Katiba, Wabunge Na Biashara Ya Ukweli!

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246


Ndugu zangu,

Kuna kisa cha kijana aliyehangaika sana kuusaka ukweli. Katika pitapita zake akaliona duka. Kibao kimeandikwa dukani ; ” Hapa tunauza ukweli”.



Dukani hapo ukweli unauzwa kwa kilo. Bei ya robo kilo ya ukweli imeandikwa, vivyo hivyo, bei ya nusu kilo ya ukweli. Lakini, mwenye duka hakuandika bei ya ukweli mzima, kwa maana ya kilo nzima ya ukweli.



Kijana yule akauliza; ” Mie nataka ukweli kilo nzima, mbona hujaandika bei?”


” Alaa, unataka kilo nzima ya ukweli?” Aliuliza mwenye duka.
” Naam” Akajibu kijana yule.
” Basi, zunguka uje ndani nikuambie bei yake”.

Alipoingia ndani dukani, kijana yule akaambiwa;


” Kijana, hatukuandika bei, maana, gharama ya ukweli mzima ni uhai wako. Je, uko tayari?”

Kijana yule akatimua mbio. Nyuma aliacha vumbi. Hakuwa tayari kulipa gharama ya ukweli mzima.


Katika Uislamu inasemwa; quljaa lhaq walahu kana muraa- sema ukweli, hata kama unauma na kwamba unaweza kupelekea umauti wako.

Yumkini ukweli utakaousema mwanadamu waweza usiwafurahishe wachache , walakini, ukawa wenye kuleta tija , furaha na matumaini kwa walio wengi.



Itakumbukwa, WaTanzania walipoonyesha furaha na matumaini yao juu ya uwezekano wa kuandikwa kwa Katiba Mpya, Waziri mwenye dhamana alitamka; Hakuna haja ya kuwa na Katiba Mpya, iliyopo inakidhi. Wenye kuzungumzia Katiba Mpya ni watu wa barabarani. Hawaijui Katiba.



Na Mwanasheria Mkuu alipoulizwa akatamka akiwa kijijini kwake; Katiba iliyopo inahitaji viraka tu. Wanaongelea Katiba wanaongea kama mabata!



Baadae tukamsikia Rais wetu Kikwete akitutamkia kuwa wakati umefika kwa WaTanzania kuwa na Katiba Mpya.


Na watendaji wa Rais akiwemo Waziri mwenye dhamana ghafla nao wakageukia kulia.

Nao wako Dodoma wakati huu wakishiriki kwa karibu mjadala wa mchakato wa Katiba. Kwenye nchi za wenzetu wangekuwa wameshajiuzuru zamani kwa kujichanganya kwa kauli kwenye suala la msingi kwa taifa kama ilivyo kwa suala la Katiba.



Mwandishi na mwanafalsafa Shaaban Robert anaandika; ” Tone dogo la maji, lile nililolidhania kuwa litakauka lenyewe mara moja, limekuwa mlizamu wakuwafariji kwa siri wanafunzi wa mshtakiwa! Mshtakiwa alikuwa akiwafunza watu, siyo kuomba msamaha na huruma katika baraza tu, lakini, hata kuzibatilisha hukumu za baraza za Kusadikika kwa njia zote. Hili lilionyesha mgogoro mkubwa sana utakuwapo kati ya sheria za nchi na watu wake” ( Shaaban Robert, Kusadikika)



Na ukweli siku zote ni mzigo mzito. Ukweli una sifa moja kuu; kwamba hata ukiuficha uvunguni mwa kitanda kwa miaka 50, iko siku, ukweli utatoka wenyewe nje hata bila kuvaa viatu. Naam, mwanadamu hupaswi kuubeba ukweli, bali kuutua na kila mmoja akauona. Si inasemwa, panapo ukweli uongo hujitenga.


Na tuwe wa kweli kwa nchi yetu. Maana, hakuna dhambi mbaya kwa mwanadamu kama kuyasaliti maslahi ya nchi uliyozaliwa. Huko ni sawa na kumsaliti mama aliyekuzaa kwa kumwangalia akiingia shimoni na kupoteza maisha ili hali ulikuwa na uwezo wa kutamka; ” Mama, shimo hilo mbele yako!’



