Kijo Bisimba ni nani??

Kijo Bisimba ni nani??

Upanga Mkali

Member
Joined
Dec 24, 2014
Posts
96
Reaction score
83
KWA kawaida, huwa sina mazoea ya kujadili watu binafsi. Mara nyingi napenda kujadili mambo muhimu ya kitaifa yenye manufaa kwa nchi yangu. Nafanya hivyo kwa sababu nchi yangu Tanzania ni muhimu kuliko kitu kingine chochote.

Hata hivyo, wanapotokea baadhi ya wasomi ninaowaheshimu, tena wasomi ambao walau hutenga muda wao kwa kuandika mada mbalimbali zinazochapishwa magazetini ili zisomwe na wasomi wenzao na watu wa kawaida wasiokuwa wasomi wa kaliba yao, wakaandika mambo ambayo kimsingi hayafanani nao, najikuta nalazimika kuwajadili wao binafsi ili umma uweze kuwafahamu zaidi.

Kabla ya kuendelea na mada yetu ya leo, kwanza naomba nichukue fursa hii kuwashukuru wasomaji wa safu hii kwa kuniunga mkono katika kipindi chote cha mwaka uliopita wa 2014.

Aidha, napenda niwapongeze pia wasomaji wangu hao kwa kuuona mwaka mpya wa 2015, na zaidi niwaombee kwa Mwenyezi Mungu aendelee kutupa pumzi, nguvu na akili sote kwa ujumla wetu ili tuendelee kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi yetu.

Baada ya shukurani na pongezi hizo, sasa naomba tuje kwenye mada ya leo. Dk. Hellen Kijo Bisimba, anatambulika miongoni mwa jamii ya Watanzania kama Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Kitaaluma, mama huyu ni msomi aliyebobea katika masuala ya sheria. Ni kwa sababu ya usomi wake huo, ndiyo maana wenzake katika taasisi hiyo wamemwamini na kumpatia nafasi hiyo ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa chombo hicho kinachojinasibisha kama mtetezi wa kisheria kwa wanyonge wa nchi hii wasiojua haki zao wala kuwa na uwezo wa kifedha wa kudai haki zao kwenye vyombo vya kutoa haki.

Kwa kuwakumbusha wasomaji wangu tu ni kwamba mama huyu alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kabisa kuibukia Muhimbili wakati Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, alipopigwa, kuteswa na kutupwa katika msitu wa Mabwepande, jijini Dar es Salaam kabla ya kuokotwa na wasamaria wema waliomkimbiza hospitalini hapo kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Dk. Ulimboka anadaiwa kutekwa na wananchi wenye hasira zao kutokana na vifo vya ndugu na jamaa zao vilivyosababishwa na mgomo wa nchi nzima wa madaktari usiokuwa na ukomo, ambao uliratibiwa na kusimamiwa na kiongozi huyo madaktari nchini.

Aidha, wakati wa sakata hilo, Dk. Hellen Kijo Bisimba aliwaongoza wanaharakati wenzake kufunga barabara ya Ali Hassan Mwinyi katika eneo la Daraja la Salenda, akimpigania Dk. Ulimboka na madaktari wenzake, badala ya kupigania mamia ya wagonjwa waliokuwa wanapoteza maisha yao kila siku katika hospitali mbalimbali nchini kutokana na mgomo huo wa madaktari, ambao ulifanyika wakati tayari Serikali ilikuwa imetoa tamko la kuahidi kutekeleza madai yao.

Kimsingi, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, kilianzishwa kwa malengo ya kuwa sauti ya wanyonge wanaonyanyaswa kwa namna moja au nyingine katika nchi hii. Kwa hiyo, wakati wa sakata hilo la Dk. Ulimboka, wengi wetu tulimtarajia Kijo Bisimba na Kituo chake hicho wawe nyuma ya wanyonge, wagonjwa waliokuwa wanapoteza maisha yao hospitalini kutokana na kukosa huduma za madaktari waliokuwa kwenye mgomo, ambao walisoma kwa kodi za wananchi hao wanyonge. Lakini haikuwa hivyo, wanyonge walipuuzwa!

