Kiongozi atokane na ushindi wa mapambano ya kifikra (...)

Oct 29, 2012
22
4


Salaam sana ndugu zangu wana wa Tanzania nchi yenye neema na amani ( ...). Kipekee niwashukuru sana kwa jinsi mchangiavyo na kutoa mawazo na maoni endelevu kwa lengo moja. (la kukomboa na kuokoa Tanzania inayopotea). Leo hii nimepata wazo litakalo mjadala na ukosolewaji wa kifikra ili liweze kujenga...


Licha ya kuwa na rasilimali nyingi, Tanzania imeendelea kuwa ni nchi masikini inayotegemea misaada. Sababu kubwa ya kuwepo kwa hali hii ni uongozi mbovu!.

Baadhi ya viongozi wa kitanzania waliokabidhiwa dhamana ya usimamizi wa rasilimali hizo wamekuwa ndio viranja wa kuhamisha rasilimali hizo kwenda nchi za nje, pasina kumnufaisha Mtanzania wa hali ya chini.


Ni dhahiri kwamba kero hizi zinaweza kukwepeka iwapo tutajongea na
kuwakataa viongozi ‘uchwara' na kuwachagua viongozi kwa ‘mwanga mpya'ifikapo 2014 (mitaani) na pia 2015 (uchaguzi mama). Hatuna budi kuwaangalia viongozi makini na kuwapa jukumu la kusimamia rasilimali zetu, la sivyo tutakuwa tunarudia - rudia makosa yale yale.


Katika kumpata kiongozi sahihi kwa mwanga huu mpya, Watanzania t
unapaswa kuachana na fikra za zamani na kuanza kufikiri kwa namna mpya kabisa. Ninamaanisha namna mpya ya kuwapima viongozi wetu tunaowataka.Zamani mgombea alikuwa anakuja huku akituringishia vyeti vyake vya elimu na wapi amesoma, na Watanzania tulivutiwa sana na yule aliyeonekana kusoma sana na kumfikiria kwamba huyo anafaa kutokana na elimu yake.

Uongozi ni ‘uwezo'. Uongozi siyo elimu, uzoefu au umri. Hivi vyote vinaweza kumsaidia mtu kuwa kiongozi mzuri (...), lakini havimfanyi mtu kuwa kiongozi mzuri au hata kuwa kiongozi. Mtu anayetaka kutuongoza ni lazima awe ni yule mwenye uwezo wa kutufanya tuamini kwamba anaweza, na ni lazima awe na maslahi yetu moyoni mwake. Lakini pia kiongozi huyo awe yuko tayari kusimamia maamuzi yake na kukubali matokeo ya maamuzi hayo.

Siyo sahihi kusema kwamba kiongozi mzuri ni yule anayetuahidi nini atakachotufanyia, bali ni yule ambaye yuko tayari kutufanyia sisi Watanzania yale tuyatakayo kama wananchi. Uwezo huu wa kiuongozi ndio unaomtofautisha mfuasi na kiongozi,na uwezo huu huoneshwa katika maamuzi. Mara nyingi masikio yetu yamekuwa yakishuhudia Watanzania tukilalamika huku tukisema kwamba tunahitaji la kiongozi mwenye maamuzi magumu ili aoneshe uongozi wake.

Ukweli ni kwamba uongozi siyo kufanya maamuzi magumu, bali uongozi ni kufanya maamuzi bora ambayo mara nyingi kwa viongozi wetu huwawia vigumu kuyafanya.Tunapolilia maamuzi magumu kutoka kwa viongozi, wakati mwingine tunawapa nafasi ya kurithishana nchi (mh...).

Pia hata kutowachukulia hatua za kinidhamu mafisadi bado ni maamuzi magumu ambayo wameshayafanya kwani yanapelekea taifa kuteseka na kupata kipindi kigumu kwa ujumla. Uamuzi tunaoutaka ni uamuzi bora ambao kwa viongozi wetu imekuwa ni vigumu kufanya ubora huo hivyo kuitwa uamuzi mgumu. Uamuzi bora hutanguliwa na misimamo bora na hii ndiyo tofauti iliyopo baina ya ‘viongozi bora' na ‘bora viongozi'. Mathalan kiongozi bora ni lazima awe na msimamo wa kuichukia rushwa ili awe na uwezo wa kuchukua maamuzi (bora) ya kupambana na rushwa, kwani rushwa ni mzaliwa wa kwanza wa uongozi mbovu.

