Kikwete na sera zake za jeshini;tutafika??

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,720
21,778
Kikwete awaonya wabunge adai mijadala yao yaweza kuleta machafuko





Rais wa Jamauhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete ambaye jana aliwaasa wabunge wa jumuiya ya madola kuepuka mijada ambayo inaweza kusababisha migogoro na machafuko katika nchi zao

Leon Bahati, Arusha na Salim Said, Dar

RAIS Jakaya Kikwete ameyataka mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola hayo kuepuka mijadala ambayo inaweza kusababisha migogoro na kuyaingiza mataifa yao kwenye machafuko.


Kauli ya Kikwete imekuja wakati kukiwa na mjadala mkubwa kuhusu uendeshaji wa Bunge la Jamhuri ya Muungano baada ya vyombo vya habari kuripoti kuwa Spika Samuel Sitta alibanwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kwa madai kuwa anaruhusu mijadala inayokichafua chama tawala na serikali yake.


Awali jana asubuhi katika mahojiano na televisheni ya Shirika la Utangazaji (TBC1), Spika Sitta, ambaye ni rais wa Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA), alisema serikali nyingi za Afrika zimekuwa hazitaki Bunge lifanye kazi yake ya kuidhibiti serikali, jambo ambalo alisema linasababisha migongano baina ya mihimili hiyo mikuu miwili ya nchi.


Akifungua mkutano wa 55 wa mabunge hayo mjini Arusha, Rais Kikwete, ambaye pia ni mlezi msaidizi wa CPA, alisema bila ya mabunge hayo kuepuka mijadala hiyo, mataifa hayo yatajenga mazingira mabaya na ambayo hayana matumani kwa kizazi kijacho.


Rais Kikwete alisema: "Mojawapo ya matazamio kwa mabunge haya ni kuweka mazingira mazuri kwa nchi zao na dunia kwa ujumla katika hali ambayo ni ya kujenga badala ya kubomoa misingi ya amani katika nchi zao."


Alifafanua kwamba CPA ina wajibu wa kuhakikisha dunia inakuwa mahali penye matumaini ya uhai na si tu kwa sasa bali hata kwa vizazi vijavyo kisiasa, kiuchumi na kiteknolojia.


Mkutano uliopita wa Bunge la Jamhuri ulikuwa na mambo mengio yaliyoashiria shauku ya wabunge kutaka serikali ieleze hatua ilizochukua katika masuala mbalimbali, yakiwemo maazimio ya chombo hicho cha kutunga sheria.


Miongoni mwa masuala hayo ni taarifa ya utekelezaji wa maazimio 23 ya Bunge dhidi ya kashfa ya utoaji zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond Development (LLC), kashfa ambayo ilisababisha Edward Lowassa kujizulu wadhifa wake wa waziri mkuu na mawaziri wawili- Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha.


Mjadala juu ya kashfa hiyo unatarajiwa kuibuka tena bungeni mwezi ujao wakati wa mkutano wa 18. Wabunge pia walikuwa wakihoji masuala mengine kama mgodi wa Buhemba, ununuzi wa mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira na kashfa ya ununuzi wa rada.


Nchini Kenya, Bunge limeitikisa serikali hadi kulazimisha mkuu wa Tume ya Kupambana na Rushwa, Jaji Aaron Ringera kujiuzulu baada ya shinikizo la karibu mwezi mzima sasa tangu ateuliwe tena na Rais Mwai Kibaki, katika mazingira ambayo bunge lilisema yamekiuka mamlaka yake ya kuidhinisa wateule.


Rais Kibaki alikuwa akitaka Jaji Ringera kutumia muhula wa pili kama mkuu wa tume hiyo maarufu kama Kenyan Anti-Corruption Commission, lakini uteuzi wake ulipingwa na baadhi ya nchi za magharibi na wananchi wengi kwa madai kuwa alishindwa kupambana na ufisadi katika awamu ya kwanza.


Akizungumzia mazingira, Kikwete alisema CPA haina budi kuyaundia sera masuala kadhaa, likiwemo tatizo la mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanatishia uhai wa binadamu pamoja na viumbe wengine.


Alisema kwamba tayari athari za hali hiyo zimeanza kutishia uwepo wa viumbe duniani akitoa mfano kupanda kwa joto la dunia ambako kumesababisha barafu kwenye milima na maeneo ya kusini nakaskazini mwa dunia kuyeyuka huku uoto wa asili ukianza kupotea na jangwa likizidi kuenea.


Awali akimkaribisha Rais Kikwete kufungua mkutano huo, Sitta alisema wajumbe wa mkutano huo wamefika kwa wingi na wamneonyesha ari kubwa ya kuchangia mada mbalimbali za mkutano huo.


Miongoni mwa mada za mkutano huo ni kukabili matatizo ya mabadiliko ya tabia nchi, mtikisiko wa kiuchumi duniani, haki za kijinsia na athari za demokrasia kwenye serikali za mseto.


Makamu wa Rais wa CPA ambaye pia ni Spika wa Bunge Kenya , Kenneth Marende, alisema CPA imelenga katika kuimarisha demokrasia na haki kisiasa kwa nchi wanachama.


Spika Marende alimwagia sifu Rais Kikwete kwa kuonyesha uwezo mkubwa kiuongozi katika eneo la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, akitoa mfano wa jinsi alivyojihusisha kumaliza machafuko ya kisiasa yaliyotokea mapema mwaka jana baada ya kutangazwa kwa matokeo ya urais na kusababisha zaidi ya watu 1,000 kupoteza maisha.


