Kifo cha Sokoine: Tujiondoe jela ya kifikra

DaveSave

JF-Expert Member
Nov 20, 2010
440
634
I. NYERERE ANATANGAZA KIFO CHA SOKOINE

Ilikuwa majira ya jioni tarehe 12 April 1984 kwenye taarifa ya habari ya saa 10.00 jioni mwaka 1984; kama ilivyokuwa kawaida ya nchi zote za Kikomunist vyombo vya habari vyote vilikuwa ni mali ya serikali, na ilikuwa na desturi ya kila Mtanzania kuhakikisha anakuwa karibu na redio kila inapofika wakati wa taarifa za habari kwa vile ilikuwa ndiyo njia pekee ya kupata habari mbali mbali za hapa nyumbani na nje ya nchi. Ilikuwa ni desturi ya Watanzania popote walipokuwa na wakati wowote inapofika muda wa taarifa ya habari shughuli zote husimama kwa muda wa dakika 10 ili kila mtu asikilize mambo muhimu yaliyotokea ndani na nje ya nchi.


Katika taarifa ya habari ya saa 10 jioni ya siku hiyo ilikuwa tofauti na taarifa za habari za siku nyingine kwa vile siku hiyo mtangazaji wa taarifa ya habari alikuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na alianza kwa kusema: “Watanzania wenzangu, ndugu yetu, kijana wetu, Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine amefariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea huko Dakawa nje kidogo ya mji wa Morogoro akitokea Dodoma kulihutubia bunge; ajali hiyo ilitokea wakati alipokuwa katika ziara yake ya kukagua mashamba ya mahindi katika mkoa wa Dodoma na Morogoro.

Msafara wa waziri mkuu ulivamiwa na gari aina ya Toyota Land Cruser ya mkimbizi mmoja wa kutoka Afrika ya Kusini kwa jina Dube ambaye alikuwa anaishi kwenye kambi ya wakimbizi ya Mzimbo mjini Morogoro; Dube alisimamishwa na polisi lakini alikaidi na kwa vile alikuwa katika mwendo mkali akasababisha ajali kwa kuigonga gari aina ya Mercedes Benz iliyokuwa imembeba waziri mkuu na kusababisha kifo chake.
Watanzania wenzangu nawaombeni sana mkubali kwamba Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine amefariki kwa ajali ya gari.”


Sokoine.jpg

Hayati Edward Moringe Sokoine
1938-1984​

Hayo yalikuwa ni maneno yaliyotamkwa na Nyerere katika taarifa ya habari alipokuwa anatoa taarifa ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine. Ukitaka kuthibisha maneno haya Nyerere waweza kuyapata kwenye maktaba ya redio Tanzania, au unaweza pia kuyakuta kwenye maktaba za magazeti ya Uhuru na Daily News.

Ikumbukwe kwamba Sokoine akifariki ndipo vita dhidi ya wahujumu uchumi (mafisadi kwa jina la kizazi kipya) imepamba moto; vita ambayo aliianzisha na alikuwa hachagui wala habagui mkubwa wala mdogo, na wala alikuwa haangalii kwamba wewe ni kigogo au kabwela, wote alikuwa anawashughulikia kikamilifu na sawa sawa bila upendeleo. Sokoine alikuwa anatisha, jina lake mafisadi walipokuwa wakilisikia walikuwa wanajikojolea na hata kuenda haja kubwa bila ya wao wenyewe kujijua, wengine walikuwa wanapata kiwewe na kuzirai na hata wakati mwingine kupoteza maisha;

Sokoine alikuwa anatisha, alikuwa hataki mizaha na wala alikuwa habagui bali alikuwa anafuata sheria. Vigogo wote wa nchi hii akiwemo Nyerere ambaye alikuwa Bosi wake Sokoine walikuwa wanamuogopa sana Waziri Mkuu huyu wa aina yake tangu nchi hii ipate uhuru toka kwa Waingereza.

Wahujumu uchumi walitupa magunia ya pesa barabarani, walitupa nyakula magunia kwa magunia, walitupa bidhaa mbali mbali kwa kuogopa kukamatwa na Sokoine! Wahujumu uchumi walikimbilia nchi za jirani kujificha na wengine walikimbilia nchi za mbali kwa kuliogopa jina la Sokoine; ndugu zangu Watanzania mliozaliwa miaka ya mwishoni mwa thamanini na kuendelea Sokoine alikuwa anatisha na pia alikuwa mbabe kwa manufaa ya umma, na kusema kweli huyo ndiye kiongozi pekee tangu nchi hii ipate uhuru wake toka kwa Wakoloni ambaye alikuwa ni kiongozi mwadilifu, mchapa kazi, mbunifu, alikuwa na maono ya mbali, na alikuwa ni mtu wa watu kweli kweli; alikuwa hana makuu, alikuwa na suruali mbili na shati mbili na viatu pair mbili!

