KASARANI, KENYA: Yaliyojiri Sherehe za kuapishwa Rais mteule, Uhuru Kenyatta na William Ruto

Trump2

JF-Expert Member
May 28, 2017
1,553
2,608
Kenya leo linatekeleza shughuli muhimu ya kikatiba ya kumuapisha kiongozi wa taifa hilo Kufuatia ushindi wake wa marudio ya uchaguzi wa Oktoba 26 uliosusiwa na upinzani.

Uhuru Kenyatta leo anaapishwa rasmi kuwa rais wa nchi hiyo kwa muhula wa pili baada ya kuibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu.

Wageni mbalimbali wanatarajiwa kushuhudia sherehe za kuapishwa kwa kiongozi huyo wa Kenya huku ulinzi ukiimarishwa kila kona

Uchaguzi wa uliofanyika Agosti ulifutwa na mahakama kutokana na kile kilichotajwa kuwa uchaguzi usio huru na haki.

Marudio ya uchaguzi wa Oktoba 26 ulimpatia Uhuru Kenyatta asilimia 98 ya kura huku waliojitokeza kushiriki katika shughuli hiyo wakiwa na asilimia 39

Fuatilia yanayojiri kupitia uzi huu..

======

UPDATES:


uhu4.jpg

Rais Uhuru Kenyatta akila kiapo cha Urais,kuwa rais wa awamu ya nne nchini Kenya,kwenye sherehe zilizofana kwa kiasi kikubwa ndani ya uwanja wa kasalani.

=> Rais Mstaafu, Jakaya M. Kikwete atuma salamu za pongezi kwa Uhuru Kenyatta, hata hivyo amesema hatoweza kuhudhuria kutokana na muingiliano wa majukumu..

=> Majira ya saa 4 asubuhi hii, Makamu wa Rais wa Tanzania, Samiah Suluhu Hassan amewasili nchini humo kumuwakilisha Rais John P. Magufuli.
uhu5.jpg


UPDATES: 12:20 HRS: Msajili wa mahakama ajiandaa kumlisha kiapo rais
Msajili wa Mahakama Anne Amadi amechukua usukani, ambapo anatarajiwa kumlisha kiapo rais mbele ya Jaji Mkuu David Maraga.

Anafafanua kuhusu utaratibu wa kulishwa kiapo ulivyo kwenye katiba na sheria.

UPDATES: 12:22HRS: Maraga aalikwa jukwaa la kumwapisha Rais
Bi Amadi amekaribishwa jukwaa la kumwapishia rais. Amemtambua Rais mteule Uhuru Kenyatta, huku hadhira ikishangilia. Amemtambulisha mkewe rais, Margaret, Naibu Rais mteule na mke wake William Ruto na Rachel.

Amewatambua pia wageni wengine waheshimiwa.

UPDATES: 12:24HRS: Maraga amtambulisha Rais Mteule Uhuru Kenyatta
Jaji Mkuu David Maraga amesema kwa mujibu wa Katiba na Sheria: "Mimi David Kenani Maraga, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Kenya, hapa, namtambulisha kwa watu wa Kenya Rais Mteule Mheshimiwa Uhuru Kenyatta." Hadhira inashangilia.

UPDATES: 12:27 HRS:
Rais Kenyatta ala kiapo cha utiifu
Rais Kenyatta: "Naapa kwamba nitakuwa mwaminifu, kikamilifu, kwa Jamhuri ya Kenya, kwamba nitatii, nitahifadhi, kulinda na kutetea Katiba ya Kenya kama ilivyo kwenye sheria, na sheria nyingine zote za Jamhuri. Na kwamba nitalinda mipaka na heshima ya watu wa Kenya. Ewe Mwenyezi Mungu nisaidie."

