Kibaka anapouawa, dunia imepoteza...! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kibaka anapouawa, dunia imepoteza...!

Discussion in 'Mahusiano, mapenzi, urafiki' started by Mtambuzi, Jul 9, 2012.

 1. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #1
  Jul 9, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  Sasa naujua ukweli mkubwa kuhusu maisha.......................!

  Ni miaka 20 iliyopita, wakati huo nikiwa ninaishi na wazazi wangu Tandika, Dar es Salaam. Nilikuwa nasoma kidato cha kwanza wakati ule. Nakumbuka siku hiyo nilikuwa nimekaa mahali karibu na soko la Tandika [la zamani]. Nikiwa hapo, kijana mmoja alikurupushwa kutoka huko aliko kurupushwa. Nadhani alikuwa amefanya kosa, ingawa waliokuwa wanamfukuza walikuwa wakipiga kelele za mwizi.

  Huyu kijana alipofika pale nilipokuwa, alivua shati na kujifanya kichaa anayechakura takataka zilizokuwa pale, huku akitafuna baadhi. Halafu aliniambia, "wakija waambie mwizi amepita," kabla hajamaliza kusema, wale waliokuwa wakimfukuza walifika pale. Kuna waliokuwa na mapanga, marungu, visu, mawe na silaha nyingine. Nilijua yule kijana alikuwa ni mwizi na miaka ile kulikuwa na kundi la vijana wahalifu ambalo lilikuwa likifahamika kama Kiboko Msheli.

  Nilikuwa ni miongoni mwa wale ambao waliokuwa wanawaogopa sana hao Kiboko Msheli baada ya shangazi yetu aliyekuwa akiishi Magomeni Makuti kucharangwa mapanga na vijana hao na kuporwa kila kitu nyumbani kwake. Kwa hiyo, nilitaka kuwaambia wale watu kwamba, mwizi wao yuko pale mbele yao. Lakini kitu fulani kiliniambia niache, "amekuomba kwa wema, mwache, huenda anastahili kuishi." Sauti iliniambia kutoka ndani mwangu.

  Ni kweli wale watu waliokuwa na hasira waliniuliza, "mwanafunzi, huyu Kiboko Msheli ameelekea wapi?" Waliniuliza kwa sababu, eneo nililokuwepo ilikuwa vigumu kwa mtu kuvuka upande wa pili. "Kaenda huku, karuka hapo akapandia kwenye bati, akaondoka." Nilisema nikiwa natetemeka. Halafu mmoja kati ya watu wale aliuliza, "shati ameliacha hapa. Mbona huyu naye hana shati?" Alisema akimwangalia yule jamaa aliyejigeuza chizi.

  Nilisema, "huyu ni kichaa na shati sio lake, shati nila yule Kiboko Msheli, kalivua akaliacha hapa" Kundi lile ambalo tayari lilikuwa limegeuka kumkabili yule kijana, lilibadili mawazo na kuanza kuondoka. Nilikuwa na tetemeka kupindukia. Yule kijana alipoona watu wale wameondoka kabisa wakiishia kusema, "bahati yake" aligeuka na kunitazama kwa mda mrefu.

  "Umeokoa maisha yangu. Yaani sijui nikushukuru kwa namna gani, sina hata la kusema. Ni kweli, nimemkwapua mama mmoja mkoba, nikakosea stepu. Lakini, kuanzia leo sidhani kama nitaiba tena, sidhani. Unaitwa nani rafiki yangu?" Yule kibaka aliniuliza. Nilikuwa natetemeka sana, hasa baada ya kijana yule kukiri kwamba, ni kibaka na ametoka kufanya jaribio la kumpora mama mmoja. "Naitwa Punja, jina langu Punja…"

  Alinitazama huku akiwa anatabasamu. "Umefanya nini shavuni?" Aliniuliza, kwani nilikuwa na kovu la duara kwenye shavu. Nilimwambia nilizaliwa hivyo. "Una roho ya kibinadamu, nimeelewa sasa, bado kuna watu wanaopenda watu." Alisema, ingawa sio kwa maneno kama hayo moja kwa moja. Alizungumza kama vile kwenye maisha yake hajawahi kukutana na mtu anayeweza kumpenda. Halafu aliniomba fulana. Nilikuwa nimevaa fulana ya michezo ndani ya shati la shule. Kwa hofu zaidi kuliko wema, niliivua na kumpatia. Aliivaa na kumuenea. Hakuwa na mwili mkubwa, bali alikuwa amekomaa.