Kwanini nimeamua kumzungumzia Hellen Kijo Bisimba katika makala yangu hii ya leo? Jumapili ya Desemba 28, 2014, gazeti moja linaloheshimika nchini lilichapisha makala ya mwana mama huyo, iliyokuwa imebeba maudhui ya uchambuzi wa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete kupitia kwa Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, na hasa eneo lililofafanua suala zima la sakata la akaunti ya Tegeta Escrow. Makala hiyo ilibeba kichwa cha habari kisemacho: “Mkuu anapokuwa Wakili wa IPTL/PAP.”

Kwa maana rahisi, Hellen Kijo Bisimba, alikusudia kuwasilisha ujumbe kwa umma wa Watanzania kwamba Rais Kikwete, katika hotuba yake hiyo na Wazee wa Dar es Salaam, suala hilo la Tegeta Escrow, aligeuka kuwa Wakili Mtetezi wa kampuni ya IPTL na PAP, ambayo kwa sasa inamilikiwa na mfanyabiashara, Harbinder Sigh Seith.

Katika makala yake hiyo, Bisimba amehoji mambo mengi kuhusiana na msimamo wa Rais Kikwete katika sakata hilo pamoja na hatua alizokwishakuchukua na zile alizoahidi kuendelea kuzichukua.

Hata hivyo, katika hitimisho la makala hiyo, Bisimba anahitimisha kwa kuandika: “Nirudie kauli ya Rais Kikwete aliyosema mwanzoni mwa hotuba yake kwamba mtumishi wa umma anapaswa kufahamu kuwa asipotimiza wajibu wake, basi ategemee kuwa kuna adhabu ambayo pia itakuwa ni fundisho kwa wengine.

“Naomba nimueleze Rais Kikwete kuwa sisi pia kama Watanzania, tunapenda afahamu kama alivyowaambia watumishi wa umma, kwamba nchi hii wenyewe tupo na tunafahamu kukasirika, tunaweza kuchukua hatua pale tunapoona tuliowapa nafasi ya kuchukua hatua, hawataki kuchukua hatua.”

Nawaomba wasomaji wangu tuanzie hapo kwenye nukuu yake hiyo ya kwamba nchi hii ya Tanzania, wenyewe wapo, ni akina Bisimba. Wanafahamu kukasirika, na wanaweza wakachukua hatua pale watakapoona wale waliopewa nafasi ya kuchukua hatua, hawataki kuchukua hatua.

Kwa sasa, waliopewa na Watanzania nafasi ya kuchukua hatua, ni Rais Kikwete na Serikali yake ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Kwa hiyo, Bisimba anamtangazia Rais Kikwete, Serikali yake na chama chake, CCM, kwamba siku watakaposhindwa kuchukua hatua ambazo kina Bisimba wanataka zichukuliwe, wao watakasirika na kuchukua hatua dhidi ya Rais, Serikali na CCM!

Niseme mapema hapa kwamba mimi siyo mwanasheria kitaaluma, lakini naamini kwamba kauli kama hiyo haipaswi kamwe kutoka kichwani mwa mwanasheria kitaaluma. Ikifika mahali mwanasheria kitaaluma akatoa kauli kama hiyo, ni wazi kwamba anaidhalilisha taaluma yake, anawadhalilisha wanataaluma wenzake.

Hivi katika nchi hii yenye Watanzania zaidi ya milioni 45, hao kina Bisimba wako wangapi? Je; ni hatua zipi wanaweza wakazichukua dhidi ya Rais Kikwete, Serikali na chama chake ikiwa Rais atashindwa kuchukua hatua kulingana na matakwa yao? Katika aya yote hiyo ya nukuu ya Bisimba, sheria na haki za binadamu viko wapi? Maswali ni mengi!

