Kikwete, Makamba nani mkweli? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kikwete, Makamba nani mkweli?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Supervisor, Feb 9, 2011.

 1. Supervisor

  Supervisor JF-Expert Member

  #1
  Feb 9, 2011
  Joined: Oct 29, 2010
  Messages: 553
  Likes Received: 31
  Trophy Points: 45
  Kikwete, Makamba nani mkweli?​  Joseph Sabinus


  SAKATA la malipo ya shilingi bilioni 94/- za Tanzania kwa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans Tanzania Limited, sasa linawagonganisha uso kwa uso, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi –CCM, Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba.
  Mgangano wa kauli zao kwa nyakati tofauti na mazingira tofauti, unazua utata kwa tafakari makini kiasi cha kushindwa kujua nani anamaanisha kile anachokisema; nani msanii au basi kana kwamba wote ni wale wale isipokuwa majina na vyeo tu kwamba wote ni wasanii walewale isipokuwa tofauti ya nyimbo.
  Gazeti la Nipashe, Februari 5, 2011, uk. 1 lilikuwa na kichwa cha habari MAKAMBA: RUKSA KUHAMA CCM KUIPINGA DOWANS. Habari hiyo iliyanukuu mazungumzo baina ya Makamba na gazeti hilo huku Makamba akiridhia kuwa ni ruksa kwa mwanachama yeyote wa CCM anayetaka kukikahama chama hicho kama njia ya kupinga malipo ya Dowans.
  Mazungumzo hayo yalitokana na tishio lililotolewa na wanachama wa CCM Wilaya ya Rorya mkoani Mara kuwa watarudisha kadi za CCM endapo Serikali itakubali kulipa fidia ya sh bilioni 94 kwa Dowans.
  Licha ya Makamba kusema ni hiari ya mwanachama kutoka au kubaki katika chama, kama ilivyo ada yake, alijigamba kwa kusema hata kama wanachama hao wataondoka ndani ya CCM, hali hiyo haiwezi kukiathiri chama hicho.
  Anadai tangu zamani wanachama wamekuwa wakitumia hiari yao kujiunga na hata kutoka katika chama lakini, chama hicho kikabaki imara bila kuyumba. Hii ni sawa na kusema kuwa, wabaki au watoke, shauri zao, awike au asiwike jogoo, kutakucha.
  Kauli ya Makamba inaonesha kutojali wala kutoona thamani ya wanachama wa CCM wa Wilaya ya Rorya. Hii ni kauli inayotoa taswira kuwa Makamba ni mtetezi mzuri wa kufanyika kwa malipo ya Dowans, hata kama ni kwa gharama ya chama kupoteza wanachama, lakini Dowans ilipwe.
  Makamba hajui kuwa TANESCO au serikali haina mahali pengine pa kupata pesa hizo bila kuwakamua Watanzania mithili ya ng’ombe anayeweza kukamuliwa hadi damu kutoka kupitia njia mbalimbali; haijalishi utata wowote uliopo kisheria.
  Wakati Katibu Mkuu Makamba akiwa na hilo linalozusha maswali mengi kuliko idadi ya majibu ya kuridhisha huku likijenga hisia kuwa huenda “Makamba ana agenda nyuma ya pazia”, Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa CCM, naye amekuja kwa gia tofauti.
  Kikwete ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametoa amevunja ukimya na kukata kiu ya Watanzania. Kiu iliyolenga kumsikia akijibu kama “ana mkono wake ndani yake, au na yeye ni mtazamaji tu wa filamu ya Dowans”.
  Amevunja ukimya baada ya watu wengi wakiwamo viongozi wa dini, kuingilia na kuhoji kulikoni awe na kigugumizi mintarafu mambo magumu kama hilo la Dowans linalopasua vichwa vya Watanzania ambao baadhi yao wanaishi katika lindi la umaskini wa kutupwa.
  Hawa, ni Watanzania wanaotembea mwendo mrefu kutafuta maji na kituo cha afya au zahanati kisha wakaambulia cheti cha mganga na maelekezo ya kwenda kutafuta dawa, eti ndio walipe shilingi zaidi ya bilioni 90 kwa kampuni yenye mkataba tata. Miongoni mwao wanaolia, wamo baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa.
