Polisi nchini Kenya imetumia gesi ya kutoza machozi kutawanya mamiya ya waandamanaji mjini Nairobi wakipinga kupanda kwa bei ya chakula na mafuta.
Polisi wazima maandamano
Mwandishi wetu, Robert Kiptoo akiwa mjini Nairobi anasema kuwa ummati huo wa watu ulipita katikati ya jiji ukiimba nyimbo za kukashifu wakati wakizuia mtiririko wa magari na kusababisha wenye maduka kuyafunga.
Kuna uhaba wa mahindi kote Afrika mashariki kutokana na ukame.
Serikali ya Kenya hivi karibuni ilipunguza kodi juu ya mahindi yanayoagizwa kutoka nje ili kuepusha kupanda kwa bei.
Maandamano kupinga gharama kubwa
Wanafunzi kadhaa wa Chuo kikuu na wanaharakati za haki za utu walikamatwa wakati wa maandamano ambayo Polisi waliyataja kama yaliyofanywa bila kufuata utaratibu wa sheria sababu hawakuomba ruhusa kuandaa maandama
Baadhi ya waandamanaji walisoma vipengee katika Katiba mpya , vilivyoongezewa mwaka jana, wakielezea haki yao ya uhuru wa kuandamana, anasema mwandishi wetu.
Hata hivyo juhudi zao za kufika kwenye afisi ya Rais na Waziri mkuu kuwasilisha malalamiko yao zilikwama pale Polisi wa kuzia fujo walipotumia gesi ya kutoza machjozi na mbwa kuwatawanya.
Mwandishi wetu anasema kuwa kupanda kwa gharama za maisha kumewaudhi raia wengi wa Kenya.
Bei ya hii leo ya mfuko wa kilo mbili ya unga wa mahindi ni sawa na dola mbili za Marekani au pauni 1.25 za Uingereza.
Bei hiyo ni kubwa kwa raia milioni 40 wa Kenya.
Waandamanaji hao pia wamewatuhumu wenye viwanda vya kusaga mahindi kwa kuhodhi mahindi ili kuona kuwa bei inapanda.
Watu takriban milioni 12 katika pembe ya Afrika wamekumbwa na ukame - ambao haujatokea katika eneo hili katika kipindi cha miaka 60.
Halikadhalika Kenya inakabiliana na mfumko wa bei huku sarafu yake ikiwa imeshuka kiasi ikilinganishwa na dola ya Marekani.