Mimi siyo mtetezi wa Rais Kikwete, Serikali yake wala chama chake, lakini naomba tuzichambue kwa pamoja hoja za Dk. Hellen Kijo Bisimba katika makala tajwa hiyo, halafu tuzipime kama kweli hoja hizo zimetolewa na msomi aliye huru kiakili na kimawazo au ni msomi ambaye ni mtumwa kiakili na kimawazo wa makundi fulani kwa madhumuni na malengo fulani.

Kijo Bisimba ameandika: “…bahati mbaya sana, Rais alipoanza kuzungumzia suala la Escrow, ilikuwa ni sauti ya mzaha na ndiyo maana akaanza kwa kicheko na kuliita ni kashfa au kadhia. Hiyo pengine ingekuwa si tatizo kama asingeendelea kutoa maelezo akionyesha kuwa yeye ni Wakili wa IPTL dhidi ya hoja zilizotolewa na Kamati ya Bunge (PAC) na kuridhiwa na Bunge.

“Rais amenishangaza alipoanza kujenga hoja kuonyesha kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Escrow wala si (hazikuwa) nyingi kama watu wanavyosema kuwa zingeweza kupangwa hapa mpaka wapi sijui; zilikuwa Sh bilioni 202.9 tu na siyo Sh bilioni 306.7.”

Ndugu zangu; wakati mwingine nashawishika kuamini kwamba hata kipengele cha kiwango cha elimu katika Katiba yetu kwa mtu anayetaka kuwa Rais wa nchi hii, kwa maana ya kuwa na walau Digrii, hakina maana kabisa, kama wasomi wetu aina ya kina Bisimba wenye Shahada za Uzamivu, wanaweza wakawa na mawazo ya aina hii na kuyawasilisha katika hadhira ya Watanzania ili wayasome!

Naamini Watanzania walio wengi, wanaompenda na wasiompenda, walau siku ile walisimamisha shughuli zao kwa lengo la kumsikiliza Rais Kikwete. Hivi katika hotuba yake ile, ni wapi Rais aliweka mzaha? Na mzaha huo, mtu anaweza akaupima kwa kutumia vigezo na mizania gani?

Je; siyo kweli kwamba Kamati ya PAC iliwaaminisha Watanzania kwamba fedha zilizochotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow zilikuwa ni Sh bilioni 306.7? Je; siyo kweli kwamba chombo kimoja cha habari kilitangaza kuwa fedha hizo zinaweza kupangwa barabarani kuanzia Dar es Salaam zikafika hadi mjini Bukoba?

Sasa Mkuu wa Nchi anapowaambia wananchi wake ukweli halisi wa wambo kwamba wakati akaunti hiyo inafungwa Novemba 20, 2013, fedha zilizokuwemo zilikuwa ni Sh bilioni 202.9 tu na siyo bilioni 306.7 kama inavyovumishwa na wanasiasa wenye malengo yao, hapo mzaha wa Rais Kikwete unatoka wapi?

Misingi ya hekima na busara inamtaka kiongozi wa nchi kutokuwa na papara, jazba, hamaki na kadhalika. Haitoshi kwa kiongozi wa nchi, anayetegemea kupata taarifa kutoka vyanzo vyake mbalimbali, tena vingine vikiwa na mamlaka ya kikatiba, akurupuke kuamua tu kuhusu jambo fulani kwa kuwa tu jambo fulani hilo limesemwa na Bunge?

Mwongozo wa hotuba yote ya Rais Kikwete katika ufafanuzi wake wote kuhusu sakata la Tegeta Escrow, ilikuwa ni Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Na ikumbukwe kwamba ripoti hiyo hiyo ya CAG, ndiyo tuliyoambiwa na wakubwa wa PAC bungeni kwamba ndiyo waliyoizingatia katika kuandaa taarifa yao iliyozaa maazimio nane.

