Jongea Mtanzania

Oct 29, 2012
22
4
MIFUMO YA KINYONYAJI, TULIPOKOSEA HAPAZUNGUMZIWI:

Matamanio ya kuwepo kwa jamii adilifu isiyokuwa na matajiri na masikini, wenye kunyonya na wenye kunyonywa, wenye kukandamiza na wenye kukandamizwa, wenye kuyafaidi mafanikio yote ya utamaduni na wenye kunyimwa fursa kama hiyo yana historia za karne.Hapo zamani kulikuwa na wataalamu hodari si haba waliojaribu kuasisi nadharia kadha wa kadha za ujenzi wa jamii adilifu, ambazo baadae ziliitwa kuwa ni nadharia za ndotoni.(Utopian thinkers) Miongoni mwa wanafikira hao walikuwa ni Thomas Moor, Robert Owen, Charles Fourier na Anrie Saint Simon. Tunawiwa kujua kwamba imani za kuania haki, uhuru, usawa na udugu (Fraternity, liberty, and equality) wa binadamu pia zilianza zamani sana hata mnamo miaka ya 1848 katika Mapinduzi Makuu ya Kibwenyenye nchini Ufaransa.

Lengo lilikuwa ni mwito wa imani za kiutu kwa mfumo wa Kibepari (capitalism). Huu ni mfumo uliotegemezwa juu ya miliki ya kibinafsi ya nyenzo kuu za uzalishaji mali.

Ni mfumo wa miliki ya kibinafsi unaomwezesha mtu mmoja au kikundi cha watu kujitwalia matunda ya jasho la wenzio walio wengi na kuigawanya jamii katika matajiri na masikini, makabaila na watwana (wakulima), mabepari na wafanyakazi na makundi mengine katika jamii.Kutokana na kuwepo kwa mfumo huo wa kujilimbikizia mali (concentration of capital into the hands of few), Ufisadi hauwezi tokomezwa Tanzania kwani viongozi wanatumia fedha na rasilimali nyingi ili waweze kupata madaraka katika nyanja za kisiasa ili pia waweze kulinda maslahi yao binafsi kama vile biashara.

Hii ni kweli tupu kwani uwezo wa wachache kutawala shughuli za kiuchumi kunawawezesha pia kuzitawala shughuli za kisiasa, kuisimamia serikali na kuielekeza katika kutetea maslahi yao ya kichoyo pamoja na fursa zao nyingine huku wakiwanyima Watanzania walio wengi haki zao. Ni katika mfumo huu wa kujilimbikizia mali kwa wachache ambako hata haki ya kupata ajira haijatajwa kabisa
Nitakuwa niko sahihi kabisa nisemapo kwamba ukosefu wa ajira (massive unemployment) ni mwandamizi wa kudumu wa mfumo wa kibinafsi.

Mara nyingi mfumo wenye kutegemezwa juu ya miliki ya kibinafsi ya nyenzo kuu za uzalishaji mali hupotosha malengo na madhumuni ya kiasili ya maendeleo ya kiuchumi ya jamii kwa ujumla na badala yake mabepari hawa hutafuta kunako faida zao wenyewe ili waweze kuunda na kuzidisha faida za kikundi cha matajiri wachache.
Mfano hai ni baadhi ya viongozi wa serikali wanaopewa dhamana ya kusimamia baadhi ya shughuli zenye manufaa kwa jamii kama vile ujenzi wa shule, ofisi na barabara. Wengi wao huwa wanakuwa na shauku ya kupata faida kutokana na shughuli wanayosimamia, katika shughuli za ujenzi wa nyumba mathalan, wengi hutamani kwamba pindi wamalizapo shughuli hizo basi nao wawe wamejenga zao majumbani mwao kwani lengo lao ni kuongeza faida (Profit maximization). Hatma ya hali hii ni kwamba hawa wachache waliojilimbikizia mali wanakuwa na sauti na kauli ya mwisho dhidi ya maisha ya masikini walio wengi.

