Kikwete aficha siri

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,791
288,003
Kikwete aficha siri

na Charles Mullinda
Tanzania Daima

KATIKA hali ambayo haikutarajiwa na wengi, Rais Jakaya Kikwete, ameamua kuwa msiri katika utendaji kazi wake.
Hali hiyo ilidhihirika Alhamisi wiki hii wakati alipokutana na kuzungumza na wahariri wa vyombo vya habari, Ikulu, Dar es Salaam kuhusu maadhimisho ya kutimiza kwake miaka miwili akiwa madarakani.

Katika mkutano wake huo na wahariri, Rais Kikwete alisema taarifa zinazoelezwa kuwa ana mpango wa kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri ni uvumi usio na ukweli wowote, lakini atakaa chini na kuangalia iwapo kutakuwa na haja ya kupunguza au kuliacha baraza hilo likiwa katika muundo wake wa sasa.

Kauli hii ya Rais Kikwete inapingana na uhalisia wa mambo unaoonyesha kwamba kwa hali yoyote, na kwa kuzingatia staili yake ya utendaji kazi ya kurejesha matumaini kwa wananchi kuhusu uongozi wake na serikali yake kwa ujumla, atalazimika kulivunja baraza lake la mawaziri wakati wowote kuanzia sasa.

Ukweli huu unathibitishwa na hatua kadhaa ambazo Rais Kikwete amekuwa akizichukua tangu aliposhika madaraka, miaka miwili iliyopita katika kuhakikisha kuwa serikali yake inabaki na mvuto kama iliokuwa nao wakati akiingia madarakani.

Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Rais Kikwete ili kulinda hadhi ya serikali yake ni pamoja na kuunda tume ya kuchunguza mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini, wenyeji wa Mahenge, waliodaiwa kuuawa na polisi.

Kikwete aliunda tume hiyo baada ya malalamiko ya wananchi kuhusu taarifa iliyotolewa na polisi kuwa waliouawa walikuwa majambazi na si wafanyabiashara, jambo lililopingwa na wananchi na kulitia doa Jeshi la Polisi.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alilazimika kuunda kamati ya kupitia upya mikataba ya madini, akiwajumuisha pia wabunge kutoka kambi ya upinzani, baada ya kuwepo kwa kelele nyingi kutoka kwa kambi ya upinzani, wanaharakati na baadhi ya wananchi kuhusu usiri uliogubika mikataba hiyo inayodaiwa kulitia hasara taifa, huku ikiwanufaisha zaidi wawekezaji.

Mwenendo huo wa Rais Kikwete, unaonyesha kuwa kamwe hataifumbia macho ripoti ya Utafiti wa Mpango wa Elimu ya Demokrasia (REDET) inayoeleza kuporomoka kwa umaarufu wake binafsi pamoja na ule wa serikali yake.

Ripoti hiyo ambayo yeye mwenye na hata baadhi ya wasaidizi wake wa karibu wameikubali, akiwemo mshauri wake wa masuala ya siasa, Kingunge Ngombale-Mwiru, ni moja ya mambo yatakayomlazimisha Rais Kikwete kufanya mabadiliko ya haraka katika baraza lake la mawaziri ili kurejesha umaarufu wake na serikali yake ambao umeelezwa kuporomoka kwa kiwango kikubwa katika ripoti hiyo ya REDET.

Aidha, hatua ya Rais Kikwete kukubaliana na ripoti hiyo na kutamka kwake kuwa anaangalia uwezekano wa kulipunguza au kuliacha kama lilivyo baraza lake la mawaziri, ni dalili kuwa ana tafakari kwa kina kuhusu mabadiliko atakayoyafanya, jambo ambalo limechelewesha hata kuteuliwa kwa mrithi wa kiti cha marehemu Salome Mbatia, aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.

Rais Kikwete ambaye utawala wake unaelekea kutimiza nusu ya muhula wake atasukumwa pia na kauli za watu mashuhuri, kama Paul Rupia, aliyepata kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais kwa miaka mingi, aliyekaririwa na vyombo vya habari akizungumzia kuhusu haja ya rais kuchukua hatua hiyo.

Pamoja na wadadisi wengi wa mambo kuona haja ya lazima ya kufanyika kwa mabadiliko ya mawaziri sasa, matukio mengine kadhaa ya hivi karibuni, mbali na ripoti ya Redet, yanatoa mwelekeo huo huo wa mambo kubadilika.

Matokeo ya uchaguzi wa ndani katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) ulioshuhudia kuondoka madarakani kwa baadhi ya viongozi waandamizi katika sekretarieti ya chama hicho ni moja ya mambo yanayoonekana kuwa sehemu ya sababu zitakazomfanya Kikwete alazimike kuchukua hatua hiyo ya kubadili mawaziri.

