JK atoa salamu za mwaka mpya | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

JK atoa salamu za mwaka mpya

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by MziziMkavu, Jan 2, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jan 2, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,613
  Trophy Points: 280
  JK atoa salamu za mwaka mpya

  1st January 2012


  Awakaripia wanaowatisha umma mjadala wa Katiba
  [​IMG] Aridhishwa kwa utulivu na usalama uliopo nchini
  [​IMG] Asikitishwa kwa majanga yaliyotokea mwaka 2011  [​IMG]
  Rais Jakaya Kikwete


  Rais Jakaya Kikwete amekaripia hatua ya watu wanaotoa vitisho na kuzuia umma usishiriki katika mjadala unaohusu uundwaji wa Katiba mpya.
  Mjadala kuhusu muswada huo unafuatia kupitishwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, inayotoa mwongozo wa namna mchakato wa kupata Katiba hiyo utakavyoendeshwa.
  Rais Kikwete alisema hayo katika salama za mwaka mpya kwa Watanzania alizotoa jana kupitia vyombo vya habari na NIPASHE JUMAPILI kupata nakala yake.
  “…tujiepushe na vitendo vya kuzuia watu kutoa maoni yao kwa uhuru hasa wale wenye maoni tofauti na yetu. Kutoa maoni katika Tume hiyo ni haki ya kila mwananchi.
  Iwe ni mwiko kwa mtu yoyote au kikundi chochote kumzuia mtu au watu wowote kutumia haki yao hiyo,” alisema.
  Pia Rais Kikwete alisema haipaswi kuwepo mtu, watu au taasisi yoyote inayojaribu kuhodhi mijadala hiyo, na kuongeza “ni vyema tukajua kuwa tunatengeneza Katiba ya watu wote na kwa maslahi yetu sote….”
  “Hatutengenezi Katiba ya watu fulani wateule au kikundi fulani cha kisiasa au kijamii kwa maslahi yao. Tuwaache watu watoe maoni yao kwa uhuru ili tupate Katiba ya watu wote.”
  Alisema kutakuwa na Bunge maalum la Katiba litakalopokea na kujadili rasimu ya Katiba itakayotayarishwa na Tume ya Katiba.
  Baada ya Bunge kujadili rasimu hiyo na kufanya uamuzi wake, (rasimu) itapelekwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kwa njia ya kura ya maoni.
  Rais Kikwete alisema ndani ya robo ya kwanza ya mwaka huu, uundaji wa Tume ya Katiba utakuwa umekamilika na kuwa katika robo ya pili au ya tatu, tume hiyo itaanza kazi yake ya kukusanya maoni.
  Miaka 50 ya Uhuru
  Rais Kikwete alielezea kuridhishwa kwake na adhimisho hilo, alisema mwaka jana ulikuwa wa kihistoria kwa nchi yetu na wenye mchanganyiko wa mambo.
  Mpango wa Maendeleo
  Alisema serikali imejipanga vizuri kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano katika bajeti ijayo, na kwamba ameunda Kikundi Kazi kinachoongozwa na Profesa Benno Ndulu, kushauri juu ya vipaumbele na kufuatilia utekelezaji wa mpango huo.
  HALI YA USALAMA NCHINI
  Rais Kikwete alisema usalama wa nchi yetu katika mwaka 2011 ilikuwa ya kuridhisha na Tanzania iliendelea kuwa nchi yenye amani na utulivu.
  “Kwa jumla, mipaka yetu yote ilikuwa salama isipokuwa ule wa majini kwa upande wa Bahari Kuu ya Hindi ambako kumekuwepo na matukio ya uharamia,” alisema.
  Uhalifu
  Alisema juhudi za kupambana na kudhibiti uhalifu nchini ziliendelea na mafanikio yameendelea kupatikana.
  Alisema taarifa za jeshi la polisi za kati ya Januari na Novemba, 2011 zinaonesha kuwa matukio ya makosa makubwa ya jinai yamepungua ukilinganisha na hali ilivyokuwa kipindi kama hicho mwaka 2010.
  Kwa mujibu wa Rais Kikwete, makosa hayo yamepungua kutoka 86,150 hadi 69,678 na punguzo kubwa zaidi limetokana na kupungua sana kwa makosa ya wizi, pamoja na yale ya kubaka, kunajisi, kutupa watoto, unyang’anyi wa kutumia silaha, kuchoma nyumba, na dawa za kulevya.
  Ajali za Barabarani
  Rais Kikwete alisema matukio ya ajali za barabarani yamepungua kutoka 22,440 mwaka 2010 hadi 22,000 mwaka jana.
  Hata hivyo, alisema ajali zilizosababisha watu kupoteza maisha ziliongezeka mwaka huu kuliko mwaka wa jana na kufafanua, “mwaka jana ajali hizo zilikuwa 2,833 ukilinganisha na 3,012 mwaka 2011 na watu waliopoteza maisha walikuwa 3,332 ukilinganisha na 3,707 mwaka 2011.”
  Alisema ongezeko la ajali barabarani linasababishwa na ongezeko kubwa la vyombo vya usafiri hasa magari na pikipiki na kutoa mfano kuwa katika miaka sita iliyopita, magari 514,136 na pikipiki 1,206,679 zimeinginzwa nchini.
  Ajali ya Mabomu, Meli na Mafuriko
