KARMA - Kidamali: Wewe Mwenyewe Ndiye

Je, bado nina haki ya kumchukia mama Maila ama niwe mpole kama mfalme Daudi?

  • Una haki ya kumchukia (we all have a past lakini alichokifanya sicho)

  • Unavuna ulichopanda (It's Karma!)

  • Nipo katikati (Matukio hayana uhusiano kwangu; so reaction zote mbili naziona justified)

  • Sijui (bado sijaamini kilichotokea, nimeshindwa kutafakari, ...)


Results are only viewable after voting.

Mentor

JF-Expert Member
Oct 14, 2008
20,328
23,879
KARMA - Kidamali: Wewe Mwenyewe Ndiye

Ilifika mahali sikuogopa tena kuuliza ni kiasi gani walichohitaji kuhakikisha mipango yangu inakamilika. Hali ilikuwa mbaya kiasi hicho. Rushwa haikuwa siri tena. Asiyetoa kitu kidogo alikuwa mkosaji na aliyerefusha mkono wake japo kidogo alionekana sahihi na kupata huduma haraka na kwa ukarimu wote. Ndivyo nilivyoweza kuukuza mtaji wangu. Katika mizigo niliyokuwa nikiingiza nchini ni nusu tu ya mizigo hiyo ndiyo ilikuwa imelipiwa ushuru. Nusu nyingine haikuhesabiwa. Nilikuwa mkarimu kwa kutenga kabisa kiasi cha fedha kwa ajili ya kila mhusika. Kuanzia mamlaka ya mapato, polisi hadi kwa mtumiaji wa mwisho. Sikusubiri kusimamishwa njiani ndipo nianze kupiga simu kwa wahusika. Nilihakikisha taarifa zangu zimefika muda kabla ya mizigo yangu kupita. Wakati huu, wasafirishaji wakubwa tulikuwa wachache. Kutokana na kuwa mtoaji mzuri niliweza kupanua biashara zangu. Kila mkoa uliokuwa na mpaka na nchi nyingine basi nilikuwa na ofisi hapo.

2015
Nikiwa na umri wa miaka 34 nilifikia maamuzi ya kufunga ndoa. Nilitamani nami niwe na mtu wa damu yangu wa kuja kurithi na kuendeleza mali hizi. Nilikuwa nimepunguza kwa kiasi kikubwa biashara za magendo. Nilijua nisingeweza kufanya hivyo kwa muda mrefu hivyo niligawanya biashara zangu katika makundi mawili. Biashara moja ilikuwa ya halali kabisa huku nikilipa kodi zote stahiki ingawa kwa kuwa hali ya rushwa ilikuwa imekithiri haikuwa na faida yoyote. Hivyo, biashara hii ya pili ndiyo ilikuwa inanipa faida ya kuweza kuishi mjini. Lakini pia, nilitaka kutulia sehemu moja nisiwe nasafiri kila wakati. Niliyatamani maisha hayo. Ndani ya wiki moja ninaweza kuwa nimetoka Mtwara na kukatiza mikoa ya kati yote na kujikuta nipo Mwanza. Huo ndio ulikuwa mwenendo wa maisha yangu.

Haikuwa kazi rahisi kuamua ni nani hasa angefaa kuwa mwenza wangu wa maisha maana kutokana na kutokuwa na makazi maalumu, sikuwa na marafiki wa kudumu. Ni kweli, maisha yangu yalinikutanisha na mabinti wa aina nyingi; wazuri, wakubwa kwa wadogo, lakini wote hao niliishia kuwatumia tu na kuwaacha. Sikuwaza kama kuna siku nitapata hamasa ya kutaka kuoa achilia mbali kuwa na familia na watoto. Niliyaona maisha kwa lensi ya ujana. Kwa kweli, pesa iliongea. Nilijua hakuna siku nitakosa mwanamke wa kunituliza moyo nitakapomhitaji na ndivyo ilivyokuwa. Sijui ni mkoa gani sikuwa na wanawake si chini ya watano ambao muda wowote nitakaofika ningeweza kupiga simu na tukaonana. Na, ni wa kada zote; wahudumu wa bar, wanafunzi wa vyuo, hadi wafanyakazi serikalini, benki na wenye biashara zao binafsi.