Baraza.jpg

Baraza la Mawaziri akiwepo marehemu Sokoine wa nne kutoka kushoto mbele. Picha ya
Nkoromo Blog....​

Wakati Sokoine ni Waziri Mkuu kulitokea ugonjwa wa mifugo ambao uliua mifugo mingi sana mkoani Arusha; Sokoine alienda bank kuu kumuona Gawana wa bank hiyo wakati huo Mr. Charles Nyirabu ambaye alikuwa Binamu yake Nyerere ili ampe US $ 80,000 kwa ajili ya kuagiza madawa ya mifugo nchi za nje. Alipofika bank kuu na kumueleza Nyirabu kuhusu tatizo hilo Nyirabu alikataa kutoa pesa; Sokoine akamwambia Nyirabu unajua unaongea na nani? Unaongea na Waziri Mkuu wa nchi hii ukifanya mzaha nitakufukuza kazi sasa hivi, Sokoine alisema kwa sauti ya ukali, basi baada ya maneno hayo Gavana Nyirabu akanyanyua simu kuzungumza na binamu yake Nyerere akilalamika kwamba Sokoine anataka apewe pesa baada ya kumkatalia anamtishia kumfukuza kazi; Nyerere alimwamuru kwamba ampe kwa kusema maneno yafuatayo: Ni kweli huyo ni Waziri Mkuu hataki mchezo, anaweza kukufukuza kazi, mpe hicho kiasi anachokitaka. Ndipo Sokoine alipopewa pesa hizo na kuagiza madawa ya mifugo ili ainusuru mifugo ya mkoani Arusha.

Wakati Sokoine anateuliwa na Nyerere kuwa waziri mkuu tulikuwa na mfumo wa chama kimoja na Nyerere wakati huo alikuwa anajulikana kwa jina maarufu kama Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi hivyo system yake ilikuwa imejenga utaratibu kwamba mtu yeyote anapokuwepo katika mkusanyiko wa watu (mikutano, sherehe, au kongamano) lazima anapoanza kuzungumza aanze kwa kusema:

“Zidumu Fikra za Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi” halafu wanaokusikiliza wananyanyua mkono wa kulia juu kwa nguvu na huku ukiwa umekunja ngumi kwa kusema: “Zidumu” hivi ndivyo system ya Nyerere ilivyokuwa imemtengenezea kiongozi wake umaarufu na watu wote wakaiga na ikatokea bahati mbaya umepanda jukwaani ukajisahau kusema maneno hayo ya kumsifia Mwenyekiti wa chama, basi watu wote watakuona kama wewe si mtu wa kawaida, lazima utakuwa na mapungufu fulani, na wakati mwingine waweza hata kuadhibiwa na kitengo chake cha usalama wa taifa kwa kosa la kutomtambua Mwenyekiti wa chama cha Kikomunist!

Sokoine alipoingia tu madarakani akayaona hayo makosa na akawasahihisha Watanzania kwamba wasiseme tena kwamba “Zidumu Fikra za Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi” bali waseme “Zidumu Fikra Sahihi za Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi” aliongeza neno Sahihi kwa kusisitiza kwamba siyo kila fikra za Mwenyekiti ni sahihi, kitu ambacho hakikumfuhisha Nyerere kwa vile alikuwa ni mtu aliyekuwa anajiamini kupita kiasi na alikuwa hapendi ushauri wa mtu yeyote wala alikuwa hategemei kwamba kuna mtu anayeweza kumkosoa kutokana na jinsi alivyokuwa anaogopewa; lakini Sokoine alimkosoa na kumrekebisha na Watanzania wakajisahihisha kwa hilo.

