Kariakoo: Wamachinga Msimbazi waua mtu kwa kukanyaga nyanya

barafu

JF-Expert Member
Apr 28, 2013
6,739
32,874
image.jpeg
image.jpeg
image.jpeg
Watanzania tunaelekea wapi? Wamachinga wamuua kijana kwa mawe Dar kisa nyanya

DAR ES SALAAM: Mfanyabiashara mkubwa wa Kariakoo jijini Dar, Stephen Elija Silas (27) ameuawa kwa kupigwa mawe na wafanyabiashara wadogowadogo ‘Wamachinga’ kwa madai ya kukanyaga kwa gari lake nyanya walizopanga barabarani, Uwazi limefuatilia.

Tukio hilo lenye simulizi ya kusikitisha lilijiri usiku saa nne ya Februari 8, mwaka huu katika makutano ya Mtaa wa Msimbazi na Aggrey, Kariakoo jijini Dar es Salaam wakati marehemu huyo alipokuwa akilikwepa gari lililobeba maziwa. Marehemu Stephen alikuwa akiendesha gari lake aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T 312 AZU ambalo pia lilipondwa kwa mawe na Wamachinga. Alikuwa njiani kuelekea nyumbani kwake, Kinondoni, Dar.

MBALI NA MAWE, ALICHOMWA KISU taarifa zaidi zinadai kuwa, mbali na marehemu huyo kupigwa mawe, pia Wamachinga hao walimchoma kisu kwenye kwapa la mkono wa kulia akiwa ndani ya gari. SHUHUDA ASIMULIA Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alisema marehemu alikuwa akitokea upande wa uliyokuwa mzunguko wa Shule ya Uhuru, akaingia Barabara ya Msimbazi.

Alipofika makutano ya mtaa huo na Aggrey, mbele yake kulikuwa na gari lililobeba maziwa ambalo liliyumba, hivyo ili asiligonge akalikwepa na hivyo kujikuta akikanyaga kwa bahati mbaya nyanya za Wamachinga hao ambao palepale walianza kumshambulia kwa maneno, baadaye mawe na kumalizia na kisu. WALICHANGANYIKA NA WAHUNI “Jitihada za wasamaria wema kumuokoa zilishindikana licha ya jamaa kuomba msaada.

Mimi naamini kuwa, mbali na wamachinga pia wahuni wa mitaani walikuwepo kwa lengo la kupora vitu vyake,” kilisema chanzo hicho. ALIOMBA MSAMAHA Chanzo: “Kwanza jamaa alipobaini amekanyaga nyanya za biashara ya Wamachinga hakufanya fujo kwa kunena mabaya, aliomba asamehewe au alipe fedha kulingana na nyanya zilizoharibika lakini Wamachinga na wahuni hao hawakumsikiliza, waliendelea kumwadhibu.

“Kulikuwa na wananchi waliokuwa wakitokwa machozi walipomuona jamaa akipigwa mawe kwa kosa ambalo halina kichwa wala miguu.” WANANCHI WAPIGA SIMU POLISI Inaelezwa kuwa, baadhi ya wananchi waliamua kupiga simu Kituo cha Polisi Msimbazi ili wakamuokoe Stephen lakini licha ya kuwahi katika eneo la tukio, walimkuta akiwa hoi kutokana na kipigo na alifariki dunia wakati polisi wakimkimbiza Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu.

UWAZI LAFIKA MSIBANI Uwazi kama ada yake, lilifika kwenye msiba wa Stephen, kwa baba yake mkubwa marehemu aitwaye Charles Losaru, Mtoni Kijichi jijini Dar na kuzungumza na mdogo wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Rebeca Elija ambaye alisema alikuwa na marehemu muda mfupi kabla ya kifo chake. Alikuwa na haya ya kusema: “Marehemu kaka Stephen alikuwa mfanyabiashara mwenye maduka ya bidhaa mbalimbali, Kariakoo na Sinza. Huwa ana kawaida ya kutusindikiza na gari lake baada ya kufunga maduka. Mimi na ndugu zangu wengine tunaishi Kitunda yeye Kinondoni.

Amekuwa akitusindikiza hadi Banana na kutuacha tupande daladala. “Siku ya tukio, alitusindikiza na kutuacha Buguruni. Ilikuwa saa tatu usiku. Ni sisi tuliamua atuache hapo badala ya Banana. Yeye akarudi akipitia Kariakoo kwa vile kuna ndugu zetu wengine wana maduka maeneo hayo.” SIMU YAKE YAPIGWA, YAITA TU! Rebeca anaendelea: “Tuliposhuka kwenye daladala pale Banana, nilimpigia simu mara tatu ikawa inaita bila kupokelewa. Nikampigia simu mchumba wake, anaitwa Neema William ambaye ilikuwa wafunge ndoa hivi karibuni. Nilitaka kujua kama kaka alishafika nyumbani, Neema akasema hajafika.

