singidadodoma
JF-Expert Member
- Nov 11, 2013
- 4,394
- 1,536
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar, Kamanda Sirro alisema katika oparesheni hiyo, Desemba 22, 2015 alikamatwa mtuhumiwa aliyejulikana kwa jina la Simba S. Said (44) mganga wa kienyeji na mkazi wa Vingunguti jijini na alipohojiwa alikiri kuwafanyia majambazi dawa kabla ya kwenda kufanya matukio ya ujambazi.
Kamada Sirro alisema katika kipindi hicho cha Desemba, pia jeshi la polisi lilipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa, kuna majambazi maeneo ya Tabata yamekimbilia huko yakiwa na pikipiki ambapo polisi walifuatilia na kufanikiwa kukamata bunduki mbili aina ya PUMP ACTION ambazo namba zake zilikuta zimefutwa na zikiwa zimekatwa mtutu.
Aliwataja pia watuhumiwa wanane waliokamatwa kwa kipindi hicho cha Desemba, kuwa ni pamoja na Ibrahim Mussa (40), Mohammed Shaibu (20), Khamis Jafari (44), Abdulaziz Kikwanda (44), Juma Bakar Msangika (40), Fitina Ramadhan Chaupele (43), Dunia Rashid (50) na Khamis Omar Bankara (36).
Aidha, afande Sirro alisema kwa kipindi cha Januari 7, mwaka huu maeneo ya Gongo la Mboto, Dar jeshi lake lilimkamata jambazi sugu mmoja ambaye kwa kipindi kirefu alikuwa akitafutwa, jambazi huyo anaitwa Mkama Hassan, mkazi wa Mbagala Maji Matitu, Dar na alipopekuliwa nyumbani kwake alikutwa na bastola aina ya CHINESE ikiwa imefutwa namba na magazine yenye risasi 7.
Mahojino na mtuhumiwa huyo bado yanaendelea ili kuweza kuwabaini watuhumiwa wengine.
Akizungumzia upande wa pikipiki zilizokamatwa kwa tuhuma mbalimbali, Sirro alisema jumla ya pikipiki 600 zilikamatwa katika Mikoa ya Kipolisi ya Kinondoni, Temeke na Ilala huku akisisitiza kuwa, wote wanaoendesha pikipiki wakati taa za barabarani za kuongoza magari hazijamruhusu kupita lazima watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali hata sehemu ambazo hawaruhusiwi kufanyia biashara za bodaboda.