Baadhi ya watu wanaotajwa kuwa wanaweza wakaingia katika baraza hilo jipya ni pamoja na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Jaka Mwambi na mwenzake aliyekuwa akishikilia wadhifa wa Katibu wa Uenezi na Itikadi, Aggrey Mwanri, ambao wote waliachwa katika sekretarieti mpya.

Wanasiasa hao wawili ambao kuachwa kwao katika uongozi wa kisiasa hauhusishwi na kushindwa kwao kazi, wanapewa nafasi kubwa kutokana na ukaribu wa kihistoria wa kikazi waliojijengea kwa Kikwete kwa miaka mingi.

Wakati Mwambi akitajwa kuwa komredi wa miaka mingi wa Kikwete tangu miaka ya 1970, Mwanri yeye anapewa nafasi kubwa kutokana na uwezo wake binafsi na eneo anakotokea wilayani Hai, ambako wapinzani na hususan Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kina nguvu kubwa.

Mbali ya tukio hilo, tuhuma na kasoro zilizopata kuzikumba baadhi ya wizara kama ile ya Nishati na Madini, Afya na Ustawi wa Jamii na Maliasili na Utalii ni jambo jingine linaloonekana kuwapo kwa uwezekano wa mabadiliko hayo kutokea.

Matukio ya namna hii kwa mfano, ndiyo ambayo kwa sababu za wazi yanamweka Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, kushikwa na kihoro cha kuweza kukumbwa na mabadiliko hayo, lengo likiwa ni kuondoa kiwingu alichojengwa tangu Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, alipomuunganisha na utiaji saini tata wa mgodi wa Buzwagi miezi kadhaa iliyopita.

Ingawa bado haijathibitishwa kwa uhakika kabisa iwapo Karamagi alifanya kosa au la katika uamuzi huo, bado taswira yake kama waziri imekuwa na viulizo vingi, tangu suala hili lilipoibuka bungeni na baadaye kutumiwa na wapinzani kama turufu muhimu ya kujiimarisha.

Mbali ya hilo, kifo cha Mbatia aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na nafasi yake kuendelea kubakia wazi pasipo mtu mwingine kuteuliwa kuziba nafasi yake mapema, kunaongeza dalili za kuwapo kwa dhamira ya rais kufanya mabadiliko makubwa zaidi ya kuziba zaidi ya pengo hilo moja.

Historia ya utendaji wa Rais Kikwete tangu alipofariki aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Juma Akukweti, na baadaye kuondoka katika baraza kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Asha - Rose Migiro, ni sehemu ya mambo yanayoonyesha kuwa hata safari hii anaweza kutumia kifo cha Mbatia kuwa sababu ya kulipangua na pengine kulibadili baraza lake la mawaziri.

Kama ilivyokuwa kwa kifo cha Akukweti na baadaye kuondoka kwa Migiro, Rais Kikwete alifanya mabadiliko madogo ya mawaziri kiasi cha kumfanya Bernard Membe, kwa mfano, kuguswa na matukio yote mawili, akihama kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani na kwenda Wizara ya Nishati na Madini, alikokuwa naibu waziri, kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Wengine walioguswa na matukio hayo ni Emmanuel Nchimbi, Lawrence Masha, Batilda Burian, Karamagi, Daniel Nsanzugwanko, Dk. Ibrahim Msabaha, na David Mathayo ambao walihama kutoka wizara moja kwenda nyingine.

Aidha, katika matukio hayo mawili, wanasiasa, Gaudence Kayombo na William Ngeleja waliokuwa nje ya baraza waliweza kuingia wakiwa naibu mawaziri kuziba mapengo yaliyotokea.

Sura za wanasiasa zinazotarajiwa kuwemo katika baraza jipya ni pamoja na ile ya Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye kitaaluma ni mtaalamu wa sheria, au ile ya Mbunge wa Mbeya Vijijini, Richard Nyaulawa, mtaalamu wa uchumi.

Wanasiasa hawa wanapewa nafasi kubwa ya kuwamo katika baraza jipya kutokana na mwenendo wa mambo ulivyo katika serikali na joto la kisiasa nchini.

Hata hivyo iwapo Rais Kikwete atamchukua mmoja kati ya wanasiasa hawa katika baraza lake jipya, majaliwa ya kuendelea kubakia katika baraza hilo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Prof. Mark Mwandosya, na mwenzake, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Prof. David Mwakyusa, yanaweza kuwa shakani, kwa kuzingatia kuwa wanasiasa hao wanatoka katika mkoa na wilaya moja.
 
