baada ya kukatwa kodi, kila mmoja atatumia kiasi chake kwa uhuru bila bughudha.

Utamfikisha mtu mahakamani kwa sheria ya wapi ikiwa tayari umeshatakatisha fedha zake haramu kwa kumlipisha kodi? Kortini mlalamiji ni serikali kwa maana ya jamhuri, jaji atauliza serikali inalalamika nini ikiwa tayari ilishzitambua pesa zilizoibwa kuwa ni halali na kumlipisha kodi mlalamikiwa?

Ilikuwa ni "talking past each other", watu wanasema fedha zote za Escrow zirudi, Mwigulu akaanzisha hoja waliogawiwa walipe kodi. Ilikuwa ni kupotosha. Leo tunasikia kuna michakato ya kuwatoza kodi waliogawiwa fedha za Escrow. Si kwamba zote zirudi, kodi tu! Wengine wanafikishwa mahakamani. Huu ni mkorogo wa mambo (mismatching).

Hata hoja ya shilingi bilioni 31 ya kodi ambayo PAP wangepaswa kulipa endapo fedha walizochota zingekuwa halali yao, haikupaswa kusimamiwa leo kuwa ilipwe. Hoja ni kuwa fedha zimechotwa bila kufuata utaratibu, kwa hiyo ni wizi. Zinatakiwa kurudi zote. Msisitizo wa kulipa kodi wa nini?

Novemba 23, 2014, ikiwa ni siku tatu kabla ya Mwigulu kuwasilisha mchango wake wa Tegeta Escrow bungeni, alikaririwa na gazeti la Mwananchi akisema kuwa mali zote za IPTL zikamatwe na wahusika wote wakamatwe, maana kila kitu kilikuwa wazi kwamba fedha za umma zimeibwa.

Mwananchi lilimkariri Mwigulu akisema kuwa haiwezekani wahusika wawajibike tu kwa kujiuzulu, kwa kuwa huko ni sawa na kutoa likizo wakatumie mabilioni yao, hivyo wachukuliwe hatua ipasavyo na wafilisiwe.

Hii ilikuwa ni kauli bora kabisa ya Mwigulu na yeye mwenyewe kwa kuitambua aliinukuu kwenye ukurasa wake wa Facebook, lakini kwa bahati mbaya hakuiwsilisha kama ilivyo katika mchango wake bungeni, hivyo kuleta hali ya ukigeugeu.

Najua kwamba siku hizi Mwigulu anaitwa Sokoine wa pili, je, ni sahihi kwa kiongozi mwenye sifa za kuchukua nchi awe anabadilika kwa kiwango hicho? Maneno ya jana hayafanani na ya leo. Labda ana tatizo la kujiamini mbele ya macho ya watu fulani, kama ndivyo basi bado mchanga, aachwe akomae zaidi. Ni mtazamo tu!


ILA KWA HAKIKA MWIGULU NI NYOTA NJEMA;

Tangu Januari, 2014, Mwigulu alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha, ameonesha wazi kuwa nafasi hiyo alipaswa kupewa tangu muda mrefu na kwa hakika kama ingetokea hivyo angekuwa amekwishafanya maajabu mengi na makubwa.
Kuna mambo mawili ambayo Mwigulu ameyasimamia kikamilifu na kwa hakika anastahili pongezi kwa hayo. Na kwa sura aliyoonesha, hata anapoitwa Sokoine wa Pili (Sokoine II), kwa kufananishwa na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu mara mbili, hayati Edward Moringe Sokoine, sioni tatizo.

Mosi; Amepigana kwa vitendo kuhusu suala la uwepo watumishi hewa ambao wanalipwa mishahara kila mwezi. Watumishi hewa ni wizi mkubwa ambao umekuwa ukifanywa na watendaji ambao siyo waaminifu kwa lengo la kujipatia fedha nje ya utaratibu.

Katika kupambana na hilo, Mwigulu amekuwa akisimamia hoja kuwa Tanzania inaweza kujiendesha yenyewe kama mianya yote ya matumizi mabaya ya fedha za serikali, itazibwa pamoja na kukata minyororo yake yote.

Pili; Jambo lingine ambalo Mwigulu amekuwa akilivalia njuga ni vitendo vya ukwepaji kodi ambavyo vinafanywa na wafanyabiashara wengi wakubwa. Ameshasuka mipango na kuvamia ofisi kadhaa ambazo anakuwa amepenyezewa taarifa ya kuwepo kwa mashine feki za risiti. Hakika ni mpambanaji.

Kama amekuwa imara hivyo kwa nafasi yake ya Unaibu Waziri, hali itakuwaje pale atakapoteuliwa kuwa waziri kamili wa Wizara ya Fedha? Kwa hakika ameonesha nyota njema kwamba anaweza kuwa msimamizi imara wa rasilimali za nchi hii.
Upande mwingine, Mwigulu ni baba mzuri wa familia, sifa ambayo inampambanua kiongozi mwenye msimamo unaoeleweka. Picha zake akiwa na mkewe pamoja na watoto wake watatu, zinaonesha ndani ya nyumba yake ni mlezi mzuri.

Kiwango chake cha elimu ni bora kabisa. Hivyo unaweza kutathmini kipimajoto hiki, kama unaona anafaa sana ni sawa, ila ni imani yangu kwamba Mwigulu anahitaji muda zaidi, anaweza mtu sahihi sana kwa nyakati zijazo.

Na Luqman Maloto
 
Tatizo chama chake hakitaki watu wenye sifa ya kupambana na mafisadi hasa wala rushwa na wakwepa kodi

Usishangae msimamo wake kuhusu ESCROW ukawa umewachukiza watu wengi ndani ya CCM kuliko misimamo ya akina Asumpter na wabunge wengine

Leo kuna mafisadi ambao chama kinawakumbatia tena mafisadi ambao hawawezi hata kidogo kutoa kauli za kukemea Rushwa ambayo ni tatizo kubwa sana ndani ya nchi


Wapo wagombea hata vijana ambao hawakusikika kabisa bungeni kwenye sakata la ESCROW na perfomance zao ni za chini kwenye wizara zao lakini kila siku wanatangaza Urais kwa nguvu kubwa.Ni aibu na hawana tofaauti na wagombea wengine dhaifu na wale mafisadi

Huwezi kurekebisha mfumo kama huwezi kujitoa muhanga kupambana na ufisadi
 
Yeye mwenyewe ni debe tupu, chama cha mafisadi asiyefisadi anafanya nini huko??? tulimwamini 6, je unakumbuka alichokifanya hivi juzi kati? Mwigulu hasara nyingine kwa taifa
 
NI KWELI MWIGULU ANAJUA LAKINI ASUBIRI MIAKA 20 mbele baada ya Lowassa/January au mwanaCCM mwingine~zitto~Mwigulu.
 
Back
Top Bottom