Kampuni ya kada maarufu wa CCM ndugu Bulembo matatani

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,899
Na Paul Sarwat wa Raia Mwema

KAMPUNI ya New Metro Merchandise Ltd ambayo mmoja wa wakurugenzi wake ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo, imeingia matatani ikidaiwa zaidi ya shilingi milioni 227 na Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Bulembo pamoja na kuwa kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi ambacho kwa sasa Mwenyekiti wake ni Rais John Magufuli, ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho na ndiye aliyekuwa kinara wa kampeni za Dk. Magufuli wakati wa kugombea urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.

Hatua ya Bulembo kuhusishwa na kampuni hiyo inatokana na kusaini mkataba wa makubaliano na Halmashauri ya Jiji la Arusha ambapo anajitambulisha kama mkurugenzi wa kampuni ya New Metro Merchandise Ltd yenye anwani ya posta 80134 Dar es Salaam.

Taarifa na nakala ya mkataba iliyopatikana kutoka ndani ya Jiji la Arusha zinabainisha kuwa kampuni hiyo inadaiwa kiasi hicho cha fedha baada ya kupewa zabuni ya kukusanya ushuru wa mabango ya biashara (billboards) katika mwaka wa fedha 2009/10 na 2010/11.

Kwa mujibu wa nakala ya mkataba huo kampuni ya Bulembo iliingia katika mgogoro na Halmashauri ya Jiji la Arusha na kufikishana mahakakamani kwa kufungua kesi ya madai namba 8/2011.

Hata hivyo pande hizo mbili zilifikia muafaka na kumaliza mgogoro huo nje ya mahakama na kuingia mkataba mpya kwa New Metro Merchandise Ltd kuendelea kukusanya ushuru kwa miezi mingine minne na pia kusamehewa deni la shilingi 244,598,880.

Mkataba mpya baina ya kampuni hiyo na Jiji la Arusha ulianza Julai Mosi 2011 hadi Oktoba 31 mwaka huo huo wa 2011 akitakiwa kuwasilisha shilingi 56,813,720 kila mwezi.

Hata hivyo, taarifa zinaonesha kuwa New Metro Merchandise haikuwasilisha kiasi cha shilingi 227,254,880 kinyume cha makubaliano katika mkataba wa kumaliza mgogoro baina ya pande hizo mbili.

Kipengele cha nne cha mkataba baina kampuni hiyo na Jiji la Arusha uliosainiwa Julai 19 mwaka 2011 unaelezea kuwa wakala ataruhusiwa kuendelea na mkataba wake uliovunjwa baada ya kusaini hati ya makubaliano na mapendekezo ya kamati ya usuluhishi kuridhiwa na Baraza la Madiwani.

“Hivyo wakala ataendelea kukusanya ada hizo kuanzia mwezi Julai hadi Oktoba 2011 ambapo kila mwezi atailipa halmashauri shilingi 56,813,720 kama ada ya mabango ya matangazo kwa mujibu wa mkataba,” unasomeka mkataba huo.

Lakini pamoja na mkataba huo kuainisha kuwa Bulembo na kampuni yake walipaswa kuwasilisha kiasi cha fedha kila mwezi kwa mujibu wa makubaliano, fedha hizo hazikuwa zikiwasilishwa licha ya kuzikusanya kutoka kwa wateja mbalimbali.

Mwenyekiti wa kamati ya kuhakiki madeni sugu ya Jiji la Arusha inayoundwa na madiwani watano, Ephata Nanyaro, alilithibitishia Raia Mwema kuwa kampuni hiyo ni miongoni mwa wadaiwa sugu wa Jiji la Arusha.

