Saturday, 03 September 2011 18:54 |
Na Julius Samwel Magodi WASWAHILI wanasema zubaa uliwe. Hilo ndilo linalotokea katika nchi yetu Tanzania kwa sasa. Sikushangaa baada ya msomaji wangu mmoja wiki hii kuniandikia meseji (sms) kupitia simu yangu ya mkononi akisema anashangazwa na Serikali ya Tanzania kulia kuwa haina fedha za kuhudumia wananchi wake wakati Afrika Kusini wanachuma mamilioni ya fedha kupitia madini ya Tanzanite yanayochimbwa katika ardhi yetu. Msomaji huyu anasema katika Mtaa wa Aderlay na Long kwenye Mji wa Cape Town nchini humo (Afrika Kusini )kuna jengo refu la ghorofa ambalo linaitwa Tanzanite House ambako madini ya Tanzanite ndipo yanapigwa bei. Meseji hii ya msomaji huyo imenikumbusha takwimu ambazo zilitolewa hivi majuzi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati akiahirisha Bunge mjini Dodoma kuwa, kampuni kubwa za madini nchini ikiwamo Barrick inayomiliki migodi ya dhahabu ya Bulyanhulu na Buzwagi, mkoani Shinyanga, North Mara kule Tarime na Tulawaka mkoani Kagera haimo katika orodha ya walipa kodi wakubwa nchini. Badala yake katika orodha hiyo iliyosomwa na Pinda, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ndiyo inayoongoza ikiwa imelipa kodi ya Sh165.4 bilioni, ikifuatiwa na Benki ya NMB (Sh108.6 bilioni), Kampuni ya Sigara (TCC) (Sh92.1 bilioni), Benki ya NBC (Sh89.9 bilioni) na Kampuni ya Saruji ya Tanzania Portland (Sh73.4). Hata hivyo, katika orodha hiyo kunakosekana kampuni kama Vodacom na Tigo (simu) huku Kampuni ya Airtel ikiwa imelipa Sh63.6 bilioni kwa mwaka. Hali hii inazua maswali mengi kwa nini kampuni za madini siyo miongoni mwa walipakodi wakubwa nchini, wakati wanasafirisha tani nyingi za mchanga wa dhahabu na madini hayo kila mwaka kwenda kuuza katika soko la dunia? Nadhani kuna tatizo hapa ama huenda kuna mikopo ya watu wazito nchini ambao wamekubali baadhi ya wawekezaji wakubwa wasichangie katika pato la nchi. Kinachosikitisha zaidi ni kwamba kampuni hizi za madini na simu zinazidiwa kwa kulipa kodi na kampuni ya kutegeneza pombe ya Chibuku iliyoko Dar es Salaam ambayo ililipa kiasi cha Sh13.4 bilioni. Hivi kweli pombe ya kienyeji ya Chibuku ambayo haiuzwi hata nje ya nchi, inaweza kushinda ulipaji kodi kampuni za madini? Hapa nadhani kuna haja sasa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuangalia upya utaratibu wa ulipaji kodi kwa kampuni kubwa za madini. Haiwezekani kuona kampuni kubwa ambazo ndizo zinatakiwa kuongoza kwa kulipa kodi ndizo ambazo sasa zinalipa kodi kidogo. Kinachoshangaza zaidi ni kwamba baadhi ya kampuni hizo za madini zimekuwa kila mwaka zikieleza kuwa zimeshindwa kufikia malengo na baadhi yake zikisema kuwa zimepata hasara na badala ya kuondoka zinaomba kuongezewa muda wa kuchimba madini. Hivi mtu anaye anapata hasara anaweza kukubali kuendelea kuchimba madini wakati fedha zake zinateketea? Ni wazi hapa kuna kitu kitu, lazima Watanzania tufumbue macho na hasa viongozi wetu wakiongozwa na Wizara za Nishati na Madini, Fedha, lazima waelewe kuwa hawa ni wawekezaji ambao kama hatutaweza kuwabana wataendelea kutolipa kodi inayotakiwa. Katika orodha hiyo ya Pinda, kampuni ya madini ya Tanzanite haimo wakati kule Afrika Kusini ni moja ya kampuni ambazo zinatengeneza mabilioni ya fedha kila mwaka kutokana na kuuza madini hayo katika soko la dunia. Ni wazi kuwa kama Serikali haitaweza kuwabana wawekezaji kulipa kodi inavyotakiwa Tanzania itaendelea kubaki kuwa nchi inayosifiwa kuwa fursa nzuri ya uwekezaji, lakini ambayo hainufaiki na badala yake wageni ndio wanaoneemeka. Mbali ya kampuni hizo za madini kushindwa kulipa kodi kubwa, fedha ambazo wanalipwa wananchi wanaozunguka migodi bado ni ndogo ambayo hainufaishi. Kwa mfano, leo nenda katika migodi mikubwa nchini angalia maisha ya wananchi wale wanaoishi karibu na migodi hiyo, wanaishi kwenye nyumba za tope, huku usiku wakitumia vibatari na vijinga vya moto, lakini jirani yao mwanga wa taa za umeme za mgodi ukiwaka. Fedha zinazotolewa kama mrabaha na kampuni hizi kwa mwaka ni ndogo mno sawa na mtu kumlambisha asali mdomoni huku wewe ukibaki na kibuyu kizima. Kwa kufika mahali hapa, inafaa Watanzania tuamke, tutafakari na tusikubali kuendelea kugeuzwa shamba la bibi, wawekezaji watulipe kodi zetu kama inavyotakiwa. Vinginevyo, TRA na Hazina watuambie kulikoni kodi zetu kutoka katika kampuni hio hazilipwi ipasavyo? 0754 304336 juliusmagodi@yahoo.com This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it |