  "Nimebadilika, siwezi kuwa Kiboko Msheli tena. Nakuahidi mwanangu, kweli amini tu…" Alisema kwa lugha ya kihuni, alafu aliondoka akiliacha shati lake pale chini. Nilipumua kwa ahueni. Niliondoka kwenda shuleni huku nikijiuliza ingekuwaje kama ningewaambia wale watu wenye hasira kwamba, yule jamaa hakuwa kichaa bali ndiye kibaka mwenyewe. Damu ilinikimbia, nilipofikiria namna ambavyo wangemuuwa.

  Siku zinaenda. Nilimaliza kidato cha nne mwaka 1994, lakini sikufanya vizuri, kwani matokeo yalikuwa ni divisheni ya nne, tena inayokaribia ziro. Nilikuwa nimebakisha point mmoja niingie ziro. Mwaka huohuo mwezi wa Agost baba yangu alifariki. Baba alikuwa akifanya kazi serikalini na mama alikuwa ni mama wa nyumbani, ingawa alikuwa na vijishughuli vyake.

  Kufariki kwa baba kuliharibu kila kitu katika mipango yangu ya baadaye, hasa masomo na mambo mengine. Baada ya mazishi ya baba ambayo yalifanyika kijiji cha Ulaya, Kilosa, Morogoro, nilikaa kule kwa miezi mitatu kwa baba mdogo. Baadae nilirudi Dar kuanza kuangalia ningeishi vipi. Lakini mambo hayakuwa rahisi kwani baba hakuwa ameacha kitu cha maana kwetu watoto. Mimi nilikuwa ni mtoto wa kwanza na nilikuwa na wadogo zangu watatu.

  Pesa za malipo yake ya kazini zilitumika zaidi kulipa Madeni ya watu na zilizobaki kidogo tulinunua kiwanja eneo la Mbezi ya Morogoro Road. Kwa hiyo kuanzia pale tukawa tunaishi kwa kuhangaika sana. Maisha yalizidi kuwa magumu na mdogo wangu anayenifuatia aliacha shule kidato cha pili mwaka 1996. Wawili walikuwa shule ya msingi na mmoja alimaliza mwaka huo huo wa 1996. hakufanikiwa kupata nafasi shule ya serikali, hivyo akalazimika kukaa nyumbani.

  Mama alilazimika kuuza kiwanja cha Mbezi ambacho kilikuwa hakijafanyiwa chochote ili mdogo wangu aliyesimamishwa shule aweze kuendelea na masomo.
  Alikiuza, lakini bei ilikuwa ni ndogo sana kwani hakikuwa mahali pazuri sana. Alikiuza kwa shilingi 300,000. Ilibidi bwana mdogo arudi shule. Wakati huu mama alikuwa ameanza kuumwa mara kwa mara. Afya yake ilianza kuzorota siku hadi siku. Kufikia mwishoni mwa mwaka 1997 hali yake ilikuwa ni mbaya sana. Tulimpima hadi Ukimwi lakini hakuonekana na tatizo lolote. Alikuwa akiumwa mwili mzima na kuna wakati alikuwa akipoteza fahamu. Kwa hiyo alisimama kabisa kufanya chochote.

  Kwa kuwa ndiye aliyekuwa akiilisha familia, hali ilianza kuwa ngumu kupita kiasi. Kuna wakati tulikuwa tunashinda na kulala na njaa . Yule mdogo wangu wa Sekondari alisimamishwa tena shule. Ilibidi nitafute vibarua kwa nguvu zangu zote lakini nikawa kama vile nina mkosi, kwani sikuwa napata vibarua hata vile ambavyo tunasema ni vya watu wa chini kabisa. Labda pia kwa sababu umbo langu lilikuwa ni dogo na vibarua vya aina hiyo vilikuwa vinahitaji nguvu.

  Mwaka 1998, mama alikuwa hajiwezi kabisa. Mwenye nyumba naye akawa anatutishia kwani tulikuwa hatujamlipa kwa karibu mwaka mmoja. Pamoja na kumwona mama katika hali ile ya kushindwa hata kusimama, alikuwa akitutishia kututoa kwenye nyumba yake . Kwa kweli nilijua hasa maana ya maisha katika kipindi kile.