Hata hivyo nilifurahi kuwa walau nimepata msukumo mwenyewe kutoka moyoni wa kutaka kuwa na familia. Wazazi waliniuliza uliza wakati nimetimiza miaka 30 hivi ila baada ya muda nao waliacha kuniuliza. Walijua sasa wajukuu watawapata kutoka kwa ndugu zangu tu, kwangu walishakata tamaa. Pili, waliwaambia ndugu zangu nao wasiendelee kuniuliza wakiogopa nisije kuoa kwa kusukumwa kisha nikafanya chaguzi mbaya.

Suala la kumpata binti sahihi halikuwa rahisi maana sikuwa na binti niliyekuwa na mahusiano ya maana naye. Ila baada ya muda nilifanikiwa. Kumpata kwake ni mkasa tosha nitakaoulezea wakati mwingine. Tulifunga ndoa na kuianza safari hii pamoja.

Miaka miwili baadaye…
Ndoa! Ndoa! Ndoa! Maisha ya ndoa yana changamoto nyingi kwa kweli. Unaweza kujiandaa kwa mengi kabla ya ndoa lakini ukaja kukutana na mapya na mageni kabisa. Nilijiamini kuwa kutokana na umri wangu na uzoefu wangu nisingepata shida katika ndoa. Niliamini pia kuwa nimejijenga vya kutosha kifedha hivyo suala la mahitaji ya kifedha lisingelikuwa tatizo kabisa kwetu. Zaidi nilijiamini kuwa, katika sekta muhimu ile, nisingepata changamoto yoyote kwani nina uzoefu wa miaka nenda rudi. Kwa hakika nilikuwa nimejidhatiti.

Miaka miwili hii ilikatika bila changamoto kubwa zozote. Mengi yalikuwa ya kawaida na yaliweza kutatulika, na hapa ndipo nilipojipa kichwa kuwa nilikuwa nimejiandaa vyema. Sikujuta kuchelewa kuoa kama ambavyo jamii ilitaka kuniaminisha. Mke wangu alikuwa akimalizia masomo yake ya uzamili na kwa kuwa tulikwisha liongea hata kabla ya ndoa, tulikubaliana kuwa tusubiri hadi amalize shule kabla ya kutafuta mtoto.

Siku moja nilishtuka usingizini baada ya kusikia sauti bafuni. Mke wangu hakuwa kitandani nami. Baada ya kusikiliza kwa makini nikagundua ni yeye yupo bafuni na alikuwa akitapika. Niliamka ghafla na kwenda kumuangalia. Alisema alijisikia kichefuchefu. Kichwani kwangu kengele ya hatari ikalia. Ilikuwa imetimia miezi sita sasa tangu amalize shule hivyo siku yoyote tulitegemea hali kama hiyo. Sikutaka kuendekeza wazo hilo nikaharakisha kwanza kumpa huduma ya kwanza na kumpa maji ya kusukutua. Hakutumia dawa yoyote maana baada ya hapo alisema anajisikia vyema na huenda ni chakula tu kilikataa. Tulirudi chumbani na kuendelea na usingizi. Huenda naye alikuwa na wazo kama langu lakini hakuna mmoja wetu aliyetaka kusema kwanza. Na sikutaka kujiaminisha sana maana kweli alitapika chakula chote tulichokula usiku. Sikupata usingizi kwa muda nikaanza kufikiria ambavyo mtoto wetu atakuwa. Nilipanga kumpa mema yote ya nchi. Tulishapanga na jina la mtoto. Saa ya ukutani ililia kuashiria ni saa tisa usiku. Sikuwa na hofu ya kuchelewa kuamka kwa kuwa sikupanga hata kwenda kwenye miradi yangu hadi saa nne hivi. Kwa furaha niliyokuwa nayo nikajisemea hata gym kesho sitokwenda. Raha ya kuwa bosi wako mwenyewe. Niliwaza kama akiniambia ni mjamzito kweli tutakwenda safari Zimbabwe kuyaona maporomoko ya Victoria. Alitamani kwenda huko siku nyingi. Naam, lazima nimpeleke huko. Ghafla saa ikalia tena, saa kumi usiku. Nikajiambia, ‘sasa inakubidi ulale bosi’. Nikatabasamu moyoni na kupotelea usingizini.