“Kampuni hii ya New Metro Merchandise ilisamehewa deni la shilingi milioni 229 kwa njia za kifisadi na bado akaongezewa mkataba wa kukusanya ushuru kwa miezi minne ya kiasi cha shilingi milioni 227 ambayo nayo hajalipa jumla yote halmashauri imepoteza zaidi ya nusu bilioni,”

“Ni aibu kwa kiongozi mkubwa kutolipa ushuru wa umma kwa kuwa tu yeye kiongozi mkubwa ndani ya chama cha siasa huu ni utamaduni mbaya sana, tunawomba Rais Magufuli atusadie kwani mdaiwa ni kampeni meneja wake. Kwa sasa tunakamilisha ripoti yetu ambayo itasomwa muda wowote wiki hii kulingana na ratiba ya vikao vya Baraza la Madiwani,” alisema Nanyaro.

Alisema miongoni mwa mapendekezo ya kamati hiyo ni kuwekwa kwa zuio kwa kampuni zote zinazodaiwa (black listed) kutopewa zabuni yoyote katika Halmashauri Jiji la Arusha na ikiwezekana zuio hilo liwe kwa halmashauri zote nchini.

Kwa upande wake Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro, alisema kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu na kanuni za sheria zinazoongoza serikali za mitaa kutokana tabia ya baadhi ya watendaji kushirikiana na wazabuni kuhujumu mapato ya jiji.

“Kuna ushahidi mwingi tu jinsi halmashauri ilivyohujumiwa katika mapato yake na matumizi ya fedha uliofanywa na wanasiasa na watendaji katika miaka 15 iliyopita, hivyo basi sisi tutahakikisha kuwa fedha zote zinalipwa bila ya kujali hadhi na wadhifa wa wahusika,” alisema Meya Lazaro.

Akijibu madai hayo mkurugenzi wa New Metro Merchandise, Abdallah Bulembo alikiri kuwa mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo inayodaiwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Bulembo alifafanua kuwa kampuni yake ilishindwa kuwasilisha fedha hizo baada ya kuingia katika mzozo wa kibiashara na kampuni mbili za simu ya Tigo na Zantel na kuzifikisha mahakamani.

“Tigo tunawadai zaidi ya shilingi bilioni moja na kesi bado iko mahakamani na Zantel kesi imekwisha wiki mbili zilizopita tumewashinda na wanatakiwa kutulipa milioni 135 na viongozi wote wa Halmashauri ya Jiji wanalifahamu hilo,” alisema Bulembo.

Bulembo aliongeza kuwa suala hilo halina uhusiano wowote na shughuli zake za kisiasa na kuongeza kuwa, kamati hiyo ya madiwani inapaswa kueleza ukweli kuhusu hatua waliyofikia kwa kuwa katika kesi zilizofunguliwa Jiji ni mshirika katika maombi ya mashitaka.

“Walipaswa kuwa wakweli hao madiwani kwa sababu tumefungua kesi pamoja na Halmashauri ya Jiji na makubaliano ni kwamba tukilipwa fedha zetu na sisi tunawapa chao Halmashauri ya Jiji, sasa hapo tatizo liko wapi?”alihoji Bulembo.


Chanzo: Raia Mwema
 
Tatizo aambiwe Bulembo ni conflict of interest. Kwani yeye maadili ya uongozi hayamuhusu?
 
Tenda zinaenda kwa mwanachama. Kingunge aliojuvua uanachama tu zabuni yake ya kukusanya ushuru ubungo terminal ikaota mbawa.
 
Huwezi kutenganisha ufisadi na makada wa chama mana ndio majambazi wakubwa wa uchumi wetu....wengine wanatengeneza ARV feki kuua wananchi

Habari ya mujini kwa sasa ni Dj kutupiwa virago nje na UKUTA kubomoka kamanda.
 
Mwenzake Mbowe vitu vyake vimetupwa street kule Makunganya kwa kushindwa kulipa kodi, dawa ya deni ni kulipa kama anadaiwa alipe tu asilete visingizo kama mwenzake, anajifanya tajiri kumbe analiibia shirika la umma
 
Back
Top Bottom