Kibanda na Uandishi wake Makini | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kibanda na Uandishi wake Makini

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Josh Michael, Oct 8, 2009.

 1. Josh Michael

  Josh Michael JF-Expert Member

  #1
  Oct 8, 2009
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 2,525
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Na Absalom Kibanda

  ACHA nianze makala hii kwa kujisifu kidogo. Nilikuwa miongoni mwa wachambuzi wa mwanzo kueleza wasiwasi wangu kuhusu mwenendo usiofaa ulioanza kutawala katika vita ya ufisadi.

  Nilipoandika katika safu hii kwamba, vita ya ufisadi ilivyozidi kupamba moto ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano ilikuwa imeanza kuchukua mkondo wa utekwaji nyara na kikundi kidogo cha watu wenye malengo mahususi ya kisiasa, uhusiano wangu wa kikazi na binafsi na lile kundi la watu waliojipambanua kuwa majemedari wa vita hiyo ulianza kuzorota.

  Leo hii, baada ya muda mrefu kupita, kidogo kidogo hali ya mashaka na mwenendo wa kutiliwa shaka dhidi ya vita hiyo umeanza kujitokeza na pengine kukua kadiri siku zinavyokwenda mbele.

  Kukua kwa wasiwasi katika mwenendo mzima wa masuala hayo leo hii, kumesababisha baadhi ya maandishi yetu kuhusu vita hii kusutwa na kuonekana yakichukua mrengo wa kishabiki, kinazi na wakati mwingine kidikteta.

  Kama hiyo haitoshi, wasiwasi kuhusu mwenendo wa vita hiyo kupoteza mwelekeo, ulianza kuongezeka baada ya baadhi ya majemedari wake, ambao siku zote wamekuwa wakinyoshea wengine vidole, nao kugeukwa na kuanza kuandamwa, wakihusishwa na vitendo vya ufisadi na wakati mwingine vya matumizi mabaya ya madaraka katika maeneo waliyopo.

  Hali hiyo ya wasiwasi na kutoaminiana ilizidi kukuzwa na baadhi ya matukio yaliyoonyesha dhahiri kuupotosha ufisadi kutoka katika sura yake halisi ya kuwa tatizo sugu la kimfumo na kiutawala, na kulifanya lionekane kuwa ni ajenda ya kisiasa iliyokuwa ikikilenga kikundi cha watu fulani fulani tu, ambao hata kama ni kweli wanastahili kuonekana mafisadi, lakini wao si hitimisho la tatizo tuliloamua kupambana nalo kufa na kupona.

  Kugeuka kwa hali hiyo, kulihitimishwa na kile ambacho baadhi wanakiona kuwa ni upotoshaji wa wazi wa kundi mojawapo linalopambana na ufisadi, kuamua kwa malengo wanayoyafahamu wao wenyewe kumtanguliza Rais Jakaya Kikwete kuwa ndiye jemedari wao mkuu katika mapambano haya ya ufisadi.

  Uamuzi wa kundi hili lenye nguvu, ambalo hakuna shaka kwamba leo hii linazo nguvu kubwa pengine kuliko kundi jingine lolote nchini, likiubwaga chini hata mtandao uliomhalalisha Kikwete mwaka 2005, umeibua wasiwasi na maswali mengine katika jamii.

  Miongoni mwa maswali ambayo hadi leo hii yanaibuliwa na watu ni; Je, ni kweli Kikwete ndiye jemedari wa mapambano ya rushwa na ufisadi? Je, watu hawa wanaompamba Kikwete wanafanya hivyo kwa kutambua na kuheshimu mchango wake au wanampaka mafuta kwa mgongo wa chupa kwa sababu tu yuko madarakani?

  Wingi wa maswali haya ambayo wengi wanayoyauliza chinichini wakihofia kutandikwa bakora na majemedari wa kundi hili, ambao wanaendesha vita kwa staili ya kuwararua maadui zao kwa hoja thabiti na wakati mwingine ya uzushi na kuchafuana, umesababisha kuongezeka kwa hali ya mashaka na wasiwasi katika mapambano haya.

  Hata hivyo ni ukweli ulio wazi kwamba, hata kabla hajaingia madarakani, Kikwete alitamka hadharani kwamba, iwapo angeshinda urais mwaka 2005, basi angepambana na rushwa kwa kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya.

  Ni wazi kwamba, kama si kwa mtazamo huo wa kiongozi mkuu wa nchi, huenda leo hii wingi wa kesi zinazohusisha matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi waliopata kushika madaraka ya juu ya nchi, ubadhirifu wa mali ya umma na uhujumu uchumi, usingekuwa kama ulivyo leo hii. Katika hili wanaweza kuwa na sababu za kumtanguliza Kikwete.

