Kada CCM alia na Sitta, Mwakyembe | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kada CCM alia na Sitta, Mwakyembe

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Tasia I, May 24, 2011.

 1. T

  Tasia I JF-Expert Member

  #1
  May 24, 2011
  Joined: Apr 21, 2010
  Messages: 1,226
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 135
  • Asema walimshawishi ajiunge na CCJ

  na Salehe Mohamed


  [​IMG]
  UPEPO wa kisiasa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) unazidi kuchafuka baada ya Katibu Msaidizi wa chama hicho wilaya ya Moshi, Daniel Ole Porokwa, kutoboa siri kuwa yeye na vigogo wenzake walikisaliti chama hicho tawala na kushiriki kwenye mchakato wa uanzishaji wa Chama cha Jamii (CCJ).
  Porokwa alisema aliyekuwa Spika wa Bunge la tisa ambaye hivi sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ndiye aliyekuwa kiongozi wa vikao wa mchakato huo ambao uliwahusisha pia Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM na Nape Nnauye.
  Kiongozi huyo alitoa akauli hiyo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu usaliti alioufanya kwa kushirikiana na wenzake katika kuanzisha CCJ.
  Porokwa alisema aliingia kwenye mchakato huo baada ya kufuatwa na Nape, Mwakyembe na Sitta wakitaka ashiriki kuianzisha CCJ huku wakimshawishi kuwa atapewa nafasi ya kuwania ubunge wa jimbo la Monduli kwa tiketi ya chama hicho akikabiliana na Edward Lowassa wa CCM.
  Alibainisha kuwa vigogo hao wa CCM walikuwa wakimhamasisha afanye haraka kukihama chama hicho, ili aharakishe mchakato wa uanzishaji wa CCJ, ili chama hicho kiweze kushiriki katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 30 mwaka jana.
  Alisema amefikia hatua hiyo ya kutoboa siri za wao kushiriki kwenye mchakato wa uanzishwaji wa CCJ baada ya kusikia Nape, Mwakyembe na Sitta wakipinga kauli iliyotolewa na makada wa CHADEMA kuwa vigogo wa CCM walihusika na mchakato wa uanzishaji wa CCJ.
  “Ni kweli niliwahi kuombwa kuwa mmoja wa wanachama waanzilishi wa CCJ, nilikutana mara kadhaa na Nape, Mwakyembe na Mpendazoe kabla hajahamia CCJ na baadaye CHADEMA, hoja kubwa ilikuwa ni kukianzisha chama hicho, ili kuitoa CCM madarakani,” alisema.
  Porokwa aliongeza kuwa makada hao wa CCM, walimuambia kuwa wamefikia hatua ya kushiriki kwenye uanzishaji wa CCJ, ili kuondokana na utawala wa kiimla ambao umekifanya chama tawala kutoaminiwa kukabidhiwa madaraka ya dola.
  Alisema makada wenzake walimuambia CCM imekosa mvuto mbele ya jamii kwa sababu kiliacha misingi iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Julius Nyerere, ya ukombozi wa kupigania haki za wanyonge lakini kilipuuza jukumu hilo na kimekuwa hakijali maslahi ya walio wengi na maadili ya viongozi wake yameporomoka.
  Alibainisha kuwa aliamua kuachana na CCJ baada ya kubaini kuwa Nape, Sitta, Mpendazoe na Mwakyembe walikuwa na ajenda binafsi na wala si kutetea maslahi ya Watanzania kama walivyokuwa wakisema.
  Porokwa, aliongeza kuwa kuyumba kwa CCM na kupoteza baadhi ya majimbo, kata na vitongoji kwenye uchaguzi mkuu uliopita kumesabishwa na uwepo wa viongozi wenye ajenda na masilahi binafsi tofauti na zile za chama.
  Kiongozi huyo pia alimnanga aliyekuwa Spika wa Bunge la tisa, Samuel Sitta, kuwa alitumia madaraka yake vibaya kwa kufanikisha uanzishwaji wa CCJ badala ya kuimarisha CCM.
  Porokwa, amemshauri Rais Jakaya Kikwete, kuachana na Sitta, Mwakeyembe, Nape na wengineo, ili kukinusuru chama na serikali yake inayoshutumiwa kwa kutojali maslahi ya wananchi. “Katika timu ya Rais Kikwete kuna wachezaji ambao wako tayari kujifunga na kuinyima timu yao ushindi, ni vema kuachana na wachezaji hao ili timu ipate matokeo mazuri uwanjani,” alisema
  Majibu ya Waziri Sitta

