USHAHIDI WA KUWEPO KWA MAJINI KATIKA MAFUNDISHO YA MTU (SWALLA ALLAAHU ‘ALAYHI WA SALLAM) 'SUNNAH'
Katika 'Sunnah', (mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), wameelezea Maimam Al-Bukhaariy na Muslim katika vitabu vyao vilivyo sahihi kwamba Ibni 'Abbaas (Radhiya Allaahu anhu) amesema:
"Majinni waliposhindwa kupata siri kutoka mbinguni na wakawa wanafukuzwa kwa vimondo kila wanapojaribu kuzisogelea mbingu, wakarudi makwao. Na jamii zao walipotaka kujua sababu ya kurudi kwao huko na kushindwa kwao kupata siri za mbinguni, maana kabla ya hapo walikuwa wakiweza kupata baadhi ya habari za huko, wakawajibu:
"Pamewekewa vizuizi baina yetu na baina ya (kupata) habari za mbinguni".
Wenziwao wakasema:
"Bila shaka pana jambo kubwa lililotokea, tembeeni ardhi yote Mashariki na Magharibi mtafute ni kitu gani kilichokuzuwieni msiweze kupata habari za mbinguni.”
Walipofika mahali paitwapo; “Soko la Akadha”, waislamu walikuwa wakiswali Swala ya Alfajiri, na majini hao wakaisikia Qur-aan ikisomwa, ndipo waliposema:
"Hii (Qur-aan) wAllaahi, ndiyo iliyokuzuwieni msiweze kupata habari za mbinguni."
Wakarudi kwa watu wao na kuwaambia;
"Enyi jamii yetu! “Hakika sisi tumesikia Qur-aan ya ajabu"
Allaah Amesema katika Suratul Jinn aya ya mwanzo:
"Sema:“Imefunuliwa kwangu kuwa kundi moja la majini lilisikia (Qur-aan) likasema; “Hakika tumesikia Qur-aan ya ajabu.”
Suratul Jinn - 1
Hizi ni dalili zilizo wazi za kuwepo kwa viumbe hawa, na kukanusha kuwepo kwao kwa sababu ya kutokuonekana kwao si hoja maana vitu vingi hatuvioni na tunakubali kwamba vipo kutokana na athari zake. Kwa mfano, joto, baridi, umeme nk. Hivi vyote hatuvioni lakini tunakubali kuwepo kwake baada ya kuona athari zake.