Vita dhidi ya wahujumu uchumi aliyoianzisha Sokoine ilivuma kila kona ya nchi hii, mijini na vijijini wahujumu walinywea, nakumbuka kule mkoani Kilimanjaro kuna mto unaitwa mto kikavu basi baada ya Sokoine kuanza kuwakamata wahujumu uchumi, baadhi ya wafanyibiashara wa mkoani humo walichukuwa magunia kwa magunia ya sukari waliyokuwa wameyaficha kwa ajili ya kufanya ulanguzi na kuyatupa ndani ya mto Kikavu na maji ya mto huo yakageuka maji ya sukari; watu waliokuwa wanaishi kando kando ya mto huo walikuwa hawanunui sukari bali walikuwa wanachota maji ya mto huo kuyaweka majani kuyachemsha na kunywa chai!

Sokoine alisema ninaanza kuwashughulikia mawaziri wangu, nikimaliza kuwapekuwa namfuata Nyerere naye nikampekue. Kutokana na kauli ya kijasiri na ya aina yake iliyotolewa na Sokoine, Nyerere alipata wakati mgumu sana, na alihangaika vibaya mno, wakati huo Sokoine ana umaarufu mkubwa kuliko Nyerere, wananchi wametokea kumuamini Sokoine kama yeye ndiyo rais wa nchi kutokana juhudi zake za kweli na za vitendo za kuusaidia umma.

Jina la Sokoine wakati huo linatajwa na hata watoto wadogo, katika mazingira kama haya na kulingana na tabia ya Nyerere hakufurahishwa kabisa na hali kama hiyo. Kipindi hiki ndicho Sokoine alipompa Mzee Rashidi Mfaume Kawawa (Waziri katika ofisi ya rais wakati huo) siku 7 arudishe pesa za umma shilingi milioni sitini ambazo aliuza meli ya serikali lakini hakupeleka pesa hazina bali akaziweka mfukoni mwake! Sokoine alimwambia Kawawa kama ifuatavyo: “Nakupa Siku Saba Urudishe Pesa za Wananchi, Ukishindwa Nitakupeleka Radio Tanzania Uwaambie Watanzania kwa Njia ya Radio Pesa Zao Umezipeleka Wapi?; Mimi Naenda Dodoma Kuhutubia Bunge, Nikirudi Nipate Majibu” Wakati Sokoine anaenda kulihutubia bunge Dodoma, Kawawa akarudi kijijini kwake huko Liwale mkoani Lindi na Nyerere akafanya safari ya ghafla ya kwenda kumuona rafiki yake mpenzi rais wa Mozambique wakati huo Samora Machele.

Nyerere alipofika kwa Samora alimlalamikia kwamba nimemchagua waziri mkuu Sokoine lakini ananipeleka puta kweli kweli hata najuta kwa nini nilimchagua, na sijui nifanyeje? Samora akamshauri kwamba amfukuze kazi; Nyerere akamuambia siwezi kumfukuza kazi kwa vile Wananchi wanampenda kuliko wanavyonipenda mimi, na jina lake linavuma na ni kubwa kuliko mimi, hivyo nikimgusa tu wananchi hawatakubali kabisa! Nyerere akarudi Dar es Salaam na huku akiwa na hofu kwamba Sokoine akimalizana na mawaziri wake zamu inayofuata ni yake (Mwenzio akinyolewa na Wewe Tia Maji)! Kabla ya siku saba hazijaisha Sokoine anakufa kwa ajali ya gari iliyotokea huko Dakawa nje kidogo ya mji wa Morogoro.

Kwa muda wote huo Kawawa bado alikuwa yupo huko kijijini kwake Liwale mkoani Lindi lakini aliposikia tu taarifa za kifo cha Sokoine alirudi Dar es Salaam siku hiyo hiyo na kusisitiza kwamba Sokoine azikwe mara moja bila ya kuchelewa, lakini aliambiwa haiwezekani kiongozi wa kitaifa azikwe haraka haraka kiasi hicho, hivyo zikafuatwa taratibu za kuchunguza mwili wake kama inavyokuwa kwa watu wengi kabla ya kuzikwa. Ni mila na desturi za kila jamii kote duniani kuwaruhusu wanafamilia wa marehemu kuwa huru na mwili wa marehemu kama ambavyo ilivyo tabia na desturi zetu sisi

Watanzania, lakini utawala wetu umekuwa na utaratibu tofauti na zilivyo nchi zingine hasa akifa kiongozi wa kitaifa wanafamilia hawana haki na mwili wa marehemu: tunakumbuka alipokufa makamu wa rais Ali Juma pia wanafamilia hawakuwa huru na mwili wa ndugu yao; au alipokufa Gavana wa Bank Kuu Balali pia wanafamilia hawakuruhusiwa si kuuona tu mwili wa marehemu bali hata hawakuruhusiwa kuliona kaburi lake! Inaonekana huyu alikabidhiwa kwa malaika na kuzikwa huko mbinguni!