Katika hatua nyingine, Spika Sitta aliliambia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) jana asubuhi kuwa kazi za Bunge ni kuidhibiti serikali lakini serikali nyingi za Afrika hazipendelei Bunge kufanya kazi hiyo, hivyo kumekuwa na mivutano mingi baina ya mihimili hiyo mikuu miwili ya dola (Serikali na Bunge)


Alifafanua kwamba kazi mojawapo ya Bunge ni kutetea maslahi ya wananchi na nyingine ni kuidhibiti Serikali, lakini akabainisha kuwa ni vigumu sana kwa Bunge kutenda kazi ya kudhibiti serikali kwa sababu serikali zenyewe haziko tayari kudhibitiwa na kwa sababu zinataka ziwe mdhibiti mkuu.


"Hii kazi ya kudhibiti serikali ina ugumu wake na hapo ndipo migongano inapotokea baina ya Bunge na Serikali. Kwa kawaida Bunge ndilo linalopaswa kutetea maslahi ya wananchi na kulinda maslahi ya nchi, mara nyingine kazi hizo za Bunge hupingana na misingi ya utendaji wa serikali," alisema Sitta.


Spika Sitta hakutaja mifano ya serikali za nchi zilizoonyesha udhaifu huo, lakini kauli yake inaonyesha kuwepo kwa mgongano wa kimaslahi kati ya mihimili mikuu ya dola ambayo inapaswa ifanye kazi ya kudhibitiana.


Akizungumzia suala la ufisadi Spika Sitta alisema suala hilo ni la ubia kati ya nchi tajiri na masikini na sio lawama kutupiwa nchi zinazoendelea pekee.


"Sasa tunawambia wenzetu ambao ni mabunge ya nchi zilizoendelea kwamba hapa kuna ubia katika masuala ya rushwa na ufisadi, kwa sababu ili wafanikiwe katika biashara zao kwenye nchi zetu, wanaweka rushwa kama motisha ili maamuzi yanufaishe kampuni ambayo inaweza kushinda zabuni," alisema Sitta.


Wakati Spika Sitta akisema hayo Tanzania ni muathirika mkubwa wa mikataba mibovu na zabuni zinazotolewa na kampuni kubwa za kimataifa, ambazo zinatoa rushwa kama motisha kwenye zabuni zao.


Miongoni mwa mikataba na zabuni zilizoitia hasara Tanzania ni pamoja na ile ya ununuzi wa rada, ufuaji wa umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond na hata ununuzi wa ndege ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Alisema kutokana na hali hiyo si sahihi kuziangushia lawama za rushwa na ufisadi nchi zinazoendelea pekee, bali mambo hayo yanapaswa kuangaliwa katika pande zote mbili za sarafu.


"Kwa hiyo lawama si kusema tu kwamba waafrika ni wala rushwa, hilo si kweli kwa sababu kuna vishawishi vya kila namna katika kufikia uamuzi wa nani apewe zabuni katika mikataba ya makampuni makubwa ya kimataifa," alisema Sitta.


"Hivyo sisi tunazungumza kwamba hili ni suala la ubia na kwa hiyo sisi sote tushirikiane na tuhakikishe kwamba sheria za kuwabana watoa rushwa wakubwa, makampuni makubwa zinakuwa imara."


Alifafanua kwamba Tanzania kwa upande wake itajitahidi kwa nafasi yake kuzuiya mikataba ya namna hiyo, ambayo inasababisha hasara kubwa sana kitaifa na kimataifa.


"Juzi nilizungumza kwamba, fedha ambazo zilitoroshwa yani fedha ambazo zilizopatikana kwa hila kutoka bara la Afrika kwa mwaka 2007 tu, ni dola 20 bilioni za Kimarekani, wakati misaada yote iliyoingia Afrika nzima kwa mwaka huo ni dola 18 bilioni za Kimarekani," alisema.


"Kwa namna hiyo huwezi kuniambia kwamba maendeleo yanawezekana kama kinachotoka ni kikubwa zaidi kuliko kinachoingia. Sasa tatizo ni kubwa kiasi hicho, lakini kwa ubia na kwa mazungumzo tunaweza kulimaliza."


Alisema, tafsiri ya maslahi ya umma inayotolewa na bunge mara nyingi huwa inapingana na ile ya serikali, lakini uzuri ni kwamba mara kwa mara katika tafsiri ya bunge kuhusu maslahi ya wananchi ndiyo inakuwa na usahihi zaidi.


"Hii ni kwa sababu wao ndio wawakilishi wa moja kwa moja wananchi," alisema Sitta.


Akizungumzia uamuzi uliofikiwa na bunge la Kenya hivi karibuni wa kumuengua aliyekuwa msimamizi wa masuala ya rushwa na ufisadi kwa madai kuwa ameshindwa kufanya kazi, Spika Sitta alisema uamuzi huo ulikuwa sahihi "kwa sababu hakuna mtu yeyote anayependa rushwa ziendelee".


Leo wajumbe wa mkutano huo, ambao umepangwa kumalizika Jumanne ijayo, watatembelea vivutio vya utalii, ikiwa ni pamoja na kwenda Zanzibar, Serengeti na Mlima Kilimanjaro.
 
Back
Top Bottom