Lakini pia kiongozi ni lazima achukie uonevu ili awe na msimamo wa kutochukua maamuzi ya kumwonea mtu. Msimamo bora hutanguliwa na fikra bora. Kiongozi hawezi kuchukua msimamo bora kama fikra zake na mtiririko wa fikra zake siyo sahihi. Kiongozi ambaye ni mvivu kufikiri na kujenga hoja na kuzipima kwa kina hujikuta akichukua misimamo mibovu kila mara. Hivyo basi, ili mtu aweze kufikiria misimamo bora ni lazima awe na fikra bora ili hatimaye aweze kuchukua ‘maamuzi bora'. Nje na hapo misimamo yake itakuwa ya kutuingiza sisi wananchi katika hasara za rasilimali zetu mathalan katika mikataba ya madini.

Ni kwa sababu hiyo, kama taifa na kama wazalendo unapofika wasaa wa uchaguzi ni lazima tumpime kiongozi siyo kwa kile anachokisema, bali kwa kile anachokisimamia. Hiki anachokisimamia huwa kinaonekana kwenye historia yake. Tusikubali kudanganyika na kurubuniwa tena na viongozi hewa 2015... Jongea Mtanzania!.

Kiongozi anayeibuka kipindi cha uchaguzi na misaada kwenye jimbo lake ni kiongozi wa kuogopwa. Viongozi bora hawaanzi wakati wa chaguzi, bali ni wananchi wenzetu na tumekuwa nao wakituonesha njia na kutushawishi katika shughuli mbalimbali za maendeleo hata bila ya wao kuwa na maslahi ya uchaguzi au kuchaguliwa. Hawa ndio viongozi ambao hutambulika kwa fikra zao, misimamo na maamuzi yao bora, na hawa ndio tunaowahitaji ili kuanza ujenzi wa misingi ya kuushinda ufisadi na kuasisi taifa jipya la Tanzania.

Hii inatokana na sababu kwamba viongozi wengi wa Tanzania wamepungukiwa na kiasi kikubwa cha maadili hasa baada ya kifo cha ‘Baba wa Taifa', jambo ambalo linahatarisha amani, utulivu, maendeleo na ustawi wa Tanzania. Mmomonyoko wa maadili unadhihirishwa na mambo kadha wa kadha ikiwemo ongezeko kubwa la rushwa na ufisadi,uvunjwaji wa haki za binadamu, tabia na hulka ya viongozi kujilimbikizia mali, kutoheshimiana na hata kujengeka kwa mitandao mbalimbali isiyo rasmi yenye sura za kisiasa (hata makwetu uZito upo)

Hawa ndio viongozi wanaoigawa jamii katika makundi kwa maslahi yao (divide and rule). Leo wameona rasilimali zinajitosheleza ukanda huu watasema ‘tutengane na wale' kesho mkoa huu ukigundua kwamba una rasilimali ya mafuta,basi nao unajitenga na mikoa iliyobaki ili uweze kufaidi rasilimali hiyo kipekee. Lakini wanaokaa nyuma ya mapazia haya ya kiasimu ni wale tuliowapa dhamana ya kutuongoza ambao ni wavivu wa kufikiri na kushirikisha historia na mantiki Mambo haya yameondoa uzalendo, uadilifu, ufanisi na imani ya wananchi kwa viongozi na serikali yao kwa ujumla.

Hivyo basi,... ni dhahiri kwamba Watanzania tunahitaji viongozi imara wenye fikra za kujenga taifa na kutumia rasilimali zetu kwa manufaa ya Watanzania wote na siyo kama ilivyo sasa (...).

Hakuna kazi ngumu sana ya kuwapata viongozi hawa kwani tunaishi nao, nao wanaishi miongoni mwetu, hivyo ni kujitahidi na kuhakikisha kwamba hatutoi kura zetu kiholela.

