Katiba ya Tanzania inasemaje baada ya kujiuzulu kwa Spika?

lwambof07

JF-Expert Member
Jul 12, 2016
4,593
5,203
Baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, wiki iliyopita - akiweka historia ya kuwa wa kwanza kujiuzulu nafasi hiyo, kipyenga kimepulizwa kuashiria kuanza kwa mchakato wa kutafuta mbadala wake.

Mkutano wa Bunge ujao ulipangwa kuanza Februari mosi mwaka huu na kwa sababu Katiba ya Tanzania imeweka bayana - kupitia Ibara ya 84, kuwa hakutakuwa na shughuli yoyote ya Bunge itakayofanyika kabla ya kuwa na Spika, maana yake ni kwamba ni lazima apatikane kabla ya siku hiyo.

Tayari Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachotarajiwa kutoa Spika ajaye kimeshatangaza kuanza kwa mchakato huo ambapo kuanzia Januari 10 mwaka huu wanachama wake wenye vigezo wanaanza kuchukua fomu kwa ajili ya kupewa fursa ya kuwania nafasi hiyo.

Kwanini Ndugai amejiuzulu? na historia ikoje?
Kupanda na kushuka kwa Ndugai
Spika atakayepatikana atakuwa wa saba tangu Uhuru - akiwa ametanguliwa na Chifu Adam Sapi Mkwawa, Chifu Erasto Mang'enya, Pius Msekwa, Samuel Sitta, Anne Makinda na Job Ndugai.

Zipi ni sifa za kuwa Spika wa Bunge la Tanzania? Ni watu wa aina gani wanaweza kupewa nafasi hiyo? Uchambuzi huu - kwa kuzingatia historia ya miaka 60 iliyopita ya mhimili huo wadola, inajibu swali lako.

Katiba ya Tanzania inasemaje?
Katika Ibara ya 84, Katiba inataja sifa zifuatazo kuwa Spika; "(1) Kutakuwa na Spika wa Bunge ambaye atachaguliwa na wabunge kutoka miongoni mwa watu ambao ni wabunge au wenye sifa za kuwa wabunge; atakuwa ndiye kiongozi wa Bunge na atawakilisha Bunge katika vyombo na vikao vingine vyote nje ya Bunge".

Hii maana yake ni kuwa Spika anaweza kutoka miongoni mwa wabunge na wasio wabunge ili mradi anatimiza sifa za kikatiba. Kupata sifa za mtu anayeweza kuwa mbunge - pamoja na mambo mengine, Katiba inataja sifa kama vile kuwa mwanachama wa chama cha siasa kilichosajiliwa kisheria, kuwa na umri wa zaidi ya miaka 21, kutokuwa waziri au naibu waziri, kuwa na akili timamu na kutowahi kuhusishwa na makosa ya uhaini.

Katika historia ya Bunge la Tanzania, kumekuwa na sifa kadhaa - zisizo katika Katiba wala sheria zozote, ambazo ziliwapa maspika waliotangulia fursa ya kupata nafasi hiyo adhimu na hivyo kuongoza chombo hicho ambacho kazi zake kuu ni kutunga sheria na kuisimamia serikali.

Uzoefu bungeni
Chifu Mkwawa na mwenzake Chifu Abdieli Shangali, walikuwa Watanganyika weusi wa kwanza kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria mnamo mwaka 1947. Kwa maana hiyo, wakati Tanganyika inapata Uhuru wake mwaka 1961, Mkwawa tayari alikuwa mbunge kwa takribani miaka 14. Ndiye alikuwa mbunge wa muda mrefu zaidi kupita wengine.

Msekwa alikuwa bungeni kabla ya Uhuru akiwa Naibu Katibu wa Bunge na baadaye kuja kuwa Mbunge wa Ukerewe na wakati anachaguliwa kuwa Spika, tayari alikuwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 30 ndani ya taasisi hiyo.

Sitta na Makinda nao walikuwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 30 kama wabunge kabla ya kuchaguliwa kuwa maspika wa Bunge. Kwa sababu hiyo, hata kama haijaandikwa popote kwenye sheria, kuwa mbunge mzoefu kuna sifa ya ziada kwa yeyote anayewania nafasi hiyo.

Kuwa Naibu Spika
Historia ya Bunge la Tanzania inatuonyesha pia kwamba katika maspika sita waliotangulia, watatu kati yao walikuwa kwanza manaibu spika kabla ya kuwa maspika. Maspika hao ni Msekwa, Makinda na Ndugai. Hii maana yake ni kwamba kimahesabu, ukiwa Naibu Spika, una walau asilimia 50 ya kuwa Spika wa Bunge.