  Pamoja na hayo yote, mwenendo usiofaa katika mapambano haya, ndiyo ambao leo hii umesababisha baadhi ya maandishi ya wachambuzi wakubwa wa mambo, wasomi, viongozi wa dini na wanasiasa kuanza kidogo kidogo kueleza wasiwasi kuhusu hali ambayo hakuna shaka kwamba, isipodhibitiwa inaweza kuliletea matatizo makubwa taifa huko tuendako.

  Ukiwaaacha wachambuzi wa kawaida ambao wanaongezeka idadi kila kukicha, miongoni mwa watu ambao tayari wamejitokeza na kueleza wasiwasi wao kuhusu vita hiyo na ambao safu hii haina budi kuwataja kwa majina kutokana na kuwa na nafasi ya kipekee katika jamii yetu, ni pamoja na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo ambaye aliwanyoshea kidole wapambanaji wa ufisadi.

  Katika kauli yake, Pengo aliwaasa watu hao kupigana vita hiyo katika misingi ya haki, ili nao wasije kuonekana kuwa ni watu wenye uchuro wa kuwa mafisadi.

  Katika rai yake hiyo, Pengo, mmoja wa viongozi wa kiimani wanaoheshimika kutokana na kuwa na msimamo thabiti katika masuala ya msingi, alisema iwapo vita hiyo ya ufisadi itapiganwa katika misingi isiyo ya haki, upo uwezekano wa watu kuanza kuamini kwamba huenda hata wapambanaji wenyewe wa vita hiyo wanapigana kwa sababu ya kuwa na hulka za kifisadi na kwamba wanalalamika kwa sababu moja au nyingine walikosa fursa hiyo.

  Mbali ya Pengo, mtu mwingine aliyetoa rai yenye mantiki hiyo hiyo hivi karibuni, ni waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, ambaye yeye alifikia hatua ya kumuasa Rais Jakaya Kikwete na serikali yake kuwa makini wakati wanaposhughulikia kesi zinazohusu tuhuma mbalimbali za ufisadi.

  Warioba ambaye ni mwanasheria kitaaluma na mtu aliyepata kuwa waziri wa sheria na mwanasheria mkuu wa serikali, alitoa rai hiyo wakati alipotakiwa na waandishi wa habari kutoa maoni yake kuhusu vita hio ya ufisadi ambayo hakuna shaka ni moja ya ajenda kuu za wakati huu.

  Katika rai yake hiyo, Warioba alionyesha waziwazi kuguswa na mwenendo wa kishabiki ambao unaonekana kutawala vita hii ya ufisadi kwa kiwango ambacho alisema kinaweza kufananishwa na mapambano mengine ya namna hiyo hiyo, ambayo yaliihusisha serikali na jamii ya Watanzania miaka mingi iliyopita kabla ya kumalizika kwa serikali kuwa majeruhi baada ya kushindwa mahakamani.

  Waziri Mkuu huyo mstaafu alikwenda mbele na kuiasa serikali kuepuka jazba za namna hiyo wakati kesi zinazohusu tuhuma za ufisadi zinapopelekwa mahakamani, kwani kukosekana kwa umakini katika kuzifungua na kuziendesha, kunaweza kusababisha malipo ya fidia kubwa ya fedha za umma siku za usoni.

  Ni wazi kwamba, unahitaji kuwa mtu usiyefikiri sawasawa iwapo utayapuuza pasipo kuyapima kwa umakini maoni ya namna hii yanayotolewa na mtu ambaye uzoefu na ujuzi wake katika masuala ya namna hii si wa kutiliwa shaka hata kidogo.

  Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, ripoti ya Tume ya Jaji Warioba, huyu huyu anayetoa rai hii, ndiyo ambayo ilitumiwa na serikali ya awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa kumfikisha mahakamani kwa tuhuma za kifisadi aliyewahi kuwa Waziri wa Ujenzi, Naila Kiula.

  Matokeo ya kesi hiyo ya Kiula kila mtu anajua kwamba, serikali iliangushwa mahakamani na upo uwezekano mkubwa kwamba mwanasiasa huyo mstaafu anaweza kuvuna mamilioni ya fedha kutokana na matokeo hayo. Huu ni uzoefu wa kutosha ambao Jaji Warioba ataendelea kubakia nao.

