Jinsi wanaume wanavyoweza kupata fistula

real G

JF-Expert Member
Feb 7, 2013
5,227
5,287
Unafahamu fistula huwapata pia wanaume?

Madaktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya njia ya mkojo wamesema ajali, saratani ya kibofu na magonjwa ya njia ya mkojo yamekuwa sababu za kasi ya kukua kwa ugonjwa huo kwa wanaume nchini kwa sasa.

Wakati sababu hizo zikitajwa, Tanzania ina wastani wa wanawake 3,000 ambao kila mwaka wanapata tatizo la fistula wakati wa kujifungua, huku 1,600 pekee ndio hujitokeza kutibiwa.

Akizungumza na Mwananchi jana, daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya njia ya mkojo kutoka Hospitali ya Tumaini, Profesa Cholonde Yongolo alisema japokuwa fistula imekuwa ikijulikana zaidi kwa wanawake, wapo wanaume wanaougua.

Profesa Yongolo alisema zipo saratani ikiwamo ya kibofu ambazo husababisha ugonjwa huo kwa wanaume na wakati mwingine hutoboa hadi njia ya haja kubwa.

“Tatizo la mwanaume kutokwa mkojo bila kujizuia linatokea zaidi kwa walio na saratani ya kibofu,” alisema.

“Mara nyingi saratani hii husababisha kuzalishwa tundu ambalo hutokea njia ya haja kubwa na wakati mwingine mkojo unaweza kuziba mbele hautoki na ukatafuta kupenya kati ya njia ya mkojo na ngozi chini ya hashuo, hiyo ni fistula.”

Alisema wanaume hupata aina nyingi kadhaa za fistula ambazo wakati mwingine hutokana na magonjwa ya zinaa yanayosababisha njia ya mkojo kuota majipu.

Profesa Yongolo alizitaja aina nyingine kuwa ni fistula ya koo na mfumo wa hewa ambayo ni njia ya kumeza na kukohoa, utumbo, kuumia, kupata ajali.

Alisema tundu lolote likitokea kati ya mifumo hiyo, huitwa pia fistula.

“Ni rahisi sana mwanaume kupata fistula ila hawezi kupata kwa njia ya uzazi kwa sababu saratani ya kizazi ni ya wanawake na yenyewe inaweza ikachimba na kutokezea kwenye njia ya haja kubwa au mkojo, lakini ambayo huwapata wote ni ile ya haja kubwa,” alisema Profesa Yongolo.

Sababu za kutokea kwa wanaume

Daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya njia ya mkojo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Obadia Nyongole alisema awali kulikuwa na wagonjwa wachache wa fistula kwa wanaume, lakini sasa wanaongezeka .

Alisema hata hivyo, ugonjwa huu huwapata wanawake kwa njia tofauti kwani fistula imegawanyika katika makundi na zipo ambazo mtu huzaliwa nazo.

“Mara nyingi huwepo tundu linalounganisha kiungo kimoja na kingine ambalo kwa kawaida halitakiwi kuwepo, zipo fistula ambazo mtu anazaliwa nazo katika maumbile kunakuwa na viungo ambavyo vimetengeneza muungano usio rasmi na kuna tundu linalounganisha,” alisema Dk Nyongole.

Alifafanua kuwa zipo ambazo hutokana na matibabu ya upasuaji. “Ikiwa likatokea tundu kwenye kiungo kingine na katika kupona likashindwa kupona vizuri au katika kufanya upasuaji kuna kiungo kiliguswa na kifaa kingine bila kugundulika wakati wa upasuaji kikaachwa hivyo hivyo, kinaweza kutengeneza fistula hasa sehemu ya utumbo,” alisema.

Alisema wengi wanaopata fistula ni wale waliofanyiwa upasuaji kwa njia ya mkojo wakawekewa mpira baada ya kutolewa kuna kovu ambalo hutakiwa lipone lenyewe, ikishindikana mkojo huanza kutokea tumboni chini ya kitovu sababu tundu limeshindwa kuziba.

“Wapo wanaopata kovu kwenye njia ya mkojo na litakaposhindwa kutibiwa kwa wakati hivyo patatengeneza jipu na baadaye likipasuka na kutengeneza njia, ni fistula kwa mwanaume,” alisema Dk Nyongole.


Chanzo: Mwananchi
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom