Jeshi lisihusishwe na masuala ya siasa

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
UNAPOZUNGUMZIA amani na utulivu ambao nchi yetu imekuwa ikiufurahia kwa kipindi chote, unamaanisha mambo mengi ikiwa ni pamoja na kazi nzuri inayofanywa na majeshi yetu ya ulinzi na usalama.

Majeshi yetu ambayo kikatiba yanafanya kazi katika sehemu zote mbili za muungano; Jeshi la Ulinzi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) pamoja na Jeshi la Polisi, yamekuwa yakituhakikishia Watanzania usalama wa ndani na mipakani.

Hii imekuwa ikichangiwa pia na Watanzania kuheshimu majeshi yetu na kuyaacha yafanye kazi zao kwa mujibu wa taaluma zao bila kuingiliwa na wanasiasa. Zipo nchi ambazo majeshi ambayo yalitazamiwa kuwa mlinzi wa amani na usalama wa wananchi, yaligeuka na kuwa chanzo cha machafuko na mifano iko mingi.

Sababu za kutokea kwa hali hiyo ni pamoja na wanasiasa kuingilia shughuli zinazofanywa na walinda amani hao. Katika Bunge linaloendelea mjini Dodoma, juzi Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu masuala ya Muungano, Ally Abdallah Saleh (CUF) aliibuka na madai kwamba eti Zanzibar imetekwa na jeshi la Tanganyika, kana kwamba nchi iko katika vita.

Msemaji huyo alikuwa akilalamikia kuwepo kwa askari wengi Visiwani wakati wa Uchaguzi Mkuu uliokwisha na ule uliorudiwa visiwani humo ambao ulisusiwa na chama chake. Kinachotushangaza ni msemaji huyo, ambaye yuko kwenye Bunge la Muungano, kutumia kauli za kibaguzi akiliita Jeshi letu ambalo linafanya kazi pande zote za Muungano tangu nchi hizi zilipoungana mwaka 1964, kuwa ni jeshi la Tanganyika.

Je, hata bungeni alimokuwa nalo ni la Tanganyika? Tunaungana na mawaziri waliokereheshwa na matamshi ya msemaji huyo na pia tunaunga mkono ufafanuzi uliotolewa kwa ajili ya kuwakumbusha watu wanaojisahau kama mbunge huyo.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, alisema haitotokea jeshi kutumika kisiasa lakini akafafanua kwamba takribani kila nchi duniani, huimarisha ulinzi wakati wa uchaguzi na bila shaka sababu za hatua hiyo hata mbunge huyo anazijua.

Waziri alifafanua pia kwamba Jeshi limekuwa likitekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria iliyojiwekea pamoja na za kimataifa na wala haliwezi kutumika ili kutumiza malengo ya kundi fulani. Alizidi kumfahamisha Salehe kwamba mbali na ulinzi wa mipaka na amani, jeshi pia hutoa msaada kwa mamlaka za kiraia au vyombo vingine vya ulinzi na usalama inapohitajika.

Ilielezwa pia kwamba wakati wa uchaguzi, mbali na vituo vya uchaguzi, wajibu wa jeshi pia ni kulinda maeneo muhimu kama vile bandari, redio za serikali na viwanja vya ndege, kama sehemu ya tahadhari.

Waziri Mwinyi alisema madai kuwa jeshi hilo limetumika kuandikisha wananchi kwenye kambi zao za jeshi Visiwani Zanzibar si ya kweli na hakuna mwenye ushahidi kwa kuwa ni uzushi. Kama alivyosema Dk Mwinyi na mawaziri wengine, ni vyema wabunge na Watanzania kwa ujumla, tukajikita kuzungumza siasa bila kushirikisha jeshi kwani ni jambo lisilo na tija.
 
Back
Top Bottom