Jiandae na magumu wakati mambo ni mazuri

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,781
3,074
Karibu Mstoa kwenye makala yetu ya kuendelea kujifunza misingi ya ustoa na kuiweka kwenye maisha yetu, ili tuweze kuwa na maisha bora na tulivu.

Wote tunajua kwamba wanajeshi huwa wanafanya mazoezi makali wakati wa Amani kama maandalizi ya kupambana wakati wa vita. Wanajeshi hawajiambii ya nini kujitesa sasa hivi wakati kuna amani, tupumzike halafu vita ikianza tutajiandaa. Wanajua kabisa kwamba vita ikishakuja, hakuna tena muda wa kujiandaa bali kutumia maandalizi yaliyofanyika kabla katika kupambana.

Kadhalika kwa wachezaji wa michezo mbalimbali, huwa wanafanya maandalizi yao muda mrefu kabla ya mashindano. Hawasubiri mpaka siku ya mashindano ndiyo wafanye maandalizi. Mwanariadha atakimbia kila siku kwa mwaka mzima, kujiandaa na mashindano matano tu kwa mwaka. Sasa kwa nini mtu huyu ajitese siku 365 kwa sababu ya siku tano? Kwa sababu anajua ushindi wake kwenye siku hizo tano, unategemea sana maandalizi ya siku 365.

Sasa inapokuja kwenye maisha yetu ya kila siku, huwa tunasahau kabisa umuhimu huu wa maandalizi. Tunaishi kama vile sisi ndiyo tunaopanga maisha yetu, mpaka siku tusiyoyategemea yanatokea na hapo tunaanza kulalamika na kulaumu.

Tumekuwa tunaona jinsi watu wanavyopokea kwa mshtuko taarifa za kufukuzwa kazi au biashara kufa. Watu hawa walifanya kazi au biashara miaka mingi na wakafikiri wana udhibiti kwenye kile wanachofanya. Wakasahau kuwa na maandalizi na hatimaye kuja kukutana na wasilotegemea kwa mshangao.

Falsafa ya Ustoa inatupa msingi muhimu sana wa kuendesha maisha yetu kwa namna ambayo hakuna chochote kinachotokea kinaweza kutusumbua, hata kama hatukukitegemea.

Kwenye moja ya barua zake kwa rafiki yake Lucilius, Mwanafalsafa Seneca anashauri hatua ifuatayo ambayo kila mtu anapaswa kuichukua; tenga siku kadhaa kila mwezi ambapo utaishi maisha ya kimasikini na ya chini kabisa, kwa kuvaa nguo chakavu, kula chakula cha chini kabisa na kisha jiambie “je hii ndiyo hali ambayo nimekuwa naihofia?”

Set aside a certain number of days, during which you shall be content with the scantiest and cheapest fare, with coarse and rough dress, saying to yourself the while: "Is this the condition that I feared?" – Seneca.

Zoezi ambalo Seneca anatushirikisha hapa ni kuchagua kuishi maisha ya chini kabisa, hata kama tuna uwezo wa kuishi maisha tutakayo. Lengo ni kwamba kwa kuyaishi maisha hayo, hutakuwa na haja ya kuhofia, kwa sababu utagundua ni maisha ambayo unaweza kwenda nayo bila shida.

Watu wengi huhofia kupoteza kazi zao, vyeo vyao, biashara zao kwa sababu hawajawahi kujaribu kuishi maisha ambayo hawana vitu hivyo wanavyovitegemea sana. Hivyo wanaishia kutegemea sana vitu hivyo na kuona maisha hayawezi kwenda bila ya kuwa na vitu hivyo.

Seneca anasema wakati ukiwa na kila kitu, ndiyo wakati unapaswa kufanya zoezi la kuishi bila ya vitu hivyo, na hili litakusaidia kwa njia mbili;

Moja, utakuwa huru na hofu ya kupoteza, kwa sasa unaogopa kupoteza ulichonacho ukijiuliza maisha yatakuwaje. Unapoyajaribu maisha hayo ya chini, huwezi kuyahofia, kwa sababu umeonja uhalisia wake.

