Kikwete, Membe na hipokrisis!

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
Kikwete, Membe na hipokrisis!

Lula wa Ndali-Mwananzela Julai 9, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

KUNA watu wanafiki na wapo waigizaji. Kuna mambo ya kinafiki na mambo ya kizugaji. Katika yote mawili (unafiki na uigizaji/uzugaji) lengo ni kutoa picha au taswira isiyo ya kweli kuhusu mtu au kitu.

Katika lugha ya Kigiriki maneno haya mawili mwigizaji na mnafiki yanahusiana. Kimsingi neno la asili hipokrisis ndilo ninalotupa neno hypocrisy katika lugha ya Kiingereza ambalo tunalitafsiri kama ‘mnafiki’.

Lakini neno hili mnafiki ambalo tumelichukua kuwa ni la Kiswahili ni neno la Kiarabu ambalo kimsingi linahusu mtu “ajifanyaye ambavyo sivyo alivyo”. Linahusiana na uigizaji ule ule lakini lina maana ya kidini (Surat Al-Munafiqun – Sura 63.) ambapo wanafiki ni wale ambao wanajifanya/wanaigiza kuwa wana imani kumbe wameiacha imani hiyo.

Ndio maana katika Uislamu, kwa mfano, mnafiki ni mtu wa hatari sana hata kuliko mtu asiyeamini. Kwa nini? kwa sababu Qurani Tukufu inasema “ Wanapo kujia wanafiki husema: Tunashuhudia ya kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu anashuhudia ya kuwa hakika wanaafiki ni waongo” (63:1)

Hili la wanafiki kupingwa kwenye vitabu vya dini siyo suala la Qurani tu bali pia katika Biblia. Tunaambiwa katika maandiko matakatifu kuwa Yesu alisema “Ole wenu Waandishi na Mafarisayo, Wanafiki! Mmekuwa kama makaburi yaliyopakwa chokaa, kwa nje mnapendeza lakini ndani ni mifupa mitupu na uchafu” (Mathayo 23:27).

Sasa utaona kuwa tofauti kubwa ya mwigizaji na mnafiki katika maana ya leo hii ni kuwa mwigizaji tunajua anaigiza kwa lengo la kuburudisha, kufundisha n.k lakini sisi sote tunajua kuwa yeye ni nani – mwigizaji. Mnafiki kwa upande mwingine lengo lake ni kupotosha watu juu yake au mambo yake kiasi cha kuwafanya waamini kitu fulani ambacho yeye anajua kuwa si kweli.

Mnafiki kweli ni mtu wa hatari, kwani lengo lake laweza kumpatia faida kubwa mbele za watu kwani watu wanaweza kuamini kile anachokifanya.

Ndugu zangu, vitendo na maneno ya Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje Bw. Bernard Membe mwishoni mwa juma kuhusu Zimbabwe, maneno ambayo yalielezea msimamo wa Tanzania na nchi za SADC kuhusu uchaguzi wa Zimbabwe, naamini ni maneno ya kinafiki.

Tulichoshuhudia wiki iliyopita si maneno ya ujasiri (kama nilivyoandika kwenye makala kuhusu serikali yetu na Mugabe) bali ni maneno ya kundi la watu ambao wanataka tuamini kitu fulani juu yao wakati wao wenyewe wanajua kuwa si kweli.

Ninachosema ni kuwa msimamo wa SADC na wa serikali yetu na hasa sababu zilizotolewa za kutomtambua Bw. Mugabe na uchaguzi wa “picha” wa Zimbabwe ni msimamo wa kinafiki.

Huu unafiki unatokana na mtazamo waliojijengea watawala wetu kuwa wao wanaweza kusimama katika kiti cha hukumu kutoa hukumu kwa haki. Kwa maneno mengine wanataka ulimwengu uamini kuwa wao ni bora kuliko Mugabe na kutokana na ubora huo, basi, wanaweza kutoa hukumu ya haki.

Nikipanua kidogo hoja ni kuwa wanataka tuamini kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake linapokuja suala la uchaguzi wao ni bora kuliko ZANU-PF na serikali yake kwenye swala hilo hilo. Huu ni unafiki.