Saa tatu asubuhi nilishtuka usingizini nikiwa nimebanwa na haja ndogo. Nakumbuka niliisikia tangu nikiwa kwenye dimbwi langu la mawazo usiku lakini nikaona uvivu kuamka tena. Nilipatwa na maumivu makali wakati wa kujisaidia. Baada ya tafakuri ya haraka nikagundua kuwa sikuwa nimekunywa maji ya kutosha siku iliyotangulia na nilikuwa nimeubana mkojo kwa muda mrefu hivyo nikajisemea hili litapita. Niliamka na furaha sana na sikutaka hali ile inikoseshe amani. Mke wangu alikuwa ameshaondoka kuelekea kazini. Nilijiandaa haraka haraka kuelekea kwenye kikao cha saa nne na kabla sijaondoka nilikwenda tena kujisaidia na maumivu yale yalijirudia. Niliishia kujishauri kuwa siku nyingine nisirudie kubana mkojo kwa muda mrefu vile kisha nikaondoka.

Masaa machache baadaye nilikuwa ofisi ya daktari nikimuelezea ambavyo maumivu yangu yalianza kimzaha mzaha asubuhi ile na mpaka sasa hayajapungua. Nilifanyiwa vipimo vya UTI na kukutwa safi. Daktari akaniambia anipime na STD ila nilitaka kukataa maana kwa hakika baada ya ndoa yangu, sijawahi kuwa na mahusiano ya nje. Hata hivyo baada ya ushawishi nilikubaliana naye kishingo upande. Majibu yalikuja kuwa niko safi pia. Daktari alinipatia antibiotics (mpaka leo sijui kwa nini alinipa antibiotics ilhali hakukuta tatizo lolote) na vidonge vya AZO kusaidia kupunguza maumivu huku akiniambia baada ya kumaliza dozi niache hivyo vidonge na mamumivu yakirudi basi nirudi hospitali. Nilirudi nyumbani na kuendelea na maisha. Mke wangu aliniambia anajisikia vyema na hajatapika tena. Sijui kwa nini, ila niliogopa kumuuliza kupima ujauzito maaana tulikuwa tunategemea hilo muda wowote. Nilikaa kimya nami nikiendelea na dozi zangu bila kumuambia kilichonitokea asubuhi. Sikutaka kuharibu furaha yetu.

Wiki mbili baadaye, nilirudi nyumbani nikiwa na huzuni sana. Nilikaa kwenye kochi huku nikisubiri mke wangu arejee. Nilikuwa kwenye hali ambayo yeye tu ndiye angeweza kunipa neno la tumaini, neno la kunifanya niitamani kesho. Alirejea nyumbani na tabasamu. Nililiona tangu alipofungua mlango maana nilikuwa nimekaa kwenye kochi ambalo akiingia tu, ni lazima nitamuona.

Mke: “baby, baby….I got news for you...” (aliongea na tabasamu kubwa usoni)

Kichwani kwangu nilikuwa nimeshajiandaa na speech yangu kuwa “I need to tell you something” hivyo sentensi yake ilinichanganya kabisa. Alianza kusakura kwenye pochi yake kama atafutaye kitu. Alitoka na kikaratasi na kunikabidhi. Alikuwa na ujauzito. Nilihisi kama jiwe kubwa limetuliwa begani mwangu. Nilinyanyuka nikamkumbatia na kushindwa kujizuia, nikalia machozi kama mtoto mdogo. Naikumbuka ile siku kama jana. Nakumbuka ambavyo alishtushwa na ‘reaction’ yangu maana alitegemea ningefurahi. Lakini machozi yangu yalikuwa ya furaha pia. Ni furaha iliyofunika huzuni iliyonitawala awali.