  Ni kwa sababu hiyo basi, niliposikia baadhi ya wanasiasa wakijitokeza si tu kumpinga, bali kumshambulia kwa hoja dhaifu Warioba, kwa sababu tu ya kutumia uhuru na uzoefu wake kutoa maoni yake, kidogo nilipatwa na wasiwasi ingawa sikushangazwa.

  Sikupatwa na mshangao kutokana na kutambua kwangu historia ya matukio makubwa ya kisiasa ya nchi hii, ambayo takriban yote yamekuwa yakiandamana na jazba na matendo ya kutumia zaidi hisia kuliko akili katika kuyatafutia ufumbuzi.

  Wakati nikiwa katika kutafakari maana na uzito wa maneno hayo ya Warioba, na kuangalia hatua ambayo taifa limefikia katika mapambano yake ya ufisadi mara moja nilianza kuona dalili za wazi za kuwapo kwa ukweli katika matamshi yaliyotolewa na kiongozi huyo mstaafu.

  Katika eneo moja, haraka haraka nilibaini kwamba, Warioba alikuwa ameanza kuingiwa na wasiwasi kuhusu mwenendo wa baadhi ya kesi zinazohusu tuhuma za ufisadi ambazo tayari ziko mahakamani.

  Ni mtu ambaye si mdadisi wa mambo na mfuatiliaji mzuri wa kesi hizo, ambaye anaweza akabisha kwamba, zipo dalili za wazi ambazo zimeanza kuonyesha kuwapo kwa hali ya vyombo vyetu vya dola na kimsingi viongozi wetu kukurupuka wakati wanapoamua kuwafikisha watuhumiwa fulani wa ufisadi mbele ya vyombo vya dola. Ni kwa nini Warioba asilitahadharishe taifa?

  Dalili hizi mbaya, iwapo zitaendelea kubakia kama zilivyo, zinaweza kulifanya taifa likabeba gharama ya kulipa fidia kubwa kwa watu ambao watashinda kesi za ufisadi kwa sababu tu ya makosa yaliyofanywa na vyombo vya dola au viongozi wa kisiasa na kiutendaji ambao waliweka mbele matakwa yao binafsi ya kuweka rekodi zilizotukuka katika vita hii.

  Wasiwasi wa kutokea kwa hali hii ndiyo ambao hakuna shaka ulimfika Jaji Warioba, na wakati fulani hata Rais Kikwete mwenyewe kwa zaidi ya mara moja alipata kuuelezea. Ni wazi kwamba kauli zilizojaa shaka za akina Pengo na Warioba katika mapambano hayo hazipaswi kupuuzwa kwa sababu tu ya kutaka kuzifurahisha nafsi zetu kwa gharama kubwa za kupoteza mwelekeo wa kitaifa huko tuendako. Iwapo kweli tunalitakia mema taifa hili, tunao wajibu wa kuhakikisha tunaziba nyufa kabla ya kuta kuanguka.
   
 2. M

  Mugerezi JF-Expert Member

  #2
  Oct 8, 2009
  Joined: Mar 28, 2007
  Messages: 454
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Hii habari ni nzuri na imesheheni vitu vizuri. Ni kweli Warioba ametoa angalizo kuwa kwenye hizi kesi inabidi kuwa makini lakini kwa kuwa mambo mengi hapa TZ yanapelekwa kisiasa zaidi badala ya kitaalamu viongozi uchwara wamemshambulia sana. Tuna kazi ngumu sana kuondoa mawazo ya maslahi kwanza kabla ya taifa.
   
 3. N

  Nanu JF-Expert Member

  #3
  Oct 8, 2009
  Joined: May 29, 2009
  Messages: 1,224
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Ni ukweli usiopingika kuwa JK anayendeshwa kama robot na WB, IMF, EU na kila wakati wakibinya misaada kidogo utasikia watu wanapelekwa mahakamani bila ya kufanyika uchunguzi wa kutosha. Ukiona au kusikia tu kuwa kuna kesi yoyote inayohusu ufisadi au matumizi mabaya ya madaraka imepelekwa mahakamani au inatayarishwa kupelekwa mahakamani ujue kuwa jamaa wa nje wamevuta kamba kidogo kumwamsha JK. Hii inaonyesha kuwa hana malengo madhubuti (action plan) ya kupambana na haya matatizo bali mengi ni funika....mwanaharamu apite.
   