UPDATES: 12:30 HRS: Kenyatta aapishwa kutekeleza majukumu ya urais.
Msajili wa Mahakama Anne Amadi, anamlisha sasa kiapo cha kutekeleza majukumu ya Ofisi ya rais.
uhu.jpg

Uhuru Kenyatta aapishwa kuongoza Kenya kwa muhula wa pili na wa mwisho.

Rais Kenyatta: "Nitatekeleza majukumu yangu, na wajibu wangu katika afisi ya rais wa Kenya, na kwamba nitatenda haki kwa wote kwa mujibu wa katiba hii kama ilivyo kwenye sheria, na sheria za Kenya bila woga, mapendeleo au ubaguzi au nia mbaya. Ewe mwenyezi Mungu nisaidie."

Baadaye, ametia saini viapo vyote viwili, kisha cheti cha kuapishwa, kuthibitisha kwamba sherehe ya leo imefanyika.

Jaji Mkuu David Maraga pia ataweka saini yake kwenye stakabadhi zote tatu (vipao viwili) na cheti cha kuapishwa kwa Rais.

UPDATES: 12:36 HRS:
Biblia ya uhuru yatumiwa kumwapisha Uhuru Kenyatta
Mfawidhi wa sherehe amefafanua kwamba nakala ya Biblia iliyotumiwa kumwapisha Rais ni ile iliyotumiwa kumwapisha rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta ambaye ni babake rais wa sasa.

Nakala ya Katiba ni iliyotiwa saini wakati wa kurasmishwa kwa Katiba ya sasa mwaka 2010 uwanjani Uhuru Park.

Usalama umeimarishwa uwanjani Uhuru Park.

UPDATES: 12:37 HRS:
Maraga: Namtambulisha sasa Rais Wakenya
Jaji Mkuu Maraga: "Wananchi, sasa ni furaha yangu kuu kumtambulisha kwenu Rais wa Jamhuri ya Kenya."

UPDATES: 12:38 HRS:
Maraga amtambulisha Naibu Rais Mteule
Jaji Mkuu David Maraga sasa anamtambulisha Rais Mteule William Ruto ambaye pia atalishwa kiapo cha utiifu na kiapo cha kuhudumu kama Naibu Rais wa Kenya.

UPDATES: 12:50 HRS: Maraga amtambulisha Naibu Rais Ruto
Baada ya Bw Ruto kula kiapo na kutia saini hati za kiapo, Jaji Mkuu amemtambulisha kama Naibu Rais kwa wananchi Kasarani.

UPDATES: 12:52 HRS:
uhu3.jpg

Sherehe rasmi ya kumuapisha rais yakamilika. Msajili wa mahakama Anne Amadi ametangaza kwamba sasa sherehe rasmi ya kumuapisha Rais na Naibu wake imekamilika. Maafisa wakuu wa mahakama na Rais na Naibu wake wamepigwa picha ya Pamoja.

Sehemu inayofuata ya sherehe, ambayo ni burudani na hotuba sasa inaanza.

Rais Uhuru Kenyatta akihutubia taifa baada ya kuapishwa. Awashukuru wakenya wote waliompigia kura na kusema kuwa atakuwa rais wa wote.

"Tutaendelea kuimarisha uhusiano wetu kiuchumi. Kila mwafrika atakayetembelea Kenya atapata Visa anapoingilia, na hii ni kwa ajili ya kuikuza Afrika"

Mizinga 21 imefyatuliwa pia kwa heshima ya Rais.

Kenya Baada yakumaliza hotuba yake, Rais Uhuru Kenyatta awaongoza wakenya kuliombea Taifa kwa lugha ya kiingereza huku Naibu wa Rais, William Ruto akiomba kwa lugha ya kiswahili.

======

Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto wameapishwa katika uwanja wa kitaifa wa Safaricom Kasarani, jijini Nairobi.
RAIS Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto wameapishwa katika uwanja wa kitaifa wa Safaricom Kasarani, jijini Nairobi.

Jaji Mkuu David Maraga na msajili wa mahakama Bi Anne Amadi ndio wameongoza idara hiyo kulisha Rais Kenyatta na Naibu wake Ruto kiapo.