Hata hivyo, kuna uchambuzi unaoweza kubainisha kwamba huenda Naibu Spika wa Ndugai - Dk. Tulia Ackson, anaweza kuwa wa kipekee katika eneo hilo. Hii ni kwa sababu, mtangulizi wake alijiuzulu wadhifa wake - jambo ambalo halijawahi kutokea kwa wengine wote. Lakini, hesabu ni hesabu na kwa hali ilivyo, Naibu Spika ana nafasi ya asilimia 50.

Ukaribu na Rais
Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere, aliheshimiana na Mkwawa kwa sababu kwanza alimkuta bungeni na kwa sababu ya umri na wadhifa wake kama Chifu. Mbadala wa Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, hakuwa na shida kuendelea naye kwenye awamu yake.

Rais Benjamin Mkapa alikuwa akifahamiana na Msekwa kwa takribani miaka 30 kabla hajashika wadhifa kama mtu wa serikali na Sitta alikuwa karibu na Rais Jakaya Kikwete kiasi cha kuwa mmoja wa nguzo imara za kundi la "Mtandao" lililomwingiza madarakani mwaka 2005.

Kwa tafsiri hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan hasa baada ya kile kilichotokea kati yake na Ndugai, ni dhahiri kuwa hatataka kuwa na Spika ambaye hawafahamiani au walau kuheshimiana. Anaweza asiwe mtu wake wa karibu lakini atataka mtu ambaye anamfahamu vizuri.

Mazingira mahususi
Kuna nyakati ambazo Spika anapatikana kwa sababu ya mazingira yasiyo ya kawaida ya wakati huo. Chifu Mang'enya alikuwa Spika katika wakati ambao uhusiano kati ya Nyerere na Mkwawa ulilegalega na Mwalimu akaamua kuonyesha kwamba yeye ndiye Mkuu wa Nchi na Dola. Makinda alipata Uspika kwa sababu serikali ya Kikwete haikuwa imefurahishwa na namna Bunge la Samuel Sitta lilivyokuwa linaipelekesha. Ndugai alipatikana kwa sababu Rais John Magufuli hakuwa na mtu wake aliyemwandaa kuwa Spika na mbunge huyo wa Kongwa akatumia umaarufu wake na kuheshimika kwake bungeni - wakati huo, kutwaa kiti hicho.

Yapi ni mazingira mahususi wakati huu?
Kuna mambo kadhaa yanayotengeneza mazingira mahususi kwa Rais. Anaweza kutumia Uspika kutengeneza kiota chake cha kisiasa ndani ya CCM kwa kumpa nafasi mtu anayeheshimika ndani ya chama hicho au kwa kumpa mtu ambaye anatoka katika eneo au kundi lisilo rafiki kwake kisiasa wakati huu ili alitulize, ama mtu anayeweza kushughulika ipasavyo na changamoto za sasa za Bunge likiwamo suala la wabunge 19 wa viti maalumu kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) au anaweza pia kumpa mtu ambaye anaheshimika katika jamii kwa lengo la kuongeza heshima ya taasisi hiyo.

Kwa vyovyote vile, katika eneo hili la mazingira mahususi ya kisiasa, ni wazi kwamba mtu mwenye kete ya mwisho ni Rais Samia - kwa sababu atakuwa na picha ya Bunge analotaka linaloakisi mwelekeo na kasi ya urais wake na mtu ambaye atakiongoza chombo hicho katika namna hiyo.

Kuna sababu nyingine moja ambayo ni lazima itajwe kwenye michakato ya namna hii - hiyo ni ile sababu isiyojulikana. Kila wakati katika siasa, kuna kitu cha kushangaza kinachoweza kuibuka wakati wowote. Pengine, na sina hakika sana na hili, labda tunaweza kupata kitu tofauti na kile ambacho tumekizoea katika miaka 60 iliyopita ya Bunge letu.

Hata hivyo, sidhani kama hilo linaweza kutokea. Ninaamini kwamba Spika atatoka katika miongoni mwa sifa zilezile zilizotumika katika takribani miaka 60 ya Bunge la Tanzania huru.

images (1).jpg
 
Mimi nauliza, Je Naibu Spika anapotaka kugombea nafasi ya Spika inapokua wazi kama hivi sasa hua anakua ameshaachia mafasi yake ya sasa au mpaka apitishwe na chama chake?
 
Kujipendekeza kwa Rais👇😁😁😁
Taifa haliwezi kuendelea kwa mihimili kujipendekeza kwa Rais.She is hopeless fool!
 
Back
Top Bottom