Baada ya kutulia nilimuomba akae chini nami nimueleze yaliyonikuta siku hiyo. Baada ya kumaliza dozi zangu na kuacha kutumia dawa zile za maumivu, bado maumivu wakati wa kujisaidia hayakuisha. Nilikuwa nimerejea hospitali kwa ushauri zaidi. Baada ya vipimo, daktari aliniambia kuwa siku ile walifanya testing ya mkojo tu ila walihitaji kufanya culture kwa uchunguzi zaidi. Leo nilienda kupewa majibu. Majibu yaliyonesha kuwa kulikuwa na chembechembe za ugonjwa ambao haukutibiwa wote hapo awali. Nilikiri kuwa hapo nyuma niliwahi kupata maambukizi ya kaswende (sijui ndo chlamydia?) lakini nilimhakikishia kuwa nilitumia dawa na nilipona kabisa. Daktari aliniambia huenda ukawa umeniathiri zaidi ya walivyoona lakini hakutaka kunipima wakati huo. Aliniandikia dawa na kunitaka kurudi baada ya miezi miwili hivi kwa vipimo zaidi. Aliniambia nisiwe na wasiwasi na ulivyonipa habari hizi basi nimesikia amani kugundua kuwa sijaathirika kiasi cha kuharibu mfumo wangu wa uzazi. Nisamehe mke wangu kwa kutokukueleza haya tokea mwanzoni. Hata hili la huu ugonjwa ni jambo lililonikuta kabla hatujafahamiana na niliona nikufiche kwani sikutegemea kama lingekuja kujitokeza mbeleni. Nilimueleza sababu ya mimi kulia ni mchanganyiko wa hofu ya majibu niliyopewa kwa kuwa sikujua ni kwa kiasi gani ugonjwa ule uliniathiri na furaha ya kugundua kuwa una ujauzito wangu.

Nilimuomba msamaha kwa kutokumueleza yote hayo awali na hasa hilo la ugonjwa maana sikumbuki hata ilikuwa wakati gani, ila kwa vyovyote vile ilikuwa kabla hatujakutana. Alinisamehe na tukahamia kwenye kufurahia suala la ujauzito. Nilimshukuru Mungu kwa yaliyotokea hata sikuweza kufikiri kukasirika kwa aibu iliyonikuta ama kwa maelezo ambayo daktari aliniambia kuwa huenda nisingeweza kuzalisha tena. Tuliendelea kuzungumza siku hadi siku juu ya yaliyotokea na kurudi katika hali ya kawaida. Ulikuwa wakati mgumu lakini tuliuvuka vyema na ujauzito uliendelea kukua.

2018
Sitaki kumuona huyo malaya, mhuni hapa kwangu! Naapa nitamuua..I hate her!” Naam, nakumbuka nikiyatamka maneno hayo kwa hasira. Ni mke wangu. Nilijihisi kudhalilishwa kwa hali ya juu. Alijifungua mwezi Disemba mwaka jana. Mtoto mzuri wa kike na tukamuita Maila. Mtoto alifanana na mama yake kila kitu. Yani ilifika mpaka kuanza kufananisha kisigino walau kutafuta ufanano na mimi. Nilijipa moyo kuwa kama kachukua mwili kwa mama, basi atachukua akili kwa baba. Nilikuwa na furaha isiyo kifani.