 4. B

  ByaseL JF-Expert Member

  #4
  Oct 8, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 2,223
  Likes Received: 22
  Trophy Points: 135
  Mimi nimeguswa na pale Kibanda anaposema kwamba wapambanaji wa ufisadi wamemtanguliza JK kwa kumpaka mafuta ya mgongo? Kwa maoni yangu inabidi wafanye hivyo. Wazungu wanasema "you can eat an elephant but bite by bite". Tembo ni mnyama mkubwa sana. Ukitaka kumla na kummaliza lazima umkate vipande vipande vidogo ndio utamla na kummaliza. Na ufisadi ni hivyo hivyo.

  Wapambanaji wanajua kwamba Rais wetu yuko njia panda katika vita dhidi ya ufisadi (he is caught between the rock and hard place) kwa maana nyingine yuko shingo upande (he is half hearted on this) katika vita hii. Alishasema hata iweje Rais Mkapa hawezi kupoandishwa kizimbani na juzi waziri wake Sophia Simba karudia msimamo wa serikali. Sasa hili kupambana na kundi lenye nguvu la ufisadi inabidi Rais wetu aonekane anaunga msimamo wa wapiganaji mia kwa mia. Bila hivyo Rais akionekana ametengwa na juhudi hizo za vita dhidi ya ufisadi itakuwa ngumu sana. Ushindi ukishapatikana bila shaka JK atakuwa na wakati mzuri wa kutueleza alijua nini kuhusu IPTL, Richmond, EPA, Mikataba ya Madini, n.k. kwa sasa mbinu ya kumpaka mafuta ya mgongo ni sahihi.
   
 5. Pascal Mayalla

  Pascal Mayalla JF-Expert Member

  #5
  Oct 8, 2009
  Joined: Sep 22, 2008
  Messages: 24,601
  Likes Received: 18,631
  Trophy Points: 280
  Lazima tukubali tusikubali, Kibanda ni mwandishi makini, ukiondoa mara moja moja ambapo huwa anaegemea upande wa mwajiri wake, Kibanda is good.Mada yake pia ni nzuri, sio kwa sababu ta Pengo na Warioba, soma thread hii "WAPIGANAJI CCM WANAPIGANIA NINI? Na. M. M. Mwanakijiji" iliwachambua kwa kina wapiganaji na kueleza wanapigania nini. Wasiwasi wa Pengo, Warioba na sasa Kibanda ni muendelezo tuu.
   
 6. Waberoya

  Waberoya Platinum Member

  #6
  Oct 8, 2009
  Joined: Aug 3, 2008
  Messages: 11,611
  Likes Received: 3,913
  Trophy Points: 280
  What is the title of this article?
   
 7. Mpita Njia

  Mpita Njia JF-Expert Member

  #7
  Oct 8, 2009
  Joined: Mar 3, 2008
  Messages: 7,012
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  Kwa maneno mengine, warioba anaitahadharisha serikali kuwa iwapo kweli ina lengo la kumfikisha mahakamani, basi ijiandae kwelikweli, la sivyo atakuja kuivuna mabilioni
   
 8. Josh Michael

  Josh Michael JF-Expert Member

  #8
  Oct 8, 2009
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 2,525
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Kibanda ni mwandishi mzuri sana na makini sana kwa ajili ya kizazi hiki na pia amekuwa ni mtu makini sana katika jamii yote
   
 9. Kamende

  Kamende JF-Expert Member

  #9
  Oct 8, 2009
  Joined: Mar 1, 2008
  Messages: 415
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 0
  Kuna watu wana bahati kuwa hata katika UZEMBE wao wanakuwa MAKINI!!
   
 10. M

  Mugerezi JF-Expert Member

  #10
  Oct 9, 2009
  Joined: Mar 28, 2007
  Messages: 454
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Mkuu usemayo ni kweli lakini JK hatujui msimamo wake. Hivyo kuna uwezekano wa hawa wanao mtumia wakaja tupwa baharini na watz tukabaki tunashangaa. Kwani lazima kama mkuu wa nchi awe na msimamo na lazima aonyeshe upande anaosimamia lakini MIMI SIJAONA UPANDE WAKE MPAKA LEO ZAIDI YA WATU KUSEMA TUKO NA KWENYE MAPAMBANO.

  Inawezekana katika mapambano naye akawa adui kwani haijulikani yuko upande upi. Hivyo mkuu sidhani kama ni busara kwa JK kuwa kimya na sisi watz kudhani kuwa inaweza kusaidia kwenye vita. ATOE MSIMAMO TUUJUE NA AUSIMAMIE
   
 11. Josh Michael

  Josh Michael JF-Expert Member

  #11
  Oct 9, 2009
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 2,525
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Kuna mtu mwingine naye ni Ngurumo ambaye anasoma Hull naye amekuwa makini sana katika uandishi wake pia
   
Loading...