Matumizi ya vyombo vya habari

Wanafiki wetu waliosimama kumhukumu Mugabe wanataka tuamini kwamba Mugabe aliwanyima wapinzani nafasi huru na sawa kwenye vyombo vya habari vya serikali yake, kitu ambacho wao (watawala wetu) hawakifanyi. Kwamba wao wanatoa nafasi sawa, na huru kwa vyama vya upinzania katika radio, televisheni na magazeti ya serikali hivyo wana uwezo wa kumhukumu Mugabe. Je hii ni kweli?

Mara nyingi imekuwa kawaida kwa Rais (tangu Mkapa) kuwa na hotuba ya mwisho wa mwezi kwa Taifa. Mara kadhaa Rais alipotoa hotuba hiyo amefanya hivyo akitumia pia nafasi yake kama Mwenyekiti wa CCM. Mfano mzuri ni hotuba yake ya mwezi wanne aliyoitoa kwa Taifa kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee ambapo alizungumza kupitia viongozi wa jumuiya za CCM. Na hata kabla ya hapo Rais ametumia hotuba zake za mwisho wa mwezi kunadi chama chake.

Cha kushangaza ni kuwa hakuna hata mara moja ambapo vyama vya upinzani vimepewa nafasi ya kujibu hotuba hiyo ya Rais kana kwamba mwenye haki ya kuzungumza na kuuza sera za chama chake kwa Taifa ni Mwenyekiti wa CCM tu. Huko Marekani kila Jumamosi (siyo kila mwezi) Rais wa Marekani anatoa hotuba kwa radio kwa Taifa, haijalishi yuko wapi na anafanya nini (wanaweza kuirekodi kabla). Mwisho wa hotuba hiyo kinachofuatia ni hotuba ya majibu ya upinzani. Hili linafanyika bila kujali Rais ni Republican au Democrat.

Mtindo wao huu wa kutoa nafasi kwa chama cha upinzani hauiishii Jumamosi tu. Kila mwaka mwanzoni, Rais wa Marekani hutoa hotuba yake maarufu ya “Hali ya Muungano” ambayo anatakiwa kuitoa kikatiba (Ibara ya Pili, kipengele cha tatu cha Katiba ya Marekani).

Kwa muda mrefu hotuba hii ambayo imekuwa ikifanyika mfululizo sasa kuanzia 1939 ilikuwa haifuatiwi na hotuba ya upinzani hadi mwaka 1966 ambapo chama kilichoko upinzani kimekuwa kikifuatia hotuba ya Rais na mtindo huo kuendelezwa hadi kwenye hotuba za Jumamosi au hotuba yoyote ile ambayo Rais wa Marekani atatumia masafa ya Taifa kuzungumzia sera au jambo lolote muhimu.

Sasa hivi imekuwa ni utaratibu kuwa Rais akizungumza basi upinzani nao lazima upewe nafasi ya kujibu.

Chombo chochote cha habari kilichobeba hotuba ya Rais kwa Taifa kinatakiwa nacho kibebe hotuba ya upinzani. Je CCM na serikali yake kama walimu wa Demokrasia kwa Zimbabwe wanaweza haya? Hebu fikiria siku ambayo tunamuona Rais Kikwete amemaliza kutoa hotuba yake kwa Taifa halafu sekunde chache baadaye Prof. Ibrahim Lipumba anatoa majibu ya upinzani!

Hili siyo kwenye masuala ya hotuba tu bali pia katika mchakato wa uchaguzi. Mojawapo ya malalamiko ambayo yamekuwepo Tanzania mara nyingi wakati wa uchaguzi ni kuwa wapinzani hawapewi nafasi sawa kwenye vyombo vya habari vya walipa kodi wa Tanzania.

Hili si suala la Bara tu bali pia Visiwani. Leo hii Rais wa Zanzibar anaweza kuzungumza jambo lolote bila upinzani Zanzibar kupewa nafasi sawa ya kujibu hoja hizo. Wakati wa uchaguzi vyombo vya habari hasa TV za Taifa na Radio za Taifa zimekuwa zikibeba ujumbe wa mgombea wa chama tawala na kumpa upendeleo wa aina ya pekee kulinganisha na vyama vingine.

