Jinsi Sultani Qaboos alivyowashinda waliotaka kumpindua/ Raia Mwema

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
BARAZANI

Na Ahmed Rajab

Kwa kila hali alikuwa ni mwanamke wa kuvutia. Wengine wangelisema kwamba alikuwa “mwanamke wa haja” lakini.leo miaka zaidi ya 50 tangu ule usiku nilipojulishwa naye jijini Dar es Salaam kuna jambo lake moja tu ninalolikumbuka.

Si macho yake aliyokuwa akiyatupa chini kana kwamba akifanya hivyo kwa maringo, wala si umbo lake lililoumbwa likaumbika. Wala si ubichi wake ingawa kimawazo alikuwa mpevu.

Jina lake limekwishafifia kwenye kumbukumbu zangu licha ya kulihifadhi kwa miaka. Pengine hilo jina halikuwa la kweli.

Ninachokumbuka ni mikono yake. Nilipoilinganisha na yangu niliudhika kidogo kwani yangu ilikuwa mithili ya hariri. Yake ilichakaa; ilikuwa migumu, ya kidume zaidi. Tulipopeana mikono kusalimiana niling’amua papo hapo kwamba mikono yake ilizoea kubeba vizito: bunduki za rashasha.

Hilo halikunishangaza kwa sababu nikijua kwamba nilikuwa ninakutana na mpiganaji. Huyo kimwana alikuwa mmoja wa wapiganaji wa Dhofar, jimbo la kusini mwa Omani. Vuguvugu lao liliasisiwa mnamo 1962 na likiitwa Chama cha Ukombozi wa Dhofar (Jabhat Tahrir Dhofar).

Kufikia Septemba 1968, chama hicho kikabadilishwa jina na kuitwa Chama cha Umma cha Ukombozi wa Ghuba la Kiarabu Lililokaliwa (al-Jabha al-Sha'abiya li-Tahrir al-Khalij al-'Arabi al-Muhtall, PFLOAG).

Wanachama wake walikuwa wakifuata siasa za mrengo wa kushoto, za kimapinduzi, za itikadi kina Karl Marx, Vladimir Lenin na mwenyekiti Mao.

Awali siasa hizo za kimapinduzi hazikuwavutia wapiganaji wa Dhofar. Lakini zilianza kuwahamasisha wapiganaji na kushika kasi Wadhofari zaidi walipokuwa wanajiunga na mapigano na walipokuwa wakipelekwa nje ya nchi kwa mafunzo ya kijeshi, mwanzoni Iraq ilipokuwa chini ya Rais Saddam Hussein, Syria na baadaye katika nchi jirani ya Yemen ya Kusini pamoja na kwenye nchi nyingine za Kiarabu zilizokuwa zikifuata zile zilizokuwa zikiitwa siasa za kimaendeleo.

Mnamo Juni 1970, kuliundwa chama kipya kaskazini mwa Omani kilichoitwa Chama cha Kitaifa cha Kidemokrasia cha Ukombozi wa Omani na Ghuba la Kiarabu (al-Jabha al-Wataniya al-Dimuqratiya li-Tahrir 'Uman wa-l-Khalij al-'Arabi, NDFLOAG). Chama hicho kiliungana na PFLOAG Desemba 1971.

Miaka miwili baadaye kulikuwa tetesi kwamba PLOAG kilishakuwa na wafuasi ndani ya majeshi ya Muungano wa Tawala za Kifalme za Kiarabu (UAE).

Ilipofika 1974 chama hicho kilibadili tena jina la kujiita Chama cha Uma cha Ukombozi wa Omani (al-Jabhat al-Sha‘abiyya li-Taḥrīr ʿUmān, kwa kimombo Popular Front for the Liberation of Oman au PFLO kwa ufupisho wake wa Kiingereza).

Wapiganaji wao wakisema kwamba lengo lao lilikuwa kuikomboa Omani lakini hasa walikuwa wakitaka eneo la Dhofar, kusini mwa nchi hiyo, liwe huru na lijitenge na Omani. Wakinung’unika kwamba Dhofar ikitupwa nyuma kwa maendeleo. Hakuna lililokuwa likifanyika huko.