  Kuna wakati nilikuwa ninakaa chini na kujiuliza ni kitu gani hasa nilichomkosea Mungu au ni laana gani familia yetu ilikuwa imepata. Mwaka 1998, mama alikuwa hajiwezi kabisa. Kuna wakati nilikuwa ninakaa chini na kujiuliza ni kitu gani hasa nilichomkosea Mungu au ni laana gani familia yetu ilikuwa imepata.Wadogo zangu wawili nao walijiunga nami kufanya vibarua huku na kule ili kumwezesha mama kupata angalau hata uji. Mdogo wetu wa mwisho ambaye alikuwa wa kike ndiye akawa anamtunza mama.

  Kumwogesha na kumbadilisha nguo ikawa ni juu yake, kwani sisi tuliogopa. Ndugu wa mama walikuwa mbali, Sikonge Tabora tena huko ndani vijijini sana. Hivyo ikawa ni sisi wenyewe kukabiliana na hali ile. Pamoija na kuumwa, mama alikuwa akituambia tusikate tamaa, "Hata nikifa msikate tamaa, mtamudu tu. Nimewalea ili muweze siyo ili msindwe, mtaweza na inabidi msaidiane. Huoni mnaweza kunilea…." Maneno yake yalikuwa yanatupa moyo lakini yalikuwa yanatuumiza kwa upande mwingine.

  Nakumbuka ilikuwa ni February 1999. Ilikuwa jioni saa moja niliporudi nyumbani nilikuta mwenye nyumba ametoa vitu vyetu nje na ametia kufuli vyumba vyake.Tulikuwa tumepanga vyumba viwili na sebule, pale nje nilimkuta mdogo wangu wa kike akiwa amejiinamia akilia. Jambo la kwanza nililouliza ni mahali alipokuwa mama. Mdogo wangu alisema, "yuko kwa jirani". Huyu jirani yetu alikuwa ni mtu ambaye hakuwa akielewana na mama sana. Lakini kwa jinsi alivyoiona hali ya mama ya kutupwa nje mchana wa jua kali aliamua kumhifadhi.

  Nilikwenda moja kwa moja kumwona. Nilimkuta nje tu ambapo nilimsalimu na kumshukuru kwa wema wake. Alisema kwa kifupi, "nashukuru, lakini nawasaidia kwa siku tatu tu. Baada ya hapo itabidi wenyewe mtafute mahali pengine. Vyombo vyenu mnaweza kuviweka stoo, mkipata pa kuishi mnaweza kuvichukua." Nilimshukuru hata hivyo. Niliomba kuingia ndani kumwona mama.

  Nilimkuta akiwa amegeukia ukutani akiwa analia. Nilimbembeleza na kumwambia "nitapata pa kukaa kabla ta siku tatu na utapona tu ." Sijui hadi leo kwa nini nilisema maneno yale huku nikiyaamini kabisa. Nilitoka nje baada ya kusema hivyo na nikawa natembea bila kujua ninakoenda. Nilitembea kutoka Tandika hadi nikajikuta niko Temeka, karibu na kituo cha Polisi cha Chang'ombe.
  Halafu wazo lilinijia kuhusu jamaa yangu mmoja ambaye tulimaliza naye shule. Nilisikia kwamba alikwenda kusomea upolisi, Moshi na alikuwa pale kituo cha Polisi cha Chang'ombe.Niliamua kwenda kumuulizia pale. Niliambiwa alikuwa ameshatoka. Wakati namuulizia kulikuwa na raia wengine kando. Mmoja kati yao alikuwa anamwekea dhamana jamaa yake, alinitazama sana na kuniomba nimsubiri amalize shughuli ile ya dhamana. "Ningeomba tuzungumze kidogo, samahani kama nitakuwa nimekusumbua." Nilimjibu "sawa." Nilitoka nje ya kituo na kumsubiri.

  Alitoka na huyo mtu aliyemwekea dhamana. "Nakwambia hivi, hii ni mara yngu ya mwisho kukuwekea dhamana. Ukifanya tena upuuzi wako, usidhani utaniona kuja kuhangaika. Nenda zako, wala sikupi lifti, tutakutana nyumbani." Alimwambia huyo kijana ambaye alionekana wazim kuwa ni mhuni. Yule kijana alisita, lakini aliondoka. "Ni shemeji yangu, anatusumbua sana, sijui ana laana gani." Yule jamaa alisema akiniambia. Kwa hali yake ambayo ilikuwa inaonesha kwamba alikuwa na uwezo, nilishindwa kujua niseme kitu gani.

