Mimi namshangaa sana huyu profesa wa sheria asiyejua au asiyetaka kufuata sheria. Huy bwana alishtakiwa na ushahidi ulipoletwa mahakamani akaonekana ana kesi ya kujibu. Tokea hapo amekuwa akifanya sarakasi za kuhakikisha kwamba hajitetei na kwa bahati nzuri mbinu zake zote zimegonga mwamba katika kila hatua.
Sasa wametengeneza njama za kutaka kuilazimisha serikali kutoa hati ya kufuta mashtaka na mbinu hizi zinaratibiwa kwa karibu sana na Mabere Marando na kiongozi mwandamizi mstaafu aliyehudumu katika awamu ya Rais mwinyi. Walianza na kumdanganya mzee Mkapa kwamba hati ya kiapo atakayoiapa inatakiwa serikalini kwa ajili ya kufuta mashtaka kwa hati maalum (Nolle Prosequi) na kwamba haitakwenda mahakamani, baada ya mawakili wa serikali kukataa wakaitoa gazetini ili kuchafua jina la Mzee Mkapa. Ilisikika kwamba wanapanga kuandika barua kwenda kwa Rais Kikwete ili kuomba atoe ushahidi lakini nia yao ilikuwa ni kufanya hivyo na hatimaye kuipenyeza barua hiyo magazetini ili ionekane Rais anafanya kiini macho uendeshaji wa kesi ya Mahalu na ionekane Mahalu anaonewa au hakuna nia thabiti ya kushughulikia ufisadi. Mambo hayo yanafanywa na wanasheria hao kwa dhamira mbaya na ovu. lakini la kujuiliza hapa ni kwamba Je, Nolle itatolewaje wakati tayari mshitakiwa ameonekana ana kesi ya kujibu, ikiwa na maana kwamba ushahidi uliotolewa ulitosha kutia hatiani kama mshtakiwa hatatoa utetezi? Na sasa hata maamuzi ya Mahakama ya Rufaa yamebainisha wazi mazingira ambayo Nolle inaweza kutolewa na kesi hii haijazingatia mazingira hayo. Walitaka itokee hivyo ili huyo huyo Marando asimame jukwaani akidai kwamba serikali inahadaa watu kuhusu vita vya ufisadi.
Wanajaribu kuunganisha hilo na Hansard inayomnukuu Rais (wakati huo akiwa waziri) akitetea kwamba ununuzi huo ulikuwa halali na uliozingatia sheria ili ionekane kwamba hata yeye alimsafisha. Lakini kilicho wazi ni kwamba Rais aliyatamka hayo kabla ukweli wa skati hili haujabainika na Rais alizingatia nyaraka zilizokuwepo wakati huo. Baadae ilipokuja kupatikana taarifa ya ufisadi na uchunguzi kufanyika ndipo ilipobainika kwamba taarifa za mwanzo hazikubainisha ukweli huo.
Mpango huu wa kupeleka habari hii kwa Mwana Halisi, ulipangwa na unajiuliza kwa nini Marando huyo huyo aliyeandaa barua hiyo aifikishe gazetini kabla hata huko Ikulu haijafikishwa! Hapa kuna siri kubwa na uovu wa hali ya juu.