Paschal Matubi
JF-Expert Member
- Sep 15, 2008
- 235
- 304
- - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - -
SOURCE: RAIA MWEMA, April 25, 2018

Msomaji, kama ulishaona msalaba wa Yesu basi juu yake una alama ina maneno “INRI”. Je, ulishajiuliza maana ya maneno “INRI” na hiyo alama inaitwaje?
Wakati serikali ya Roma inatawala bara lote la Ulaya huku kilatini kikiwa ndiyo rasmi, alama yenye maandishi ilitambulisha hicho kilichowekewa alama. Alama ya namna hiyo kwa kilatini iliitwa “titulus” na zikiwa nyingi ziliitwa “tituli”.
Hivyo, pale msalabani, Pilato aliweka “titulus” iliyoandikwa kwa kiebrania, kilatini na kigiriki. Maneno “INRI” kwenye ile “titulus” ni kifupi cha kilatini yaani “Iesvs Nazarenvs Rex Ivdaeorvm” na kwa kiswahili ni “Yesu wa Nazareth Mfalme wa Yudea” {Yohane 19:19 }.
Wakristo wa mwanzo katika utawala wa Roma hawakuruhusiwa kukusanyika au kusali hadharani. Hivyo, walikutana kwenye nyumba ya mwenzao ikiwa imebandikwa alama ya jina lake, yaani “titulus” au “tituli” kama ile ya msalabani kwa Yesu.
Kukutana kukafanya hata hizo nyumba ziitwe “tituli” na zikawa ndiyo makanisa ya mwanzo.
Kuna historia ndefu ya Roma kushindwa kuuzuia ukristo kuenea. Itoshetu kusema, mwaka 311 ukristo ukaruhusiwa na mtawala wa Roma (Constantine) akagawa maeneo ili kujengwa makanisa rasmi.
Makanisa sasa yakajengwa lakini pia zile nyumba nazo yaani “tituli”, baadhi zikaboreshwa au kuvunjwa ili kujengwa upya kanisa rasmi kubwa.
Mazoea ya kuziita zile nyumba “tituli” au “titulus” yakafanya hata makanisa mapya yaitwe pia “tituli”. Makanisa haya “tituli”, kufikia karne ya tano yalishakuwa jumla 25 pale Roma.
Askofu wa Roma, akawafanya mapadri wa hizo “tituli” kama washauri wake kwa sababu ndiyo ya makanisa ya kwanza kuueneza ukristo. Askofu wa Roma akifariki basi hao mapadri wa hizo “tituli” wanamchagua mtu anayeziba nafasi yake.
Msamiati huu “tituli” umefanya pia makanisa au majimbo mengi ya zamani kwingine duniani yasiyotumika tena yaitwe “titulus” au “tituli” na kwa kiingereza yanaitwa “titular”.
Hata hapa Tanzaniamajimbo mawili yaani Nachingwea na Rutabo ni yote “tituli”. Jimbo la Rutabo ndilo jimbo la askofu Telesphore Bilung aliyeko Ranchi nchini India, wakati la Nachingwea ndilo la askofu Benjamin Phir aliyeko Lusaka, Zambia.
Ukiachilia mbali hayo makanisa “tituli”, kanisa katoliki hutoa huduma za jamii, kama shule, hospitali, matunzo kwa wasiojiweza. Hivyo, hata hizi huduma zilianza kufanywa na mashemasi.
Shemasi kwa kilatini anaitwa “diaconus” hivyo vituo hivi vya huduma vikaitwa “diaconiae”. Hizi “diaconiae” zimeanza kutajwa mwaka 685 na kufikia mwaka 795 zilikuwa jumla 18 pale Roma.
Askofu wa jimbo la Roma ndiye kiongozi wa wakatoliki duniani. Roma kulikuwa na majimbo saba yaliyo jirani.
Majimbo hayo saba ni Ostia, Velletri-Segni, Porto-Santa Rufina, Frascati, Palestrina, Albano, Sabina-Poggio Mirteto. Udogo na ujirani wa majimbo haya ulifanya yaitwe “suburbicarian” na maaskofu wa haya wamemsaidia sana Papa kwani wako jirani naye.
Hivyo kupitia “tituli” papa akaweza kusaidiwa kazi za kipadri na mapadri wake pale Roma. Kupitia “diaconiae” akasaidiwa kazi za kishemasi na mashemasi. Kupitia majimbo ya “suburbicarian” akasaidiwa kazi za kiaskofu na maaskofu wa jirani.
Kufikia mwaka 995 vile vituo vya huduma (diaconiae) viligeuka na kuchukua sura ya kanisa, siyo huduma tu. Kukawa hakuna tofauti kati ya kituo yaani “diaconiae” na kanisa yaani “tituli.
