Kilango na katiba mpya

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
MJADALA kuhusu katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, umeendelea kupamba moto na jana Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango, aliitaka serikali kusikiliza kilio cha wananchi na kukitolea kauli kulingana na matakwa yao.Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Kilango alisema kwa mazingira yaliyopo, katiba mpya haiepukiki na kwamba serikali inapaswa kuanza maandalizi ya kupata katiba hiyo.

"Nitashangaa kama serikali haitafanya hivyo wakati wenye nchi (Watanzania) na ambao wameiweka madarakani, wana kiu ya upata katiba itakayokidhi mahitaji yao," alisema Kilango.
"Suala la katiba mpya kwa sasa haliepukiki na serikali inapaswa kushirikiana na vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa, kuhakikisha kuwa katiba inayoliliwa na wananchi, inapatikana na kukidhi matakwa yao," alisema.

Kilango alisema madai ya katiba mpya ni halali kwa kuwa yanatolewa na wenye nchi, ambao ni Watanzania.

"Wananchi wapewe katiba mpya na kingine chochote wanachohitaji kwa kuwa ni haki yao. Suala hili lisichukuliwe kisiasa tena," alionya.

Hata hivyo mbunge huyo, alitumia fursa hiyo kuwaonya wanasiasa wasilifanyie suala hilo malumbano yasiyokuwa ya msingi kwa sababu malumbano hayo yanaweza kuleta machafuko.

Alisema wanasiasa hawapaswi kulifanya suala hilo malumbano kwa kuwa wanaweza kujenga au kubomoa nchi.

"Wanasiasa hatuna haja ya kujadili hili la katiba kama mapambano. Hatuhitaji hilo," alisema Kilango akitolea mfano wa nchi za Gabon na Congo Brazaville, ambazo alisema zimeingia katika vurugu kwa sababu ya wanasiasa kujingiza kwenye mapambano ya katiba.

Alisema ni ukweli usipoingika kuwa Watanzania sasa wanahitaji katiba na namna pekee ya kufikia utekelezaji wa madai hayo ni kuvishirikisha vyama vyote vya siasa katika suala hilo, badala ya wanasiasa kulumbana.

"Nakumbuka kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliposema kuwa suala la katiba mpya linazungumzika, hiyo ni picha kamili ya kuonyesha kwamba serikali haijafunga milango katika jambo zito kama hili,"alisema.

Aliisihi serikali ijipange vizuri, ili itafute njia sahihi kabisa ya namna ya kuwapatia wananchi katiba mpya kwa amani na utulivu.

"Serikali isiache suala hili likaitwa mapambano, nina uhakika kabisa kwamba wenye nchi, wanachokihitaji na kukitamani itawapa,"alisema Kilango.

Kilango ni mbunge wa kwanza wa CCM, kuwahi kujikita kwenye mjadala wa katiba tangu suala hilo liibuliwe na Chadema baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu Oktoba 31 mwaka huu.

Tangu Chadema ilipoamua kususia matokeo ya uchaguzi wa rais kwa kutoka nje wakati Rais Jakaya Kikwete akitoa hotuba ya kuzindua Bunge na kuanza harakati za kudai katiba, suala hilo limezungumwa kwa kina na watu wa kada tofauti.

Idadi kubwa ya watu hao, wametahadharisha kuwa nchi inaweza kuingia matatizoni kama serikali haitashughulikia uandikaji wa katiba mpya.

Lakini tayari Waziri Mkuu Mizengo, ameshalitolea tamko siala hilo na kuahidi kumshauri Rais Jakaya Kikwete, kuunda timu ya watu kwa ajili ya kulishughulikia.

Pinda alitangaza uamuzi huo Desemba 17 katika mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

"Isije watu wakadhani serikali ina kigugumizi; hapana. Sasa mjadala umeiva na ni vizuri lizungumzwe kwa utaratibu. Nipo tayari kuzungumza na rais. Nitamshauri mzee (rais) na nitaweka nguvu zangu huko... hilo halitawezekana tusipoweka 'initiative' (juhudi)," alisema Pinda.