  Nilijikuta tu nikisema, "atabadilika, maisha yatamfundisha atabadilika siku moja." Yule jamaa alisema, "ni kweli, kama ulivyonibadilisha." Halafu alinyamaza. Nilibaki nimenyamaza, kwani sikumwelewa kabisa. Halafu aliniambia, "twende tukazungumze mahali penye utulivu, hapa pa wenyewe, unaweza kugeuziwa kibao." Alisema akimaanisha pale polisi . Tuliongozana hadi kwenye gari. Lilikuwa ni gari aina ya Suzuki Escudo la rangi ya dhahabu. "Karibu." Aliniambia. Kama b.w.e.g.e niliingia ndani ya gari na kufunga mlango. Aliwasha gari na kuondoka. Tulienda kwenye baa moja palepale karibu na Chang'ombe polisi upande wa juu tu kidogo.

  Tulipokaa tu vitini aliniuliza, "nitakosea nikisema weweni Punja?" Nilishtuka na kushikwa na butwaa zaidi. "Mimi ni Punja ndiyo, ndiyo jila langu….." Halafu mhudumu alikuja kutuhudumia. Yule bwana alicheka kwa furaha ya wazi kabisa. Halafu aliniuliza kama siwezi kumkumbuka, wakati tulisoma wote. "Wewe ulikuwa darasa la pili, mimi nilikuwa la sita, umesahau, hebu kumbuka."

  Nilijitahidi kurudisha kumbukumbu zangu nyuma enzi za shule, bila mafanikio. Lakini kwa sababu sikutaka kumfanya ajisikie vibaya, nilimwambia, "ni kweli kama nakukumbuka kidogo, sema jina tu nimelisahau." Yule jamaa alicheka tena na kunigonga mkononi. Alionekana kweli alifurahi.

  "Kweli kumbukumbu zako sio kali sana. Umesahau siku moja ulipokuwa sokoni Tandika kuna kibaka alitaka kuuawa ukamwokoa….." Halafu alinyamaza kama vile naye alikuwa anajaribu kuanza kulikumbuka tukio lile upya. Nilikuwa kidogo nimeanza kusahau tukio lile lakini lilirudi kwenye kumbukumbu zangu haraka. Ndiyo, sura yake haikuja kirahisi, lakini tukio lilinijia akilini kama vile ndio linatokea. Nilitabasamu, lakini pia nikiwa nimeingiwa na mshangao……

  "Nakumbuka, nakumbuka vizuri …. Lakini sijui umenikumbuka vipi, maana naona nilikuwa mdogo" Yule jamaa alinikatisha . "Jambo ulilofanya siku ile siyo tu kuokoa maisha yangu, bali ulinibadili kabisa. Ujue nilibadilika kabisa kwa sababu ya tukio lile . Nilianza maisha tofauti hadi nimefikia hapa unaponiona". Alisema.
  Kisha akaendelea
  "Siku hizi nafanya biashara na mafanikio ninayaona. Ulikuwa mtoto, lakini ulikuwa na moyo mkubwa sana, ulikuwa na utu wa kweli. Mtoto wa mjini aone kibaka, aogope kumpigia kelele……"
  Kwa kweli kwa sehemu kubwa kwa wakati ule pale, nilikuwa najiona kabisa kuwa ninaota ndoto nzuri halafu yenye utata. Aliniuliza kuhusu maisha yangu, baada ya kuona mshangao wangu umepungua.

  Nilimweleza kila kitu kwa kweli. Sikuwa napenda sana kusema matatizo yetu kwa kila mtu, ingawa pale mtaani hakuna ambaye hakuwa anayajua. "Sikiliza mdogo wangu," aliniambia baaada ya mimi kumaliza kueleza. "Mimi nihesabu kama kaka yako kabisa, yaani nichukulie hivyo kuanzia leo, matatizo yako yachukulie kama yangu pia. Naomba usijali sana, tutasaidiana." Bado nilikuwa nahisi kama ninaota na nilitarajia kuwa muda wowote ningeshtuka kutoka usingizini. Lakini, sikushtuka na nilianza kuamini kwamba ilikuwa ni kweli inatokea.