  Alisema matukio ya kulipuka mabomu katika kambi ya jeshi Gongolamboto, ajali ya kuzama kwa meli ya Spice Islander huko Zanzibar na mafuriko katika jiji la Dar es Salaam yalisababisha watu wengi kupoteza maisha, wengine kujeruhiwa na mali nyingi kupotea.
  Katika ajali ya Gongolamboto watu 25 walifariki dunia na 512 walijeruhiwa na nyumba 1,791 ziliharibiwa kwa viwango mbalimbali. Alisema Sh 817,740,849 zimelipwa kwa ajili ya kugharamia ukarabati wa nyumba zao zilizoharibiwa.
  MV Spice Islander
  Kwa upande wa ajali ya MV Spice Islander iliyotokea Septemba 10, 2011, alisema watu 619 waliokolewa na maiti 203 zilipatikana.
  Alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein aliunda tume ya uchunguzi iliyokamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti yake serikalini kwa utekelezaji.
  Mafuriko ya Dar es Salaam
  Alisema watu 40 wamepoteza maisha na nyumba na mali nyingi zimeharibiwa. Pia, watu wapatao 5,029 wamekosa makazi na kupatiwa hifadhi na jamaa zao au katika maeneo yaliyotengwa na Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam.
  Aidha, alisema serikali imekuwa ikiwahudumia waathirika hao kwa malazi, chakula na huduma ya afya. Vile vile, watu na mashirika mbalimbali yamekuwa yanatoa misaada ya kibinadamu kuwasaidia waathirika.
  Rais Kikwete alisema ana matumaini kuwa wakazi wa maeneo ya Jangwani na kwingineko hawatakaidi tena amri halali ya mkoa kama walivyofanya miaka ya nyuma.
  Matatizo ya Bei ya Mafuta
  Alisema hapa nchini makali ya ongezeko la bei ya mafuta duniani yaliongezwa na kushuka thamani ya shilingi na vitendo vya wafanyabiashara ya mafuta. Thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani ilishuka kutoka wastani wa shilingi 1,500 kwa dola ya Kimarekani mwanzoni mwa Januari, 2011 hadi shilingi 1,815 kwa dola Oktoba 27, 2011. Serikali kupitia Benki Kuu ilichukua hatua mbalimbali zilizoweza kupunguza kasi ya kushuka kwa thamani ya shilingi hadi wastani wa shilingi 1,595 kwa dola hivi sasa.
  Kwa sababu ya shilingi kupungua thamani, waagizaji wa mafuta walilazimika kutumia pesa nyingi za Kitanzania kununua dola ambazo kabla ya hapo walitumia pesa kidogo kuzipata. Hali hiyo ndiyo iliyosababisha athari za kupanda kwa bei za mafuta duniani kuwa kali zaidi hapa nchini.
  Sambamba na hilo, mwenendo wa wafanyabiashara hasa wa kukataa kutii maamuzi ya EWURA hasa pale wanapoteremsha bei limekuwa tatizo lingine. Wafanyabiashara hawako tayari kuona watumiaji wa mafuta wakipata nafuu hata kidogo. Kila bei zinaposhuka basi watapinga.
  Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi wafanyabiashara ya mafuta kutoa ushirikiano kwa EWURA inapotimiza wajibu wake.
  Kilimo
  Kwa upande wa kilimo katika mwaka 2011 juhudi za kuleta mageuzi katika kilimo chetu zinazolenga kuwanufaisha wakulima wadogo zimeendelea kutekelezwa. Ruzuku ya pembejeo iliendelea kutolewa, maafisa ugani waliongezwa vijijini na uboreshaji wa masoko na miundombinu vijijini uliendelea. Juhudi hizo zimeleta matokeo mazuri kwa uzalishaji wa mazao kuongezeka. Bahati mbaya katika mikoa ya Rukwa, Mbeya, Ruvuma na Iringa kumekuwa na usumbufu mkubwa wa ununuzi wa mahindi ya wakulima katika msimu huu.
  Kiini cha tatizo ni taratibu za kupata fedha za kununulia mahindi kutokamilika mapema. Nimewaagiza viongozi wa NFRA, Wizara ya Fedha na Wizara ya Kilimo, Chakula na
  Uwekezaji
  Katika mwaka 2011 tulitoa kipaumbele cha juu katika kukuza uwekezaji nchini na tunakusudia kuendelea kufanya hivyo mwaka ujao. Tumekuwa tunatangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini na kuwashawishi wawekezaji wa ndani na nje kujitokeza kuja kuwekeza. Pia tumekuwa tunachukua hatua za kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuifanya Tanzania kuwa nchi nzuri ya kuwekeza na kufanya biashara.
  Tumeainisha maeneo ya kipaumbele katika uwekezaji ambayo baadhi yake ni viwanda, kilimo, madini, utalii, biashara, nishati, uchukuzi na teknohama. Lengo letu kuu la kuhimiza uwekezaji nchini ni kutaka kuongeza uwezo na kasi ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa kuongeza uzalishaji mali, kuboresha huduma na kukuza ajira.
  Ni kutokana na kutambua ukweli huo ndiyo maana sisi katika Serikali tunahimiza na kuvutia wawekezaji ili nchi itumie fursa zilizopo nchini kujiletea maendeleo, kupunguza umaskini na kukuza ajira.
