Kikwete aelemewa: Raia Mwema | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kikwete aelemewa: Raia Mwema

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Halisi, Jul 9, 2009.

 1. Halisi

  Halisi JF-Expert Member

  #1
  Jul 9, 2009
  Joined: Jan 16, 2007
  Messages: 2,810
  Likes Received: 83
  Trophy Points: 145
  Kikwete aelemewa


  Mwandishi wa Raia Mwema​
  Julai 8, 2009[​IMG]
  [​IMG]Wasaidizi waelezwa kumsusia kazi
  [​IMG]Serikali yaendeshwa 'kizima moto'


  KUNA maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kuwa mfumo wa uongozi, na hasa wa Rais Jakaya Kikwete, umewafanya wasaidizi wake wengi kumbwagia shughuli nyingi, Raia Mwema imeambiwa.

  Wanasiasa wakongwe na wapya wanasema ya kuwa matokeo ya hali hiyo ni Serikali kubanwa sana katika Bunge linaloendelea sasa Dodoma na kuongezeka kwa shutuma za wananchi, zikiwamo taasisi za dini na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) mambo ambayo yameufanya utawala sasa kuongoza kwa mtindo wa kuzima matukio.

  Wanasema, kama ushahidi wa hali hiyo, kuwa baadhi ya matukio makubwa yaliyoiburuza Serikali kiasi cha kubadili uamuzi wake wa awali ambao ulipitishwa na Baraza la Mawaziri, ni pamoja na kuondolewa kwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa misamaha ya kodi kwa mashirika ya dini na NGOs.

  Mbali na misamaha ya VAT, tukio jingine ni kishindo kilichojitokeza bungeni dhidi ya Wizara ya Miundombinu kuhusu mgawanyo wa bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2009/2010.

  Mijadala ya wabunge wengi katika makadirio ya bajeti ya Wizara ya Miundombinu, wanasiasa hao ambao kwa sababu za wazi Raia Mwema haitawataja majina, wanasema ya kuwa Serikali ina matatizo makubwa ya kushindwa kujisimamia na kujiongoza.

  Wanasema kushindwa huko kwa Serikali kujisimamia na kujiongoza kunajitokeza katika mikataba kama ya uwekezaji wa Shirika la Reli Tanzania, kwa kampuni ya Railways Infrastructure, Transport and Economic Services (RITES) ya India.

  Bila kujali kuwa Rais ndiye mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na huongoza vikao hivyo, ingawa pia Makamu wa Rais anaweza kukasimiwa madaraka hayo kwa niaba ya Rais, upinzani wa bajeti kuu ya serikali ulijitokeza na hasa suala la misamaha ya VAT kwa mashirika ya dini na NGOs.

  Upinzani huo uliwaunganisha wabunge, wananchi wa kawaida na viongozi wa dini wakishangazwa na uamuzi wa Baraza la Mawaziri kufuta VAT.

  Raia Mwema imedokezwa na baadhi ya viongozi kuwa kabla ya Bajeti ya Serikali kusomwa, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, alikutana na Rais na kumpa muhtasari wa bajeti na kujadiliana baadhi ya masuala na kufikia uamuzi na kisha kuwasilisha mapendekezo hayo kwenye Baraza la Mawaziri.

  Inaelezwa kuwa mawaziri wengi walishindwa kukosoa moja kwa moja bajeti hiyo, na hasa kipengele cha msamaha wa VAT kutokana na staili ya kuongoza vikao ya Rais Kikwete.

  Inaelezwa kuwa Rais Kikwete amekuwa akiongoza vikao kwa kuanza kutoa maoni yake hali inayowaweka njia panda wajumbe kumkosoa au hata kumpinga.

  Wanasiasa hao wanasema mtindo huo wa kuendesha mambo haumnufaishi Rais Kikwete, na kwamba ndio ambao amekuwa akiutumia kuongoza vikao kama vya Kamati Kuu ya CCM, Halmashauri Kuu ya CCM na Baraza la Mawaziri.

  Habari zaidi zinasema hata ilipowasilishwa Bajeti ya Serikali katika Baraza la Mawaziri, Waziri wa Fedha na Uchumi alisoma muhtasari wa Bajeti kwa mwelekeo wa kuonyesha kuwa Rais alikwisharidhia awali; huku mara kwa mara akitamka akirejea maneno kama “… kama nilivyo ku-brief mheshimiwa Rais.”

  Ni hali hiyo inayoelezwa kuwa hata mawaziri wale ambao kwa kawaida hupenda kuhoji na katika suala hilo la VAT walikuwa wakiona kuwa mambo si sawa na dhahiri kulikuwa na tishio kwa Serikali, walinywea kwa kuwa ilielekea ya kuwa tayari Rais alikwisha kuridhia hivyo, na hatimaye Baraza la Mawaziri likapitisha mapendekezo hayo ili yawasilishwe bungeni ambako yaligonga ukuta.

  Mapendekezo hayo yaligonga ukuta kiasi cha kuilazimu Serikali kufuta pendekezo la kuondoa msamaha maalumu wa VAT, kwa mashirika ya dini na asasi zisizo za serikali (NGO’s), hali ambayo ingezimwa ndani ya Baraza la Mawaziri kama Rais angekuwa na kawaida ya kuendesha vikao kwa kuanza kusikiliza maoni ya wajumbe na kisha kuhitimisha.

  Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ndiye ambaye alitangaza uamuzi wa Serikali kugwaya, akisema Serikali ilifanya hivyo kwa kuwa Rais Kikwete ni msikivu.

  Pinda alisema uamuzi huo wa Serikali ambao kwa upande mwingine ulidhihirisha nguvu walizonazo viongozi wa taasisi za dini, ulipata baraka zote za Rais Kikwete.

  Waziri Mkuu Pinda alisema Rais Kikwete aliridhia uamuzi huo baada ya kusikia maoni ya viongozi wa taasisi za kidini waliokuwa wamekutana naye (Pinda) mjini Dodoma, siku chache mara baada ya Bajeti ya Serikali kusomwa.

  Kwa maelezo yake, Waziri Mkuu Pinda alisema uamuzi wa kurejesha misamaha hiyo umekuja baada ya Serikali kubaini kuwa, mpango wake wa awali umepokewa kwa upinzani mkali na wabunge, viongozi wa mashirika ya dini, wananchi na wahisani wa nje, ambao wanasaidia miradi ya maendeleo kupitia mashirika ya dini.

  Kwa lugha ya kidiplomasia ili kuficha udhaifu wa Serikali, Pinda alisema Serikali imeona mpango huo haujaeleweka vizuri, kwani azma yake ilikuwa si kufuta misamaha ya kodi hata katika huduma muhimu za jamii kama afya, maji na elimu kama ilivyoeleweka.

  Alisema lengo lilikuwa kujaribu kubana mianya ya matumizi mabaya ya misamaha hiyo kwa baadhi ya viongozi wa mashirika ya dini, ambao wamekuwa wakitumia misamaha ya kodi katika masuala ya elimu, afya, ujenzi na ununuzi wa magari kwa kujinufaisha wenyewe.

  “Baada ya kuona kuwa suala hili limekuwa na mjadala mkubwa, hasa kwa wabunge wa CCM, ambao wametushauri tuliangalie upya suala hilo kutokana na mchango mkubwa wa mashirika hayo kwa wananchi, Serikali tumeona ni vizuri tukaufanyia kazi ushauri huo.

  “Kutokana na Serikali kuwa sikivu, nilikutana na viongozi wa dini na tukalijadili suala hili ili kuona nini cha kufanya,” alisema.

  Pinda alisema pia pande hizo mbili zimekubaliana kukutana ili kujadiliana mfumo mzuri utakaowezesha mashirika ya dini kuendelea na mfumo wa kutolipa kodi, lakini wakati huohuo kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi, hatua ambayo ingepangwa kwenye Baraza la Mawaziri tangu awali.

  Kwa upande mwingine, wachambuzi wa masuala ya uongozi wanaamini jambo moja kati ya haya, yanaikabili Serikali na hususan Baraza la Mawaziri.

  Kwanza, kuwapo kwa mawaziri wengi wasio na uwezo wa kuchambua mambo kwa upeo wa mbali, na hivyo baraza hilo kuwa na idadi kubwa ya mawaziri lakini wasio na tija ya wazi kimjadala. Pili, ni Rais Kikwete kutowapa mawaziri uhuru unaostahili kimjadala.

  Kama vile hali hiyo haitoshi, suala la kukwamishwa kwa siku moja kwa Bajeti ya Wizara ya Miundombinu pia ni tatizo jingine linalothibitisha upungufu.

  Mbunge wa Ilemela, Anthony Diallo, ambaye aliwahi kuwa Waziri kwenye Serikali ya Awamu ya Nne, alionyesha kile kilichobainishwa na wachambuzi wa masuala ya uongozi kuwa, ama uwezo wa mawaziri kupima mambo kwa upeo wa mbali ni mdogo au Rais anawabana mno.

  Katika hali isiyo ya kawaida, hivi karibuni, bungeni mjini Dodoma, Diallo alitaka mabadiliko makubwa kwenye matumizi ya Wizara ya Miundombinu, akionekana kupinga mgawanyo wa bajeti uliopendekezwa na Waziri Dk. Shukuru Kawambwa.

  Mbali na Diallo, michango ya wabunge ilionyesha dhahiri kuigawa nchi katika mapande mawili makubwa, yaani wabunge wakigawanyika kimjadala kulingana na mikoa wanakotoka.

  Wabunge kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Tabora na Dodoma walionekana kuwa kambi moja wakiwakilisha Kanda za Ziwa na Kati, wakipambana kimjadala na wabunge kutoka Kanda ya Mashariki.

  Wabunge wa Kanda ya Kati na Ziwa walijenga hoja kuwa Serikali inawapendelea wenzao wa Kanda ya Mashariki, wengine wakithubutu kuhoji kwamba hali hiyo inatokana na Rais kutoka huko, lakini pia wakisisitiza kuwa hata kwenye mikoa yao mfano Shinyanga kuna wapiga kura wengi, na baadhi wakitaja mkoa wao ndiyo ulioongoza kwa kumpigia kura Rais Kikwete.

  Nguvu za mijadala hiyo pamoja na hoja ya kutaka mabadiliko ya mgawo wa Bajeti kutoka kwa Diallo, zilimlazimu Spika Samuel Sitta kuahirisha mjadala wa bajeti hiyo kwa siku mbili na kuitaka Kamati ya Miundombinu ipitie na kutoa mapendekezo.

  Source: Kikwete aelemewa
   
 2. TANMO

  TANMO JF-Expert Member

  #2
  Jul 9, 2009
  Joined: Apr 12, 2008
  Messages: 8,919
  Likes Received: 219
  Trophy Points: 160  Kwa hiyo wanaendeleza ile dhana ya Zidumu fikra za Mwenyekiti siyo?​
   
 3. Steve Dii

  Steve Dii JF-Expert Member

  #3
  Jul 9, 2009
  Joined: Jun 25, 2007
  Messages: 6,416
  Likes Received: 67
  Trophy Points: 145
  ...Ukifagia kila aina ya uchafu na kuuficha chini ya zuria mwisho wake ni kupata uvundo usio na marashi ya kuupoza!!

  ...Ni ushuhuda upi tutarajie?
   
Loading...