Ukristo ulivyozidi kuenea ikaonekana Papa asiishie kusaidiwa au kushauriwa na mashemasi na mapadri wa jimbo la Roma tu. Vilevile ikaanza kuulizwa iweje Papa achaguliwe na mashemasi na mapadri wa jimbo la Roma tu?
Ufumbuzi wa tatizo hili ukawa ni kwamba yale makanisa “tituli”, Papa akaanza kuyapa mapadri hata kutoka majimbo mengine duniani nje ya Roma.
Pia vile vituo vya mashemasi (“diaconiae”), Papa akaanza kuvipa mashemasi kutoka kwingine duniani. Yale majimbo jirani (“suburbicarian”) akaanza kuyapa maaskofu toka sehemu mbalimbali duniani.
Kwa lugha rahisi, Papa akaanza kufanya “uhamisho”. Shemasi wa jimbo fulani anahamia Roma kwenye moja ya vile vituo (diaconiae). Kama ni padri naye anahamia Roma kwenye moja ya yale makanisa (tituli). Kama ni askofu naye anahamia kwenye jimbo jirani na Roma liitwalo “suburbicarian”.
Uhamisho wa namna hii ndiyo unaitwa “ukardinali”, hivyo tunaanza sasa kujadili neno lenyewe “kardinali”.
Asili ya neno “kardinali” ni neno la kilatini “cardo”, linalomaanisha kitu chochote kinachoning’iniza au kushikilia kitu kingine. Ukianika nguo kwa vibanio ili isipeperushwe, kile kibanio ni “cardo”. Ile nguo ukiining’iniza kwenye “hangers”, hizo “hangers” ni “cardo”.
Chuma kinachoushikilia ubao wa “mlango” au “dirisha” ukutani ufungwe na kufunguliwa kwa kiswahili kinaitwa “bawaba”, nacho kinaitwa “cardo”.
Hata ukitoboa ukuta kwa msumari, ule msumari ukaning’iniza vitu, msumari ule unageuka kuitwa “cardo”.
Kitendo cha kuhamisha kitu kutoka kwingine ukakitundika kwenye “cardo” kama niliyoyataja kinaitwa “incardinale”. Sasa hili jina“cardo” lililozaa kitendo “incardinale” vina uhusiano gani na hoja hii ya leo?
Msomaji, neno “incardinale” lina herufi 11. Hebu ondoa herufi mbili za mwanzo yaani “in-” na herufi ya mwisho yaani “-e” uone utapata neno gani.? Utaona linabaki neno “-cardinal-”. Kwa mbali sasa unaona uhusiano unakuja maana hoja nzima ya leo ni maana ya neno “kardinali”.
Kitendo cha padri, shemasi kutokea kokote alikokuwa na hatimaye akajiunga na jimbo au wamisionari, kilifananishwa mtu kuondoka alikokuwa na kwenda kubanwa na “askofu wa jimbo” au “wamisionari” aliojiunga nao.
Kilatini cha wakati huo kikafananisha kitendo hiki na ule utundikaji wa nguo kwenye kibanio, au mlango kwenye bawaba, au chombo kwenye ule msumari, yaani “incardinale”.
Unapoanza kuwa “shemasi”, “padri” au “askofu” lazima utakuwa kwenye eneo linaloitwa “jimbo” au kikundi cha “wamisionari”. Hivyo, kila padri au shemasi aliitwa “cardinali” kwani ni lazima ana mahala anapoendeshea huduma yake.
Hivyo “incardinale” ni kitendo cha kusajiliwa au kuhamishiwa kwenye “jimbo” au kundi fulani la “umisionari”, wakati kitendo cha kuondoka huko kikaitwa “excardinale”: {The Oxford Dictionary of the Christian Church, ISBN: 9780192116550, uk. 584 na 825}.
Tumeshaona jinsi mashemasi, mapadri na maaskofu wa majimbo mengine wakawa wanahamishiwa Roma kwenye yala makanisa “tituli” au vile vituo “diaconiae” au yale majimbo yaani “suburbicarian”. Wote hawa walikuwa wanaitwa “kardinali” maana wote walifanyiwa kitendo kile “incardinale”, yaani kuhamishiwa au kusajiliwa jimboni Roma.
Hivyo, neno “incardinale” ni la msingi kuliko maneno yote katika hii makala, kwani ukilielewa utakuwa umeelewa makala hii na utakuwa umeelewa maana ya “ukardinali”.
Hata neno “incardinale”nimefanya makusudi kulitaja la kilatini lilikoanzia na unaweza kuhakikisha tafsiri yake katika kiingereza ambayo ni “incardination”.