Binafsi niliwahi kutoa maoni yangu kwenye kikao ambacho kililenga kumpata Rais wa Serikali ya wanafunzi Chuoni. Nilitaharuki sana (!!!) kwa wachangiaji wengi waliowahi kusema na kutoa maoni yao kwenye kile kikao kwani wengi wao walilienga sana kutafuta spika, tarumbeta na ngoma ili kuwateka na kuwafurahisha wapiga kura ili mwisho wa siku tushinde. Kila mmoja alisema ‘tutafute spika na mziki mkubwa' (...).

Nilipopata nafasi nililisema hili "ni kweli kwamba ili tuweze kuwapata wapiga kura na kisha kuvuta makini yao tunahitaji hizo spika na redio, lakini tukumbuke kwamba wapiga kura wanataka wampate ‘mshindi wa mapambano ya kifikra' ambaye watampa kura. Ni vyema pia kujiandaa na kuomba mdahalo ambao tutautumia kuudhihirishia umma kwamba tunajua tunachokitaka na pia tuna sababu za kuwaomba kura". Nashukuru kwamba kiongozi wetu tuliyekuwa tumempendekeza tangu awali alikuwa ‘anajitosheleza'. Ilinivutia sana na hadi leo (na kesho) natamani (na nitatamani) sana tuwapime wagombea wetu kwa njia ya midahalo ambayo yatoa fursa sawia kwa kila mmoja (wa wagombea) kujieleza nasi tuweze kutumia muda huo kumpima.... Jongea Mtanzania

Hii ni kutokana na ukweli kwamba viongozi wengi wa ki-Afrika hupenda kuendesha siasa za majungu na za kumjadili mtu, huku wakisahau kujadili mustakabali wa taifa jambo ambalo linasababisha wawekeze kwenye maendeleo ya vitu na kuacha maendeleo ya watu (content) mara tu wapatapo fursa za uongozi.

Leo hii dhamana imekuwa ni kazi. Ubunge, uenyekiti na urais vyote hivi kwa bara letu la Afrika tunaviona kama kazi pasina kutambua kwamba uongozi ni dhamana na kiongozi ni mali ya jamii. Ni yupi kati ya viongozi wetu wa kitanzania tunaweza sema ni ‘mali ya jamii'?. Ni Chuo kipi Kikuu leo hii kina viongozi wenye udhubutu kutetea maslahi ya umma kama zamani?. Ni kiongozi yupi wa kitaifa anayekubali kupata ushauri kutoka tabaka la vijana?. Ni ofisi ipi au kitengo kipi cha kitaifa ambacho miongoni mwa jopo la washauri kuna kijana (msichana ua mvulana?). Hakuna. Hawapo kabisa. Ukihoji utaambiwa ‘aah vijana siyo waelewa wa mambo bwana!'. ‘Kijana hana uzoefu (experience) wa kujitosheleza na kushauri'!.

Lakini leo hii viongozi wanakimbia midahalo vyuo vikuu na vya kati. Kesho watakimbia sekondari, primary na baada ya hapo wataanza kukataa kuonana n a wananchi kwa kuhofia ‘uwezo' wao na ukaribu wao na matatizo ya wapiga kura wao. Ni imani yangu kwamba viongozi wanaotokana na mapambano ya kifikra wana uwezo na maadili ya kiuongozi na hufuata maadili ya kiuongozi katika utendaji wao, kwa mfano, kwa kuheshimu katiba ambayo ndiyo sheria mama, kutambua kwamba cheo ni dhamana, kusimamia vyema rasilimali za wananchi kwa faida ya pamoja, kutambua na kuheshimu maamuzi ya wananchi waliowapa dhamana hiyo, na pia kujenga utamaduni wa kuwajibika pale wananchi wanapo wahusisha na kashfa na makosa ya kimaadili.


Tuwachague viongozi wenye kujua matatizo yanayotukumba na kututesa sisi wananchi wa Tanzania, na siyo wale ambao hawajui hata uwepo na vyanzo vya matatizo yetu, na cha kushangaza ni kwamba hawa hawa ndio wanaokuwa mstari wa mbele kukimbilia na kung'ang'ania nyadhifa mbali mbali tena za ngazi za juu katika uongozi pasina wenyewe kuwa na maslahi ya wananchi kwa ujumla katika fikra, mawazo, na mioyo yao... Jongea Mtanzania!

Naomba kuwasilisha.
 
Back
Top Bottom