Wajerumani walipinga kifo cha Sokoine, hawakuamini kwamba Sokoine amekufa kwa ajali ya gari kwa vile alikufa akiwa amepanda Mercedes Benz magari ambayo yanatumiwa na viongozi wote mashuhuri duniani, ni magari yanayoaminiwa kiusalama kulingana na yalivyodizainiwa kwamba hata itokee ajali ya namna gani si rahisi kiongozi kufa; Wajerumani walipinga vikali wakiilamu serikali ya Tanzania kwamba inalichafua jina la Benz na kwa kufanya hivyo wanawavunjia soko la magari yao yasiendelee kununuliwa na nchi mbali mbali duniani!

Wajerumani walipinga wakisema hata kama Mercedes Benz iliyokuwa imembeba Waziri Mkuu ingekuwa imegongana na SCANIA BOUBLE TRAILER ikiwa na mzigo wa tani 40 bado isingeweza kumuua Waziri Mkuu, sasa imetokeaje agongane na Toyota Land Cruiser afe! Haiwezekani kabisa, walihoji Wataalamu wa Benz wa Ujerumani.

Kulingana na msimamo huo kampuni inayotengeneza magari ya Mercedes Benz ambayo ni ya kutoka nchini Ujerumani, ilituma ujumbe wa watu 7 kuja kuchunguza ajali inayodaiwa imemuua Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine.

Walipofika hapa nchini na kumuona Nyerere kuhusu mpango wao huo wa kutaka kufanya utafiti juu ya kifo cha Sokoine, Nyerere aliwaomba waondoke nchini mara moja kwa vile alishawaomba Watanzania waamini kwamba Sokoine amekufa kwa ajali ya gari na Watanzania wameshaamini! Sasa wakichunguza wakileta ushahidi mwingine Watanzania watamuelewaje wakati yeye ni rais wa nchi!? Wajerumani waliondoka lakini hawakufurahishwa na kitendo cha magari yao ya Benz kusingiziwa uongo ambao unaweza kuyadhuri katika soko la ushindani.

Kuanzia wakati huo hadi leo hii kifo cha Sokoine kimebakia Siri ya Taifa kama ambavyo alisema IGP Said Mwema kwamba swala Dr. Stephen Ulimboka la kuteswa na maafisa wa Ikulu ni Siri ya Taifa!

Pamoja na kwamba kifo cha Sokoine kimebakia kuwa Siri kubwa ya Taifa tangu mwaka 1984 hadi leo hii, lakini Watanzania wengi wamekuwa wakijiuliza maswali mengi bila ya majibu, hasa wanapojaribu kuitafsiri kauli ya Nyerere ya kusema: “Nawaombeni Muamini kwamba Sokoine Amefariki kwa Ajali ya Gari!” Hivi mtu aliyefariki kwa ajali ya gari unahitajiwa kuombwa uamini kwamba mtu fulani amekufa kwa ajali ya gari, wakati ajali yenyewe inaonekana!? Na kama Mercedes Benz imeweza kusababisha ajali kwa kiongozi wetu wa kitaifa, kijana wetu mpendwa Edward Moringe Sokoine kwanini tusingewaruhusu Wajerumani wathibitishe ajali hiyo ili waweze kutulipa fidia kwa kutuulia kiongozi wetu!?

Tuliogopa kitu gani kuwaruhusu Wajerumani kufanya uchunguzi huru, ili wakithibitisha ubovu wa magari yao waturudishie gharama zetu zote tulizotumia kuyanunua magari hayo!? Je, hatuoni kwamba kiuchumi hatuchukua hatua sahihi!? Je, huu siyo ufisadi wa aina yake!?

Nikirudi upande wa Tanzania ni kwamba wote tunafahamu fika kwamba msafara wa Waziri Mkuu unakuwa na magari yasiyopugua sita yakitanguliwa na pikipiki yenye king’ora ambayo inakuwa mbele kuyatahadharisha magari yote yaliyopo barabarani kwamba sasa mkubwa anakuja hivyo wekeni vyombo vyenu vya usafiri pembeni.

