Kikwete: Kununua uongozi sasa basi

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,125

pix.gif
Akihutubia Taifa jana katika hotuba yake ya mwisho ya mwezi, Rais Kikwete alisema chimbuko la kutungwa sheria hiyo ni mwenendo usioridhisha wa matumizi ya fedha katika uchaguzi nchini.

“Kuna matumizi mabaya ya fedha katika uchaguzi ndani ya vyama vya siasa na baina ya vyama vya siasa katika chaguzi za kiserikali,” alisema Rais Kikwete aliyetumia hotuba yake hiyo kuzungumzia Muswada huo wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi uliopitishwa na Bunge katika Mkutano wake wa 18 mwezi uliopita mjini Dodoma.

Aidha, amesema itakomesha kabisa tabia mbaya inayoanza kujitokeza ya wapiga kura kugeuza kura yao kama bidhaa ya kuuza kwa wagombea.

“Hivi sasa kwa sababu ya kutokuwepo ukomo, wako watu wenye pesa ambao wanafanya matumizi kupita kiasi. Wapo wanaopitiliza au hata kukufuru na kuwadhalilisha wenzi wao wasiokuwa na uwezo kama wao,” alieleza Rais Kikwete.

Wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Takukuru mjini Mwanza wiki iliyopita alisema atasaini muswada huo kuwa sheria kwa mbwembwe ili kuwabana wanaotumia fedha kupata uongozi.

Alisema sheria hiyo mpya imetungwa kwa nia ya kupata majawabu kwa tatizo la matumizi mabaya ya fedha katika shughuli za uchaguzi.

“Tunatambua kuwa matatizo haya si mageni, yamekuwepo tangu miaka mingi huko nyuma na hata historia ya Bunge letu ina ushahidi wa ushindi wa baadhi ya wabunge kutenguliwa kwa makosa ya rushwa.

“Lakini, siku hizi matatizo ya matumizi mabaya ya fedha yamekuwa makubwa zaidi na yanakua kwa kasi inayotishia kugeuzwa kuwa ndiyo utaratibu wa kawaida au utamaduni katika chaguzi zetu,” alisema na kuongeza:

“Ni hali ambayo haifai kuachwa kuendelea na kuzoeleka. Hatuna budi kuchukua hatua za dhati kurekebisha mambo na kulirejesha taifa katika mstari ulionyooka.”

Alisema serikali iliamua kuwa hatua muafaka ya kuchukua ni kutunga sheria ya kuongoza na kudhibiti matumizi katika uchaguzi.

“Sheria hii ikitekelezwa ipasavyo itazuia kugeuza uongozi kuwa ni kitu cha kununuliwa kama bidhaa na wenye pesa au wanaoweza kupata pesa za kufanya hivyo. Aidha, itakomesha kabisa tabia mbaya inayoanza kujitokeza ya wapiga kura kugeuza kura yao kama bidhaa ya kuchuuza kwa wagombea,” alieleza Rais Kikwete. Alisema ametumia muda mwingi katika hotuba yake kuelezea mambo ya msingi yaliyomo katika sheria hiyo, akilenga mambo matatu muhimu.

“Kwanza, kuwathibitishia Watanzania wenzangu kwamba tunalitambua tatizo la rushwa katika uchaguzi na tunayo dhamira ya dhati ya kupambana nalo. Kukemea peke yake hakutoshi, lazima tutumie nguvu ya sheria kudhibiti vitendo vya rushwa na kuwaadhibu ipasavyo wahusika,” alisema Rais Kikwete.

“Pili, kuwathibitishia kuwa sisi wenzenu tuliopo katika serikali tunatambua wajibu wetu wa kuhakikisha kuwa sheria hii inatekelezwa kwa ukamilifu. Nimekwishaviagiza vyombo vya Dola, ikiwemo Takukuru, kujipanga vizuri kuisimamia sheria hii.

“Nawaomba wananchi mtoe ushirikiano kwa vyombo vyote vinavyohusika na usimamizi wa Sheria hii ili vitimize kwa ukamilifu malengo yake ambayo yana maslahi kwa nchi yetu na kwetu sote.” Alisema jambo la tatu ni kwamba serikali inatambua wajibu wa kuhakikisha kuwa wananchi, wanachama na viongozi wa vyama vya siasa wanaelimishwa vya kutosha ili waielewe vizuri sheria hiyo.

“Umuhimu wa kuielewa vizuri Sheria hii hauhitaji kusisitizwa kwani watu wakiielewa vizuri inarahisisha utekelezaji wake. Na, kwa vyama vya siasa na wagombea, uelewa mzuri utasaidia kuepuka makosa ambayo yanaweza kuwa na gharama kubwa ya wao kupoteza ushindi,” alieleza.

Rais Kikwete alisema anaamini hatua zilizomo katika sheria inayokuja zikitekelezwa, zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza au hata kudhibiti kabisa vitendo na hisia za rushwa katika uchaguzi.

“Mara nyingi vitendo hivyo vinapofanyika, au hata kule kuwepo hisia tu kwamba vinaweza kuwa vimefanyika, huwa ni chanzo cha manung’uniko na kukosekana utulivu. Wakati mwingine huathiri taswira ya demokrasia yetu na heshima ya uongozi uliochaguliwa hasa pale uhalali wa matokeo ya uchaguzi unapotiliwa shaka,” alisema.

“Tunachukua hatua hizi ili kulinda hadhi ya chaguzi zetu nchini na kuzifanya kweli ziwe huru na za haki na kufanya mfumo wa demokrasia uzidi kustawi. Hatima ya yote haya tufanyayo ni kusaidia nchi yetu kuwa na viongozi wanaotokana na ridhaa ya wananchi.”

Akifafanua baadhi ya masharti ya sheria hiyo, Rais Kikwete alisema ieleweke kuwa si nia ya sheria hiyo kuzuia wananchi kuchangia shughuli za siasa au za kampeni za chama wakipendacho au mgombea wanayempenda, isipokuwa inaruhusu michango ya aina yoyote kutolewa kwa chama chochote au kwa mgombea yeyote ila inataka michango hiyo itolewe kwa utaratibu ulio wazi. “Kusiwe na usiri au kificho cha namna yoyote,” alisema.

Akizungumza michango kutoka nje ya nchi, alisema, “najua suala la masharti yaliyowekwa kwa watu wa nje kuchangia vyama vya siasa na wagombea nchini lilizua mjadala miongoni mwa wadau mbalimbali.

“Kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa kupinga masharti yaliyowekwa. Naomba ieleweke kuwa, kwa kweli, si jambo jema kwa chama cha siasa au mgombea nchini kufadhiliwa na watu wa nje.

“Wahenga wanasema “anayemlipa mpiga zumari huchagua wimbo”. Ipo hatari kwa kiongozi au chama kupokea amri kutoka nchi za nje kwa kuwasikiliza wale watu wa nje waliowasaidia badala ya kujali maslahi ya nchi yetu na watu wake.”

Kuhusu viwango vya gharama za uchaguzi, alisema utaratibu huo ni muhimu katika kujenga nidhamu na usawa miongoni mwa vyama na wagombea katika uchaguzi.

CHANZO: HABARILEO
 
Back
Top Bottom