Kesi ya DC mstaafu, shahidi akiri kuutambua mukhtasari

buswelu moja

JF-Expert Member
Aug 24, 2014
226
180
Shahidi wa tano katika kughushi mukhtasari wa serikali ya mtaa Levolosi jijini Arusha,Joachim Kivuyo amekiri kuutambua mukhtasari uliofanikisha utengezaji wa hatimiliki ya kiwanja nambari 231 kitalu DD kilichopo eneo la Mianzini jijini hapa na kusema kwamba mukhtasari huo ulikidhi vigezo vyote wakati wa kuuandaa.

Akiwasilisha ushahidi wake jana mbele ya hakimu mkazi,Mwankuga Gantwa wa mahakama ya hakimu mkazi Arusha shahidi huyo aliiambia mahakama kwamba anathibitisha ya kwamba mukhtasari huo ni halali na wajumbe waliupitisha kihalali.

Mbele ya mahakama hiyo shahidi huyo ambaye ni mjumbe mstaafu wa serikali ya mtaa wa Levolosi aliiambia mahakama hiyo kwamba pamoja na kwamba hakushiriki kikao kilichoketi kuuandaa mukhtasari huo lakini anathibitisha ya kwamba ulikuwa halali kwani mukhtasari unaweza kuandaliwa na wajumbe wote au nusu ya wajumbe na wengine kushirikishwa kwa njia ya simu.

Akihojiwa na wakili upande wa utetezi,Ephraim Koisenge je anakumbuka ya mwaka 2015 aliwahi kutoa ushahidi wake mbele ya mahakama wa wilaya ya Arusha kuhusu mukhtasari huo kwamba ni halali shahidi huyo alisema ni kweli anakumbuka aliwahi kutoa ushahidi huo na kukiri kwamba alisema maneno hayo.

Shahidi huyo aliiambia mahakama kwamba anakumbuka mwaka 2015 aliitwa mbele ya kituo kikuu cha polisi cha kati na kuhojiwa kuhusu mukhtasari huo na kudai kwamba anautambua mukhtasari uliopo mbele ya mahakama hiyo na kwamba umekidhi vigezo vyote.

Naye shahidi wa sita,Mohammed Abraham mkazi wa Sokon One jijini Arusha akiwasilisha ushahidi wake mbele ya mahakama hiyo alisema kwamba hajui nani ni mmiliki halali wa eneo linalogombaniwa lakini amekuwa akimwona mshtakiwa ,Mollel akiishi katika eneo hilo kati ya mwaka 1980 hadi 1989.

Akihojiwa na wakili upande wa utetezi,Koisenge kwamba je aliwahi kumwona mkuu wa wilaya mstaafu,Dan Makanga akiishi katika eneo linalogombaniwa shahidi huyo alisema hapana hajawahi kumwona hata siku moja akiishi katika eneo hilo.

Hatahivyo,shahidi huyo aliiambia mahakama kwamba hafahamu mahusiano kati ya Makanga na Mollel lakini anakumbuka ya kwamba marehemu mama yake mzazi,Halima Hassan aliwahi kumpatia Makanga eneo la kiwanja lakini hakuwahi kushiriki makubaliano yoyote zaidi ya wadogo zake.

Mara baada ya kumaliza kuwasilisha ushahidi huo mahakamani hapo hakimu Gantwa alimtaka mwendesha mashtaka wa serikali,Mary Lucas kuhakikisha anawaleta mashahidi wawili waliobaki katika kesi hiyo kwa ajili ya kufunga ushahidi wao na kuihairisha kesi hiyo hadi Mei 24 mwaka huu.

Katika kesi hiyo nambari 430 ya mwaka 2016 Makanga ambaye aliwahi kuwa mbunge wa jimbo la Bariadi Mashariki alifika mbele ya kituo kikuu cha polisi cha kati na kumtuhumu mme mwenzake Mollel kughushi mukhtasari wa serikali ya mtaa wa Levolosi na kujipatia hatimiliki ya kiwanja namba 231 kitalu DD kilichopo Mianzini jijini hapa.

Mwisho.
 
Back
Top Bottom