Kulingana na ukweli huu ni kwamba ni vigumu kwa mtu yeyote mwenye akili timamu kuamini kwamba Waziri Mkuu akiwa katika msafara anaweza kupata ajali ya kugongwa na gari iliyotokea kichochoroni! Kwa vile hata akatokea mwendawazimu akaamua kukaidi na kuendelea kuendesha gari, asingeweza kumgonga Waziri Mkuu kwa vile kuna magari yasiyopungua matatu ambayo yapo yanatangulia mbele ya gari la Waziri Mkuu, hivyo magari hayo kwanini yasiligonge hilo gari lililokaidi amri ya kusimama!?

Ni kwanini gari hilo liachwe mpaka liende likamgonge Waziri Mkuu!? Na kwanini Waziri Mkuu alikufa peke yake katika ajali hiyo!? Na baada ya kufa kwanini hakuna tume yoyote huru iliyoundwa kuchunguza kifo cha kiongozi wa kitaifa!? Kwanini badala ya kuunda tume ya kuchunguza kifo chake, badala yake Nyerere anawaomba Wananchi waamini kwamba Sokoine amefariki kwa ajali ya gari!?

Je, ndugu zangu Watanzania mpaka hapo hatuoni kwamba Nyerere na utawala wake walikuwa na chuki binafsi na Sokoine!? Inakuwaje Waziri Mkuu afariki kifo ambacho siyo cha kawaida na serikali ibaki kimya bila ya kuchukuwa taratibu zinazotakiwa, bali ikiwashawishi Wananchi waamini kwamba kiongozi wao amekufa kwa ajali ya gari!?

Kwanini tangu mwaka 1984 hadi leo serikali bado haijawachukulia hatua wale wote waliokuwepo katika msafara wa Sokoine kwa kuwafikisha mahakamani na kujibu mashitaka kwa kusababisha kifo cha waziri mkuu kwa uzembe wao!? Au ndiyo desturi na mila zile zile za Nyerere za kulindana na kuhamishana huku na kule!?

Hivi Watanzania tumekuwa watu wa namna gani, yaani Watanzania wote tunaombwa tuamini kwamba mtu amekufa kwa ajali ya gari na sisi tukakubali na tumekaa kimya! Kolimba akapewa kipaza sauti aeleze ni jinsi gani CCM imepoteza dira na mwelekeo ile kukifikisha kipaza sauti puani akafa! CCM wakasema amepaliwa na mate na madaktari wakasema hivyo hivyo! Wauza madini wakauwawa na kunyang’anywa madini yao, na kesi ilipoenda mahakamani maafisa wa serikali waliokuwa wanashutumiwa wakaachiwa huru kama vile mchezo wa kuigiza!

Leo ametekwa Dr. Stephen Ulimboka ameteswa na kutupwa porini na maafisa wa Ikulu; serikali inasema hiyo ni siri ya taifa! Kwa utaratibu huu tumefika wapi na tunaelekea wapi!? Pamoja na sinema zote hizi bado akina Mzee Malecela wanasema hawataki rais apunguziwe madaraka, bali wanataka aongezewe madaraka zaidi ili afanye kazi vizuri!

Baada ya Sokoine kufariki dunia watu wote walioshuhudia kifo chake walibadilishiwa kazi na kupewa kazi zingine ikiwa ni pamoja na wengine kupelekwa kufanya kazi katika balozi zetu huko nchi za nje: Mzee Harris Kolimba wakati kikitokea kifo cha Sokoine alikuwa mkuu wa mkoa wa Morogoro ambaye alihamia Dar es Salaam na kuwa katibu mkuu wa CCM, ambaye naye mwaka 1993 alikorofishana na Nyerere baada ya kusema CCM haina Dira na imepoteza mwelekeo, baada ya maneno hayo alikufa kifo cha kutatanisha! Wengine waliomfanyia postmortem kwenye hospitali ya Muhimbili kama akina Dr. Shaba walipewa kazi maalumu huko kwenye ubalozi wetu nchini Marekani na kadhalika!

Baada ya kifo cha Sokoine ndipo vita dhidi ya wahujumu uchumi ilipozikwa rasmi kule Dakawa na hata zile pesa alizokuwa anazidai Sokoine kwa niaba ya umma toka kwa Kawawa hakuna aliyezifuatilia tena, bali tukaendelea na maneno yale yale ya kinafiki ya majukwaani ya kukemea rushwa kwa mkono wa kulia na huku mkono wa kushoto unapokea rushwa na kuisukumia mfukoni! Wakati Kawawa akiuza meli ya umma, tulikuwa na meli moja tu, sasa waziri katika ofisi ya rais ameuza meli moja tu inayomilikiwa na serikali bila ya rais kujua licha ya kwamba magazeti yalindika sana!