  "Nilikuahidi siku ile kwamba, nitaacha kabisa tabia ya wizi. Niliacha kweli na kuamua kuwa mtu tofauti sana. Hata nyumbani walishangaa sana na sikumwambia yeyote niliweza vipi kujitoa kwenye tabia ile. Lakini, siri yangu ilikuwa hapa, moyoni.Wewe ndiye ambaye ulinifanya nitoke kwenye tabia ile. Nilijisikia vibaya sana nilipoondoka na fulana yako siku ile." Alisema na ilibidi nicheke pamoja naye.

  Usiku ule tulitoka pale hadi nyumbani kwa jirani yetu ambapo mama alikuwa amehifadhiwa. Kufika pale tulikuta ugomvi. Yule jirani aliyemfadhili mama alikuwa akiwafokea ndugu zangu kwamba, wamewaruhusu wageni kuja kumuona mama na hivyo watamletea wezi nyumbani kwake. Ilikuwa bahati, kwa sababu yule jamaa yangu naye alisikia kila kitu, kwani nilishamwambia kuhusu yule jirani yetu na msaada wake wa masharti.

  Ilibidi yule jamaa ambaye sasa nilikuwa namwita kaka, ajitambulishe mwenyewe kwa yule jirani yetu. Alisema yeye ni mtoto wa dada yake mama na amekuja kumshukuru kwa kutoa msaada ule. Halafu alimuomba kama angeturuhusu tumchukue mgonjwa wetu. Nilishangaa na kuogopa. Tumchukuwe tumpeleke wapi? Nilijiuliza.

  Yule jirani alisema ni afadhali na kuanza kuponda kwamba, yule kaka amemwacha mama yake anatimuliwa kwenye nyumba nakudhalilishwa na hadi wakati ule ndiyo anajitokeza. Yule kaka yangu hakujibu kitu. Aliniomba nikatafute pick-up ambayo ingetosha vitu vyetu.

  Nilikwenda kituo cha pick-up haraka na kuchukua gari nikiwa sijui kitafanyika kitu gani. Niliporudi, yule kaka yangu mpya aliniambia nipakie mizigo yetu garini, kwani tungehama usiku uleule. Wakati tuna pakia mizigo alipiga simu kumwita kijana wake mmoja. Alimuelekeza mtaa tuliokuwepo.

  "Akija huyu kijana wangu, atawachukua ndugu zetu hadi Tabata. Kule kuna nyumba yangu ambayo haina mpangaji, mtaingia mle na tutaangalia baadaye mipango mingine. Kwa sasa mtaishi mle kwanza. Mimi na wewe, akishafika huyu jamaa tuta mchukua mama hadi hospitalini." Alisema kwa kujiamini.

  Ukweli ni kwamba nilihisi kama, sinema fulani hivi, kama ndoto tupu ambayo ingefika mwisho muda wowote. Bila shaka nawe unaposoma Habari hii sasa hivi unahisi kama ndoto au hadithi tu. Nataka uamini, kwa sababu itakusaidia kwenye maisha, sio hadithi.

  Watu walijaa pale kwenye nyumba ya jirani wakishuhudia kuhama kwetu. Bila shaka nao walikuwa wamepigwa na butwaa kuona au kugundua kwamba, kumbe tuna kaka mwenye uwezo. Natamani siku ile ijirudie tena, kwani ndio siku ambayo nilihisi furaha na hali nyingine ambayo wala nisingeweza kuielezea. Nilihisi hali fulani ambayo naijua mwenyewe huko ndani, siwezi kuisema kwa maneno.

  Yule kijana wa kaka alifika na kaka alimpa maagizo ya kuwapelekea wale ndugu zangu kwenye nyumba ya Tabata. "Hakikisha wanapata chakula pale kwa Ben, mwambie malipo kesho." Alitoa maelekezo.

  Yule kijana wake alikubali na kuanza kusaidia kupakia vyombo garini. Lakini, kaka alimuita na kumuomba tukasaidiane kumchukua mama ndani.Tulimtoa mama ndani kwa msaada wa jirani zetu na kumuingiza garini. Ilibidi tuondoke kumpeleka hospitalini. Tulimpeleka mama hospitali ya Agakhan.

  Baada ya kufanyiwa vipimo na kupatiwa kitanda, tuliondoka kurudi nyumbani, ambapo sasa ilikuwa ni Tabata. Yule kaka alinihakikishia kwamba, nisijali kabisa kuhusu yote anayoyafanya, kwani anayafanya kwa moyo mmoja. Aliniambia kwamba huenda Mungu aliniweka pale sokoni siku ile ili kupitia kwangu, yeye waweze kujifunza ukweli mkubwa kuhusu maisha.