2018 March
Furaha yangu haikuchukua muda mrefu kukatishwa. Wahenga walisema, “hakuna msiba usiokuwa na mwenzake.” Sijapata kukutana na mwanamke katili namna hii duniani. Ama kweli nimefika mahali nimeamini wanaowasema vibaya viumbe hawa wana haki hiyo. Viumbe wasiojua wakitakacho. Nilitamani kumuondoa katika dunia hii kwa alilonitendea. Hata wewe msomaji wangu naamini utakubaliana nami kuwa kwa alilofanya, hakustahili kuishi hata siku moja ya ziada. Kwa lipi hasa alilokosa kwangu? Alikuwa na kila kitu. Nilihakikisha anapata kila kilichokuwa ndani ya uwezo wangu. Kwenda kwake kazini ilikuwa tu kama hobby. Alipenda alichokuwa akifanya nami sikuona sababu ya kumzuia kisa tu nina pesa za kumtunza. Sikutaka pia kumlazimisha kuingia kwenye biashara zangu. Nilimuahidi wakati tunafunga ndoa kuwa nitamsapoti kwa ndoto zake zozote alizonazo na sitomlazimisha kufanya asichotaka kukifanya kisa tu ni ndoto yangu. Kuwa, kuolewa na mimi isiwe sababu ya yeye kuua ndoto zake. Niliahidi kutekeleza ahadi hiyo siku zote za uhai wangu na ndoa yetu. Lakini kama wasemavyo, wao wenyewe hawajui wakitakacho. Women!

Nitakueleza alichonifanyia kabla hujaaanza kunisema kwa kumhukumu vibaya. Msiba wa kwanza; Maila hakuwa binti yangu! Naumia hata sasa kuyaandika haya. Nashindwa kujua wapi nilipokosea. Nimefika mahali nikatamani hata nisingelijua hili, nimlee tu mtoto kama wa kwangu. Lakini ndiyo nimeshajua. Sioni tena umuhimu wa kuendelea kuishi na kutafuta mali. Vya kazi gani tena. Ili nani aje kuvifaidi?

Naam, msiba wa pili. Baada ya uchunguzi zaidi wa hali yangu, iligundulika kuwa nilikuwa na uvimbe ambao walikuja kugundua ni kansa. Daktari wangu aliniambia kuwa ni mara chache sana hali kama hii kuwatokea wanaume maana sisi magonjwa ya zinaa yakitukumba hupatwa na dalili mapema mno. Na kama tukitumia dawa bila ugonjwa kwisha, bado dalili zitajitokeza tena. Zaidi sana, athari za ugonjwa huu kufikia hatua mbaya ya kuathiri via vya uzazi ni ndogo sana kwa wanaume (mara nyingi kwa wanawake ambao hawajatibu ugonjwa huu hupelekea kupatwa Pelvic Inflammatory Disease ambayo huweza kuzuia kabisa uwezo wake wa kushika mimba). Nilimshukuru Mungu kuwa wakati ninaanza matibabu mke wangu alikuwa mja mzito hivyo hata kama mionzi ile itaniathiri basi walau Mungu amekuwa mwema kwangu akanijaalia kupata mtoto mmoja wa damu yangu, kutoka viunoni mwangu. Nilishukuru kwa neema ile, na ninaiita neema, kwa kuwa sikuistahili na niliona ni mavuno ya matendo yangu ya zamani. Ninaapa kabisa, tangu nimpate mama Malia, sikuwahi kutokuwa mwaminifu katika ndoa yangu hivyo sikutegemea madhambi yangu ya nyuma kuja kunifuata huku. Ila sasa, mtoto si wangu. Nilimchukia sana mama Maila. Nimeangalia yote mema niliyomfanyia, nimeangalia jinsi nilivyobadilika na kuwa mume mwema tangu tuoane na sijaona sababu ya mimi kuyapitia haya.

2018 April 08, Jumapili Ibadani...
Na Mungu akamtuma Nathani kwa Daudi. Basi akaja, akaingia kwake na kumwambia: “Palikuwa na wanaume wawili waliokuwa katika jiji moja, mmoja alikuwa tajiri na yule mwingine alikuwa maskini. Yule mwanamume tajiri alikuwa na kondoo na ng’ombe wengi sana; lakini yule mwanamume maskini hakuwa na chochote isipokuwa mwana-kondoo jike mmoja, aliye mdogo, ambaye alikuwa amenunua. Naye alikuwa akimhifadhi hai, na huyo kondoo alikuwa akikua pamoja naye na wanawe, wote pamoja. Kondoo huyo alikuwa akila tonge lake, na kunywa kutoka katika kikombe chake, naye alikuwa akilala kifuani pake, na kondoo huyo akawa kama binti kwake. Baada ya muda, mgeni akaja kwa yule mwanamume tajiri, lakini hakuchukua kutoka kati ya kondoo zake na ng’ombe zake ili kumwandalia yule msafiri aliyekuja kwake. Kwa hiyo akachukua yule mwana-kondoo jike wa yule mwanamume maskini, akamwandalia yule mtu aliyekuja kwake.”