Baada ya kuapishwa Rais aidha ameahidi kuheshimu katiba ili kuendesha taifa hili mbele, la muhimu akitilia mkazo umuhimu wa amani nchuni na kuleta jamii zote pamoja. "Tumeapa kuheshimu matabaka yetu, dini, mila na katiba kwa jumla. Lazima tuishi kwa amadi kama vile tumeapa kuhakikisha imedumu nchini," amasema Bw Kenyatta.
Amedokeza kwamba yeye kama Rais atahakikisha ametekeleza majukumu yake kama kiongozi wa taifa.

Rais Kenyatta aidha amemtaka kila Mkenya kuheshimu katiba na endapo ana malalamishi yoyote atumie mkondo wa sheria kueleza ila si kwa kuvuruga amani ya taifa.
Hali kadhalika, Rais amewashauri watumishi wa umma kufanya kazi kwa mujibu wa katiba.

"Lazima kila mtu afanye kazi yake kulingana na katiba, kwa kufanya hivyo tutaweza kuafikia ndoto na sera zetu kwa wananchi," ameeleza.

Hata hivyo, ameonya kuwa hataruhusu yeyote kuvuruga amani akiwa mamlakani kama rais. "Hakuna atakayeruhusiwa kuharibu taifa hili lenye zaidi ya wananchi milioni 45. Tuishi kama ndugu na dada, jirani yako umheshimu na muishi kwa amani," amesema.
Hafla hiyo imehudhuriwa na zaidi ya wajumbe 100,000 kutoka hapa nchini na kitaifa. Aidha zaidi ya marais 10 kutoka barani Afrika, na viongozi kadha madhuhuri kutoka sehemu mbalimbali za dunia pia wamehudhuria.

Aidha Rais Kenyatta amesema kwamba taasisi hizo hazitaweza kufanya kazi iwapo zitaendelea 'kushambuliwa' na wanasiasa. "Taasisi kama vile za usalama, mahakama na za uchaguzi zimetatizwa utendakazi wake na joto la kisiasa. Tuzipe nafasi zifanye majukumu yake," akasema Rais.

Idara ya mahakama na tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka (IEBC) kwa kipindi cha miezi minne iliyopita, zimekuwa zikipitia wakati mgumu kutokana na uchaguzi mkuu wa Agosti 8 na marudio ya urais ya Oktoba 26.

Septemba 1 mahakama ya juu iliharamisha ushindi wa Rais Kenyatta na Naibu wake Ruto waliotetea nyadhifa zao kwa tiketi ya Jubilee, baada ya muungano wa National Super Alliance (Nasa) kuupinga katika mahakama hiyo.

IEBC iliagizwa kuandaa uchaguzi mpya, ambao ulifanyika Oktoba 26. Hata hivyo, uamuzi huo wa mahakama ulikashifiwa na wanasiasa wa Jubilee akiwamo Rais Kenyatta na Ruto. Nasa inayoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga imekuwa ikishinikiza marekebisho yafanyike katika IEBC, ikiwa ni pamoja na kutaka makamishna kadha wafurushwe tumeni.

Mkurugenzi wa IEBC Ezra Chiloba alilengwa na Nasa ikimtaka ajiuzulu. Bw Chiloba alilazimika kuchukua likizo ya lazima kabla ya Oktoba 26, ili kuruhusu uchaguzi ufanyike. Hata hivyo, Nasa ilisema aliacha kama 'amepanga' uchaguzi kabla ya likizo yake ya wiki tatu.

IEBC inaongozwa na mwenyekiti wake Bw Wafula Chebukati.
Bw Raila aidha alijiondoa kushiriki uchaguzi huo. Rais Kenyatta kwenye hotuba yake amesema kila taasisi inafaa kupewa mwanya wa kuimarika kufanya kazi. "Taasisi hizo zisipofanya kazi kwa matumaini yetu, tuzipe muda zijirekebisha na kuendelea na kazi. Tuwache kuzipa presha, tusiziharibu kamwe," akaeleza.

