Habari hii ni ya Gazeti la Uhuru la Chama Cha Magamba (CCM), hebu isome kisha linganisha na habari iliyoandikwa na Habari Leo.
JK akemea wahandisi
WEDNESDAY, 06 JULY 2011 10:38 NEWSROOM



Na Fadhili Abdallah, Kigoma
RAIS Jakaya Kikwete amesema serikali itawachukulia hatua wahandisi washauri wanaoshindwa kuwasimamia ipasavyo makandarasi wa ujenzi wa barabara. Kiongozi huyo pia amewataka Watanzania kusali ili kuhakikisha amani iliyopo nchini inadumishwa kwa ajili ya maendeleo. Rais alisema hayo mjini hapa jana, kwa nyakati tofauti alipozindua ujenzi wa daraja la mto Malagarasi, na alipokuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Kidahwe Uvinza, yenye urefu wa kilomita 76, inayojengwa kwa kiwango cha lami na kampuni ya Chico ya nchini China. Alisema hatua ya wahandisi hao kushindwa kusimamia kazi kikamilifu imekuwa ikisababisha hasara kubwa kwa serikali, huku barabara nyingi zikijengwa chini ya kiwango. Rais Kikwete akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Kidahwe hadi Uvinza juzi, alisema tatizo la ujenzi chini ya kiwango halitokani na makandarasi pekee, bali ni matokeo ya usimamizi mbovu unaofanywa na wahandisi washauri.
Kuhusu kudumishwa amani, alisema kuvurugika kwake kutakuwa na athari kubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ukiwemo wa daraja la Malagarasi. Alisema miradi ya barabara na madaraja imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha za ndani na nje ya nchi kutoka kwa wahisani, hivyo kuvurugika amani kutawafanya wahisani kusita kutoa fedha za kutekeleza miradi. Rais alisema ametimiza ndoto aliyoingia nayo Ikulu mwaka 2005, kuhusu kuanza ujenzi wa daraja la mto Malagarasi, ambalo lilikuwa kero kubwa kwa wananchi.Alisema makandarasi wamemhakikishia mradi huo utakamilika ndani ya kipindi cha miaka mitatu, na litaleta ukombozi kiuchumi kwa wananchi wa mkoa wa Kigoma.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alisema sh. bilioni 85 zitatumika katika utekelezaji wa mradi huo, gharama ambayo inahusisha ujenzi wa kilomita 48 za barabara kwa kiwango cha lami, kati ya hizo kilomita 24 ni kwa kila upande wa daraja hilo. Dk. Magufuli alisema utekelezaji wa mradi huo unahusisha ujenzi wa daraja kubwa lenye urefu wa mita 200 na madaraja ya pembeni mawili yenye urefu wa mita 50 na mita 25. Pia kutajengwa makaravati 10 makubwa ya zege na mengine 80 madogo.
Naye Balozi wa Jamhuri ya Watu wa Korea nchini, Yoong Hoon Kim, alisema ujenzi wa daraja hilo umeonyesha ushirikiano wa karibu na wa kindugu uliopo kati ya serkali ya Tanzania na Korea. Alisema nchi hiyo itaongeza misaada maradufu. Wakati huo huo, baadhi ya wabunge wamewajia juu wenzao wanaobeza safari za nje zinazofanywa na Rais Kikwete, kwa madai kuwa hazina tija. Wakichangia makadirio ya matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Stephen Ngonyani (Korogwe Vijijini -CCM), alisema katika awamu ya kwanza ya uongozi wa Rais Kikwete amefanya mengi. Alisema kumekuwa na utawala bora katika nchi ambayo kila Mtanzania amekuwa huru kuzunguza juu ya kero mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuikosoa serikali. Ngonyani alisema rais hajaenda kujifurahisha nje ya nchi, bali kuomba misaada kwa ajili ya Watanzania bila kujali itikadi.
"Hata hapa tumekaa tunatanua midomo kuhusu safari hizo, huu ni utawala bora alioleta Rais Kikwete na tutamkumbuka akiondoka. Tumepata misaada mingi ya kuimarisha miundombinu, wanaomsema vibaya wana husda na urais," alisema.
Naye Said Jafo alisema baadhi ya wabunge wamekuwa wakitumia vibaya midomo yao kwa kumbeza Rais Kikwete.
Alisema rais anapokuwa safarini haendi kwa manufaa ya familia yake, bali kwa Watanzania wote.
Tatizo kubwa la Waandishi wa habari walio wengi walikimbia Hisabati kwa madai kuwa ni somo gumu, sasa angalia wanavyopotosha umma na kusababisha wananchi kuichukia serikali yao hasa kipindi hiki ambapo ufisadi umeshika kasi.