Mbili, utathamini ulichonacho. Sisi binadamu tuna tabia ya kuzoea vitu. Kabla hujawa na kitu unakitamani na kukithamini sana, unapambana ili uweze kukipata au kukifikia. Lakini ukishakipata, unakizoea na unaona hakina thamani tena. Unapochagua siku za kujinyima kitu hicho, unapokirudia unakithamini zaidi. Mfano unaweza kuwa umezoea kulala kwenye godoro kila siku kiasi kwamba huoni thamani ha godoro, sasa jaribu kulala nchini usiku mzima na utakaporudi kwenye godoro utaona thamani yake.

Seneca anaonya kwenye ufanyaji wa zoezi hili, usijidanganye kwa kujaribu hali ya chini, badala yake unapaswa kuiishi hali hiyo kweli, ili upate uhalisia wake. Mavazi yawe makuu na ya chini kweli, chakula kiwe cha chini na kidogo na fanya hivyo kwa siku tatu au nne mfululizo, ikiwezekana zaidi, ili liwe ni jaribio kamili na siyo tu kwa kujisikia.

Hapa Seneca ametupa angalizo muhimu sana, ni rahisi kula chakula cha chini au kujinyima kwa siku moja, kila mtu anaweza kufanya hivyo. Hilo haliwezi kukuandaa na magumu utakayokutana nayo kwenye maisha, hivyo fanya kwa siku kadhaa, kwa muda mrefu ambao utayapata maumivu ya kweli kwa aina hiyo ya maisha. Na hapo utakuwa umeonja ile hali unayoihofia, na utagundua siyo mbaya kama ulivyofikiri.

Seneca anamalizia kwa kusema hakuna sababu ya kujisifia kwa kufanya zoezi hili, kwa sababu wakati wewe unalijaribu kwa siku kadhaa, kuna mwenzako ndiyo maisha yake ya kila siku. Lakini unaweza kujipongeza kwa kuwa umechagua kufanya hili mwenyewe na kama mambo yataenda hivyo basi hutasumbuka. Tusijiweke mbali sana na umasikini, tusijisahau kisha asili ikatujia na kutushangaza. Utauthamini zaidi utajiri wako ukishajua ni jinsi gani uko karibu na umasikini na kwamba unaweza kukujia muda wowote.

Mstoa mwenzangu, chagua namna utakavyoishi msingi huu, chagua vile vitu ambavyo umeshazoea kufanya kila siku na unaogopa kuvipoteza, kisha tenga siku ambazo utaishi bila ya vitu hivyo, angalau siku 3 mpaka 5, kisha jiulize kama ulichokuwa unahofia kina nguvu uliyokuwa unadhani kinayo.

Zoezi hili siyo tu litakupa uhuru, bali pia litakufanya uthamini kile ulichonacho.

Je ni eneo lipi la maisha yako utaanza kufanya zoezi hili? Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini.

Naamini kupitia makala hii umeweza kujifunza jinsi ya kuwa huru na kuthamini ulichonacho sasa. Karibu tuendelee kujifunza na kuishi misingi ya falsafa ya Ustoa kupitia mtandao wetu wa Falsafa Ya Ustoa Tanzania, tembelea www.ustoa.or.tz

Makala hii imeandikwa na Dr Makirita Amani, ambaye ni daktari wa binadamu, kocha wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali.

makirita@ustoa.or.tz / 0717396253
 
Nashukuru sana mkuu kwa huu uzi, swali langu ni hili umeeleza falsafa ya kujiandaa na magumu anapokuwa katika hali nzuri, vipi kwa upande wa wapili utajiandaaje kuishi maisha mazuri wakati wa mambo magumu?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom