John Pombe Magufuli Anavyotarajiwa kuibeba CCM kwa kete ya kukosa makundi.

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482

Dk John Joseph Pombe Magufuli.


August 5, 2015
Wakati ikiaminika kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaingia katika Uchaguzi Mkuu kikiwa ‘kimepasuka' kutokana na baadhi ya makada wake muhimu kuhamia kambi ya upinzani, mgombea urais wake John Magufuli amechukua fomu rasmi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).

Hiyo ni hatua muhimu ya kutambulika kwake rasmi kuianza safari ya kuutafuta urais, nafasi ya juu kuliko nyingine katika taifa hili lililopata uhuru wake Desemba 9, 1961.

Ingawa kwa misingi ya siasa na kuimarisha umoja na mshikamano wapo wanaoweza kupinga hoja ya kuwapo mtikisiko CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu, matukio kama ya kuhama kwa waliowahi kuwa mawaziri katika serikali na viongozi wake siyo jambo lenye tija.

Lakini jambo linaloweza kubeba maana sana wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu ni ukweli kwamba Magufuli anaiwakilisha CCM ‘iliyopasuka' akiwa si mmoja wa vyanzo vya hali hiyo.

Pamoja na kuwa na kikundi cha watu waliomshawishi ama kumuunga mkono aombe kuteuliwa katika nafasi hiyo, Magufuli hakuwahi kubainika wakati na mahali popote akiwa na kundi la wana-CCM wanamuunga mkono dhidi ya wale wasikuwa pamoja naye.

Kuwa na makundi ndani ya chama cha siasa kiasi cha kuibua mvutano miongoni m wao kumebainika kuwa moja ya sababu iliyovifanya vyama vingi vilivyokuwa madarakani kushindwa kwenye Uchaguzi Mkuu.

Hata CCM ‘inapopasuka' kwa kiwango ambacho hakikutarajiwa, kwamba hata aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Mkurugenzi wa masuala ya uchaguzi, Matson Chizii, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai, Naibu mawaziri, Goodluck Ole Medeye na Dk Makongoro Mahanga wakiwa miongoni mwa wana-CCM wanaoonekana upinzani, si jambo la kupuuzia.

Lakini miongoni mwa mambo ambayo ‘yataibeba' CCM katika kukabiliana na hali hiyo ni kuwapo kwa mgombea urais (Magufuli) asiyetokana na makundi yaliyojiimarisha ndani ya chama hicho.

Magufuli anapotoka katikati ya wanachama wa CCM wasiogawanyika dhidi yake (kutokana na kutoasisi na kuendeleza siasa za makundi) inakuwa tija kwa chama hicho na kupata nguvu kubwa za kisiasa katika kukabiliana na mgombea Edward Lowassa atakayesimamishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mbali na Chadema, Lowassa ataungwa mkono na vyama vinne vilivyo katika vuguvugu la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Hivyo ni Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD. Hii ina maana kuwa uteuzi wa Magufuli unawaweka wana-CCM pamoja katika kumuunga mkono na kuzisimamia kampeni za chama hicho pasipo hila, kinyongo wala hujuma zinazoweza kuwaathrii katika kuchuana kwao na nguvu ya Ukawa.

Inawezekana isiwe ndani ya waliopo ndani ya CCM pekee, lakini Magufuli anaweza kuwavuta hata walioikimbia CCM kutokana na sababu tofauti, wakimuona kuwa si mshiriki wa kadhia zilizowafanya wakihame chama hicho na hivyo kumuunga mkono na kumpigia kura.

CHANGAMOTO

Hata hivyo, pamoja na hali hiyo Magufuli atarajie kukutana na changamoto zitakazojengwa kwa hoja nyingi zikihusishwa na utendaji kazi, uamuzi ama kauli alizowahi kuzitoa akiwa Waziri katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Orodha ya mambo hayo inaweza kuwa ndefu, lakini kinachotarajiwa zaidi ni kile kinachoitwa kashfa ya uuzaji wa nyumba za serikali uliofanyika akiwa Waziri wa Ujenzim katika serikali ya awamu ya tatu iliyoongozwa na Benjamin Mkapa.

Ndiyo maana wanaoijenga hoja hiyo wana kauli kwamba ‘Magufuli aliuza nyumba za serikali'. Ni kweli kuna nyumba za serikali zilizouzwa wakati huo.

Hata hivyo, bado ukweli unabaki kwamba ukiondoa maslahi ya kisiasa, waziri mmoja kama Magufuli hawezi kufanya uamuzi (kama wa kuuza nyumba za serikali) pasipo idhini ya Baraza la Mawaziri linaloongozwa na Rais aliyepo madarakani.

Ufahamu wa kawaida unadhihirisha wazi kwamba idadi ya nyumba zilizouzwa na mahali fedha zilipolipwa (kuhifadhiwa) ni mchakato usiohitaji kumuweka mtumishi mmoja kama Waziri katika hatia, isipokuwa kama aliigeuza ofisi ya umma na `kufanya mambo yake' kwa maslahi binafsi.

Lakini kama ni suala la kuuzwa kwa nyumba za serikali pekee, tukio lilioibua hasira kiasi kwamba hata sasa bado halikubaliki kwa walio wengi, ukweli unabaki kuwa lawama hazimstahili mtu mmoja isipokuwa mfumo na washiriki wote wanaotambulika kwa mujibu wa Katiba, kufikia uamuzi huo.

Hivyo ikiwa jambo hilo litaeleweka vizuri kwa umma, bado Magufuli ataendelea kuwa ‘msafi' dhidi ya tuhuma hizo, hali itakayochagiza CCM kugusa hisia chanya za wananchi na hivyo kuwa na uhakika wa kupata kura kwa mgombea huyo.