Mimi nilidhani wasomi aina ya Dk. Hellen Kijo Bisimba, wangesimama na kuwahoji wakubwa wa PAC na Bunge kwa ujumla wake, wawaonyeshe umma wa Watanzania ni wapi katika ripoti ya CAG panasema jumla fedha iliyotolewa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow na kukabidhiwa kwa IPTL ilikuwa ni Sh bilioni 306.7.

Nilidhani baada ya wasomi hao kuwahoji wakubwa hao wa PAC na Bunge swali hilo, halafu wakubwa hao wakashindwa kuonyesha kifungu hicho katika ripoti ya CAG, swali ambalo lingefuata kutoka kwa wasomi wetu hao, lingehoji dhamira zao katika kuupotosha umma kwamba fedha zilizochotwa ni Sh bilioni 306.7 wakati ukweli halisi ni Sh bilioni 202.9.

Lakini msomi huyo anayeheshimika kitaifa na kimataifa, anashangaza na kutia shaka juu ya usomi wake huo pale anapojiaminisha katika akili zake, kwamba Rais Kikwete alipohitimisha kwa kutoa jibu sahihi la swali ambalo lilisumbua sana vichwa vya Watanzania ndani na nje ya Bunge, juu ya nani hasa mmiliki halali fedha zile, na kusema ni IPTL, basi hapo Rais amekuwa Wakili wa kampuni hiyo.

Kwa hiyo, Bisimba yeye angefurahi sana na kumuona Rais Kikwete ni wa maana kama naye angekuwa mtu wa bendera fuata upepo, kwa kufuata mkumbo wao wa kusema zile zilikuwa ni fedha za umma hata kama anajua ni uongo! Fedha za umma zinakaa kwenye Escrow kufanya nini wakati nchi hii ina miradi kibao inayosubiri fedha za umma, wakati walimu wanasubiri kulipwa madai yao? Usomi wa ajabu kabisa!

Akielezea msimamo wa Rais Kikwete kuhusu azimio la Bunge linalomtaka awawajibishe watendaji wa chini yake, wakiwemo mawaziri kwa madai ya kuhusishwa na sakata hilo la Escrow, msomi wetu huyo ameandika:

“Hili la kuwajibishwa kwa Waziri Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, alielea (Rais Kikwete) kama ana utani na Watanzania, kuwa Waziri wa Ardhi tumemuomba atupishe tuteue mwingine.

“Rais hana uchambuzi wa nini hasa kinafanya achukue uamuzi huo wa Tibaijuka, na Muhongo amuweke kiporo na aendelee kuchunguzwa. Ni nani anawachunguza hawa dhidi ya chunguzi ambazo tayari zimefanyika? Iwapo wanachunguzwa, iweje wawe bado kazini, huo ndio utaratibu?”

Kwa bahati nzuri sana, Hellen Kijo Bisimba ninamfahamu. Ni mama mwenye umri wa zaidi ya miaka 50 anayekaribia kupindukia kwenye miaka 60 sasa. Kwa umri huo na usomi wake, hatarajiwi ahoji maswali ambayo yanafanana na ya vijana wa vijiweni.

Nimesema hapo juu kwamba mwongozo wa hotuba ya Rais Kikwete katika kufafanua sakata zima la Tegeta Escrow ni ripoti ya CAG. Hiyo ndiyo pia ilitumiwa na PAC katika kuandika taarifa yake kwa Bunge na hatimaye Bunge kuibuka na maazimio yake manane.

Kwa vyovyote vile, Bisimba atakuwa ameisoma na kuirudia tena na tena ripoti hiyo ya CAG, maana ipo wazi kila mahali kwa yeyote anayehitaji kuisoma. Ni wapi na pendekezo gani la CAG katika ripoti hiyo, imewatia hatiani hao anaowataja akitaka wawajibike?

