Kamati ya Mwinyi yaparaganyika | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kamati ya Mwinyi yaparaganyika

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Saint Ivuga, Dec 14, 2009.

 1. Saint Ivuga

  Saint Ivuga JF-Expert Member

  #1
  Dec 14, 2009
  Joined: Aug 21, 2008
  Messages: 39,454
  Likes Received: 19,825
  Trophy Points: 280
  Kamati ya Mwinyi yaparaganyika
  • Wajumbe waanza kuchimbana, hofu yatawala
  KAMATI iliyoundwa kuchunguza chanzo cha chuki na uhasama miongoni mwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na baina yao na serikali, imeanza kuparaganyika, hasa baada ya kuvuja kwa taarifa za kile walichokiandika kwa ajili ya kupeleka katika Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC).
  Habari kutoka ndani ya kamati hiyo inayoongozwa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa na Abdulrahman Kinana, zinabainisha kuwapo kwa mvutano baina ya wajumbe hao, hasa mapendekezo waliyoyaandika kwa ajili ya kuchukuliwa hatua kwa baadhi ya wanachama wanaoonekana kukiyumbisha chama.
  Mvutano mkubwa uliopo hivi sasa umetokana na baadhi ya vigogo wa chama hicho kupata taarifa za mapendekezo ya kamati hiyo, ambayo yanataka baadhi yao wang'olewe, huku wengine wakiiona hatua hiyo ni kali na yenye kupendelea upande fulani.
  Hali hiyo imeanza kuzusha hofu ndani ya chama hicho, hasa kwa baadhi ya vigogo wa chama hicho kuanza kufanya mikakati ya kupita huku na huko kuwaandaa wajumbe wa NEC ama wapinge au wakubaliane na mapendekezo ya kamati hiyo.
  Mmoja wa wajumbe ndani ya Kamati ya Mwinyi ameliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa hivi sasa wameanza kuchimbana kubaini ni nani aliyevujisha siri za mapendekezo yao waliyoyatoa, baada ya kufanya mahojiano na wabunge.
  "Katika hii kamati kuna watu watatu, taarifa zetu sasa zimevuja, hatujui ni nani aliyezivujisha, tunachunguzana kubaini nani aliyezivujisha," alisema mjumbe huyo.
  Aidha, chanzo hicho kimebainisha kuwa tayari kuna baadhi ya vigogo wameanza kufanya mbinu za kueneza taarifa mbalimbali ambazo si zile zilizomo kwenye mapendekezo ya kamati hiyo.
  Kuanza kwa mikikimikiki hiyo ya vigogo hao, kunamfanya Rais Jakaya Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM kuwa katika wakati mgumu, hasa kutokana na ukweli kuwa shutuma nyingi za ufisadi zinaelekezwa kwa baadhi ya watu alio karibu nao.
  Rais Kikwete ambaye aliunda kamati hiyo, atakuwa na wakati mgumu kutuliza jabza za pande zinazohasimiana katika chama hicho, ambazo zimeshamiri zaidi hivi sasa, hasa baada ya kutokea kwa kashfa ya Richmond ambayo ilimfanya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa kujiuzulu.
  Tangu kutokea kwa kashfa hiyo, kumekuwa na makundi mawili, moja la wapambanaji wa ufisadi linaloongozwa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta na lile jingine ambalo linadaiwa kuwa chini ya Lowassa na Rostam Aziz, likipinga kuhusika na ufisadi wa Richmond.
  Uwepo wa makundi hayo ndiyo unaokifanya chama hicho tawala kuwa na wakati mgumu hivi sasa, kwani baadhi ya maamuzi ya kichama na serikali yamekuwa yakipata wakati mgumu kupitishwa kutokana na kutofautina kwa makundi hayo.
  Wachambuzi wa masuala ya siasa, tangu mapema walishaonyesha wasiwasi na Kamati ya Mzee Mwinyi kushindwa kazi yake kutokana na mbinu zilizobainishwa kutumiwa, ambapo ilitajwa kuwa mahojiano hayatafanywa kwa mbunge mmoja mmoja, bali wote kwa pamoja.
  Aidha, jambo jingine lililokuwa likitoa hofu ya kushindwa kwa kamati hiyo ni uwepo wa Msekwa, ambaye alikuwa Spika wa Bunge kabla ya kiti hicho kuchukuliwa na Sitta aliyepata msaada mkubwa kutoka kundi la wanamtandao lililokuwa chini ya Lowassa na Rostam.
  Wachambuzi wa masuala ya siasa walibainisha pia kuwa, Msekwa asingeweza kumtendea haki Sitta kutokana na majeraha aliyoyapata kufuatia uchaguzi wa Spika uliojaa vimbwanga vya kila aina.
  Hofu ya wachambuzi hao ilitimia pale ulipofanyika mkutano wa pamoja ambao badala ya kutatua tatizo, wabunge walijikuta wakitoleana maneno ya kashfa ndani na nje ya kikao, jambo lililoashiria mbinu iliyotumika haikuwa muafaka.
  Lakini pamoja na machafuko yote yaliyotokea, kikao cha NEC chini ya Rais Kikwete kama mwenyekiti wa chama, ndicho kitakachoamua hatima ya wanachama wa CCM wanaoonekana kukiyumbisha chama hicho.
  source.tanzannia daima
   
Loading...