Kesi ya wanafunzi Kiu yakwama mara ya nne

Kesi ya wanafunzi Kiu yakwama mara ya nne

kirerenya

JF-Expert Member
Joined
Aug 27, 2013
Posts
1,698
Reaction score
2,262
Dar es Salaam. Kesi ya kusambaza taarifa za uongo kwenye mtandao wa Whatsapp inayowakabili wanafunzi wanne wa Chuo Kikuu cha Kampala (Kiu), imeshindwa kuendelea kutokana na shahidi kutofika mahakamani.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Mahakama ya Wilaya ya Ilala, imeshindwa kuendelea baada ya upande wa mashtaka kueleza shahidi yupo masomoni, hivyo kuomba shauri liahirishwe.

Hii ni mara ya nne kwa kesi hiyo kuahirishwa katika kipindi cha miezi mitatu. Julai 6, mwaka huu ilishindwa kuendelea baada ya wakili wa upande wa mashtaka Florida Wenceslaus kutokuwepo mahakamani.

Agosti 3 kesi hiyo iliahirishwa baada ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Maria Tweve (20) kuwa mgonjwa na Agosti 25 haikuendelea baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuwasilisha vielelezo mahakamani.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni Amenitha Kongo (19), Maria Tweve (20), Agnes Gabriel (21) na Anne Mwansasu(21).

Wakili wa Serikali, Jackline Werema ameiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi kutokana na shahidi kuwa masomoni hivyo kushindwa kufika mahakamani.

“Mheshimiwa hakimu, shahidi aliyepaswa kutoa ushahidi leo ameshindwa kufika mahakamani kwa sababu yupo shule na amebanwa na masomo, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na ushahidi,” ameeleza Werema.

Hakimu Mkazi, Catherine Kiyoja anayesikiliza shauri hilo amekubali ombi hilo na kuahirisha kesi hadi Septemba 21.

Wanafunzi hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Februari wakikabiliwa na shtaka la kusambaza taarifa za uongo kwenye mtandao wa kijamii wa Whatsapp.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo Juni 9, 2016 jijini Dar es Salaam. Inadaiwa walichapisha picha ambazo zinaonyesha Rais John Magufuli akiwa amevaa hijabu na kuzisambaza kwenye mitandao, huku wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Washtakiwa wanadaiwa kutengeneza picha hizo kwa kutumia kompyuta na baadaye kuzisambaza mtandaoni kwa lengo la kumuudhi na kumkashifu Rais.

Mahakama ilitoa dhamana kwa washtakiwa ambao walitimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili kila mmoja ambao walisaini bondi ya Sh2 milion

Chanzo: Mwananchi
 
Asante mkuu kwa taarifa..

Tuwe makini na taarifa tuzisambazazo mitandaoni
 
  • Thanks
Reactions: mwl
Back
Top Bottom