KAULI ZA JEURI
Changamoto nyingine inayotajwa dhidi ya Magufuli ni ujeuri. Wapo wanaoamini kuwa mwanasiasa huyo ni jeuri na amekuwa akitoa kauli zisizokubalika kwa wananchi wa kawaida.

Miongoni mwa kauli hizo na ambayo inaweza kutumika wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu ni alivyowaambia wakazi wa Kigamboni wasiokuwa na uwezo wa kulipia nauli ya kivuko, wapige mbizi, waongelee kuvuka bahari ya Hindi wanapokuja maeneo ya katikati ya jiji hilo.

TAFSIRI YAKE
Lakini zipo taarifa zaidi zikiwamo zinazomhusisha Magufuli na kutofautiana na wataalamu katika wizara alizowahi kuziongoza hivyo kuibua wasiwasi kwamba huenda akaiathiri nafasi ya Urais ikiwa atachaguliwa kushika wadhifa huo.

Upo ushahidi wa kimazingira unaoweza kutumika kumuweka Magufuli kando ya kusudio la kuwataka wakazi wa Kigamboni kupiga mbizi ili wavuke kutoka kwenye makazi yao kuja maeneo ya katikati ya jiji.

Mazingira hayo ni pamoja na hulka ya Watanzania kuzungumza kwa mifano na utani pale mhusika anapohitaji kufikisha ujumbe kwa namna na mazingira yaliyopo. Lakini inawezekana ikatokana na umma unaomsikiliza mhusika kama Magufuli, kutompa nafasi ya kuwasilisha kile alichokikusudia hivyo kutoa kauli iliyotafsiriwa kwa mtazamo hasi.

Changamoto hiyo na ile ya utendaji kazi wake unaotofautiana na ushauri wa wataalamu wizarani inapaswa kujibiwa na Magufuli anayeujua ukweli ama wasaidizi watakaomnadi katika kuhakikisha kuwa anapata ushindi.

MTAJI WA UJASIRI

Lakini hoja hiyo inaweza pia kugeuka kuwa mtaji wa ujasiri kwa Magufuli kwamba si kiongozi mwenye hulka ya kuridhishwa na ‘taarifa za kwenye karatasi' hata kama haziakisi ukweli unaogusa maisha ya watu.

Kwa maana zipo taarifa nyingi za watalaamu, mathalani ya kuhusu bei elekezi za mazao zinazotokana na gharama za uzalishaji, kutokuwa rafiki kwa mkulima hivyo kuzidisha hali ngumu ya maisha kwa kada hiyo.

Mfano mwingine ni wakati aliyekuwa Waziri wa Maji, Stephen Wasira alipotofautiana na wataalamu wa wizara hiyo waliositisha kusukuma kiasi kikubwa cha maji kutoka Ruvu Chini kwa madai kuwa ‘huenda' mabomba yakapasuka.

Wasira alikataa ushauri huo baada ya wataalamu kushindwa kumthibitishia ikiwa hali hiyo iliwahi kufanyika na matokeo yake yakawa ni kutoboka kwa mabomba hayo.

Kwa hiyo pamoja na hoja ya ‘ujeuri' kuelekezwa kwa Magufuli, bado kuna upande mwingine unaomjenga katika sifa ya kuwa kiongozi mwenye msimamo na asiyeyumbishwa na hila zinazojengwa kwa ‘mgongo' wa utaalamu.

Kwa hali ilivyo, bado Magufuli anatarajia kupata ushindani mkubwa kutoka kwa Lowassa, lakini hadi kura zitakazopigwa Oktoba 25, mwaka huu zitakapohesabiwa, zitatoa matokeo yenye kumpa ushindi mgombea atakayeshinda.

MAGUFULI NI NANI?

Magufuli, alizaliwa Oktoba 29, 1959 wilayani Chato, wakati huo ikiwa ni sehemu ya mkoa wa Kagera. Hivi sasa ipo mkoa mpya wa Geita.

1967 – 1974: Shule ya Msingi, Chato
1975 – 1977: Shule ya Msingi Katoke, Biharamulo, Kagera
1977 – 1978: Shule ya Sekondari Lake, Mwanza
1979 – 1981: Shule ya Sekondari ya Juu Mkwawa, Iringa
1981 – 1982: Stashahada ya Kemia na Hisabati, Chuo cha Mkwawa, Iringa.
1985 – 1988: Shahada ya Kwanza ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Kemia na Hisabati).
1991 – 1994: Shahada ya Uzamili (Kemia), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza.
2006 – 2009: Shahada ya Uzamivu ya Kemia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mafunzo
Machi –Juni 1984: Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mpwapwa mkoani Dodoma.
Januari –Machi, 1984: JKT Makuyuni, Arusha.
Julai – Desemba 1983: JKT Makutupora, Dodoma.
Uzoefu wa kazi
2010 – hadi sasa: Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Chato.
2008 – 2010: Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Samaki.
2005 – 2008: Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
2000 – 2005: Waziri wa Ujenzi
1995 – 2000: Naibu Waziri wa Ujenzi.
1989 – 1995: Mkemia Chama cha Ushirika cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.), Mwanza.
1982 – 1983: Mwalimu Shule ya Sekondari Sengerema

Chanzo: NIPASHE
 
mkuu hizo Porojo watu wamechoka wanataka mabadiliko ambayo CCM imeshindwa kuwaletea wananchi miaka kenda sasa na tumekatat tamaa na CCM, mkuu unajua hilo. hata Ukiweka JIWE pamoja na Magufuri watu tunachagua JIWE!!!
 
Back
Top Bottom