Kalamu Yangu
JF-Expert Member
- Dec 21, 2016
- 1,110
- 1,077
Tumeshafika nyikani,rungu huku sime kule,
Na mikuki mabegani,mbwa huku na kule,
Hatutorudi nyumbani,bado tunasonga mbele,
Kama hukuja kuwinda, usingekuja nyikani.
Ungebakia nyumbani,cheza na wadogo zako,
Mkaenda kisimani,uwatwishe ndugu zako,
Mkaziosha sahani,huku kweli sio kwako,
Kama hukuja kuwinda,usingekuja nyikani.
Eti waogopa mwitu,eti waogopa miba,
Mara unahofu chatu,na mkuki umebeba,
Eti wataka viatu,katambuga umebeba,
Kama hukuja kuwinda,usingekuja mwituni.
Eti huku kuna simba,mara waogopa mvua,
Unaulizia nyumba,wahisi tumepotea,
Utaja kosa mchumba,ukishindwa vumilia,
Kama hukuja kuwinda, usingekuja nyikani.
Wahangaikia uyoga, hiyo kazi ya dadako,
Mara waenda kuoga,huyataki masumbuko,
Umejawa na uoga,kama vipi rudi huko,
Kama hukuja kuwinda,usingekuja nyikani.
Bado washangaa kenge,swala anakukimbia,
Nawaza nikucharange,bakora kukushitua,
Mara vijiti uchonge,muda watupotezea,
Kama hukuja kuwinda,usingekuja mwituni.
Mwanaume huna haya,waogopa hata nyani,
Nyoka naye wamgwaya,mbonde rungu kichwani,
Eti wenzetu Ulaya,nyoka anawekwa ndani,
Kama hukuja kuwinda,usinge kuja nyikani.
Kitoweo wakipenda,kikiwekwa bakulini,
Nyikani wataka kwenda,na mikono mfukoni,
Utapikiwa mlenda,wende kula kwa jirani,
Kama hukuja kuwinda,usingekuja nyikani.
Hulka kubwa ulonayo,tutapofika nyumbani,
Maneno yakutokayo,eti wewe namba wani,
Hutaki kupiga mbiyo,ngoja tukwache mbugani,
Kama hukuja kuwinda,usingekuja nyikani.
Sungura tumempata,haraka kutia kisu,
Nafsi haijakusuta,asante wairuhusu,
Na mvi zitakuota,tabaki kuomba busu,
Kama hukuja kuwinda,usingekuja nyikani.....
"Kauli za Makabwela 2017"