Nyota ya Sokoine iliibuliwa toka mafichoni na rais wa kwanza wa nchi moja ya Afrika magharibi ijulikanayo kama Guinea Conakry Mr. Ahmed Sekou Toure. Rais Ahmed Sekou Toure alifanya ziara ya kiserikali hapa nchini, alipotembelea wilaya ya Mondoli alionyeshwa watoto wawili wa kimasai ambao walikuwa yatima; Sekou Toure aliwaomba hao watoto awachukue akawalee; alipewa watoto hao wawili aondoke nao, na Sokoine wakati huo alikuwa ni afisa katika wilaya Monduli aliombwa awasindikize hao watoto hadi Guinea Conakry pamoja na rais huyo wa Guinea.

Walipokuwa kwenye ndege Sokoine na Rais Ahmed Sekou Toure walipata muda mwingi wa kuongea mambo mengi sana yanayohusu nchi za kiafrika kwa ujumla, na pia walipofika Guinea Sokoine na Ahmed Sekou Toure waliweza kuongea mambo mengi yanayohusu Tanzania na Guinea kwa ujumla; Rais Ahmed Sekou Toure akawa amevutiwa sana na fikra pevu za kijana Edward Moringe Sokoine na kumwandikia Nyerere barua kwamba amchukue Sokoine awe karibu naye kwani ni mtu mwenye busara sana anaweza kumsaidia kwenye uongozi wake; baada ya mapendekezo hayo ndipo Nyerere alipomsogeza Sokoine karibu na yeye, na kweli alikiona kipaji cha Sokoine licha ya kwamba hakukipenda, lakini kwa sisi wanyonge huyu ndiye alitakiwa awe kiongozi wetu. Wale watoto waliosindikizwa na Sokoine kwenda Guinea wamesharudi nchini na mmoja wao ni Dr. Toure yupo katika moja ya hospitali za hapa nchini anafanya kazi.

Inasemakana kuna mtoto wa kiume wa Marehemu Edward Moringe Sokoine ambaye amajitahidi kwa muda mrefu sana ili aingie kwenye siasa kwa kutaka kugombea ubunge kwenye jimbo lake la Monduli, lakini ameshindwa kabisa kulingana na hali ya siasa za chuki za nchi yetu; kama baba yako alikosa au alikosana na Nyerere na kwa bahati mbaya akafa kabla hajaomba msamaha, basi jina lake likiambatana na wanae na kizazi chake chote wataendelea kupata adhabu! Hiyo ndiyo Tanzania ninayoijua mimi inayosifiwa kuwa kisiwa cha amani na utulivu!

Pamoja na ujasiri aliouonyesha Edward Moringe Sokoine lakini hakuna hata mwanasiasa, mwanaharakati wala raia anayetaka kulitaja jina lake hasa tunapopambana na wimbi kubwa la ufisadi, kinyume chake wote hawa wanasema eti angelikuwepo Nyerere yote haya yasingetokea! Nyerere hakupambana na ufisadi hata siku moja, bali alikuwa hodari wa kupiga blaa blaa za majukwaani ambazo hazina vitendo vyovyote bali Sokoine ijitolea kufa kwa kuupigania umma wa Watanzania. Utawala wa Nyerere ndiyo ulioanzisha ufisadi nchi hii hasa baada ya kuanzisha utaratibu wa kutonunua kitu chochote bila ya kupata kibali toka kwa wale walioteuliwa kuvitoa vibali hivyo; hakuna kibali kilichotolewa bure, lazima utoe kitu kidogo kwa wateule!

Sokoine alikuwa ni kiongozi wa pekee si hapa Tanzania tu bali hata kidunia ukichunguza kwa makini, si rahisi kwa viongozi wengi duniani kusimamia haki wakati anaonekana akifanya hivyo atamuudhi boss wake; viongozi wenye ujasiri wa aina hiyo kwa dunia ya leo niwakutafuta; Sokoine alikuwa si mtu wa mitandao wala majungu, alikuwa ni mtu anayefanya mambo kulingana na taratibu zilizowekwa; alikuwa habagui watu kimatabaka kama ilivyo viongozi wengi wa nchi hii; Sokoine alikuwa hana hulka ya Udini kama alivyokuwa Boss wake na viongozi wengi wa serikali yetu; Sokoine alikuwa anajua kuna watu wanaitwa Watanzania na raia wake ni Watanzania basi.

