Kuogopa mauti!
Watu wengi wana mtazamo wa kutishia kuhusu mauti, na kwa hivo, si wengi wasiohofia kufa. Lakini, watu tofauti hupata athari tofauti kutokana na hofu hii. Wengine huona wataweza kuikimbia hofu hii kwa kukusanya mali mengi, kwani mali huwafanya wasiogope sana uhakika wa mauti.
Wengine nao huona kuwa mauti yanatishia kwani wengi wanayafkiria kuwa yana maumivu. Kwa hivyo, hawa hujiambia kuwa mauti hayana maumivu, na mwanadamu hahisi lolote baada ya kufa kwake.
Wengine nao huhepa hii hofu kwa kutofkiria wa kuzingatia mauti, na kuwanasihi wengine pia wasitafakari kuhusu mauti, ili wasiogope mauti.
Uzoefu unaonyesha kuwa njia zote hizi hazisaidii kuondoa hofu ya mauti.
Kwanini watu wanaogopa mauti?
1. Kupenda maisha ya dunia ni sababu kubwa ya kuogopa mauti, haswa kwa yule ambaye lengo lake lote ni huu ulimwengu. Mtu akam huyu huogopa mauti kwani huona kama mauti itamuondolea raha na anasa zote anazozijua.
Mtu anafaa azingatie: je, kama ulimwengu wa baada ya mauti ni bora na wa kupendeza na kufurahisha kuliko dunia hii, lengo lake litakuwa kufikia dunia ile nyingine, na hatohofia kupoteza raha za dunia hii.
2. Kutojua uhakika wa mauti ni sababu nyingine ya hii hofu ya mauti. Hajui kuwa mauti ni mapito tu, au mlango wa kumpeleka kutoka dunia hii kuingia dunia nyingine, na hudhani kuwa mauti ni mwisho wa yote. Mtu akifikira hivi bila shaka atakuwa na hofu kuhusu mauti, na kuona mauti kama jambo la kutisha.
3. Hofu ya kujibu kuhusu aliyoyafanya katika hii dunia pia humfanya mtu ambae hakumtii Mungu, lakini anaamini kuwa kuna akhera, au dunia nyingine baada ya mauti, kuogopa mauti.
Tumeangalia kuhusu uhakika wa kifo hapa. Katika makala yajayo, tutazidi kuangalia uhakika wa jambo hili.