Sasa leo wanasimama bila haya kumhubiria Mugabe juu ya nafasi sawa ya kutumia vyombo vya habari kwa upinzani? Kama huu siyo unafiki tuupatie jina gani?

Kitu kingine kinachoonesha unafiki ni pale SADC na serikali yetu wanapokumbatia ripoti ya waangalizi wa uchaguzi wa SADC kama msingi wa maamuzi yao ya kutomtambua Mugabe. Hivi wanafikiri sisi ni wasahaulifu hivi? Si waangalizi kama hao walitoa taarifa kuhusu Kibaki na uchaguzi Kenya? Si waangalizi hawa walitoa ripoti kama hii kwenye chaguzi za Zanzibar na tukazitolea nje ripoti zao?

Iweje leo ripoti ya waangalizi iwe imebeba ukweli katika Zimbabwe ambacho chini ya watu 100 wameuawa lakini ripoti hiyo isiwe na uzito kule Kenya ambako karibu watu 1000 waliuawa?

Hivi kweli serikali ya CCM inataka kutuambia kuwa sasa hivi imeongoka na inaamini kuwa taarifa za waangalizi zina ukweli? Au zina ukweli zinapohusu nchi nyingine lakini ikija kwa Tanzania ni “maoni yao” tu. Kama huu si unafiki tuupe jina gani?

Leo hii serikali yetu inajaribu kumshawishi Mugabe aunde serikali ya Kitaifa, maneno ambayo yamerudiwa na Rais Kikwete kwenye mkutano wa G8 huko Japan. Yaani hivi kweli tuamini kwamba Rais Kikwete ameona mwanga wa kuona haja ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa Zimbabwe lakini mwanga huo unazimika inapokuja Zanzibar?

Ndio, najua jibu lao litakuwa hivi: “ Mazingira ya Zanzibar yana tofauti”! Hivi watu wa Zimbabwe wameumbwa na damu ya ubuyu? Hivi wananchi wa Zimbabwe wameumbwa kutoka sayari ya Zebaki au Zuhura?

Hivi wanataka tuamini kwamba CCM ina tofauti sana na ZANU-PF katika haja ya kukamata na kukumbatia madaraka yake na dola? Kama wana tofauti kwa nini walibadilisha Katiba na kumfanya Rais wa Tanzania awezekane kuchaguliwa na kura chache kabisa?

Kwa nini hadi leo hii bado wameweka uwezekano wa Rais kutangazwa usiku wa manane ili kuharakisha kumuapisha kama ilivyotokea Zimbabwe na Kenya. Ni kitu gani kinaweza kumzuia Rais kuapishwa barabarani kwa haraka haraka kama alivyofanyiwa Kibaki?

Leo ndugu zetu watawala wanataka tuamini kwamba wao wanaheshimu sana sheria na hawapendi vurugu kutokea nchini? Kwa nini basi wanakwepa kutengeneza uwezekano wa marudio ya kura kama Zimbabwe? Si angalau Zimbabwe kura zisipotosha wanaweza kurudia uchaguzi, lakini Tanzania hakuna kitu kama kura kutotosha!

Wapinzani mbalimbali wakigawana kura kwa asilimia sabini na CCM ikapata kura 30 mgombea wa CCM atatangazwa Rais usiku wa manane na kuapishwa kabla chapati hazijapikwa! Leo wanathubutu kumnyoshea kidole Mugabe cha kutomtambua? Nikiita unafiki nitaambiwa ninawakejeli?

Kuna mambo mengine mengi ambayo naweza kusema lakini nitaawachia wengine waseme. Kikubwa ninachosema ni kwamba msimamo wa SADC na wa serikali yetu kuhusu Mugabe ni wa kupuuzwa kwani misingi yake haina ukweli.

Ni mpaka pale nchi za SADC na serikali ya Tanzania zitakapoweza kusafisha uchafu wao kwenye mambo yao ya uchaguzi ndipo kwa haki wataweza kumnyoshea kidole mtu mwingine.