Tupende tusipende Sokoine pamoja na kwamba hakudumu kwa muda mrefu lakini Sokoine ni kiongozi wa aina yake katika karne ya 20, na kusema kweli itatuchukuwa karne nyingi mbele kuja kumpata Sokoine mwingine katika nchi hii.

Hivi karibuni tumesherehekea miaka 50 ya uhuru, lakini fumbo la kifo cha Sokoine limebakia kuwa Siri ya Taifa, na hata jina lake pia limebakia nao kuwa shubiri katika majukwaa ya siasa hapa nyumbani. Ningependa kuwaasa wanasiasa na wanaharakati kwamba kama wana nia ya kweli ya kuukomboa umma wa Watanzania ambao umekuwa katika mikono ya wagandamizaji kwa zaidi ya miongo mitano, basi hawana budi kulienzi jina la Sokoine kwenye kila jukwaa la kutetea maslahi ya umma kama ishara ya Ukombozi wa kweli; pia ningependa kuwaonya wanasiasa na wanaharakati waache kulitaja jina la Nyerere kwenye majukwaa yanayotetea haki za umma kwa vile kulitaja jina hilo ni kama kutonesha kidonda cha dhuluma na ugandmizaji uliozagaa kila pembe ya nchi hii, ugandamizaji ambao umeufanya umma kuwa masikini wa kupindukia wakati watawala wakiendelea kujineemesha wao na vizazi vyao vingi tu vijavyo!

Sokoine amefariki tumeachwa wakiwa, tuombe mungu atushushie Sokoine mwingine kabla ya uchaguzi mkuu ujao wa 2015; tusilale tukeshe tukiomba kwani tukifanya hivyo mungu aweza kusikia kilio chetu; tusikate tamaa, tuendelee kuomba bila ya mapumziko, mungu ana huruma sana, hawezi kukubali umma wake uendelee kuteseka miaka mingine 50 ijayo; miaka 50 tuliyoteseka inatosha.

Katiba mpya iweke wazi akifa kiongozi wa kitaifa katika mazingira tatanishi ni lazima iundwe tume huru kuchunguza kifo chake.

Posted 12th March 2013 by Jella N
 
... Alipofika bank kuu na kumueleza Nyirabu kuhusu tatizo hilo Nyirabu alikataa kutoa pesa; Sokoine akamwambia Nyirabu unajua unaongea na nani? Unaongea na Waziri Mkuu wa nchi hii ukifanya mzaha nitakufukuza kazi sasa hivi, Sokoine alisema kwa sauti ya ukali, ... Ndipo Sokoine alipopewa pesa hizo na kuagiza madawa ya mifugo ili ainusuru mifugo ya mkoani Arusha.
Kwa hiyo alipewa fedha za umma baada ya kutishia kumfukuza kazi mtumishi wa umma. Huu ndio ufisadi wenyewe, watu wanachota fedha za umma kwa vimemo vya amri tu. Bunge ndio linatakiwa kuidhinisha matumizi ya serikali, sio mtu anaibuka na kusema sijui hela zielekezwe kwenye nini sijui bila hata usimamizi
 
Nakumbuka enzi hizo tupo wadogo maeneo ya kijitonyana watu walikuja usiku wakamwaga ngano nzima lorry zima tuliamka usiku huohuo tukaanza kujichotea. Watu walitupa magunia ya sukari mtoni. Yaan sipati picha mtu km Sokoine angekuwa kipindi hiki cha Magu. R.I.P HE. Edward Moringe Sokoine
 
Eti Mzee Rashid Mfaume Kawawa alikuwa Fisadi!!
Mwl katika moja ya Vitabu vyake( nadhani kinaitwa Siasa yetu na hatima ya Tanzania) nilivyosoma anamsifia Rashid Mfaume Kawawa anasema Mungu ameumba watu wachache sana wenye sifa ya Uadilifu kama Kawawa anakiri Watu wa aina ya Kawawa hawaumbwi kila siku.
Anasema ilifika siku akachoka tu akataka kubadili Waziri Mkuu enzi hizo akamwita Kawawa akamueleza nia yake nae bila ya hiyana akaunga mkono na akashauri ateuliwe Sokoine!
 
Back
Top Bottom