Bw David Maraga ndiye 'rais' wa idara ya mahakama, na ndiye ameongoza idara hiyo kumuapisha Rais Kenyatta na Naibu wake Ruto.

Rais aidha ameahidi kushirikiana na idara ya mahakama ili kuimarisha utendakazi wake. Bw Kenyatta amesema anajaribu kila awezalo kuleta pamoja viongozi wa mirengo mbalimbali ya kisiasa nchini. "Nimeshaanza harakati za kuleta pamoja viongozi wa kisiasa ili tufanye kazi kwa ushirikano," akasema.

Pia Rais Kenyatta ametangaza afueni ya ada ya stima inayotozwa watengenezaji bidhaa. Kiongozi wa taifa amesema bili imepunguzwa kwa asilimia 50 kati ya saa nne usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi.

Kubatilisha ushindi
Bila shaka, wakati Jaji Mkuu, David Kenani Maraga na majaji watatu walipobatilisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta mnamo Septemba Mosi, kulishuhudiwa hasira miongoni mwa wafuasi wake.

Rais alikuwa am,etawazwa mshindi na tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) ikiongozwa na mwenyekiti wake, Wafula Chebukati kufuatia ujumlishaji wa kura za Agosti 8, 2017.

Maraga, Jaji Isaac Lenaola, Smokin Wanjala na Naibu Jaji Mkuu, Philomena Mwilu wakaubatilisha baada ya mrengo wa National Super Alliance kuwasilisha mahakamani kesi ya kupinga ushindi huo.

Rais mwenyewe na Naibu wake, William Ruto hawakuchelea katika siku chache zilizofuatia kukashifu uamuzi huo, hata ashakum si matusi majaji hao kupewa majina ya 'kuwadunisha'.

Ingawa hivyo, onyo hapa na pale kutoka kwa wadau mbalimbali walioonya kuwa kushambulia mahakama hiyo na majaji wake hakufai, walilegeza kamba ya kauli hasi.
Katika hafla ya kuapishwa kwa UhuRuto Jumanne, wafuasi wao waliokuwa wamejaa katika uwanja huo walimshangilia Jaji Mkuu, David Maraga bila kuonyesha hali yoyote ya kuwa na kijiba naye.

Alipoalikwa na msajili Mkuu wa Mahakama, Anne Amadi kushuhudia UhuRuto wakiapishwa, wafuasi hao walishangilia bila kuonyesha uhasama wowote na hata wengine wakasimama juu kumpungia mikono yao, hali iliyompa tabasamu ya dhati Jaji Maraga.
Katika hotuba za Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake, William Ruto, kila mara ambapo walitaja jina “Jaji Mkuu na Idara ya Mahakama”, wafuasi hao walikuwa wakishangilia kwa dhati.

Ni hali ambayo ilitoa ukweli halisi wa Wakenya kuwa leo kunaweza zuka tofauti kuhusu lolote lile, lakini kesho yake wako tayari kusahau tofauti hizo, wasameheane na wasonge mbele na maisha yao.

Chanzo: Swahilihub
 
Acha akasafishe macho ajifunze kwa wengine namna viongozi wanavyoheshimu demokrasia na mawazo ya wengine.
 
Aje tu lakini atakapoingia uwanja wa Kasarani awe tayari kusikia umati umeanza kumzomea. Leo ndo atawafahamu Nyang'au vizuri.
 
Wacha aingie London ya kipikee South of the Sahara, North of the Limpopo.
 
Fuatilia live kupitia CITIZEN TV, KBC TV, KTN TV.
Rais wa Jamhuri ya Muungano. Wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli atahudhuria sherehe hizo.Tumtakie safari njema Rais wetu mpendwa.
Atakuja na wazo jipya atelist
 
Back
Top Bottom