Pia wakitaka kuuangusha utawala wa kisultani wa Said bin Taimur al Said. Walikuwa wakimtuhumu sultani Said bin Taimur kwamba alikuwa mikononi mwa Uingereza. Kusema kweli alikuwa hawezi kufurukuta. Waingereza walimbana.

Mshauri wake mkuu alikuwa Mwingereza, waziri wake wa ulinzi pamoja na mkuu wa idara ya usalama na intelijensia walikuwa wanajeshi wa Kiingereza. Waziri wake mmoja tu alikuwa Muomani. Waliobaki wote walikuwa Waingereza.

Sultan Said bin Taimur hakuwa na uhusiano mzuri na mwanawe Qaboos tangu arejee masomoni Uingereza Desemba 1964 alikopelekwa kusoma kwenye chuo cha kijeshi cha Sandhurst. Baba mtu akishuku kwamba mwanawe alikuwa akila njama za kumpindua.

Ripoti iliyoandikwa Januari 13, 1965 na John Duncan, balozi mdogo wa Uingereza huko Maskati, inaeleza jinsi uhusiano wa baba wa kifalme na mwanawe ulivyokuwa. Duncan aliandika kuwa alimuuliza Qaboos iwapo alimuona kasuku wa baba yake. Naye Qaboos akajibu kwamba hamuoni baba yake seuze kasuku wake. Licha ya kwamba nyumba zao zilikuwa karibu karibu Qaboos alimuona baba yake mara mbili tu tangu arudi kutoka Uingereza.

Qaboos alikuwa amewekwa kwenye kizuizi cha nyumbani na baba yake. Kila siu toka saa tatu za asubuhi hadi saa sita alikuwa akitalii Qur’ani akidarisishwa na Sheikh Ibrahim as Saif, aliyekuwa mmoja wa makadhi wakubwa wa Maskati.

Hatimaye Said bin Taimur alipinduliwa na mwanawe Qaboos akisaidiwa na Waingereza mnamo 1970. Baada ya hapo wapiganaji wa wapiganaji wa PFLO walizilenga nguvu zao dhidi ya sultani mpya.

Wakati huo ndipo zilipochacha harakati za wapiganaji wa Dhofar. Wapiganaji hao walikuwa wakiungwa mkono na serikali ya Kikomunisti ya iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Yemen (Yemen ya Kusini), Iraq, China na Muungano wa Jamhuri za Kisovieti.

Cheche za mwanzo za uasi dhidi ya Sultan Said bin Taimur ziliwashwa na mtu aliyekuwa na kazi ya kuitunza bustani ya sultani huyo kwenye kasri yake ya huko Salalah. Jina lake ni Musallam bin Nufl wa kabila kubwa la jangwani liitwalo al Kathiri.

Bwana huyo alikasirishwa bila ya kiasi alipofukuzwa kazi 1963. Ghadhabu zake zilizidi kupanda wataalamu wenye kuchimba mafuta walipomiminika kwenye ardhi yake. Inasemekana kwamba risasi za mwanzo za vita zilipigwa na waasi wakiongozwa na Musallam bin Nufl mwezi wa Aprili ya mwaka huo.

Waliyashambulia magari ya kampuni ya mafuta halafu wakavuka mpaka na kukimbilia Saudi Arabia walikokwenda kuonana na Ghalib bin Ali al Hinai, Imamu yaani kiongozi wa kidini wa Kiomani aliyekuwa hasimu wa ukoo wa kifalme wa al Said. Utawala wa Omani ulikuwa umegawika sehemu mbili: sehemu za ndani zikitawaliwa na Imamu aliyekuwa akichaguliwa na sehemu za mwambao zikitawaliwa na sultani.

Ghalib al Hinai alikuwa imamu wa mwisho wa kuchaguliwa. Alikuwa akiishi uhamishoni Dammam, Saudi Arabia, hadi alipofariki 2009 akiwa na umri wa miaka 96.

Mwandishi, msomi na mtaalamu wa uhusiano wa kimataifa, Fred Halliday, ambaye kabla ya kufariki 2010 aliwahi kuwa profesa kwenye chuo kikuu cha London School of Economics (LSE) aliwatembelea wapiganaji hao walipokuwa wakipigana kwenye majabali ya Dhofar wakijificha katika mapango ya huko.

Kwenye kitabu chake kilichochapishwa 1974 na kiitwacho “Arabia without Sultans” (Arabuni bila ya masultani) Halliday ameeleza jinsi wanawake wa Dhofar walivyokuwa tofauti na wanawake wa sehemu nyingine za Ghuba. Tofauti hiyo, amehoji Halliday, ndiyo iliyowapelekea wanawake hao washiriki zaidi katika harakati hizo za kimapinduzi.

Tofauti yenyewe ni kwamba wanawake wa Dhofar hawakukandamizwa sana na jamii yao kama wanavyokandamizwa wanawake wa nchi nyingine za Ghuba. Wanawake wa Dhofar waliolewa wanamiliki ng’ombe na wanajiweza. Wanayakimu maisha yao na ya familia zao. Si hayo tu lakini wanaweza pia kupata talaka kwa urahisi na kuolewa tena bila ya kuingia doa na kusemwa na jamii.

Halliday alipata fursa ya kuzungumza na kuwahoji wanawake kadhaa waliokuwa wapiganaji wa PFLO kama yule niliyekutana naye Dar es Salaam.

Siku hizo jiji la Dar lilikuwa kama simaku ya kuwavutia wakombozi kutoka nchi mbali mbali, nyingi zikiwa za Kiafrika kwani kamati ya ukombozi wa Afrika ilikuwa na makao yake huko. Tanzania ya siku hizo, ikiwa chini ya Mwalimu Julius Nyerere, ilijitolea kuwasaidia wote waliokuwa wakisema kwamba wanapigania ukombozi wa nchi zao.

Tanzania ya Nyerere ilikuwa pia ikiuona ufalme wa Omani kuwa adui yake kama ilivyokuwa ikiuona utawala wa kifalme wa Zanzibar uliopinduliwa Januari 12, 1964 hasa kwa vile masultani hao wawili walikuwa wa ukoo mmoja.

Katika miaka ya hivi karibuni serikali ya Uingereza imeziweka wazi nyaraka nyingi zilizokuwa za siri zinazohusiana na jinsi majeshi ya Uingereza yalivyopigana Dhofar yakiusaidia utawala wa Sultani Qaboos. Mapigano yaliendelea hadi 1976 na yalimalizika kwa ushindi wa Qaboos, akisaidiwa pia na majeshi ya mfalme mwengine, Shah wa Irani, kabla hajapinduliwa na wafuasi wa Ayatollah Khomeini 1979.

Wakati huo huo wapiganaji wa Dhofar waligawika na kundi moja la waliokuwa wakifuata siasa za mrengo wa kulia lilikubali kuacha uasi wao na kumuunga mkono Qaboos aliyeanza kuleta maendeleo katika eneo hilo kwa msaada wa fedha za nchi za Magharibi. Miongoni mwa waasi hao alikuwa Yusuf bin alawi bin Abdullah, ambaye sasa ni waziri anayeshughulikia mashauri ya nchi za nje na ambaye majuzi tu alimpokea Profesa Palamagamba Kabudi, waziri wa nchi za nje wa Tanzania, alipokwenda Maskati kuwasilisha salaam za rambirambi kwa kifo cha Sultani Qaboos kwa niaba ya Rais John Magufuli.

Licha ya kwamba Qaboos alikuwa rafiki wa Shah uhusiano baina ya Omani na Irani umeendelea kustawi hadi hii leo. Omani imekuwa ikikataa kufuata maamrisho ya Marekani na ya nchi jirani zenye nguvu na utajiri mkubwa kuliko wake zilizoitaka iwe na uhusiano hasi na Irani. Uhusiano huo mzuri wa Omani na Irani ndio ulioipelekea Omani iwe na uwezo mkubwa kwa kuwa msuluhishi kila palipokuwa pakizuka matatizo baina ya Irani na mahasimu zake wa Magharibi au wa Kiarabu.

Omani ina umuhimu mkubwa kimataifa kwa sababu nchi hiyo iko sambamba na Njia ya Bahari ya Hormuz inayotumiwa na meli zinazosafirisha mafuta ya nchi za Ghuba kwenda kuuzwa nchi za nje.

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter:mad:ahmedrajab






Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom