POLISI mkoani Kigoma imewaua kwa kuwapiga risasi watu watatu wanaosadikiwa kuwa majambazi kutoka nchi jirani ya Burundi na kukamatwa bunduki moja na risasi 69.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Otieno alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Kakonko. Alisema majambazi wengine wanne waliokuwa katika tukio hilo, wamekimbia.
Tukio hilo lililotokea juzi kijiji cha Kigina wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma. Kamanda Otieno alisema kuwa awali majambazi hao, walimuua kwa kumpiga risasi kichwani mwananchi mmoja wa kijiji cha Kigina, Lucas Luchapa ambaye walimkuta katika eneo ambalo walikusudia kuweka magogo kufanya utekaji, hivyo mwananchi huyo alihisi kuwa watu hao hawakuwa wema.
Aliongeza kuwa baada ya kuuawa kwa mwananchi huyo, polisi iliendesha msako na kuwazingira majambazi hao katika maeneo ya msitu wa kijiji hicho wakielekea mpakani na Burundi. Ndipo kukawa na kurushiana risasi, zilizosababisha vifo vya majambazi watatu na wengine wanne walikimbia. Kamanda Otieno alisema kuwa baada ya majambazi hao kukimbia, walikamata bunduki moja aina ya AK 47 ikiwa na risasi 60 zilizokuwa kwenye magazini tatu tofauti, huku bunduki hiyo ikiwa na usajili wa nchi ya Burundi.
Katika tukio lingine kamanda huyo wa Polisi alisema watoto wawili wa familia moja wamekufa baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kushika moto na kusababisha vifo vyao. Alisema tukio hilo ni la Kijiji cha Kazage kata ya Shunguriba wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, wakati watoto hao wakiwa ndani wamelala huku mama yao, Maombi John (25) akiwa amekwenda kisimani kuchota maji.