Vinginevyo, kwenye nchi ya wanafiki, kikombe wanachowanywesha wengine, wao wenyewe hawanywi. Lakini wataimba nyimbo na kupiga panda wengine wanywe. Kwa nini? Kwa sababu wanafiki ni waigizaji.

Niandikie: lulawanzela@yahoo.co.uk
 
I like this one, if I may say so...

Ni mpaka pale nchi za SADC na serikali ya Tanzania zitakapoweza kusafisha uchafu wao kwenye mambo yao ya uchaguzi ndipo kwa haki wataweza kumnyoshea kidole mtu mwingine.
 
Hiyo Hypocris yako..Hipokrisis...IMENIMALIZA.
Hata hivyo safi sana kwani hata chinga watakuelewa.
Na hivyo basi ujumbe umefika kuwa ni UNAFIKI kwa serikali yetu kwa kupitia Membe kutoa kauli hizo.
Maneno ya Bibi Ntilie naona tunayafanyia kazi pale alipotoa mfano wa siasa za mwalimu wakati wa ujenzi wa TANU pale alipomwachia Simba wa Vita U PM na yeye kuwapelekea wananchi message nchi nzima.
 
I like that, sound good. Mwandishi ni wakupigiwa mfano! straight to the point hakuna longolongo, chungwa limeitwa chungwa na ujumbe umefika. Keep it up
 
Mmhhhh.... Mwandishi mwanasiasa... dunia yote inajua CCM sio sawa na ZANU-PF! Pamoja na Udhaifu wake ambao unachangiwa na jamii yenyewe ya Watanzania ikiwa ni pamoja na Upinzani.
 
Mmhhhh.... Mwandishi mwanasiasa... dunia yote inajua CCM sio sawa na ZANU-PF! Pamoja na Udhaifu wake ambao unachangiwa na jamii yenyewe ya Watanzania ikiwa ni pamoja na Upinzani.
labda dunia yako ndo yajua hivyo, manake mi kwenye dunia yangu naona hakuna chembe ya tofauti, basi utufafanulie wewe manake mwandishi kaeleza kinagaubaga.
 
Je serikali ya CCM inatoa nafasi sawa kwa vyombo vya habari vya serikali kwa vyama vya upinzani hasa ufikapo uchaguzi?
 
Je serikali ya CCM inatoa nafasi sawa kwa vyombo vya habari vya serikali kwa vyama vya upinzani hasa ufikapo uchaguzi?

Hiyo statement yako haitoshi kuifanya CCM iwe sawa na ZANU-PF... well you wish CCM to be like ZANU-PF... but that can't happen anyway...
 
Hiyo statement yako haitoshi kuifanya CCM iwe sawa na ZANU-PF... well you wish CCM to be like ZANU-PF... but that can't happen anyway...


no sir... kama CCM haitoi nafasi sawa kwa wapinzani kutumia vyombo vya habari wakati wa kampeni, na ZANU-PF inafanya vivyo hivyo, ni jinsi gani basi kwenye eneo hilo CCM siyo kama ZANU PF?
 
Date::7/9/2008
Waziri Membe, Goli la Karume pia 'lina utata wa kuotea'
Na Ally Saleh
Mwananchi

HAIBA ya nchi inatokana na matendo yake kwa wananchi wake, nchi jirani na ushiriki wake katika masuala ya kikanda, kibara na hata kidunia.

Katika kila hatua kuna mambo yake na kiwango ambacho nchi inategemewa kufanya au kujizuia kufanya kwa mujibu wa hali ilivyo kwa mnasaba na katiba yake ya nchi, mikataba ya kikanda, kibara na kidunia.

Hali kadhalika nchi moja inatakiwa iwe na msimamo wenye kufanana katika suala la aina moja na sio kutoa maamuzi haya hapa na kufanya vyengine tofauti katika hali inayofanana kwenye sehemu nyingine.

Huo ndio msingi wa kujenga sera ya mambo ya nje ya nchi yoyote ile ikiwemo Tanzania, ambayo kwa bahati kwenye Bara la Afrika inaheshimiwa pamoja na kuwa si nchi yenye kipato kikubwa na nafasi yake kiuchumi ni ya kusikitisha.

