Jinja: Zanzibar ni ya Wazanzibari

aleesha

JF-Expert Member
Oct 17, 2016
597
1,000
WIKI iliyopita Zanzibar iliondokewa na mmoja wa wanawake wake maarufu. Kwa muda wa miaka mingi, Bi Fatma “Jinja,” aliyefariki alfajiri ya Mei 26, akiwa na umri wa miaka 87, alipata umaarufu kutokana na umaarufu wa watu wengine.

Ama umaarufu wa waliohusiana naye kwa damu au wa wengine walioyagusa maisha yake.

Lakini katika miaka ya mwisho wa uhai wake, umaarufu wa Fatma Jinja ulikuwa wa jitihada zake mwenyewe akiwa mtungaji wa vitabu vitatu. Na pengine zaidi kwa kukubali kitabu kiandikwe kuhusu kumbukumbu za maisha yake. Anastahiki sifa kwa mawili.

Kwanza, kwa kuchukua kalamu na kuikumbatia tasnia ya uandishi akiwa na umri mkubwa. Si zamani sana watu wa umri wake walikuwa wakijikalia ndani majumbani mwao wakilea virembwe na kutafuna tambuu.

Pili, anafaa kusifiwa kwa kuwa miongoni mwa wanawake wachache Wakizanzibari waliothubutu ama kuandika kuhusu maisha yao au kukubali kuyahadithia ili yaandikwe kwenye vitabu.

Alionyesha ujasiri mkubwa kwa kufanya hivyo, hususan kwa mtu wa rika lake. Yeye pamoja na wanawake wenzake Wakizanzibari walioandika kuhusu maisha yao au walioyahadithia maisha yao ili yaandikwe wamezifuata nyayo za Seyyida Selma bint Said, mwanamke wa kwanza wa Kizanzibari aliyeandika kitabu kuhusu maisha yake.

Selma alikuwa binti wa sultan wa kwanza wa Zanzibar, Seyyid Said bin Sultan, ambaye wakati huohuo alikuwa mfalme wa Oman. Maisha ya Selma yalikuwa ya kusisimua na ya kuhuzunisha.

Kwa muhtasari, binti huyo wa sultan alipendana kwa siri na Rudolph Heinrich Ruette, mfanyabiashara wa Kijerumani aliyekuwa akiishi karibu naye, Mji Mkongwe, Unguja. Baada ya kushika mimba, Selma ilimbidi atoroke Zanzibar pamoja na Ruette kuelekea Aden na hatimaye Ujerumani.

Alipowasili Aden, Selma alibadili dini akawa Mkristo wa madhehebu ya Protestanti. Baada ya kutanasari alibadili na jina, akawa anaitwa Emile Ruette. Alifariki Ujerumani Februari 1924, akiwa na umri wa miaka 79.

Maisha yake yalikuwa magumu baada ya mumewe kufariki katika ajali mwaka 1870. Siku hizo kulikuwa na ushindani mkubwa baina ya madola ya Ulaya, hususan Uingereza, Ufaransa, Italia na Ujerumani kutamalaki nchi mbalimbali za Afrika.

Baada ya kufariki mumewe, Wajerumani walimgeuza Emile awe kama karata yao ya kuicheza katika njama zao za kutafuta makoloni Afrika.

Kulikuwa na tetesi kwamba Otto von Bismarck, aliyekuwa kiongozi wa Ujerumani kutoka 1871 hadi 1890, alitaka kumtawaza mtoto wa kiume wa Emile awe sultan wa Zanzibar. Bismarck angefanikiwa basi Zanzibar pengine ingefuata mkondo mwingine wa kihistoria kwa kutawaliwa na sultan aliyekuwa na baba wa Kijerumani.

Tunaweza kuyachungulia maisha ya Selma au Emile kwa kusoma kitabu cha kumbukumbu zake alichokiandika kwa Kijerumani na alichokiita “Memoiren einer arabischen Prinzessin” (Kumbukumbu za binti wa Kifalme wa Kiarabu).

Kitabu hicho kilichapishwa 1886 na haikuchukuwa muda ila tafsiri yake ikachapishwa kwa Kiingereza, kwa jina la “Memoirs of an Arabian Princess from Zanzibar” (Kumbukumbu za binti wa Kifalme wa Kiarabu kutoka Zanzibar).