Ndipo hasira ya Daudi ikamwakia sana yule mwanamume, naye akamwambia Nathani: “Kama Mungu anavyoishi, mtu huyo aliyefanya hivyo anastahili kufa! Na kuhusu yule mwana-kondoo jike, atamlipa mara nne, kwa sababu yeye amefanya jambo hili na kwa sababu hakuwa na huruma.

Nikiwa katika hali ya kufadhaishwa, aibu, hasira nilienda kanisani Jumapili hii. Kwa kweli tangu mwezi jana nimekuwa na hasira na Mungu kwa nini ayaruhusu haya yanipate mimi. Nimejiuliza ni kosa gani nilimfanyia binti huyu hadi Mungu kuruhusu haya yanifike mimi. Hata kwenye biashara yangu, nilikuwa nimeachana kabisa na magendo na kama ni rushwa basi sikuhusika moja kwa moja. Ni ngumu kuendesha biashara bila rushwa. Kama si kodi zisizo na mantiki basi utawekewa vikwazo vya kiutendaji. Kwa vyovyote vile utafanyiwa figisu ambazo kwa nje mtu mwingine ataona ni utendaji wa kawaida lakini kwa ndani, kwa yule mfanyabiashara, ndiye anayejua nini hasa kinachoendelea. Hata hivyo ni kwa kiasi kikubwa nilikuwa nimeweza kujiepusha na hayo. Ni nini basi nilichokosea kustahili fedheha hii? Kwa nini Mungu kaamua kuniadhibu mara mbili, hata yule niliyedhani atanifuta machozi leo ninaambiwa si wangu. Nilijihisi kama maskini aliyenyang’anywa kondoo wake na nilitamani kama walau kwa siku moja ningekuwa na mamlaka ya mfalme Daudi, niliona hukumu aliyostahili mke wangu ni kifo tu. Nilikuwa nimemkasirikia Mungu. Ndiyo nilikubaliana na aya ya mwisho ya neno lililokuwa linasomwa, “...mtu huyo anastahili kufa!

2012, Kidamali Iringa
Mentor: “Ayayayaya! Unaona ninachokiona lakini?” Niliongea huku nikimgusa mwenzangu kuangalia upande niliokuwa nikiuangalia.

Rumbete: “Ah! Ah! Ah! Mangi acha achia hapo hapo. Miaka 30 itakuhusu.

Mentor: “What!?? Yani ule mzigo wote bado ni under 18?

Tulikuwa tumefikia Kidamali katika shughuli zetu za biashara. Sijui siku hizi, enzi hizo Kidamali ilikuwa kakijiji kadogo tu huko mkoani Iringa. Kwa sasa nadhani kipo ndani ya jimbo la Kalenga. Hata sasa nakumbuka kanisa lile la Orthodox, sijui lilijengwa mwaka gani. Ni hapa nilipomuona binti huyu, akiwa amevaa sketi nyeusi ya marinda na kubeba ndoo ya unga kichwani akitokea mashine. Rumbete alikuwa mwakilishi wa kampuni yangu mkoani Iringa hivyo wakati wote ninapokuwa Iringa ilikuwa sina budi kusafiri naye. Rumbete ndiye aliyenionya kuwa binti yule pamoja na umbo lake lile alikuwa mwanafunzi wa kidato cha nne tu na ndiyo kwanza alikuwa ametimiza miaka 17. ‘Ama hakika watoto wa siku hizi wanakua haraka,’ nilijisemea moyoni huku nikiendelea kummezea mate. Wakati huo yupo kijijini, amevaa nguo zilizofubaa tu na bado hajakomaa vya kutosha lakini anavutia vile. Pamoja na kwamba baada ya pale sikumueleza tena Rumbete lakini moyoni niliendelea kummezea mate.

Tulirudi Kalenga jioni ila akili yangu ya kipuuzi na kihuni haikutulia. Ilitaka kumfahamu binti yule. Niliwasha gari na kurudi Kidamali kesho yake jioni kwenda kumsaka. Haikunichukua muda kufahamu binti yule anapoishi baada ya kuwauliza watoto waliokuwa wanacheza pale. Nilimpa mtoto mmoja shilingi mia na kumuambia akamuite aje dukani. Kwa kuwa kulikuwa kumeshaingia kagiza niliweza kujificha nisionekane na watu wengi. Nilikuwa nimeshaongea na muuza duka pale na ingawa alijua lengo langu ni ovu, niliweza kumnyamazisha kwa fedha kidogo. Baada ya binti kufika ilinichukua muda kumshawishi hata kunisikiliza lakini nilitumia udhaifu wa dhiki zake kumshawishi. Nilimueleza kuwa ningerudi kesho yake nimchukue twende Iringa mjini nikamnunulie nguo nzuri na mahitaji yake mengine. Nilimuachia elfu kumi, fedha ambayo tangu azaliwe hakuwa amewahi kuimiliki. Nilijua nimeshaweza kumteka. Tatizo la kutoroka kwao halikuwa kubwa kwani siku iliyofuata ilikuwa siku ya shule. Tulikuwa tumeshazungumza mahali pa kumkuta na kama ilivyokuwa nilimkuta. Sitaki kukumbuka sana maana ninapatwa na aibu.

Binti wa watu alikuwa amejitunza na yuko bize na maisha yao ya dhiki akijitahidi kufanya bidii shuleni lakini tamaa zangu zilikuwa zikikaribia kumfutia ndoto za maisha mema na kumhukumu katika umasikini wa kudumu. Sikuliona hilo kwa wakati huo. Nilifurahi kuokota dhahabu Kidamali, Iringa. Nilimuona tena kama mara mbili au tatu zaidi na miezi miwili baadaye niliporudi pale aliniambia anajihisi ni mja mzito. Hapo ndipo nilipoiona miaka 30 ikinitazama. Nilimtafutia vidonge lakini havikusaidia chochote. Binti ilimbidi kusema kwao kuwa ana ujauzito. Mtoto pekee kwa mama yake. Baba yake alikuwa mpita njia kama mimi na hajulikani. Mama yake alikuwa akijitahidi kulima kumsomesha binti yake. Alitishia kwenda kushitaki kwa mtendaji wa kijiji lakini wote hao niliwafumba midomo kwa fedha. Nilimdanganya mama yake kuwa nitawahudumia kama asiponishitaki polisi. Nilimuambia nikifungwa mimi basi hata wao maisha yao yataharibika. Kwa kutumia dhiki ile ile nilifanikiwa kumnyamazisha mama yake pia. Niliwatumia fedha japo kwa siri kubwa maana mimi mwenyewe niliona aibu kwa nilichokifanya. Sikutaka mtu yeyote afahamu kwani sikutaka habari ile ifikie mamlaka husika. Rumbete, kama utasoma hapa utaelewa sasa kwa nini nilizidisha safari za Iringa na sikuwa nikikutafuta uambatane nami.

Kutokana na umri wa binti, nilitaka pia kujiweka mbali nao. Hivyo baada ya muda nilianza kupotea. Sikuwa na mpango wowote na binti yule zaidi ya tamaa za mwili tu. Neno la mwisho nililolipata kupitia muuza duka ni kuwa binti alijifungua salama lakini mfuko wake wa uzazi uliharibika. Asingeweza kushika tena mimba. Mama yake alimpeleka kwa ‘wajomba zake mama yake’ huko mkoani Ruvuma. Hakujua zaidi ya hilo. Baadaye mama yake naye alifariki na hakuna mtu mwingine tena pale kijjini aliyekuwa akifahamu kuhusu binti yule.