Ni heri kuikabili gharama ya umauti kwa kuusema ukweli kwa nchi yako kuliko kuishi kwa kuisaliti nchi yako. Hilo la mwisho ni dhambi kubwa kwa mwanadamu. Nami niseme ukweli wangu; mjadala wa kuanzisha mchakato wa kupata Katiba Mpya kwa Nchi yetu ni jambo jema ambalo Rais wetu Jakaya Kikwete ameweka wazi kuwa angependa lifanyike.



Lakini, mimi ni mmoja wa WaTanzania wengi wenye mashaka na mwanzo wa safari yetu kuelekea kwenye kuitafuta Katiba Mpya kwa nchi yetu. Tumeanza na mguu mbaya. Na hilo nilishaliona na kuliandikia makala tangu mwezi Aprili mwaka huu . Ni pale Muswaada wa Sheria ya kuanzisha mchakato wa Katiba ulipofikishwa Bungeni.



Hakika, tuliyoyaona Bungeni Dodoma kuanzia Jumatatu hadi alhamisi ya leo hii yanaashiria giza nene mbele yetu. Na kwenye giza hilo kuna shimo ambalo WaTanzania tunaweza kuingia na kuangamia kama Taifa.



Naiona hatari iliyo mbele yetu.
Kuna wengi wengine wameanza kuiona. Huu ni wakati wa kutangulia busara. Ni wakati wa WaTanzania kuizunguka bendera ya nchi yetu. Ni wakati wa kuitetea nchi yetu. Tufanye hivyo ili nchi yetu isije kupelekwa kwenye maangamizi kutokana na wachache kati yetu walio tayari kufanya lolote lile kulinda maslahi yao binafsi, maslahi ya makundi yao au vyama vyao vya siasa.


Ona hili la Katiba, ni wapi tunapata tabu ya kuitafuta busara na kuukubali ukweli, kuwa hatuwezi kulazimisha mchakato uendelee huku Wananchi wengi wakionyesha kiu ya kutaka kushiriki kwa kutoa maoni yao kwenye maandalizi ya kuanza kwa mchakato wenyewe.



Kule Bungeni Dodoma tunaona haraka ya ajabu ya Wabunge wa CCM ya kutaka jambo hili kubwa la Katiba ya nchi litungiwe sheria ya kuanzisha mchakato na mchakato wenyewe uanze mara moja. Kuna kosa kubwa linataka kufanywa kule Dodoma. Linaweza kufanywa kesho Ijumaa na madhara yake yakawa ya muda mrefu na kutuacha tukiduwaa. Tutakuwa tumechelewa. Tumeshindwa kutanguliza busara.



Huu si wakati tena wa kufikiria kutunga Katiba Mpya kwa kufikiria juu ya ’Rais Ajaye’ au chama kitakachoshika madaraka 2015. Huu ni wakati wa kutunga Katiba Mpya kwa kufikiria ’ Tanzania Ijayo’ na vyama vitakavyoingia madarakani hata baada ya mwaka 2035. Inahusu mustakabali wa nchi yetu. Inahusu watoto na wajukuu zetu.



Huu si wakati wa kufikiria majina ya vyama , wagombea Urais na Katiba Mpya itakavyowasaidia kuupata Urais au mamlaka ya dola. Miaka 10 ijayo wengi wanaotajwa kuwania Urais watakuwa nje ya ulingo wa siasa. Nchi yetu itabaki pale pale. Ndoto za ving’ora na misafara visije vikawa sababu ya kutupelekea kwenye maangamizi.



Hatujachelewa, bado viongozi wa vyama vya siasa wana fursa ya kukaa pamoja kama WaTanzania na kuutafuta muafaka na hatimaye kutusaidia kama taifa katika kuufikia muafaka wa kitaifa kupitia Katiba Mpya itakayotokana na Wananchi kwa kuwashirikisha kuanzia mwanzo wa mchakato hadi mwisho.



Kwa tunavyoenenda sasa, mgogoro huu wa vyama na wabunge bungenikuhusiana na Katiba hauwezi kutoa mshindi. Sote tutashindwa kama taifa. Nahitimisha.


Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania.
Maggid Mjengwa
Iringa
Alhamisi, Novemba 17, 2011
MJENGWA - Picha, Habari & Matangazo
 
Mimi nimeisha kata tamaa!
Hakuna jinsi, tusubiri kutumbukia shimoni tu!
Hatuwezi kufika Mbinguni bila kufa kwanza
 
Hapa inabidi watanzania tuamue kusuka au kunyoa. Disko limeingiliwa na Mmasai, anacheze nje ya midundo. TUKATAE KWA KAULI MOJA.
 
Back
Top Bottom