TAARIFA ZA KIFO KWA NDUGU “Sasa wakati tunapanda daladala Banana kwenda Kitunda, nilipigiwa simu na marafiki zake na kuniambia kuwa Stephen amepata matatizo yupo Muhimbili. Niliposhuka Kitunda, alinipigia simu kaka yangu mkubwa, anaitwa Silas ambaye tulikuwa naye Kariakoo, akaniambia kaka amefariki dunia (machozi). “Kaka Stephen alikuwa mpole kupita kiasi! Hivi ni kwa nini walimuua kikatili vile? Kwanza pale walipompigia mawe, mbona ni sehemu ya magari na wala si pa kupanga nyanya wala bidhaa nyingine. Inaniuma sana (machozi tena).

” MAREHEMU AAGWA DAR, AZIKWA ARUSHA Mwili wa marehemu Stephen uliagwa Alhamisi ya wiki iliyopita katika Kanisa la Anglikana lililopo Muhimbili na kusafirishwa kwenda nyumbani kwao, Daraja Mbili mkoani Arusha kwa mazishi yaliyofanyika Ijumaa iliyopita.

POLISI WAZUNGUMZIA Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, ACP Ernest Matiku alipohojiwa na Uwazi ofisini kwake wiki iliyopita, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, marehemu alipigwa na kundi la watu baada ya kugonga gari lililokuwa likiuza maziwa kisha kukanyaga bidhaa za Wamachinga zilizokuwa zimepangwa chini. Gari likiwa limehalibika vibaya.

“Mpaka sasa tunawashikilia watu kumi kutokana na tukio hilo na bado upelelezi unaendelea. Kwa sasa hakuna biashara ya Wamachinga inayoendelea maeneo yale ya Mtaa wa Msimbazi. “Nalaani kitendo kile cha mauaji kwani hata kama marehemu alifanya kosa lakini sheria zipo na siyo kuchukua maamuzi hayo mazito ya kukatisha maisha ya binadamu, wote waliofanya unyama ule watashughulikiwa kisheria upelelezi ukikamilika,” alisema kamanda huyo.

Chanzo: Uwazi
 
Tumefika mbali jamani yaani nyanya zinasababisha kifo. je angegonga Mtu sijui ingekuwaje ?
 
Kiukweli angekuwa ndugu yangu ningelipiza kisasi kwa kukata wajinga hao....
Ndo maana sinunui kitu cha machinga, ni wasemge sana hawa jamaaa, sijui ni bangi
Mungu asiwasamehe hawa kenge
 
Aghriiiiiiiii haki yamama ningekuwa ndio Mimi ningepiga MTU risasi mchana mchana mamamae. Nachukia sana watu wa sheria mkononi.
 
hao wauaji wakubwa na wahuni ....walikuwa na hila zao ...barabarani sehemu ya magari sio nyanya...wakamatwe na washugulikiwe ipasavyo
 
huu ugumu wa maisha unafanya baadhi ya watu kuwa 'wanyama' wakali!Mungu awape faraja ndugu wa marehemu!
 
TANZANUIIA ! wamachinga ndiyo Panya Roadi na ni waWakilishi wa Mbwa mwitu !! Very Sad !1 Leo nyanya kesho sijui nini...........!!
 
"haya hayawezi kutokea Tanzania bwana, hii ni nchi ya amani".
Kuna kizazi hapa miaka 15 - 22 ni hatari kuliko kitu chochote tz. Hawa zaidi ya 80% hawana elimu na hata waliobahatika kwenda hizo shule wana vyeti tu kama makaratasi! Hawa wote hawaelewi maana ya kazi ni nini lakini wote ndoto zao ni magari mazuri, wasichana, simu na matanuzi mengine. Keep watching!
 
Chalii ya R wamemuondolea uhai wake kwa kosa la kipuuzi hivo..hapana vijana wa R lazima waje kkoo kulipiza kisasi..apumzike kwa amani.
 
Poleni sana ndugu jamaa marafiki na wote tulioguswa na msiba huu Apumzike kwa Amani marehemu na serikali ichukue hatua za haraka kunusuru raia na mali zao na kuliangalia swala hili kwa makini .....sheria ichukue mkondo wake kwa kila aliehusika kumuua marehemu.
 
Back
Top Bottom