Na. M. M. Mwanakijiji
Kuna watu wanasema ‘lipeni deni la watu’ na wengine wanasema ‘dawa ya deni ni kulipa’. Katika sakata la kushikiliwa ndege ya Tanzania huko Afrika Kusini kambi mbili kubwa zimeibuka zikiwagawa Watanzania. Kambi hizi zinaonekana zinafuata mwelekeo wa kisiasa. Kuna kambi ya wanaoona kuwa serikali imejitakia na hivyo inastahili inachokipata na kambi nyingine ambayo inaonekana kuwa serikali inahujumiwa na kikundi Fulani.
Kukamatwa kwa ndege hiyo wiki iliyopita kumeacha maswali ya aina nyingi na hisia nyingi miongoni mwa wananchi. Ukimsikiliza msemaji wa Serikali Dkt. Abbas alipozungumza na waandishi wa habari leo unaweza kuona kuwa hata ndani ya serikali watu wamegawanyika na kuwa kuna hisia kuwa kilichotokea ni njama Fulani za kumkwamisha Rais Magufuli. Msimamo wa serikali kuwa itawashughulikia wale wote waliohusika katika kufanikisha kukamatwa kwa ndege hili kwa ‘kuhujumu uchumi’ linahitaji kuangaliwa kwa karibu na kufikiriwa kwa umakini mkubwa.
Mchawi Wetu ni Nani?
Swali kubwa ni kuwa ni nani alisababisha ndege hii ikamatwe kwa deni ambalo sreikali ilikuwa inalijua? Hili ni swali moja tu. Kukamatwa kwa ndege hii inaonekana kulifanywa kimkakati wa kisheria na waliohusika na waliinyemelea ndege bila vyombo vyetu vyovyote kujua au kuwa na taarifa na matokeo yake ni kile kilichotokea.
Je, mchawi wetu ni mdeni wetu Bw. Steyn? Au mchawi wetu ni wale wanasheria (wakiwemo Watanzania) ambao walibuni mkakati huu mkali? Au wachawi wetu ni vyombo vya Afrika ya Kusini ambao majuzi tu tumepokea ugeni wao na kuwaonesha ukarimu wetu na udugu wa damu? Je, Afrika Kusini ingejaribu hata kutukonyeza tu kutuambia ndege isiende Afrika Kusini kwa sababu kuna watu wanainyemelea? Au wachawi wetu ni serikali yenyewe ambayo ikijua kuwa imetia saini makubaliano ya kutekeleza hukumu za nchi za SADC na ilijua inadaiwa na kuwa mahali popote katika nchi ya SADC watu wanaweza kudai hukumu itekelezwe? Kwamba AG hakutoa ushauri mzuri wa matokeo ya kupeleka ndege huku bado kuna deni na madai dhidi ya serikali?
Haya si Maswali Muhimu Kivile
Naomba kupendekeza kuwa maswali haya siyo muhimu kivile kuliko hili swali linalofuatia. Binafsi swali ambalo ningependa nione linajibiwa na serikali ni hili: Kwanini deni la Bw. Steyn liliachwa kulipwa wakati tayari serikali ilishakubali, ilishaanza kulipa na ilikuwa inaendelea kulipa? Ndugu zangu hatuwezi kumpata mchawi au msaidizi wa mchawi bila kujua kwanza mchawi alitumia ungo gani! Hili ni swali muhimu sana; kama tuliacha kulipa deni ambalo ni deni halali basi hakuna mchawi. Mdai wetu alikuwa katika haki zake zote za kudai na kutulazimisha kumlipa. Lakini naomba kupendekeza yafuatayo katika kuangalia hili la kuamua kutokulipa deni.
1. Tuliacha Kulipa kwa Sababu Hatulipendi Deni
Hakuna mtu anayependa kudaiwa. Kudaiwa kunadhalilisha, kunafedhehesha na kwa kila kipimo kunafanya uwe unawiwa kihisia na kiakili. Ukiwa na deni kubwa inabidi uwe unalifikiria mara kwa mara, unalipigia mahesabu, na unalitafutia hela kulilipa. Lakini kama deni ni halali sisi kutokulipenda deni hilo hakuondoi uhalali wa kutakiwa kulilipa. Kutolipenda deni siyo sababu wala kisingizio cha kutokulilipa.
2. Tuliacha Kulipa kwa Sababu Hatulitaki Deni
Inawezakana tuliacha kuendelea kulipa kwa sababu hatulitaki hilo deni. Hatulitaki kwa sababu linatulazimisha kutumia fedha zetu kuwalipa watu wengine badala ya kutumia fedha hizo kufanya mambo mengine ya maendeleo. Kumlipa mtu mmoja bilioni 33 na ushee wakati nchi ina mahitaji mengine muhimu inaweza kuonekana ni matumizi mabaya ya fedha. Lakini ukweli bado ni ule ule; kama mtu anatudai basi anachodai si chetu ni chake na kutokutaka kulipa hakuondoi uhalali wa yeye kutudai au kutushinikiza kumlipa. Kutokulitaka deni siyo sababu wala kisingizio cha kutokulilipa.