"La pili, tunataka kuzungumza machache, lakini kubwa ni hili la katiba mpya. Kumekuwa na maelezo mengi, marefu, mjadala mkali; sasa hili nataka niseme tusione kama madai ya katiba si ya msingi sana; hapana. Ni ya msingi. Kwa serikali mabadiliko ya katiba ni utaratibu wa kawaida kwani ni jambo lililo ndani ya katiba," alisema Pinda.

Rais wa serikali ya awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, mawaziri wakuu wa zamani, Joseph Warioba na Frederick Sumaye, Jaji Mkuu Agustino Ramadhan, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa na majaji wengine pia wamezungumzia umuhimu wa katiba mpya na kuungwa mkono na wanasiasa na viongozi wa dini.

Tendwa, ambaye ni mtumishi wa umma, ndiye aliyeenda mbali zaidi baada ya kueleza bayana kuwa katiba ya sasa inampa madaraka makubwa rais na kwamba kama katiba mpya haitaundwa, kuna hatari ya nchi kuharibikiwa katika siku za baadaye.

Katika mazungumzo yake na wahariri, waziri mkuu alisema "mimi binafsi sioni tatizo kwa hilo kufanyika, lakini kama serikali zipo namna mbili za kulishughulikia. Moja ni kutafuta utaratibu wa kumshauri rais aunde kamati ya watu wangalie maeneo gani ya kuingiza katika katiba hata ikibidi wananchi waulizwe kuhusu ya kuwekwa mezani kwa kuhusisha vyama vya siasa na wanazuoni."

Pinda aliitaja njia ya pili kuwa ni rais kuunda timu yake ya kiserikali itakayoangalia mapendekezo ya tume zilizoundwa awali kuangalia marekebisho ya katiba na kuchukua mapendekezo yaliyojirudia yatakayoonekana kufaa kuingizwa katika katiba.

"Tume zote zina viporo vya kuanzia na kuchukua kuliko hali ilivyo sasa ambayo kila mmoja anasema lake kuhusu katiba," alisema Pinda.

Alisema kutokana na tume hizo yapo yaliyotekelezwa na yale ambayo yaliahirishwa kwa sababu ya wakati.

Hata hivyo alisema ni bora kuruhusu tume itakayokuwa pana na kuyatazama mapendekezo ya tume za awali, kuangalia na kushauri akisema kuwa huenda ikaona mambo mengine.

Katiiba ya kwanza ya Tanganyika iliundwa na mkoloni mwaka 1920 na mwaka 1961 ikaundwa katiba mpya baada ya uhuru na ikadumu mwaka mmoja baada ya katiba ya Jamhuri kuundwa mwaka 1962. Katiba ya Jamhuri ilidumu hadi mwaka 1964, wakati Tanganyika ilipoungana na Zanzibar na hivyo kuwa na katiba ya Muungano.

Katiba ya Muungano haikuandikwa upya hadi mwaka 1977 na baada ya hapo kumefanyika marekebisho 13, yakiwemo ya mwaka 1992 wakati serikali iliporejesha mfumo wa vyama vingi, lakini wanazuoni wameyapachika jina marekebisho hayo kuwa ni viraka.

Kuhusu mabadiliko ya katiba ya Zanzibar kusigana na katiba ya Muungano, Pinda alisema mapendekezo yaliyozaa marekebisho hayo ndiyo yaliyozaa maridhiano na kwamba katiba lazima ilenge maridhiano.

Hata hivyo alisema kuwa kazi iliyobaki ni ndogo ambayo alisema ni kuichukua katiba ya Zanzibar na kuioanisha na ya Muungano ili mtiririko wake uende vema bila kuathiri upande mmoja.
 
Back
Top Bottom