Katiba Mpya ya Tanzania Huru !!!

Goodrich

JF-Expert Member
Jan 29, 2012
2,091
1,177
Kinadharia ni rahisi kusema kwamba Katiba iandaliwe au itokane na mawazo ya wananchi, lakini ki uhalisia, jambo hili linakuwa gumu na linahitaji jitihada za wananchi wenyewe ambao ndio hasa wenye haki hiyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wenye uwezo wa kutoa fursa hiyo wana maslahi binafsi ya kisiasa wanayotaka katiba iyalinde. Wananchi wanapaswa kujua kuwa serikali haiwezi kuwa upande wao kuhusu suala la Katiba.

Tunaona au tunashuhudua kuwa tayari kuna mtandao au kundi la watu wenye uwezo na madaraka wanaofanya kila jitihada kuifanya hoja hii muhimu iwe ya kisiasa na kupoteza maana kwa maslahi yao binafsi. Hapa Rais asipokuwa imara itapatikana katiba ya kundi fulani la watu na sio katiba ya wananchi kama inavyopasa.

Katiba huandaliwa na wananchi kupitia Bunge la Katiba ambalo sio la kisiasa na linakuwa na uwakilishi wa wananchi wa kada zote. Vyombo vingine vya dola ikiwamo Mahakama, Bunge na Serikali ni matokeo ya Katiba. Hivyo, Rais na serikali yake ni matokeo ya Katiba, na hivyo hawezi kusimamia mchakato wa kuandaa katiba.

Katiba ni ya Watanzania, ni haki ya Watanzania kuandaa katiba yao kwa namna sahihi. Lakini, kama tunavyojua, kila haki ina wajibu. Wajibu wa watanzania ni kudai haki yao ya kuandaa katiba mpya itakayozaa taifa jipya lenye heshima, demokrasia ya kweli, uwajibikaji na uchumi imara. Katiba itakayojenga hadhi ya Mtanzania na kuondoa matabaka. Wananchi wajue wazi kuwa katika suala la kuandaa katiba, kamwe serikali haiwezi kuwa upande wao.

Vema kuhakikisha kuwa utaratibu wa kuandaa katiba mpya unatuletea katiba itakayofaa kwa wakati wa sasa na kwa vizazi vijavyo. Wananchi wanataka, pamoja na mambo mengine, kwanza wapate fursa ya kuchangia muswada wa sheria ya kuandaa katiba mpya. Hatimaye, wanataka kuona katiba inayotarajiwa, pamoja na mambo mengine inahakikisha kuwa kila chombo cha dola kinawajibika.

Wananchi wanataka mchakato makini ili hatimaye katiba mpya itakayopatikana itenganishe kabisa mihimili mitatu ya dola, yaani Bunge, Mahakama na Serikali. Mihimili hii isiingiliane kwa namna yoyote ile, wala muhimili mmoja usiwe juu ya mingine kama ilivyo sasa ambapo Rais ambaye ni mkuu wa serikali, ana madaraka juu ya Bunge na Mahakama.

Hili ni la msingi kwa kuwa litaepusha mambo mengi ikiwamo wabunge kuwa mawaziri jambo ambalo linaondoa uwajibikaji wa wabunge kwa wananchi, litaepusha majaji kuwajibika kwa serikali au kuteuliwa na Rais jambo ambalo linaondoa haki. Wananchi wanataka kuona kila Chombo cha Dola (Bunge, Mahakama na Serikali) kinakuwa na mfumo wake chenyewe.

Pia, ni vema Miundo ya Bunge, Serikali na Mahakama iwekwe kwenye katiba. Hii itadhibiti mtu mmoja kuwa na nyadhifa tatu au zaidi, itaweka muundo rasmi wa baraza la mawaziri na serikali kwa ujumla, itaepusha teuzi zisizo na maana na pia itaongeza ufanisi na kuleta matokeo yenye tija. Aidha, Tume ya Uchaguzi inaweza kuwa ni idara iliyo chini ya muhimili wa Mahakama.
Aidha, wananchi wanataka mfumo bora wa Muungano. Mpaka sasa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inapingana kabisa na Katiba ya Zanzibar. Wananchi wanataka kero hizi zipatiwe ufumbuzi kupitia Katiba.

Hayo yote yatawezekana endapo tu, utaratibu wa kukusanya maoni na kuandaa katiba kwa ujumla utakuwa mzuri na kutoruhusu watu wenye nia mbaya kuingilia.

Tukumbuke kuwa siku zote wanasiasa hudhani kuwa katiba ni mali yao. Ukiangalia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 kuanzia sura ya kwanza hadi ya mwisho utaona inahusu Vyama vya siasa, Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na serikali kwa ujumla, Bunge, Mahakama, Mambo ya Uchaguzi, Muungano na mengineyo yenye kuwahusu wanasiasa. Hakuna sura inayomhusu Mtanzania kama Mwananchi ikibainisha hadhi yake, majukumu yake, haki zake, wajibu wake kama muajiri wa dola n.k. Zimetajwa haki za uraia kwa kifupi. Hali hii hujenga jamii yenye watawala na watawaliwa. Ni wakati sasa mtanzania kupewa hadhi yake katika nchi yake.

Watanzania wana haki na wajibu wa kuandaa katiba yao. Ni wajibu wa watanzania kudai haki yao ya kuandaa katiba mpya itakayozaa taifa jipya lenye heshima, demokrasia ya kweli, uwajibikaji na uchumi imara. Katiba itakayojenga hadhi ya Mtanzania na kuondoa matabaka. Wananchi wajue wazi kuwa katika suala la kuandaa katiba, kamwe serikali haiwezi kuwa upande wao. Mambo hayo yakizingatiwa tutapata serikali inayowajibika kwa wananchi, na hivyo kujenga taifa jipya lenye heshima, demokrasia ya kweli, amani, na maendeleo ya kiuchumi.
 
Back
Top Bottom