  Tanzania Daima lilimtafuta Waziri Sitta kujibu tuhuma hizo; alisema Porokwa ni kibaraka anayejaribu kujipendekeza kwa watu fulani waliompa jukumu la kuwachafua wengine kwa sababu wanazozijua wenyewe.
  Alisema Porokwa analipwa na watu kwa lengo la kuharibu sifa za watu akiwemo yeye ambao mara kwa mara wamekuwa mstari wa mbele kukemea ufisadi wa mali za umma. “Ndugu yangu weee…. Hili nimeshalizungumzia sana mpaka sasa nimelichoka, hao wanaoendelea nalo waache wafanye hivyo kwa utaratibu wanaouona unafaa, mwisho wake tutauona,” alisema.
  Dk. Mwakyembe ajibu

  Naibu Waziri wa Ujenzi Dk. Harisson Mwakyembe alisema ni vema Porokwa akawaeleza wananchi analipwa kiasi gani na watu waliomtuma kufanya kazi ya kuwataja anaowaita kuwa ni wasaliti wa CCM.
  Mwakyembe, alisema bado hajaliona tamko la Porokwa hivyo hayuko kwenye nafasi ya kuzungumza mengi zaidi juu ya kada huyo anayefanya shughuli ya kuwasafisha baadhi ya watu huku akiwachafua wengine. “Wapo wengi walionituhumu, hili la Porokwa kwangu si jipya, nendeni katika ofisi za Msajili wa Vyama vya Siasa mkathibitishe kama jina langu limo, lakini mmemuuliza amelipwa kiasi gani kwa kazi hii anayoifanya?” alihoji.
  Nape atoa onyo

  Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema hawezi kumjibu chochote Porokwa kwa kuwa kimadaraka ni mtu mdogo kwake na endapo atamjibu atakuwa anamuonea.
  Alisema anaweza kufikia hatua hiyo kama ataona kuna ulazima wa kufanya hivyo lakini ni lazima kwanza aone tamko lake alilolitoa kwa vyombo vya habari.
  Nape alisema anatoa wito kwa wote waliotakiwa na vikao vya chama wawajibike kwa tuhuma zinazowakabili wafanye hivyo kwa njia za kistaarabu badala ya kucheza sarakasi ambazo hazitabadilisha maamuzi ya vikao hivyo.
  “Sarakasi wanazozifanya wale walioambiwa wawajibike na vikao vya chama hazitawasaidia wahusika, wafuate maamuzi ya vikao,” alisema.
  Wakati huohuo, Dixon Busagaga na Beatrice Maina wanaripoti kutoka Moshi kuwa WAZIRI Sitta ameapa kwamba maovu yote yaliyo ndani ya CCM hawezi kuyakimbia na badala yake atapambana vikali ili misingi iliyoachwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, iendelee kuwa dira katika taifa.
  Sitta alibainisha hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa akitoa mada ya maadili ya uongozi katika kusimamia rasilimali za taifa katika kongamano la miaka 50 ya uhuru na uhusiano wa maisha ya Mtanzania lililoandaliwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Stadi za Biashara Moshi (MUCCoBS) lililofanyika chuoni hapo.
  Alisema pamoja na kwamba amepitia nyakati ngumu katika uongozi wake kwa sababu ya kupambana na ufisadi na mafisadi nchini, hatoacha kamwe kupambania haki za wananchi kwa kufuata misingi na kanuni za muasisi huyo.
  “Ninaapa kwamba maovu yote yaliyo ndani ya CCM tutapigana kwa uaminifu, usawa, uadilifu na mengine yote na siwezi kukikimbia chama tumo na tutapambana kweli kweli, ili kusimamia misingi aliyoiacha Mwalimu Nyerere ya usawa wa binadamu, kutobaguana kwa misingi ya dini au kabila, uadilifu na umoja,” alisisitiza Waziri Sitta.
  Aidha, alisema Tanzania si nchi maskini na kwamba inaweza kubadili maisha ya Watanazania endapo rasilimali za nchi zilizopo zitasimamiwa vizuri kwa kufuata misingi hiyo.
  Alisema endapo hayo yote yatafuatwa Tanzania ijayo itakuwa nchi inayojitambua kwa kuwa na sera za kiuchumi zinazotekelezeka kwa kujali maslahi ya maskini kwa huduma zinazotosheleza mahitaji ya maisha ya Mtanzania.
  sorce: mtanzania Daima.
   
 2. HOMOSAPIEN

  HOMOSAPIEN JF-Expert Member

  #2
  May 24, 2011
  Joined: Mar 31, 2011
  Messages: 719
  Likes Received: 60
  Trophy Points: 45
  CCM waelewe kuwa wameingiza nyoka mlangoni,huyu mtoto yupo kimaslahi zaidi, anachoongea ni kuwa ametumwa kufanya hivyo na kwa tabia fulani nayoijua,haya anayoongea kayafanyia mazoezi kabla ya kuyatoa tena mbele ya wakubwa fulani huko Arusha
   
Loading...