Siku hizi zimepita zile zama za nchi moja au kiongozi wa nchi kufanya utakavyo na kucheza ngoma atakazo kisha kusema kuwa asiingiliwe kwa kuwa ni mambo ya ndani ya nchi.

Suala la Zanzibar, yaani kuwepo kwa mgogoro au mpasuko au jina jengine lolote lile, kunakotokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 si suala la mambo ya ndani ya Tanzania, kama ambavyo tungetaka lionekane, bali ni suala la kimataifa.

Ni la kimataifa kama ambavyo linavyofanywa suala la Zimbabwe hivi sasa na Afrika nzima na dunia nzima kutikisika kwa kuwa demokrasian haikufuata mkondo wake katika nchi hiyo kama ilivyotokea hapa Zanzibar.

Wakati Tanzania inalisimamia kidete suala la Zimbabwe haikustahili kulifutika suala la Zanzibar na kufanya kama halipo ilhali bado ni tatizo kama ambavyo pia lilikuwa ni tatizo la kiuchaguzi nchini Kenya.

Haielekei na haipendezi kwa Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe kuzunguka barani Afrika wakibeba bendera ya usuluhishi kwa migogoro ya nchi nyingine wakati mgogoro wa ndani ya nchi yao bado upo kama ulivyoanza.

Haingii akilini kwa viongozi wa nchi hii kutafuta suluhu za nchi nyingine wakati wakijua kama hapakupatikana suluhu katika suala la Zanzibar, basi ni wazi kuwa uchaguzi ujao wa mwaka 2010 unaweza usifanyike na kama ukifanyika basi utafanyika katika hali ya mashaka makubwa.

Mtu aweza kujiuliza hata hekima ya viongozi wetu iko wapi kudharau mgogoro mdogo wa kwao wakati wakienda kutatua migogoro mikubwa mikubwa ya nchi nyingine, ambazo baadhi ni jirani lakini nyingine kamwe hazitakuwa na athari ya moja kwa moja kama vile kuingiliwa na wakimbizi.

Mtanzania anayo haki ya kujiuliza hivi ni vipi sera ya mambo ya nje ya Tanzania ya kuhimiza amani na demokrasia Barani Afrika inaweza kuwa na mashiko bila ya masharti au matakwa hayo kutimizwa ndani ya nchi yake wenyewe.

Ndipo inapotokezea Tanzania kupigwa vijembe huko nje inapojitia kimbelembele kwenye usuluhishi kama alivyosema Rais Robert Mugabe kuwaambia viongozi wa Afrika ni yupi asiye na matope usoni mwake anayethubutu kumnyooshea kidole yeye.

Na hilo ni kweli kabisa, chaguzi nyingi katika Bara letu humalizia kuweko na mazingira ya utatanishi katika maandalizi yake au mazingira ya kutia shaka katika upatikanaji wa matokea yake.

Ni nchi chache sana zenye kuweza kusimama imara na kifua mbele kukemea nyingine kwa kuwa rekodi zake ni safi. Na kwa kuwa nchi hizo ni chache ndipo suala la Zimbabwe linapokuwa gumu kufumbuka na taabu kulikemea.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Bernard Membe aliwaambia waandishi wa habari kuwa matokea ya Zimbabwe hayaweza kukubalika kwa sababu goli lililofungwa na Mugabe lilikuwa la kuotea.

Sijui tumfahamu Waziri Membe alikuwa akifanya dhihaka au akijaribu kulidogosha suala hilo la Zimbabwe. Maana

kama ni mfano wa goli, basi anajua ni jinsi gani magoli ya kuotea chungu nzima yalivyokubalika na kwa hivyo sijui ni kwa nini anaona hili la Mugabe likataliwe.

Goli hilo, yaani ushindi alioupata ameuita wa kuotea kutokana na mfululizo wa matokea yanayohusiana na mchakato mzima wa uchaguzi kuanzia sheria za uchaguzi, kampeni, haki ya kupiga kura, fursa kwa wapinzani na kadhalika.