  Kikwete ametema cheche zake zilizowakuna kisawasawa wananchi, lakini kama ilivyo ada kwamba no one is perfect, hotuba ya Kikwete siku ya kilele cha maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika Dodoma, imezua maswali mengine.
  Imevutia masikioni mwa wengi kumsikia Rais wa nchi akitamka waziwazi, “Nataka kuwahakikishia kuwa mie ni miongoni mwa wale wasiotaka TANESCO ilipe…; sina uhusiano wowote wa kimaslahi kwa namna yoyote ile na kampuni ya Dowans.
  Kauli nyingine aliyosema Kikwete ni pamoja na hii, “Wapo waliosema lazima tulipe, wapo waliosema tusilipe, wapo waliosema tusiharakishe kulipa kwani kuna uwezekano wa kutolipa kwa kutumia sheria. Uamuzi wangu ukawa tusiharakishe kulipa, tutafute njia ya kuepuka kulipa…”
  Rais Kikwete; Mwenyekiti wa Kitaifa wa Chama cha Mapinduzi akaenda mbali na kusema, hana hisa na Dowans na wamiliki wake hawajui kwani hawajawahi kumuita maana hawamhitaji.
  Licha ya kutotaja jina la mtu siku hiyo, Kikwete alitumia muda mwingi kuwatuhumu baadhi ya wanasiasa akisema, “Akutukanaye, hakuchagulii tusi” kwa kuwa baadhi ya watu wanamhusisha na umiliki wa Dowans.
  Hapa kuna pande mbili kama zilivyo pande mbili za shilingi. Kwanza, ninampongeza kwa kuamua kuvunja ukimya na kutoa anayoamini ndiyo “ukweli wa ukweli”.
  Pia, nampongeza Rais Kikwete kwa kuona na kutambua kuwa ukimya wake, umesababisha baadhi ya watu wafikie hatua ya kumhusisha na umiliki wa kampuni ya Dowans jambo ambalo ni usiku wa kiza maana ni lile usilolojua.
  Hata hivyo, ni kwa vipi Kikwete alitarajia ukimya ule usizae matunda hayo wakati ndicho alichokuwa anapanda? Kwanini akae kimya namna hiyo huku hali ya hewa ikichafuka? Alikuwa anasubiri nini kuweka mambo hadharani mapema?
  Ikumbukwe kuwa kabla ya Serikali kutangaza majina “mageni masikioni mwa Watanzania” kuwa ndiyo ya wamiliki wa Dowans, Watanzania walikuwa wakihoji iweje walipe deni la mdai ambaye hajulikani? Yaani mdai hewa?
  Baada ya kuanikwa majina hayo watu mbalimbali wamepaza sauti zao akiwamo, mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia anayesema, hakuna sababu kwa serikali kulipa deni hilo wakati watu walioingia mkataba huo ambao serikali imeurithi huku wakijua kuwa ni mchafu, wapo.
  Kimantiki kama alivyosema Mbatia, waliohusika na mchezo huo mchafu wapo. Wapo na walifanya huku wakijua faida na hasara zake kwa umma wa Watanzania; kwamba walifanya makusudi ili kulinda “maslahi yao; tena ile yenye maslahi kwao binafsi”. Kama hivyo ndivyo, kwanini mali za Watanzania zichukuliwe au Watanzania walazimishwe kulipa deni hilo?
  Basi ndivyo ilivyo kwamba wakati Watanzania wanatamani kusikia serikali ya chama cha kina Makamba ikiwakamata watumishi na wanasiasa waliohusika “kulichezesha taifa segere” ili “licheze na kudundika kama sio kupigika”, Makamba anaona heri wanachama wajitoe.
  Ninachojiuliza hapa ni kwamba, hivi kweli huo ndio msimamo wa ndani wa Makamba binafsi, au ndio msimamo wa ndani wa Chama cha Mapinduzi?
  Ikumbukwe kuwa Makamba ni mtu mkubwa ndani ya chama hivyo, hata siku moja hatutarajii kusikia utetezi wa kichovu kuwa yalikuwa mawazo binafsi. Ukitaka mawazo binafsi ukiwa kiongozi, sharti ujivue kwanza uongozi.
  JK na watendaji wengine wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi na chama chenyewe mbona kauli zenu na maneno mnayoyasema yanagongana uso kwa uso mithili ya treni? Mnayoyasema yanatokna kweli mioyoni mwenu, au yanaanzia tu hapo midomoni kwenu lakini mioyoni hayapo?