  Inakadiriwa kuwa hapa nchini mwaka 2011, kuna watu wenye uwezo wa kufanya kazi 22,152,320 na kati ya watu hao 2,368,672 au sawa na asilimia 10.7 hawana ajira. Ili watu hao waweze kupata ajira itategemea kwa kiasi gani tunafanikiwa kukuza uwekezaji katika sekta na shughuli mbalimbali. Bila ya hivyo kupatikana kwa ajira itakuwa ndoto.
  Tumechukua hatua za makusudi kufufua Benki ya Rasilimali kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wawekezaji wazawa kwa shughuli za viwanda na biashara. Pia tunakamilisha mipango ya kuanzisha Benki ya Kilimo kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakulima wazawa.
  Benki hizo mbili hazitatoa mikopo kwa wawekezaji wageni. Aidha, tumeanzisha mpango wa dhamana kwa wauzaji nje na wenye viwanda vidogo na vya kati, yaani Export Credit Gurantee Scheme na Small and Medium Enterprises Guarantee Scheme”. Mifuko hiyo maalum inayosimamiwa na Benki Kuu ipo kwa ajili ya kuwasaidia wawekezaji wazawa.
  Tathmini iliyofanywa na Baraza la Uwezeshaji la Taifa zinaonesha kuwa jumla ya shilingi bilioni 37.17 zilikopeshwa na benki za NMB na CRDB na jumla ya shilingi bilioni 12.06 zilikopeshwa na asasi 12 za fedha. Jumla ya wananchi 72,912 wamenufaika na mikopo hiyo. shilingi bilioni 39.275 zimesharejeshwa ambazo ni sawa na asilimia 79.8 ya mikopo iliyotolewa. Kiwango cha urejeshwaji mikopo kinategemewa kuongezeka kwa vile baadhi ya mikopo iliyotolewa kupitia asasi ndogo za fedha bado haijaiva.
  MALIMBIKIZO YA MADAI YA WATUMISHI SERIKALINI
  Katika mwaka 2011 kero ya malimbikizo ya madai ya stahili mbalimbali za watumishi wa umma wakiwemo walimu imejirudia tena. Tatizo hili nililikuta wakati naanza kazi hii na tukafanya jitihada kubwa na kulipa madeni yote. Baada ya kubaini kuwa limekuwa linajirudiarudia kila baada ya kipindi kifupi, nilitoa maelekezo kwa Halmashauri za Wilaya na Miji na Wizara za Serikali kuhakikisha kuwa tatizo hilo linakoma.
  Kuhusu uhamisho nilielekeza kwamba kama Halmashauri au taasisi yoyote ya Serikali haina pesa za uhamisho, isiwahamishe watumishi wake. Niliagiza kuwa mtindo wa kuhamisha watumishi bila ya kuwa na fedha za uhamisho ukomeshwe mara moja.
  Nilitaka kiongozi au mhusika yeyote atakayekiuka agizo hili alipishwe yeye gharama za kumhamisha mtumishi huyo. Kuhusu madai ya likizo nilielekeza kutengwe fedha za kutosha za likizo kwani mapumziko ni haki na muhimu kwa wafanyakazi. Hata hivyo kama fedha hakuna si busara kulimbikiza madeni. Uzuri wa likizo ni kuwa hazipotei. Wakati wa kustaafu siku za likizo ambazo mtumishi hakuchukua hulipwa.
  Nilisema pia kwamba suala la kuwapandisha watumishi vyeo bila kuwarekebishia mishahara yao kwa wakati ni upungufu wa kiutendaji ambao ni lazima ukomeshwe mara moja.
  Kupandishwa watumishi vyeo ni mpango unaoeleweka na siyo jambo la dharura wala ajali. Kwa mujibu wa utaratibu wa Serikali, mtumishi hupandishwa cheo kwa misingi miwili. Kwanza, kutimiza masharti ya muundo wake wa utumishi, na pili, kuwepo kwa fedha kwenye bajeti ya Wizara au Idara husika kwa madhumuni hayo. Hivyo iweje leo mtu apandishwe madaraja bila kulipwa mshahara stahiki? Hili halieleweki na wala halikubaliki.
  Alisema baada ya hotuba yake ya Februari, 2009 na Serikali kulipa takriban shilingi bilioni 64 kwa madai ya walimu mwaka huo, bado Serikali ililipa tena shilingi bilioni 29.8 kati ya Julai 2010 na Oktoba 2011. Hivi sasa nimeambiwa tena kuna madai mapya yaliyofikia shilingi bilioni 52.7.
  Sina tatizo na madai yanayostahili kulipwa na najua kwamba shilingi bilioni 22.5 zimetolewa na kati ya hizo shilingi bilioni 19.2 zimekwishapelekwa kwenye Halmashauri husika na shilingi bilioni 3.3 ni kwa ajili ya waajiriwa wa Wizara. Zilizobakia zitalipwa kwenye mishahara yao.
  MAHUSIANO YA KIMATAIFA
  Katika medani ya Kimataifa mwaka 2011, Serikali iliendelea kutetea na kuendeleza maslahi ya Tanzania nje ya nchi. Mahusiano yetu na mataifa na mashirika ya kikanda na kimataifa yamezidi kuimarika. Ahadi yetu katika mwaka 2012 ni kuendeleza juhudi hizo maradufu kwani nchi yetu inanufaika sana kwa ajili hiyo.
  Washirika wa maendeleo wameendelea kutuunga mkono, kututia moyo na kutusaidia katika juhudi zetu za kujiletea maendeleo. Tunawashukuru sana kwa ushirikiano mzuri na misaada yao na tunawaahidi kuitumia vizuri misaada hiyo.

  SENSA
  Alizungumzia mambo mawili. Jambo la kwanza ni Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Jumapili ya tarehe 26 Agosti, 2012. Hapa nchini tumekuwa na utaratibu wa kufanya sensa kila baada ya miaka 10, na mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2002.
  Kufanya Sensa ya Watu na Makazi ni jambo lenye umuhimu wa kipekee kwa taifa. Takwimu na taarifa zitakazokusanywa husaidia taifa katika kupanga mikakati na mipango yake ya maendeleo. Aidha, husaidia Serikali kupima mafanikio ya programu zake mbalimbali za Maendeleo. Husaidia pia kujipanga vizuri katika kufanya mambo yake.
  VITAMBULISHO VYA UTAIFA
  Hatimaye azma ya tangu Uhuru ya kila mwananchi kuwa na kitambulisho cha uraia tumeweza kuanza kuitimiza. Mwezi Desemba mwaka 2011, mchakato wa utoaji wa vitambulisho vya uraia umeanza. Mchakato huu ambao ni wa miaka mitatu umegawanyika katika awamu nne kila moja ikihusisha makundi mbalimbali.
  Awamu ya kwanza imeanza na watumishi wa Dar es Salaam na Zanzibar na vitambulisho vyao vitatolewa wakati wa sherehe za Muungano mwezi Aprili 2012. Baada ya hapo zitafuta awamu nyingine.
  HITIMISHO
  Wakati tunapojiandaa kuanza mwaka mpya hapo kesho (leo), napenda kuwahakikishia kuwa mimi na wenzangu Serikalini tumedhamiria kwa dhati kuwatumikia kwa moyo wetu wote na kwa nguvu zetu zote. Tutajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu na vipaji alivyotujaalia Mwenyezi Mungu kushirikiana nanyi katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto zinazolikabili taifa letu na watu wake. Naamini kwa pamoja na ushirikiano tutaweza, kila mtu atimize wajibu wake.  CHANZO: NIPASHE JUMAPILI


   
Loading...