Nimesema, mwanzoni neno “kardinali” lilitumika kwa kila padri, shemasi na askofu duniani. Lakini kuanzia mwaka 769, likaanza kutotumika kwa wengine wote duniani, likabaki kutumika kwa pale Roma tu, tena kwa wale mapadri wenye zile “tituli”, mashemasi wenye vile vituo “diaconiae” na maaskofu wa yale majimbo yaani “suburbicarian”: {The Next Pope, ISBN: 9780615353722, uk. 44}.
Mazoea haya ndiyo tumeyakuta hadi leo. Wala hakuna aliyekataza watu bali Ulaya ilijikuta hawa tu ndiyo wamebaki wanaitwa “kardinali”.
Kwa ujumla hii ndiyo maana ya “ukardinali” wa leo. Kama umeielewa makala hii hadi hapa, utakuwa umeelewa maana halisi ya kardinali hata ukiishia hapa, kwani kilichobaki sasa ni mifano ya hapa na pale unayoijua au usiyoijua.
Kuanzia mwaka 769 ukardinali ulipochukua sura hii imepita miaka 1249 sasa. Hii ni miaka mingi na mambo kadhaa yamebadilika, lakini hakuna badiliko lililoondoa msingi huu.
Bado hadi leo, Papa akikuhamishia Roma atakupa moja ya zile hadhi tatu yaani kituo cha ushemasi yaani “diaconiae”, au kanisa la kale yaani “titulus” au jimbo la jirani yaani “suburbicarian”.
Ukihamishiwa pale Roma kwa hadhi ya “ushemasi” yaani “deacon”utapewa moja ya vile vituo (“diaconiae”) , utaitwa “cardinal-deacon”. Hii ndiyo aina ya kwanza ya ukardinali unaousikia.
Mapadri wengi wanaoupata ukardinali bila kuufikia uaskofu hufanyiwa mtindo huu. Giacomo Antonelli alipata ukardinali Juni 11, 1847, ameishia kuwa shemasi tu hakuwahi kuwa padri hadi kifo chake.
Ercole Kardinali Consalvi pamoja na kuwa kardinali tangu Agosti 11, 1800 hakuwahi kuwa padri, aliishia kwenye ushemasi tu.
Hata leo wapo mapadri wawili ambao si maaskofu lakini ni makardinali yaani padri Albert Vanhoye ambaye ni “mjesuit” na padri Ernest Simoni wa jimbo la “Shkodrë” nchini Albania.
Ukihamishiwa pale Roma kwa hadhi ya “uaskofu” yaani “bishop”utapewa lile jimbo (“suburbicarian”) , utaitwa “cardinal-bishop”. Hii ndiyo aina ya pili ya ukardinali wa sasa. Hawa huwa wako sita tu na anayepewa lile jimbo liitwalo “Ostia” ndiyo anakuwa anawazidi hadhi yaaani “dean” wa makardinali wote duniani.
Joseph Kardinali Ratzinger alipewa jimbo hili la “Ostia” tangu Novemba 30, 2002 hadi alipoteuliwa kuwa Papa Benedict XVI.
Ukihamishiwa pale Roma kwa hadhi ya “padri” yaani “priest”utapewa moja ya yale makanisa yaitwayo “tituli” , utaitwa “cardinal-priest”. Hii ndiyo aina ya tatu ya ukardinali unaousikia.
Kundi hili “cardinal-priest” ndilo lenye makardinali wengi kwani wengi huwa ni maaskofu wako mbali na Roma. Mmoja wao ni Polycarp Kardinali Pengo aliyeko D’Salaam ambako ni kilomita 6043 kutoka Roma.
Hizi ndizo aina tatu za makardinali yaani “cardinal-deacon”, “cardinal-priest” na “cardinal-bishop”. Wataalamu wa lugha watusaidie kama tafsiri ya “kardinari-shemasi”, “kardinari-padri” na “kardinari-askofu” itaweza kukubalika.
Hivyo utaona ingawa tunataja sana neno “kardinali”, ukweli ni kwamba tunalitaja nusunusu hivyo tuimeficha maana halisi ambayo ni historia yote niliyoieleza humu kifupi ya kuhesabika kwamba uko jimboni Roma.
Unaweza kujiuliza maswali kwamba sasa kwa nini mapadri na hata maaskofu wanapewa vituo vya ushemasi yaani “diaconiae” vinayosababisha waitwe “cardinal-deacon”?
Jibu ni kwamba, shemasi ni msaidizi wa padri na wa askofu, hivyo padri au askofu haondolewi uwezo wa kufanya kazi anazoziweza shemasi.
Vilevile unaweza kujiuliza, kwa nini maskofu kama Polycarp Pengo pale Roma wanapewa “tituli” ambayo ni makanisa kwa ajili ya mapadri yanayosababisha waitwe “cardinal-priest” wakati wao ni maaskofu?
Jibu ni kwamba uaskofu haumuondolei mtu uwezo wa kufanya kazi ya kipadri, wala haumuondolei mtu uwezo wa kufanya kazi ya ushemasi.
