Kijana Noel Lazaro akiugulia.
DAR ES SALAAM: Kijana mmoja mwenyeji wa Kijiji cha Mangamba mkoani Mtwara, Noel Lazaro (26) amelalamika kuwa anateseka kwa maumivu na huenda akapoteza maisha akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa kukosa shilingi 200,000 zinazotakiwa ili kuondoa vyuma mgongoni mwake.
Akizungumza na gazeti hili hospitalini hapo, Lazaro alisema awali alipata ajali ya Bajaj huko kwao na kupelekwa katika Hospitali ya Ligula, ambao walimpa rufaa ya kupelekwa Muhimbili alikofanyiwa upasuaji wa mgongo na kuwekewa vyuma.
“Nilikuwa siwezi kukaa wala kufanya chochote, kutokana na uduni wa hali yangu, baada ya kufanyiwa upasuaji nilirudi nyumbani Mangamba, Mtwara lakini sikuweza kuja Muhimbili kila mara kwa sababu sikuwa na fedha za nauli,” alisema kwa masikitiko kijana huyo.
“Yaani nilikuwa kwenye wakati mgumu, maumivu makali sana na hata haja kubwa ikitoka hadi sasa huwa sijielewi hadi ninapojiona nimechafuka, sikuweza kuwa nakuja kliniki kila mara kutokana na umaskini,” alisema huku akidondosha machozi.
Kijana alisema alimpata mfadhili, alijitolea na kumpa msaada hivyo akaweza kurejea Muhimbili kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa vyuma, lakini kwa bahati mbaya alipofika alitakiwa kutoa shilingi 200,000 ili aweze kufanyiwa upasuaji huo.
“Nimeshamaliza mwezi mzima hapa Muhimbili sijafanyiwa upasuaji kwa sababu fedha hizo zakulipia gharama sina, niko hapa nateseka, nina vidonda mgongoni mpaka hivi sasa havijapona na hapa sina ndugu, naishi kwa tabu na maumivu makali,” alisema Lazaro.
Ndugu msomaji, ikiwa umeguswa na tatizo la kijana huyo unaweza kuwaliana naye kwa simu namba 0676 299025 ili uweze kumsaidia aweze kutibiwa.