Hawa magazeti nao speculation zimezidi ndio maana muungwana JK kagoma kufuata wanachotabiri kila siku. Wao magazeti wanamtabiria mambo, halafu akiyafanya ionekane wao ndio wanaomfundisha kazi. Hapa ndipo JK anapaswa kuchukua somo kwa Chez Nkapa, kila walichotabiri waandishi hakikutokea! Mnakumbuka wakati wa uteuzi wa Waziri Mkuu? Jamaa walikuwa wana-speculate kila siku kama vile wana uhakika Sumaye angetemwa! Na wakati wa uteuzi wa makamu wa rais baada ya kifo cha Dr Omar, Mzee Mkapa alitupatia total surprize! Walikoma wenyewe, naye akamalizia kuwaita "mbumbumbu" (sishabikii hili lakini). Ninachotaka, pamoja na ukaribu JK alio nao na waandishi wa habari, wasiwe na ushawishi katika maamuzi ya serikali maana ikiwa hivyo mtu yeyote mwenye maslahi yake atayapeleka kwa waandishi waanze spinning au lobbying kiaina. Mwishowe tutakuwa tunaongozwa na magazeti badala ya Rais na serikali tulioichagua. Nadhani ndio sababu pia Ikulu wamegomea taarifa za kujiuzulu Balali ambazo zilitangulizwa magazetini kabla Rais hajaridhia.
 
Magazet wanaandika kama wanavyoyaona mambo na kusikia maoni ya wananchi mitaani. Na sasa hivi ukweli ni kwamba katika miaka miwili ya uongozi wa Kikwete serikali yake imepwaya sana katika kila nyanja.

Kiongozi yeyote anayesikia taarifa kama hizi anaweza kabisa kujifanya jeuri na asifanye mabadiliko yeyote au akaamua kubadili timu yake ili kuongeza mafanikio katika serikali yake. Kikwete akiamua kubaki na timu aliyonayo na utendaji ndio ukazidi kuwa mbaya basi anachijimbia kaburi mwenyewe hapo 2010, maana CCM hawatakubali kuwa na mgombea ambaye anaonekana hana support katika kila kona ya nchi. Hili pia linaweza kusababisha CCM kupoteza viti vingi vya wabunge (kama hawakuiba kura).

Tukumbuke sio magazeti tu yanayofanya speculation bali hata wanasiasa wakongwe kama Paul Rupia wameshamshauri afanye mabadiliko ya baraza la mawaziri maana hili alilonalo limepwaya sana. Na kuna minong'ono wengi ndani ya CCM wamemwambia afanye mabadiliko hayo. Kikwete ana haki ya kusuka ama kunyoa na magazeti wana haki ya kuandika kama wanavyoona, maana ni wajibu wao kufanya hivyo. Vinginevyo kutakuwa hakuna haja ya kuwa na magazeti....:)
 
Lolote linaweza tokea,lamsingi yawe ni mabadiliko positive.Kutabili kwa wanahabari sio kila mara kunakuwa kweli.Tunachoomba watuongoze katika njia iliyo bora.Wapunguze ukali wa maisha unaotukabili na uchumi uweze kukua.
Ikiwa mfuko wa cement kule nyumbani Mtwara ni 26,000/=hakuna maisha bora kwa mwana Mtwara.
Hivyo wazingatie hayo.
 
Kwa wana JF
Katika uzoefu wangu kutabiri kuwa JK atabadili mawaziri hili linawezekana lakini kutabiri na watakao teuliwa kama bwana Charles Mullinda wa Tanzania Daima alivyoandika hilo haliwezi tokea kwani itakuwa ni sawa na kumwambia mteue mtu fulani wakati kazi ya kuteua ni yake na wataalamu wake , likishatoka nje hiyo inakuwa dili ishaharibika. Kutabiri mtu kwa jina ni kumhaharibia uwezekano wake wa kupata hiyo nafasi, na kama mwandishi alikuwa anajaribu kuwapalilia hao jamaa ni kwamba kawatilia mchanga kitumbua chao.
 
sasa hivi je kukiwa na udhaifu wa waziwazi katika government bureacracy ambapo mabadiliko kimsingi kabisa yakawa yana hitajika na at the same time mass media wakawa wna guess changes(from what i know mass media ni mhimili usio rasmi wa dola baada ya bunge, mahakama na exucutive), ivi hapo mkuu aki reshuffle tutasema "kaamuliwa/kashawishiwa" na mass media?,lets be rational,in a rio sense for what i think changes is a must!!
 
Back
Top Bottom