“Ndipo Nathani akamwambia Daudi: “Wewe mwenyewe ndiye yule mwanamume!” mchungaji alimalizia kusoma neno lile.

Nimelia machozi baada ya kukumbuka tukio hili. Nimejiona jinsi gani nilikuwa kama mfalme Daudi. Hapana, simaanishi alichofanya mke wangu ni sawa, lakini jinsi ilivyokuwa rahisi kwangu kumhukumu bila kukumbuka kuwa nami nilifanya maovu tena zaidi ya ya kwake. Jinsi gani ilikuwa rahisi kumhukumu tajiri aliyechinja kondoo wa maskini na kusahau uuaji alioufanya kwa askari wake kisa tamaa ya mkewe. Karma imerudi kunihukumu. Nipo hapa, mali nyingi lakini sina damu yangu ya kuzirithi.


“Ndipo Nathani akamwambia Daudi: “Wewe mwenyewe ndiye yule mwanamume!”


Wasalaam wapendwa,
Mentor.
 

Kwa mara ya kwanza naomba niandike maelezo ya ziada;

- Kisa hiki ni kisa cha ukweli kabisa (wahusika wamebadilishwa kuficha uhalisia)

- hata mimi mwandishi bado nipo kwenye dilemma ya kujua nani hasa ahukumiwe (au ahukumiwe zaidi) na ndiyo maana nikafikiria kuweka poll hapo juu.

Zaidi sana, ni lengo la mimi kuelezea mkasa huu;

- HUKUMU: Kabla hujamchukia na kumhukumu mtu kwa alilokufanyia, jichunguze kama hukuwahi kufanya kama yeye. Haimaanishi kwa kila kosa basi tunastahili adhabu lakini itatufanya kuwa wapole wakati mwingine tunapofikiria kumuumiza mtu mwingine. Mara nyingi, hasa kwenye mahusiano (na hii imenikuta hivi karibuni) unamchukia mtu kwa kosa alilokufanyia. Unamtukana na kutumia maneno makali kuwa hakukupenda ndiyo maana akakufanyia A, B, C. lakini ukikaa kidogo ukafikiria 2012 huko Kidamali, utagundua nawe uliwahi kumfanyia mwingine sawa (au zaidi) ya yale uliyofanyiwa. Ila kwa kuwa sasa kibao kimegeuka kwako, huuoni uovu wako ila wa yule aliyekutenda sasa. BIN ADAMU!

- HISTORIA: Uliyoyafanya kwa kificho, yatadhihirishwa mwangani siku moja. Mara nyingi tunafanya mambo kwa kuamini hayatakuja kutuumbua mbeleni. Kuna nyakati tunafanikiwa. Lakini, amin nakuambia, ipo siku uovu unaoufanya ukijua ni uovu utakuja kuku-haunt.

- NAFASI: Unayo nafasi ya kurekebisha na kuanza upya. Zaidi sana, unayo nafasi sasa ya kutafakari na kuishi sawa. Mfalme Daudi kwenye aya niliyoandika, alijuta na kutubu (kwa bahati mbaya kwake dhambi yake ilisababisha kifo/vifo) lakini alirejeshewa baraka zake. Alirekebisha mwenendo wake na Mungu akamrejeshea ufalme wake. Kwa kiingereza kuna mahali imeandikwa, "God considered him, a man after God's own heart." Inawezekana kurekebisha, inawezekana kuanza upya kwa usahihi na inawezekana kutafakari sasa na kuepuka kufikia kwa Daudi na Mentor.

Wasalaam wapendwa,
Mentor.
 
Mentor katika ubora wako....
Sisahau ule Uzi wako kuwa una HIV, aisee niliumia as if naaga dunia on the spot..
Long live Mentor.
 
Back
Top Bottom