Kamati ya Ngwilizi: Wabunge wategwa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kamati ya Ngwilizi: Wabunge wategwa

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by mtwana, Oct 24, 2012.

 1. mtwana

  mtwana JF-Expert Member

  #1
  Oct 24, 2012
  Joined: Oct 13, 2012
  Messages: 399
  Likes Received: 85
  Trophy Points: 45
  Wakati mkutano wa tisa wa Bunge ukitarajiwa kuanza Jumanne ijayo, matarajio ya kuwasilishwa kwa ripoti ya Kamati ndogo ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge juu ya uchunguzi dhidi ya tuhuma za baadhi ya wabunge kutuhumiwa kwa rushwa imezidi kugubikwa na utata kutokana na kile kinachoelewa kuwako kwa harakati nyingi za kutaka kufunika mambo.

  Hali hii inatokana na ukweli kwamba yapo makundi mawili makubwa yanayovutana kuhusu ripoti hiyo, mmoja ukiongozwa na wabunge waliotuhumiwa na upande wa pili ukijumuisha wale wanaoipigia debe serikali katika sakata zima la sekta ya nishati nchini.

  Ingawa kuna hali ya kutokueleweka kama ripoti hiyo itawasilishwa kwa ajili ya kujadiliwa au la, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, jana aliiambia NIPASHE kuwa Kamati ya Uongozi ya Bunge inatarajia kukutana Jumatatu ijayo, ikiwa ni siku moja tu kabla ya kuanza kwa mkutano huo.

  Kamati uongozi inaundwa pamoja na watu wengine, Spika wa Bunge, Naibu wake, Waziri Mkuu, wenyeviti wa kamati za bunge na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

  Kwa mwelekeo wa mambo, moto mkubwa unatarajia kuwashwa juu ya ripoti hiyo kwa kuwa wapo wabunge wanaotaka kusafishwa dhidi ya tuhuma ambazo wanaamini wamevalishwa kwa makusudi, ilahali upande wa serikali ukiamini kwamba kulikuwa na hujuma za chini kwa chini zilizosukumwa na vishawishi vya rushwa kukwamisha makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini ya mwaka 2012/13 Julai mwaka huu.

  Ripoti hiyo inasubiriwa kwa hamu kubwa na Watanzania ili kuweka mambo hadharani kuhusu wabunge wanaotuhumiwa kuhongwa na kampuni za mafuta ili wakwamishe Bajeti hiyo na kutaka kuwajibishwa kwa viongozi wa wizara hiyo Waziri wake, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu, Eliakim Maswi.

  Kwa mujibu wa Dk. Kashililah Kamati ya Uongozi ya Bunge ndiyo itakuwa na maamuzi ya mwisho kama suala la kuwasilishwa ripoti ya kamati hiyo ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Mlalo (CCM), Brigedia Jenerali Mstaafu, Hassan Ngwilizi, liingizwe kwenye ratiba ya vikao vya Bunge kwa ajili ya kuwasilishwa na kujadiliwa.

  Habari ambazo NIPASHE imezipata kutoka vyanzo mbalimbali zinasema kuwa kumekuwa na juhudi nyingi za pande mbili zinazohusika na ripoti ya kamati ya Ngwilizi, mmoja ukitaka kombe lifunikwe, na mwingine ukitaka kila kitu kiwekwe wazi ili kulinda hadhi ya wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa.

  Kabla na hata baada ya kuundwa kwa kamati hiyo kumekuwa na mgawanyiko mkubwa ndani na nje ya Bunge na serikali kuhusu kashfa hiyo hali ambayo iliibuka wakati wa mkutano wa nane wa Bunge la Bajeti na kusababisha mvutano mkubwa wa wabunge na ndani ya serikali.

  Kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa ambazo zinaeleza kuwa huenda ripoti hiyo isiwasilishwe na kujadiliwa bungeni kutokana na baadhi ya mambo kutokuwa sawa baada ya kamati ya Ngwilizi kukamilisha uchunguzi wake.

  Habari zinasema kuwa baada ya kukamilika kwa ripoti hiyo, yameibuka makundi mamwili yanayovutaka. Moja linaitetea serikali ili ripoti hiyo iisafishe na lingine linataka haki itendeke kwa ukweli kuwekwa wazi na kujulikana.

  Kundi linalotaka haki itendeke linaamini kama kuna waliohongwa wajulikane na kama siyo ukweli ujulikane kwa kuwa baadhi ya wabunge walilalamika na kutaka ripoti hiyo itolewe mapema kabla ya kuahirishwa kwa Mkutano wa Nane wakisema kuwa bila hivyo watakutana na hali ngumu katika majimbo yao kwa kuwa wamevunjiwa haki zao.

  Ripoti ya kamati hiyo kama itawasilishwa na kujadiliwa mjadala mkali hautauepukika kutokana na kuwapo kwa mgawanyiko kwa kuwa kila upande utataka kuhakikisha kuwa unatendewa haki.

  Ingawa majina ya wabunge hao bado haijatajwa rasmi na mamlaka zinazohusika na kupambana dhidi ya rushwa, lakini wakati wa mkutano wa Nane wa Bunge ilielezwa kuwa wabunge wanaotuhumiwa kupewa rushwa ni watano, kati yao watatu wanatoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wawili wanatoka vyama vya upinzani.

  Kamati hiyo tangu ianze kazi za kuchunguza tuhuma hizo kumekuwa na usiri mkubwa wa kubaini waliotiwa hatiani baada ya uchunguzi kukamilika.

  Dk. Kashililah, akizungumza na gazeti hili hivi karibuni alisema kamati ya Ngwilizi imekamilisha kazi yake na kuikabidhi ripoti kwa Spika Makinda.

  Kwa upande wake Naibu Spika, Job Ndungai, alisema kwa mujibu wa utaratibu, baada ya kamati kuwasilisha ripoti kwa Spika, Kamati ya Uongozi ya Bunge itakaa kujadili na kama itaona kuna umuhimu ripoti hiyo itaingizwa kwenye ratiba ya vikao vya Bunge kwa ajili ya kujadiliwa.

  Mwezi uliopita, Ndugai akizungumza kwenye kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na kituo cha ITV, alisema wabunge waliotuhumiwa kwa rushwa huenda wakakabiliwa na hatari ya kuvuliwa ubunge au kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria kamati ndogo Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itathibitisha kama ni kweli walipewa rushwa.

  Alisema kamati hiyo inayo uwezo wa kupendekeza kama wabunge hao wavuliwe nyazifa zao au washitakiwe mahakamani.

  Julai 28 mwaka huu wakati wa Bunge la Bajeti, Spika Makinda alivunja Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kutokana na baadhi ya wajumbe wake kutuhumiwa kuhongwa na kampuni za mafuta nchini.

  Kamati hiyo iliyovunjwa ilikuwa ikiundwa na wajumbe zaidi ya 20 ambao ni pamoja na Mwenyekiti wake, Selemani Zedi na Makamu mwenyekiti, Diana Chilolo, Profesa Kulikoyela Kahigi, Yusufu Haji Khamisi, Mariam Kisangi, Catherine Magige, Dk. Anthony Mbassa, Abia Nyabakari, Charles Mwijage, Yusufu Nassir, Christopher Ole Sendeka na Dk. Festus Limbu.

  Wajumbe wengine waliokuwamo katika kamati hiyo iliyovunjwa kwa tuhuma za rushwa ni Shafin Sumar, Lucy Mayenga, Josephine Chagulla, Mwanamrisho Abama, David Silinde, Suleiman Masoud, Kisyeri Werema Chambiri, Munde Abdallah, Sara Msafiri, Vicky Kamata na Ali Mbaruk Salim.

  Sakata hilo la kuvunjwa kwa kamati liliambatana na vijembe miongoni mwa wabunge. Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, aliwataja kwa majina wabunge wenzake kwamba wamehusika katika kupokea rushwa.

  Kuvunjwa kwa Kamati ya Nishati na Madini kulifuatia baada ya Mbunge wa Namtumbo (CCM), Vita Kawawa, kuomba Mwongozo wa Spika, akitaka jambo hilo lijadiliwe na Bunge na kupendekeza kuwa Kamati za Bunge zinazotuhumiwa kwa rushwa zivunjwe.

  Bunge likubali kuivunja na kuiunda upya Kamati ya Nishati na Madini na kamati na baada ya hoja hiyo kuungwa mkono, Spika Makinda alisimama na kukubali hoja ya Kawawa na kutangaza kuivunja Kamati ya Nishati na Madini.

  Spika Makinda alisema ameiagiza Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge kutengeneza kanuni za kuwadhibiti wabunge wenye tabia ya kupokea rushwa kutoka kwa watu mbalimbali ili kutimiza matakwa yao binafsi.

  Baadaye Spika alinda kamati ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ambayo Mwenyekiti wake ni Ngwilizi. Wajumbe wengine ni John Chiligati (Manyoni-CCM); Gosbert Blandes (Karagwe-CCM); Riziki Omary (Viti Maalum-CUF) na Said Arfi (Mpanda Mjini-Chadema).

  Wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, baadhi ya wabunge walidai kuwa kuna wenzao wamehongwa na kampuni za mafuta ili kushinikiza Waziri Muhongo na Maswi, wangÂ’olewe katika nafasi zao kwa kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma.

  UNUNUZI WA MAFUTA MAZITO

  Moto ndani ya Wizara ya Nishati na Madini ulianza kuibuka baada ya kuwapo madai kuwa kampuni ya Puma Energy (T) Limited, ilipewa zabuni kwa kupitia mlango wa nyuma kusambaza mafuta mazito kwa ajili ya mitambo ya kufua umeme ya IPTL.

  Puma haikuwa miongoni mwa kampuni tatu zilizotimiza vigezo vya kupewa zabuni hiyo, lakini ilipewa zabuni hiyo bila kufuata taratibu za manunuzi.

  Maswi alijitetea kuwa alitoa zabuni hiyo kwa Puma kwa kuwa ilikuwa na akiba ya kutosha ya mafuta ikilinganishwa na kampuni nyingine. Pia alisema gharama zake zilikuwa za chini kuliko nyingine.

  Kutokana na uamuzi wa kuipatia zabuni Puma, yalizuka malalamiko mengi kutoka kwa wadau na umma kutaka Maswi achukuliwe hatua kwa kukiuka sheria ya manunuzi.
   
 2. d

  dotto JF-Expert Member

  #2
  Oct 24, 2012
  Joined: Sep 29, 2010
  Messages: 1,720
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 135
  Kama tukiacha kununua uongozi na mambo haya yatakwisha.
   
Loading...