Mama huyu anaongoza taasisi muhimu sana, inayojidai kwamba ndiyo mtetezi mkuu wa haki za binadamu. Kama hivyo ndivyo, ni kwanini naye anataka watu wahukumiwe bila kupewa nafasi ya kujitetea?

Watanzania kwa ujumla wao, wanatambua sasa kwamba wote waliotuhumiwa na kuhukumiwa na Kamati ya PAC hawakuwahi kuitwa mbele ya kamati hiyo kujieleza dhidi ya tuhuma zinazowakabili, si Waziri Mkuu Mizengo Pinda wala Profesa Tibaijuka, sasa ni kwanini mkuu wa taasisi inayojidai kutetea sheria na haki za binadamu, anaungana na wavunjaji wa sheria na haki za binadamu katika sakata zima hili la Tegeta Escrow?

Lakini pia, Watanzania kwa ujumla wao, akiwemo Dk. Hellen Kijo Bisimba, wanatambua kwamba hakuna jinai yoyote inayotajwa na ripoti ya CAG kwa Waziri Muhongo na Maswi, sasa msomi wetu huyo alitaka Rais Kikwete awawajibishe watendaji hao kwa kosa lipi?

Bisimba anahoji ni kwanini Rais, badala ya kuwachukulia hatua mara moja, anasema ameagiza uchunguzi ufanyike dhidi yao. Anahoji uchunguzi huo wa Rais ni uchunguzi wa nini wakati tayari uchunguzi umekwishafanyika?

Ndugu zangu; hoja kama hizi za Bisimba, zimekuwa zikihojiwa pia na wasomi wengine mfano wa Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF na wenzake katika Ukawa.

Binafsi, nashindwa niwape jina gani ili Watanzania wawaelewe watu kama hawa wanaohoji vitu vya wazi ambavyo hata mtoto mdogo anaelewa mantiki yake. Nadhani, pamoja na usomi wao, wanahitaji kuambiwa ukweli kuwa wasitumie usomi wao kuupotosha umma wa Watanzania na kukumbushwa ahadi ya mwana TANU, ambayo enzi za ujana wao waliimba sana ya kwamba; nitatumia elimu yangu kwa manufaa ya wote na taifa langu.

Wakati Rais Kikwete akitoa ahadi ya kuendelea na uchunguzi dhidi ya Profesa Muhongo na Maswi, aliweka wazi kwamba sakata hili la Escrow limezungumzwa sana ndani na nje ya nchi. Alisema, kwa lugha yao ya Kikwere, watu wamezoza sana kuhusiana na suala hili, kwa hiyo lazima lifanyiwe uchunguzi wa kina ili ukweli halisi ujulikane.

Katika kupitia ripoti ya CAG, Rais Kikwete, kama walivyo Watanzania wengine isipokuwa akina Hellen Kijo Bisimba, hakuna popote panapojitosheleza panapoweza kuwatia hatiani watendaji hao kwa makosa ya kijinai au matumizi mabaya ya madaraka yao kuhusu suala hilo la Escrow.

Kwa hiyo, uchunguzi unaofanywa na vyombo vya dola dhidi ya watendaji hao wa Wizara ya Nishati na Madini na wengine serikalini kama anavyosema Rais Kikwete, unalenga kubaini kama kuna msukumo wowote ulioko nje ya maadili ya utumishi wa umma, uliowafanya waruhusu kutolewa kwa fedha hizo kutoka BoT na kukabidhiwa kwa PAP. Kisichoeleweka hapa kwa wasomi wetu hao ni nini?

Ikumbukwe kwamba Rais Kikwete ni mkuu wa nchi. Anavyo vyombo vingi na mbalimbali vinavyompatia taarifa mbalimbali. Yeye hawezi kuishia tu kwenye ripoti ya CAG na Takukuru kwa sababu kwanza Ofisi ya CAG haifanyi uchunguzi wa masuala ya kijinai, bali inafanya ukaguzi wa mahesabu na kutoa ripoti kwa mamlaka husika.