Tukumbuke kwamba kushindwa kujipatia riziki ya kutosha kwa waliowengi kunawafanya wasiwe na sauti na kujiamulia wenyewe maswala mbalimbali. Ndiyo maana nasema kwamba wanasiasa wa Tanzania wanatumia umaskini wa waliowengi kama mtaji wao kisiasa kwani mkulima wa chini anarubuniwa na vyakula tu na kisha kutoa kura yake kwao na kisha mfumo wa kujilimbikizia mali kuzidi kushika chati katika jamii.
Lakini pia kama tutakuwa makini na waelewa wa mambo sitojali wala kushangaa wazalendo wanaomlaumu na pengine kumkosoa hayati Mwalimu Nyerere kwani ni dhahiri kwamba kama ni kosa basi "baba wa taifa" alilifanya hadharani japo hakupatikana mara moja wa kumkosoa yeye na mienendo yake ya kupambana na mifumo (…)

Moja ya kosa alilolifanya Mwalimu lipo kwenye njia zile alizozitumia kupambana na mfumo wa kibepari. (capitalism).Ndugu zangu,historia na mantiki vinatuonesha na kutufundisha. Ubepari, na kaka yake ubeberu (imperialism),ubwenyenye na "ubwana mkubwa"yote hii inaendeshwa kiuchumi na kisha kuchota nyanja nyingine zikiwemo siasa na jamii (Ni miradi ya kiuchumi). Lakini ajabu ni kwamba mwalimu alishindwa kupambana nayo. Alipambana na mifumo hii kisiasa. Ni kweli kwamba viwanda mbadala vya kuondoa bidhaa za kigeni (import substitution industries) vingepunguza kasi ya utegemezi kwa nchi ya Tanzania na hatimaye kutuepusha na ubepari ambao tungeuzalisha kutokana na matabaka mawili ya "wavuja jasho" na "wavuna jasho" (???)

Lakini pia yatupasa kujihakiki na kurejea alichokifanya Mwalimu kuwa na vipaumbele vingi vilivyoelemea mapato ya taifa na kujikuta tukishindwa kukamilisha kile tulichokua tumekidhamiria cha kujenga viwanda vya ndani (domestic industries).
Badala yake kwa wakati mmoja tunataka viwanda, na vilevile tunataka kuwa wakulima "mashuhuri". Binafsi sipingi wazo la mwalimu la kuhamasisha kilimo kwani ndiyo njia mama kwa "nchi zetu za Kiafrika" ya kupambana na njaa pamoja na kulipatia "tabaka lalwa"kipato, bali kuwa na vipaumbele zaidi ya vitatu(vingi) kwa wakati mmoja na kwa mwaka mmoja wa fedha. Kuna msemo wa wazungu kwamba "unataka kula keki yako na pia unataka kubaki nayo". Tatizo hili hadi leo hii katika serikali zetu za kiafrika ikiwemo Tanzania linazidi kututafuna. Hili ni kosa kubwa ambalo mara nyingi linasababishwa na tamaa za kisiasa za kujitahidi kumridhisha kila mtu kwa kuipa kipaumbele kazi anayoifanya.

Ndugu zangu, yatupasa sana kumtazama Mwalimu na mienendo yake ya kuikiomboa Tanzania kutoka kwa weupe (whites) na kisha tuweze kuitofautisha mienendo hiyo na ile aliyoifanya ya kujenga uchumi wa kitaifa (reformation of national economy). Mwalimu asingeweza kukosolewa kwa njia zake za kuiletea uhuru Tanganyika hata kama zingekuwa za "kiujanja-ujanja" kwa sababu sote tuliutamani sana uhuru. Lakini kwa hili la Mwalimu la kujenga uchumi wa kitaifa, kuna mapungufu yake na ni lazima tuyaseme ili leo na kesho tuweze kujirudi na kuangalia ni wapi tulipojikwaa na kisha kuondoa mitego na vikwazo vilivyopo.
Leo hii Mtanzania ataitwa mpinzani (wa maendeleo),mkosa fadhila na pengine mwendawazimu kwa kuwa tu amejaribu kuainisha aliposhidwa mwalimu Nyerere. Hii ni kwa sababu mwalimu ndiye kiongozi "pekee" aliyeweza kusimama "kwa miguu yake"(?) kuitetea nchi yake ya Tanganyika na kisha "kuiletea" uhuru mwaka 1961! (…)

Dr. Nkrumah ("Simba wa Afrika") aliishi gerezani kwa miaka na kisha kuendesha harakati za Umaimui wa Afrika (Pan-Africanism) akiwa kama kiongozi baada ya kuhudhuria kongamano la mwisho na kubwa lililowahi kutokea mnamo miaka ya 1945 kule Manchester (uingereza) ambako alikabidhiwa jukumu zito na watu weusi duniani la kutetea haki, utu na uhuru wao.Ni jukumu ambalo kwa mwanaharakati yeyote ni zito na linataka kujitolea mali, muda na hata uhai kwa ajili ya ukombozi wa taifa na bara zima kwa ujumla wake.