  Hivyo kile kilichoniweka pale sokoni siku ile ndicho ambacho kilinifanya kuzurura hovyo hadi tukakutana polisi jioni ile. Ni kweli huenda. Nilikubaliana naye. Hata hivyo, kunikumbuka, ndilo jambo ambalo lilinifanya nishangae sana. Ni kweli nilikuwa na kovu shavuni lakini hata jina nalo!

  Tulihama baadae na kwenda kuishi Buguruni ambako nilipanga nyumba. Hii ilikuwa ni miezi sita baada ya kuhamia Tabata kwenye nyumba ya kaka. Wiki moja tu baada ya kuhamia pale, aliniuliza kuhusu shughuli ambayo ningependa kuifanya.

  Nilimwambia ningependa kufanya biashra ya mipakani, Hii ni shughuli ambayo nilikuwa naipenda sana maishani mwangu, tangu utotoni.

  Alinipa mtaji na nikaanza biashara. Kwa kweli nilianza na bahati na nimeendelea kuwa nayo.

  Mama yangu alipona baada ya kukaa hospitalini kwa wiki tatu. Hadi leo anajiona kuwa anaota kwa kile kilichotokea hajaamini.
   
 2. uttoh2002

  uttoh2002 JF-Expert Member

  #2
  Jul 9, 2012
  Joined: Feb 3, 2012
  Messages: 3,679
  Likes Received: 2,743
  Trophy Points: 280
  I am a strong Man, but I cried reading this, fanya wema nenda zako bila kutegemea kitu, Mungu atakulipa ....
   
 3. Eiyer

  Eiyer JF-Expert Member

  #3
  Jul 9, 2012
  Joined: Apr 17, 2011
  Messages: 28,238
  Likes Received: 3,676
  Trophy Points: 280
  Mtambuzi,nimetokwa na machozi kwa sababu zaidi ya moja.Ila umenikumbusha mmoja kati ya watu muhimu kabisa katika maisha yangu,Munga Tehenan,bahati mbaya ameshauacha mwili!Ila kwa mtu ambae hajayaona magumu ya maisha,anaweza kuona hii kama hadithi!
   
 4. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #4
  Jul 9, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Mkuu tupo pamoja........ Nitaendelea kuzidondosha moja moja hapa kila nikipata wasaa.....
   
 5. Blaine

  Blaine JF-Expert Member

  #5
  Jul 9, 2012
  Joined: Jan 11, 2012
  Messages: 2,285
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 0
  Mtambuzi, what do you do for a living?
   
 6. Watu8

  Watu8 JF-Expert Member

  #6
  Jul 9, 2012
  Joined: Feb 19, 2010
  Messages: 47,350
  Likes Received: 2,687
  Trophy Points: 280
  well documented...
  inafunza sana maana inaonesha asili ya mwanadamu ni UPENDO,
  laiti kama kila mmoja wetu angekua na UPENDO, leo hii dhiki na mahangaiko ungekua ni msamiati.
   
 7. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #7
  Jul 9, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  I am living by helping others to reach their goal...............!
   
 8. Blaine

  Blaine JF-Expert Member

  #8
  Jul 9, 2012
  Joined: Jan 11, 2012
  Messages: 2,285
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 0
  unamaanisha counselor? thats a very fulfilling job, hongera
  i always thought you write novels/riwaya because you bring a lot of interesting stories to the forums frequently.

   
 9. H

  Henry Philip Senior Member

  #9
  Jul 9, 2012
  Joined: Jul 29, 2008
  Messages: 114
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Du! ngugu yangu, huwa sisomi story ndefu kama yako huku jamvini lakini leo nimetulia na kuisoma hii yako nukta kwa nukta hadi mwisho. kimsingi nimehuzunika sana na wakati naisoma akili na mawazo yangu yalihama na nikawa nafasi uliyokuwapo wakati ule, imenigusa sana. Hakika Mungu amepandikiza moyo mkuu na wa ajabu ndani yako. na azidi kukubariki na kukuneemesha kama alivyokufanyia miaka kadhaa iliyopita. Wape hi mama na ndugu zako na waambie kuwa Mungu yupo na familia hiyo hamkuwa warahisi hata kutetereka na kwenda kwa waganga kutafuta msaada hata wakati ambao mlikuwa katika dhiki kuu. Tumaini lenu kwa Mungu ndilo lililowaokoa. Kwa wale wanaobisha kuwa Mungu hayuko, mjue kuwa yuko kila siku ktk maisha yetu na anashuhudiwa Kwa mfano huu. Mungu aibariki familia yako/yenu na mjazwe na kila mema na baraka.
   