Ikitokea katika ripoti hiyo ya CAG kuna kasoro au kosa lolote la kijinai, ni jukumu la mamlaka husika kuagiza vyombo husika vya dola kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu. Ndiyo maana hata Takukuru yenyewe ambayo ina wataalam wa kufanya uchunguzi haiwezi kumfikisha moja kwa moja mtu inayomtuhumu bila kwanza kupata kibali cha Ofisi ya DPP ambayo ndiyo yenye uamuzi wa mwisho wa kujua kama hapa kuna shtaka la kujibu au la!

Nihitimishe makala hii kwa kuwafahamisha kina Kijo Bisimba na wenzake kwamba sehemu kubwa ya wananchi wa nchi, sasa wanatambua wazi kwamba kilichofanywa na Kamati ya PAC kupitia taarifa yake bungeni, ilikuwa ni siasa tu iliyosukwa kwa ulaghai na ghiliba kubwa ikilenga kuwajengea umaarufu baadhi ya wabunge kwa upande mmoja na pia ikilenga kutimiliza matakwa ya baadhi ya wafanyabiashara wetu waliokosa fursa ya kupata vitalu vya gesi na mafuta kwa lengo la kuvifanyia udalali kwa wawekezaji wakubwa wa nje ili wajinufaishe wao na familia zao pekee kwa upande wa pili.

Rais Kikwete, kwa miaka yake takriban 10 sasa katika uongozi wa taifa hili, ameifanyia nchi hii mambo makubwa na kuijengea nchi hii heshima kubwa, tena mbele ya mataifa makubwa dunia yakiwemo China na Marekani, kwa hiyo hana sababu ya kutafuta tena heshima ya nchi hii kupitia sakata hilo la Tegeta Escrow, wala hana sababu ya kugeuka kuwa Wakili wa IPTL/PAP kama ambavyo Dk. Hellen Kijo Bisimba anataka umma wa Watanzania umwelewe Rais wao.

Tanzania hii ina wananchi wengi wanaohitaji msaada wa kisheria kutoka kwa mwanasheria wetu huyu Kejo Bisimba. Watanzania wenzetu wenye ulemavu wa ngozi, maarufu kwa jina la albino na kina mama wengi wanaonyanyaswa katika familia zao wanaohitaji msaada mkubwa wa kisheria kutoka katika kituo chake. Namuomba kwa heshima na taadhima ajielekeze katika kuwasaidia hao badala ya kupoteza muda wake kujadili suala hili la Tegeta Escrow.
 
mimi ingekuwa wanazunguka vijijini kusaidia wanyonge wanaonyanyasika na mabaraza ya kata makatibu kata mahakimu ningewasifia akina kijo bisimba

lakini wao wapo kushindana na serikali hamna lolote ni wasakatonge tu
 
Kijo Bisimba ni mwanaharakati,sasa unauliza na huku unamjua,kichwa cha habari na Escrow yako ni vitu tofauti unatujazia server bure akina Maswi sasa wapo nyumbani wanaamuka wanakunywa chai,wanakula chakula cha mchana na cha usiku wakiwa majumbani mwao,ile chai ya ofisi na samahani boss naomba unisainie hapa na safari za bure, wameanza kuisahau kwa sasa.Endelea kupiga porojo sasa tunasubiri ''kiporo''kimwagwe kwenye shimo la taka,na tusahau kama kulikuwa na poro lililo anza kutoa funza kwa kuoza.
 
Unajaza server humu kwa ujinga kama huu. Jipange
 
Stori yako ya kutunga ndefu sana, embu isamaraizi basi. Futa pia mstari wa Dr Ulimboka eti aliteswa na ndugu wa wagojwa. Umesikia wewe majununi
 
Naona Mh. Maswi una muda wa kutosha sasa hata kutunga kitabu, umeandika kwa kirefu mkuu
 
Back
Top Bottom