Kadiri makardinali wanavyoongezeka ndiyo yale makanisa “titulus” yanavyoelekea kutotosha mengine yamejengwa majuzi.
Kanisa liitwalo “Mama yetu wa La Salette” pale Roma, yaani “titulus”, ndilo alilopewa Polycarp Pengo mwaka 1998 likamfanya akawa na hadhi “cardinal-priest”.
Usipokuwa shemasi, padri au askofu wewe ni mlei na ndiyo wengi. Teodolfo Kardinali Mertel, alipewa ukardinali Machi 15, 1858 akiwa hajafikia hata ushemasi. Hivyo, historia inaonyesha kuwa hata “mlei” ameweza kuwa “kardinali”.
Wakati mwingine Papa humpa mtu ukardinali bila kuitangazia dunia. Makardinali hawa huitwa “kardinali wa siri”, yaani “cardinal in pectore”. Papa huficha majina yao kwa usalama wao kutokana na hali ya maeneo wanamoishi.
Septemba 08, 1955, serikali ya China, ilimfunga kifungo cha maisha askofu Ignatius Kung Pin-mei wa jimbo la Shanghai alipolazimishwa aukane ukatoliki na yeye akakataa mbele ya umati mzima na dunia nzima.
Serikali ya China ilimhukumu kuwa askofu Ignatius ni mchochezi, lakini ilishindwa kugundua kwamba Juni 30, 1979, Papa John Paul II alifaulu kumpa “ukardinali wa siri”, akiwa humohumo gerezani.
Hivyo, ni rahisi kujidanganya ukihesabu “makardinali” wanaojulikana, kumbe Papa anao “makardinali wa siri” ambao jamii huwa inahangaika kuwaita ni wachochezi.
Je, Polycarp Pengo atajiuzulu ukardinali? Niliuliza swali hili wakati namalizia sehemu ya kwanza wiki jana.
Tumeona, ukardinali ni kuhesabika kwamba uko jimboni Roma, na kimsingi Papa anakuwa amekufanya ufanye kazi za upadri kwenye “tituli”, au ufanye kazi za ushemasi kwenye “diaconiae” au ufanye kazi za uaskofu kwenye jimbo lile “suburbicarian”.
Kujiuzulu majukumu mengine hapa duniani hakuhusiani kabisa na “ukardinali” wa kardinali yoyote. Makardinali wengi, tuseme wote, huwa hawajiuzulu ukardinali ambao maana yake ni kuyaachia yale makanisa (“tituli”), au kituo kile (“diaconiae”) au jimbo lile (“suburbicarian”).
Baadhi ya makardinali waliacha wosia kuzikwa kwenye vituo vyao kule Roma. Philip Kardinali Howard alikuwa mzaliwa wa England, lakini alihusia azikwe kwenye kanisa “titulus” lake liitwalo “Santa Maria sopra Minerva”. Juni 17, 1694 alipofariki akazikwa humo kama alivyohusia.
Kardinali akijiuzulu si jambo dogo duniani hata iwe kwa sababu gani. Magazeti maarufu yote duniani yatahoji. Patrick Kardinali O’Brien wa nchini Scotland alikumbwa na kashfa iliyotikisa duniani kote.
Hata hivyo, kashfa ile iliishia tu kumfanya Februari 25, 2013 akajiuzulu utawala wa jimbo la “Saint Andrews”, lakini kamwe hakujiuzulu ukardinali hadi kifo chake.
Padri Louis Billot alikuwa kardinali kwa miaka 16 hadi alipojiuzulu ukardinali Septemba 21, 1927, akaacha kuwa kardinali, akabaki na upadri wake kama “mjesuit”. Lakini kujiuzulu kwenye kulikuja baada ya mvutano wake wa muda mrefu na Papa Pius XI.
Hivyo, kimazoea, akishateuliwa kuwa kardinali anakuwa kardinali hadi kifo chake. Emmanuel Kardinali Wamala wa jimbo la Kampala nchini Uganda alijiuzulu uongozi wa jimbo hilo Agosti 19, 2016.
Hata hapa nyumbani Laurean Kardinali Rugambwa alijiuzulu kuongoza jimbo la D’Salaam lakini hadi kifo chake alikuwa bado kardinali, yaani “cardinal-priest” au “kardinali-padri” ukipenda.
Hivyo, Poylcarp Pengo atakapojiuzulu ataendelea kuwa kardinali kama wengine wote duniani hadi kifo chake.
Hivyo, kardinali anapofariki ndipo pale Roma ile “diaconiae” (kituo) au “titulus” (kanisa) au “suburbicarian” (jimbo) linapotangazwa kuwa wazi.
Tukutane wiki ijayo kwa ufafanuzi kuhusu maaskofu wanavyochaguliwa.