3. Tuliacha Kulipa kwa Sababu Deni ni Kubwa Mno
Unapochukua deni au unapokubali deni hasa haya ya fedha mara nyingi yanakuwa na taratibu za yafuatayo. Kuna deni la msingi (principle), kuna adhabu (punitive damage) na kuna riba (interest). Deni la msingi ni kile hasa kinachodaiwa na adhabu ni kile kilichoamuliwa kuwa ni adhabu kwa sisi kusababisha deni. Riba ni kile kiasi cha asilimia ambacho kinatakiwa kulipwa juu ya deni kwa kila muda au kiasi ambacho deni linakuwa halijapwa.
Riba inaweza kuwa ya aina nyingi; kuna riba zinatakiwa kulipwa kila siku deni halijalipwa, au kila mwezi na inaongezeka kwa kadiri deni halijalipwa.
Kitu kibaya katika riba ni kuwa kama deni halijalipwa kwa wakati uliotakiwa riba inaweza kuwa kubwa sana kiasi hata cha kupita deni lenyewe. Taasisi nyingi za fedha na zinazotoa mikopo zinatengeneza fedha (faida) kwa kupitia riba kuliko deni la msingi. Mtu akikopa shilingi laki moja halafu baada ya mwezi mmoja akarudisha shilingi laki moja yule mtoa mkopa anapata faida gani? Hana! Hivyo riba na adhabu ni namna ambazo mtu, shirika au taasisi inavuna kutoka kwa mkopaji.
Mkopaji hawezi kusema sitaki tena kulipa riba kwa sababu ni kubwa; hili lilitakiwa liwe limekubaliwa wakati wa majadiliano.
4. Tuliacha Kulipa Deni kwa sababu Deni Halilipiki
Sasa wakati mwingine mtu anaweza kujikuta anaacha kabisa kulipa deni (servicing a debt) kwa sababu anaamini na anajua kuwa hata ajaribu vipi hatoweza kumaliza kulilipa deni hilo; ama kutokana na ukubwa wa deni au kutokana na uzito wa adhabu na riba.
Kuelekea mwaka 2000 kulikuwa na kampeni kubwa ya kimataifa ya kutaka madeni ya nchi za dunia ya tatu yasamehewa. Hii ni mojawapo ya kazi kubwa alizofanya Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere kabla ya kifo chake akiwa na watu wengine mashuhuri kama Bono wa U2. Hoja zao zilikuwa za aina mbili tu; kwamba madeni hayo hayalipiki kwa sababu 1. Nchi maskini hazikuwa na uwezo wa kulipa madeni hayo kutokana na umaskini na 2. Madeni hayo yaliingiwa katika mazingira ambayo yaliyafanya yawe ya kionevu (immoral). Nchi tajiri hazikuwa na sababu ya kuwabana maskini wawalipe kutoka katika umaskini wao huku wao matajiri wakizidi kuongeza katika utajiri wao. Na kweli, nchi nyingi tajiri zilifutia nchi maskini madini na kuwapa nafasi ya kuanza upya.
Sasa deni hili linaweza kuangukia huko?
Je, deni la Steyn linaweza kuangukia huku? Kwamba, tumelipa kiasi kikubwa cha deni la msingi, na hata riba tumeilipa lakini inaonekana haiishi na haiwezekani kuisha. Kwamba, nchi yetu bado ni maskini na kulipa fedha hizi zote ni kukubali kuendelea kuwafanya Watanzania waishi kimaskini na kuendeleza umaskini.
Tatizo la hoja hii ni kuwa kama hii ni Imani ya serikali basi ilitakiwa ianishwe na kuwekwa bayana katika vyombo husika vya kimahakama na kufanya mazungumzo na mdai wetu kuweza kukubaliana kile kinachoitwa “settlement”.
Haja ya kuwa “Settlement”
Naomba kupendekeza kuwa kwa sababu yoyote ya hapo juu ni wazi kuwa inatulazimu na serikali inalazimika kufikiria kufikia mwafaka (settlement) na mdai wetu. Mwafaka huo unaweza kulamishwa na matokeo ya kesi iliyofunguliwa na serikali huko Afrika ya Kusini. Mahakama inaweza ikatoa muda kwa ndege kuachiliwa lakini wahusika wakae chini na kukubaliana mwafaka – bila kutafutana uchawi.
Kwamba, tukubaliane badala ya kumlipa bilioni 33 tuwe tayari kumlipa bilioni 15 kwa mkupuo bila riba wala adhabu. Lakini na yeye aondoe madai yote dhidi ya serikali na serikali kuondoa madai yoyote dhidi yake. Na kwa upande wake serikali inaweza kumrudishia ofa yake ya uraia wa Tanzania (inawezekana hili lilimuumiza zaidi).
Kumbe wakati mwingine madeni yanaweza kumalizwa kwa mazungumzo baina ya pande mbili badala ya kutumia visasi. Kwani serikali ikiamua kubana inaweza kubana tena.
Lakini vyovyote tutakavyofanya itakuwa ni kosa kubwa sana kuanza kuwatafuta wachawi nje ya wachawi wenyewe. Na ili tujue mchawi wetu hasa ni nani ni lazima tujibu hili swali: Kwani kwa nini tuliacha kulipa deni ambalo tulishakubali kuwa ni halali na tulishaanza kulilipa?
Niandikie:
mwanakijiji@jamiiforums.com