 10. Mkwai

  Mkwai JF-Expert Member

  #10
  Jul 9, 2012
  Joined: Feb 29, 2012
  Messages: 308
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 35
  nimekuwa nikisoma simulizi zako mara kadhaa, kwa kweli zinasisimua na kutufunza mengi yahusuyo maisha yetu ya kila siku. Hii ya leo imenikumbusha mengi niliowahi kukumbana nayo katika maisha. Asante
   
 11. HAZOLE

  HAZOLE JF-Expert Member

  #11
  Jul 9, 2012
  Joined: Feb 25, 2011
  Messages: 1,333
  Likes Received: 64
  Trophy Points: 145
  mtambuzi at work. imekaa vema hiyo.
  hakika maisha ni degree tosha.
   
 12. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #12
  Jul 9, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Writing Novels/Riwaya is my dream,.........
  Muda ukifika nitawajulisha hapa ni kitu gani nimefanya......... In fact natafuta mtu wa kushirikiana naye maana sitaki kufanya kila kitu peke yangu, naamini kama nikipata at least watu wawili tukaunganisha vichwa, I believe tutatoakitu kizuri kwa manufaa ya vizazi vijavyo.............

  Pamoja Daima
   
 13. Mahmetkid

  Mahmetkid JF-Expert Member

  #13
  Jul 9, 2012
  Joined: Apr 20, 2012
  Messages: 557
  Likes Received: 45
  Trophy Points: 45
  Pole kwa Punja kwa vipindi vigumu alivyopitia.
   
 14. Baba V

  Baba V JF-Expert Member

  #14
  Jul 9, 2012
  Joined: Dec 29, 2010
  Messages: 19,507
  Likes Received: 170
  Trophy Points: 160
  you mean my deili briid is injinialing and sorry i remove my name, teh, (No offence mkuu,nimekumbuka kauli ya Mbunge)
   
 15. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #15
  Jul 9, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Ahsante mkuu, salaamu hizo nitazifikisha kwa muhusika.
  Ukweli ni kwamba mimi sihusiki kabisa na mkasa huu. Hii habari tuliwahi kuiandika katika gazeti la Jitambue ambapo mimi nilikuwa ni mmoja wa waandishi wa gazeti hilo. Nimeamua kurejea baadhhi ya makala zilizowahi kuandikwa katika gazeti hilo humu jamvini ili tupate kujifunza wote kwa pamoja. anayehusika na mkasa huu yupo na ni mfanyabiashara ambaye huwa anasafiri mikoani. ni yeye mwenyewe aliyependa habari hii iwekwe katika gazeti hilo la Jitambue ili watu wapate kujifunza kutokana na uzoefu wake..................
   
 16. Ruttashobolwa

  Ruttashobolwa JF-Expert Member

  #16
  Jul 9, 2012
  Joined: Feb 22, 2012
  Messages: 43,748
  Likes Received: 12,842
  Trophy Points: 280
  Oooooooooh umeniliza!
   
 17. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #17
  Jul 9, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Umekosea bana hapo kwenye bold ilitakiwa isomeke "lemove"
   
 18. Blaine

  Blaine JF-Expert Member

  #18
  Jul 9, 2012
  Joined: Jan 11, 2012
  Messages: 2,285
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 0
  very admirable. nakutakia mafanikio na Mungu akusaidie nia yako itimie
   
 19. ndyoko

  ndyoko JF-Expert Member

  #19
  Jul 9, 2012
  Joined: Nov 2, 2010
  Messages: 4,974
  Likes Received: 279
  Trophy Points: 180
  Huu mtindo wa kuharibiana siku maofisini utatufanya watu tupewe off kwa kudhania umepatwa na msiba! Sijui kama kina Ray na wengine wengi huwa wana muda wa kupitia JF. Hakika nakwambia wangeachana na mtindo wa kukopi movies za Kinaijeria.
   
 20. M

  Mukalunyoisa Senior Member

  #20
  Jul 9, 2012
  Joined: Mar 16, 2012
  Messages: 139
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  RIP MUNGA TEHENAN nilikuwa mpenzi mzuri sana wa gazeti la JITAMBUE
   
Loading...