  ‘Kikwete aliyesema analazimika kuyasema hayo licha ya kuwa tayari yalikwishasemwa awali na viongozi wengine akiwamo Waziri Mkuu Mizengo Pinda, hakukanusha wala kukemea kauli ya Makamba ya kutoona thamani ya wanachama ndani ya chama, bali uchu wa kulipa Dowans huku yeye Kikwete ambaye ni mwenyekiti, akitamani Dowans isilipwe ovyo ovyo. Hapo tumuamini nani kati ya Kikwete na Makamba?
  Rais wangu Kikwete, unaionaje kauli ya Makamba ya kutowajali wanachama wa CCM wilayani Rorya, imekaa sawa? Hivi wanachama hao wana thamani yoyote katika chama, au wamejidanganya tu kuingia katika bwawa kubwa huku wakijijua kuwa ni samaki wadogo maana Wazungu wanasema, you better be a big fish in a small pond, rather than being a small fish in a big pond yaani, ni heri kuwa samaki mkubwa katika bwawa dogo, kuliko kuwa samaki mdogo katika bwawa kubwa.
  Samaki mdogo ndani ya bwawa kubwa daima hana thamani hata akifa au kupotea hakuna anayejua wala kujali na hata ndugu zake wakilia, machozi yao yanaishia majini tu. Hakuna jipya.
  Haya ndiyo yanawakumba wanasiasa wadogo; wanachama wa CCM wilayani Rorya, kwamba hata wakitoka CCM watoke, haina shida cha msingi ni Dowans kulipwa bilioni 94. Ama kweli akutukanaye, hakuchagulii tusi.
  Makamba na CCM yako kumbukeni kuwa wakati wewe unasema “Ya kazi gani”, mwingine atasema, “Nitaipataje”.
  Kauli za viongozi hao wakuu wa CCM wakati mwingine zinatia kichefuchefu. Hivi kweli hata kwa imani yake, Rais Kikwete anaweza kuitetea kauli yake mbele ya Mungu kuwa hawajui wamiliki wa Dowan?
  Kwamba hawajui wamiliki wa kampuni inayoliyumbisha taifa na serikali yake namna hii? Kama ni kweli, kwa nini asimwajibishe Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, ambaye hivi karibuni aliyataja majina kadhaa kwamba ndio wamiliki?
  Je, kinachodhaniwa kuwa ni majina hewa, ndicho anachokifahamu pia Rais Kikwete? Hili nalo ni jipya na tamu linaloonesha kuwa, filamu ya Dowans, imeanza kunoga.
  Kama alivyosema Mbunge wa Kigoma Kusini kwa tikiti ya NCCR-Mageuzi, David Kafulila, kitendo cha Rais Kikwete kusema hawajui wamiliki wa Dowans ni ishara ya wazi kuwa wale aliowatangaza Waziri Ngeleja kuwa ndio wamiliki wa Dowans ni “changa la macho” kwa Watanzania vinginevyo kama kweli wangekuwa wamiliki halisi, lazima Rais angewajua.
  Hatutarajii Tanzania iwe na Rais asiyejua watu wanaolidai taifa mabilioni mengi namna hiyo huku waziri akiwataja hadharani. Hiki nacho kinaweza kuwa kituko cha kuanzia mwaka 2011.
  Kikwete, Makamba na Serikali ya Chama cha Mapinduzi, wakumbuke kwamba huduma nyingi za umma zikiwamo za afya, maji, umeme, barabara na ubora wa elimu zinazidi kuporomoka nchini kiasi kwamba hata Watanzania wengi wanakufa kwa kukosa huduma hizo.
  Hivi karibuni televisheni ya taifa, TBC1, ilionyesha moja ya shule za msingi mkoani Shinyanga yenye uhaba wa vyumba vya madarasa kiasi cha kuwafanya wanafunzi wa madarasa mawili tofauti, walimu wawili tofauti, katika masomo mawili tofauti, kutumia chumba kimoja kwa wakati mmoja!
  Darasa hili wanatumia ukuta wa mbele, na darasa lingine wanatumia ukuta wa nyuma; aibu kweli kweli katika zama hizi. Mabilioni haya ya pesa yangeweza kutumika vizuri kama yangesaidia kuondoa kero kama hizo nchini. Kumekuwapo na utitiri wa migomo na maandamano katika vyuo vya elimu ya juu wanafunzi “wakililia” maisha yao. Wengine serikali kwa kusingizia vigezo, imewaacha nyikani bila msaada wala mkopo na badala yake, walio nacho wameongezewa. Ndiyo maana lugha na matamshi ya Makamba na Kikwete, kwangu zinazua “lugha gongana” na kutia shaka kuhusu umakini wao, la sivyo wanafanya yale yanayowafanya watu washindwe kujua tofauti katika familia ya kambale kuwa nani baba, mama, kaka, dada, shangazi, mjomba, bibi wala wajukuu maana wote wana sharubu
   
Loading...