Aliendesha harakati vizuri akiwa kama kiongozi na miaka kumi na miwili baadae (1957) aliongoza Ghana (nchi yake) kupokea uhuru kutoka kwa mtu mweupe. Hakuna aliyemkosoa wala kumpinga. Hii ni kwa sababau hakuna asiyependa kuwa huru. Lakini
alipoongoza nchi na kuzembea uchumi wa Waghana,alitimuliwa na Waghana na ukawa ndo mwisho wa uongozi wake kwa wana wa Ghana. Je, Mwalimu ni mtu wa tofauti sana na shujaa huyu mpambanaji ambaye pamoja na ushujaa wake wote wananchi wake waliwiwa kumkosoa pale alipokosea?

Mwalimu ni binadamu tofauti na Frantz Fanon, au mkewe aliyekuwa na maumivu makali moyoni kiasi cha kujidondosha kutoka ghorofani kwa kuona wananchi wakiteseka? Mwalimu wetu anayotofauti kubwa sana na Bishop Abel Muzorewa, Ndabaningi Sithole waliopambana kwa njia mbalimbali nchini Zimbabwe?
Steven Bico alipambana kumng'oa mnyonyaji katika nchi yake hadi mauti ilipomfika na leo hii tunamkumbuka kama shujaa wa Afrika, lakini alikuwa na mapungufu yake ambayo binadamu kamilifu yampasa kuwa nayo. Je, si sawa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere?.Au si kama Haile Selasie aliyeshirikiana na ras Imru kupambana dhidi ya uvamizi wa Italy ikiongozwa na fashisti Benito Mussolin hadi waafrika tukaona fahari atuongoze na awe kiongozi wa kwanza wa umoja wa Afrika (O.A.U)?.Tuwe makini. Tena sana. Au tukubali hukumu itakayotolewa na historia ikishirikiana na mantiki.

Ndugu zangu,mimi ni mzalendo na naipenda sana nchi yangu Tanzania na nilishaapa kuilinda kwa kuifanyia marekebisho ya kimfumo na kimuundo kupitia ushauri na ukosoaji lakini pia kiutendaji kama Mwenyenzi Mungu ataniruhusu kuendelea kuwa hai. Lakini hili haliambatani na kutetea na pengine kumtukuza Mwalimu wetu kama malaika kwa kuainisha ushujaa wake pasi na kumkosoa kwa yale aliyoyashindwa na ambayo yanawezekana kufanyiwa marekebisho.
Kuna msemo wenzetu wafaransa wanapenda sana kuutumia usemao "errare human este" na wazungu hutumia msemo "to err is human" wakimaanisha "kukosea ni ubinadamu". simkosoi mwalimu kwa kukosea au kuwa na mapungufu niliyoyasema awali kwa kuwa alikuwa binadamu, bali naikosoa na pia kuishangaa sana jamii ya wasomi wanaoshindwa na kuficha kutamka mapungufu ya mwalimu huku vinywa vyao vikibubujikwa na sifa tele kwa Mwalimu Nyerere.

Pengine hata mwalimu mwenyewe angepata fursa toka kwa Mwenyenzi Mungu ya kuitembelea Tanzania angeweza kukishangaa sana kizazi cha sasa ambacho hakijaweza kubaini mapungufu (weaknesses) yake japo yapo wazi na badala yake tumebaki kumsifia wakati tatizo kubwa alilolikumba na akashindwa kupambana nalo linazidi kuizika nchi.

Jongea Mtanzania! Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Afrika. Amen

Mwandishi wa makala hii ni Mwanafunzi wa Shahada ya Uhasibu katika sekta za Umma (BAF-LGAF)mwaka wa pili Chuo Kikuu Cha Mzumbe, pia ni Naibu Waziri Mambo ya Nje serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu Mzumbe na
KATIBU MWENEZI CHADEMA – CHUO KIKUU MZUMBE.
Ebenezer Kwayu – 0764013330
kwayuebenezer@yahoo.com
 
Back
Top Bottom