Najua Waziri Membe anajua kila kilichotokea Zimbabwe mwanzoni mwa mwaka huu vuguvugu la uchaguzi lilipoanza hadi siku ya mwisho ya upigaji wa kura ya marudio, na pia naamini kuwa anajua kila kilichotokea Zanzibar kipindi chote cha uchaguzi.

Sitaki, na siku zote nimekataa kufananisha moja kwa moja hali iliyotokea Zimbabwe na ile iliyotokea Zanzibar katika uchaguzi uliopelekea ushindi kwa Dk Amani Karume mwaka 2005 ambapo hadi sasa kuna msuguano wa kisiasa baina ya vyama vya CUF na CCM.

Lakini sitafanya makosa nikisema yaliyotokea Zanzibar kwa kiasi cha mfano yametokea yote huko Zimbabwe na kinyume chake na kwa maana hiyo kama goli lilofungwa Zimbabwe ni la kuotea na hili la Dk Karume pia lina utata wa kuotea.

Kutokana na kuwa na utata wa kuotea ndio maana kumeelezwa kuwepo na mpasuko wa kisiasa kwa maana ya upande mmoja ukisema uchaguzi ulikwenda vema na Serikali ni halali na mwengine ukisema haukwenda vema na uhalali wa Serikali una walakin.

Na ndio maana ajenda ya mwanzo iliyojadiliwa na Kamati ya kutafuta Mwafaka wa CUF na CCM ilikuwa ni uhalali wa ushindi wa Dk Karume hadi busara ilipolazimisha wazimue ajenda hiyo ili kuweza kusonga mbele kutafuta suluhu.

Suluhu ilikuwa karibu kabisa kupatikana. Ingeweza kupatikana kabla ya Kenya na mapigano yake yaliyoingiza ukabila na pia ingeweza suluhu kuja kabla ya Mugabe kufunga goli la kuotea dhidi ya Morgan Tsvangirai.

Suluhu ingeweza kuja bila ya kuingilia Ban ki Moon na Koffi Annan huko Kenya wala mkutano wa Umoja wa Afrika na mkono wa Thabo Mbeki huko Zimbabwe, maana Kamati ya Mwafaka ilikamilisha kila kitu na kubakisha jukumu kwa vyombo vya juu vya siasa na utawala Tanzania.

Ni dhahiri walioubwaga Mwafaka na Kamati Kuu za CUF na CCM, Kikwete na Karume na Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar, ilhali kila mtu anajua kuwa goli la Dk Karume lilikuwa na utata wa kuotea na ndio maana juhudi ikachukuliwa kutafuta suluhu.

Sasa Tanzania inathubutu kusema kuwa goli la mtu mwingine ni la kuotea wakati hata nayo imeucheza mchezo huo? Tanzania ina sauti gani, ina heshima gani ina hoja gani kulishikilia bango suala la Zimbabwe ilhali ndani kwake wenyewe imeshindwa kumaliza mgogoro wake? Je, hili si doa katika sera ya mambo ya nje ya Tanzania kuhusu suala la amani na demokrasia Barani Afrika?

Hivi Membe hasikii matokeo ya kutolimaliza tatizo la Zanzibar�mivutano isiyokwisha baina ya CUF na CCM, Wapemba kudai kuundwa Serikali ya shirikisho, vitisho dhidi ya wananchi wa upande mmoja na kutenga nusu ya umma wa Zanzibar?

Maana sasa pengine itabidi tuamke na tujiulize�je, kinachokwamisha nini na ni nani? Ni sisi Wazanzibari wenyewe kwa wenyewe na kwa faida gani au ni upande wa pili usiotia nguvu kulimaliza na kwa faida gani?

Kusema tu goli lilikuwa la kuotea hakutoshi, inafaa tujiulize ni nani na tuifahamu dhamira yake kisha kama bni mtu au taasisi tuiandame kama ilivyofanyika Kenya na naamini pia itafanyika Zimbabwe ingawa inashindikana kufanyika Zanzibar.

+255 777 4300 22

www.eternaltourszanzibar.net

jumbamaro.blogspot.com
 
Back
Top Bottom