Ninamtaja Selma kwa dhamiri ya kuonesha kwamba waandishi wengine wa kike wa Kizanzibari walioandika kuhusu maisha yao wamekuwa wakizifuata nyayo zake. Mmoja wao ni yeye Fatma Jinja aliyekubali kuhojiwa na Dkt. Asyah Al-Bualy kuhusu maisha yake na kukachapishwa kitabu 2015 kiitwacho “Reminiscences from a Golden Past” (tafsiri yangu huru ni “Kumbukumbu za Maisha ya Dhahabu”).

Bi Fatma alikuwa mfano mzuri wa mchanganyiko wa Kizanzibari na namna damu za Wazanzibari zinavyoziruka siasa au siasa zinavyokiuka damu. Nimegundua kwamba mchanganyiko huo umekuwa ukiwakang’anya na kuwapiga chenga wengi wa waandishi au wasomi wa Tanganyika wanaojaribu kuichambua Zanzibar na siasa zake.

Wanashindwa kuzielewa siasa za Zanzibar, hasa za baada ya Mapinduzi ya 1964 kwa sababu hawawezi kuamini namna watu walivyochanganyika. Wengi wao hukimbilia kuziangalia siasa hizo kwa kioo cha ubaguzi. Huwa wanazichambua kwa kuwagawa Wazanzibari kikabila na kwa rangi au kwa mapande makuu mawili ya kisiasa ya wafuasi wa zamani wa chama cha Afro-Shirazi Party (ASP) au cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP, maarufu kwa jina la Hizbu).

Huwa wanafanya hivyo kwa sababu ya propaganda za ubaguzi na matamshi ya baadhi ya viongozi waliofilisika kisiasa wenye kuutumia ubaguzi ili waweze kuselelea madarakani. Wasomi hao huwa wanadanganywa na wanakubali kudanganywa ama kwa sababu ya uvivu wa kutoitalii ipasavyo jamii ya Kizanzibari au kwa sababu wao wenyewe toka hapo wana chuki za kikabila.

Bibi Fatma alizaliwa katika ukoo uliojiweza wa Mabarwani kwa baba na mama. Alizaliwa na kukulia katika uluwa na hayo ndiyo “maisha ya dhahabu” aliyoyakumbuka katika kitabu cha Dkt. Asyah al-Bualy. Alikumbuka jinsi tokea utotoni mwake alivyokuwa akienda kwenye Kasri ya Mfalme kwa vile alikuwa amehusiana kwa upande wa baba yake na Bibi Nunuu bint Ahmed al-Busaidi, aliyekuwa mke wa Seyyid Khalifa bin Haroub, sultan aliyetawala Zanzibar tokea 1911 hadi 1960 na aliyekuwa babu wa sultan wa mwisho wa Zanzibar, Seyyid Jamshid bin Abdullah.

Maisha yalimgeukia baada ya Mapinduzi alipokumbana na misukosuko kadha wa kadha.

Alipofariki alikuwa mama mkwe wa Rais mstaafu Amani Abeid Karume. Mumewe wa tatu alikuwa Brigadia Yusuf Himid, aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Zanzibar yalipoanzishwa majeshi hayo baada ya Mapinduzi. Licha ya kuwa akipata taabu kuandika na kusoma alipewa cheo hicho kwa sababu siku za Vita Kuu Ya Pili ya Dunia alikuwa dereva kwenye kambi ya jeshi la Uingereza katika jangwa la Afrika ya Kaskazini.

Mwanamapinduzi huyo ndiye baba wa Mansoor, aliyewahi kuwa waziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ambaye siku hizi ni mwanasiasa mashuhuri wa Chama cha Wananchi, Civic United Front, (CUF) baada ya kutimuliwa kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa sababu ya msimamo wake wa kukikosoa chama hicho. Mansoor naye amemuolea mdogo wake Amani Karume.

Kwa hivyo, Fatma Jinja aliishi katika utukufu wa kabla ya Mapinduzi na pia katika utukufu wa baada ya Mapinduzi. Inataka mtu mwenye moyo kama aliokuwa nao kuweza kuyahimili yaliyomwangukia.

Hayo yalikuwa pamoja na kukamatwa baba yake mzazi, mara mbili, na kufungwa na hatimaye kuuliwa kinyama. Baba yake, Sheikh Muhammed Salim bin Hilal Barwani, akijulikana zaidi kwa jina la Muhammed Salim “Jinja”. Nimesikia sababu mbili za kwa nini akiitwa “Jinja”. Na zote zinahusika na umahiri wake wa kucheza soka.

Inasemekana kwamba palikuwako mchezaji soka hodari wa kizungu Zanzibar aliyekuwa akiitwa “Ginger” na kwa vile Muhammed Salim Barwani naye alikuwa si mdogo wa kulicharaza soka akabandikwa lakabu hiyo iliyomselelea maisha yake. Mtu mwingine ameniambia kwamba safari moja timu ya Zanzibar ilikwenda Jinja, Uganda, kucheza mechi na Muhammed Salim alifunga mabao mengi. Sifa za Jinja, Uganda, zikamuandama na kumganda na Jinja likawa jina lake la utani.

Muhammed Salim Jinja alikuwa na sifa nyingi. Bwana huyu aliyezaliwa Zanzibar 1905 alikuwa miongoni mwa wasomi wa mwanzo wa masomo ya kisasa visiwani humo. Baada ya kumaliza masomo katika Skuli ya Kuwafunza Waalimu (TTS) aliajiriwa awe msaidizi wa mwalimu wake mkuu wa TTS, Mwingereza D.W. Hollingsworth. Na skuli ya mwanzo ya sekondari ilipofunguliwa na serikali 1935, Jinja aliendelea kuwa mwalimu msaidizi wa Hollingsworth.

Baada ya muda alipelekwa Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza, alikohitimu stashahada ya elimu 1942. Baadaye alisoma katika Chuo Kikuu cha Oxford ambako alihitimu na kupata shahada ya B.A. mnamo 1948. Kama sikosei nafikiri Jinja alikuwa Mzanzibari wa kwanza kusoma Oxford.

Aliporudi Zanzibar alishika nyadhifa mbalimbali katika idara ya elimu na kabla hajaacha kazi ya serikali 1961, alikuwa kaimu mkurugenzi wa elimu. Tukiuacha mchango wake katika sekta ya elimu, mchango mwingine mkubwa wa Jinja ulikuwa katika siasa. Hata alipokuwa bado mtumishi wa serikali, na kabla ya kuanzishwa kwa vyama vya siasa, Jinja akijishughulisha na siasa chini kwa chini.

Alikuwa mpinzani mkubwa wa utawala wa Kiingereza na mara kwa mara akipapurana na mkurugenzi wa elimu kuhusu mfumo wa elimu uliokuwepo Zanzibar. Yeye na Wazanzibari wenzake walikuwa na jumuiya ya siri ya kusaidiana waliyoipa jina la “ANTS” na iliyojishughulisha na harakati dhidi ya ukoloni.

Alipokuwa mtumishi wa serikali, Jinja alikuwa pia akiandika kwa siri tahariri na makala ya siasa kwenye gazeti la kizalendo la Mwongozi akipinga ukoloni. Jinja alikuwa mtu wa msimamo aliyechukizwa na tabia ya kuyumbayumba. Alipoacha kazi serikalini 1961, ndipo alipojitokeza kuwa naibu mhariri wa Mwongozi.

Moja ya mambo aliyokuwa akiyapigania katika maandishi yake ilikuwa haki ya wafanyakazi kulipwa mishahara inayostahili kwa kazi zao. Alikuwa wa mwanzo kutoa kaulimbiu ya “Zanzibar ni ya Wazanzibari”. Hatutokosea tukisema kwamba yeye ndiye aliyempika kisiasa Sheikh Ali Muhsin Barwani, aliyekuwa kiongozi mkuu wa Hizbu. Alikuwa akimuongoza kisiasa tangu alipokuwa mwalimu wake alipokuwa Ali Muhsin anasoma skuli.

Jinja alikamatwa mwanzoni mwa 1964 na akafungwa jela kwa miezi mitatu. Baadaye alikamatwa tena, akateswa na akauliwa 1965. Inasemekana kwama kabla ya kuuliwa aliambiwa yeye na wenzake wasiopungua sita wachimbe shimo kubwa. Halafu wakaamrishwa wasimame na walipe mgongo hilo shimo. Hapo ndipo walipofyetuliwa risasi na wakauliwa.

Wenzake waliokufa naye walikuwa pamoja na Sheikh Amour Zahor, Sheikh Said Kombanyongo na Hamza Gidemi. Walikufa kifo cha mashahidi.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom