Je wewe utakuwa wapi milele? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Je wewe utakuwa wapi milele?

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by anin-gift, May 9, 2012.

 1. a

  anin-gift Senior Member

  #1
  May 9, 2012
  Joined: Feb 17, 2012
  Messages: 165
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 0
  Mpendwa msomaji, wewe na mimi, sote ni wanadamu, na bila kujali vyeo vyetu, utajiri wetu, umaarufu au usomi wetu, au umri wetu sisi sote tutakufa na kuiaga dunia hii. Marafiki na ndugu zetu wengi, wamekufa. Wengine wakiwa watoto, vijana, na wengine wazee. Hakuna kanuni yoyote. Maisha yetu duniani ni mafupi sana. Biblia inafananisha maisha yetu duniani na kivuli ambacho hakichukui muda mrefu kutoweka, na pia ua linalochanua na kisha likakatwa. Tunasoma hivi katika 1MAMBO YA NYAKATI 29:15, ”…Ni kama kivuli siku zetu duniani, wala taraji ya kukaa hapana“. Tena tunasoma katika AYUBU 14:1-2, ”Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke,

  siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa; hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe“.
  Wako wanawake na wanaume wazuri walioishi duniani kwa muda mfupi na sasa hawako tena duniani. Wako matajiri na wenye vyeo vikubwa waliokuwako duniani, na sasa hawako pamoja nasi tena, wameiaga dunia baada ya kuishi duniani kwa muda mfupi. Dunia ilitokea kuwapenda sana wanasiasa Edward Moringe Sokoine, Jomo Kenyatta, Mao Tse Tung, Karl Max, Samora Machel, Kwame Nkrumah, Abeid Aman Karume na wengine, lakini sasa hawako pamoja nasi. Wako wapi wanamuziki Mbaraka Mwinshehe, Hemed Maneti, Franco, Bob Marley, Jim Reeves, Lovy Longomba na wengineo? Wametutangulia, na tunafuata! Wasomi na wanasayansi maarufu kama Newton, Einstein, Michael Faraday, Antoine Bell na wengineo, hawa pia waliishi kwa muda mfupi duniani na kuiaga dunia. Wazazi, ndugu na marafiki zetu wengi, wao nao wamefariki dunia na kutuachia huzuni kubwa.Wametutangulia, na sisi tunawafuata! Tutawafuata lini? Inaweza ikawa leo! Hatupaswi kupuuza uwezekano wa kufa leo, eti kwa sababu siyo wagonjwa au siyo wazee sana. Mpendwa msomaji, ugonjwa siyo kifo wala uzee siyo kifo. Watu walioamka asubuhi wakiwa wazima kabisa wamekutana na ajali walipokuwa wakienda kazini na kufa, huku wakiwaacha wagonjwa waliolazwa hospitalini kwa miaka mitatu wakiwa bado hawajafa. Dereva mwenye kufuata sheria na mwangalifu barabarani, amegongwa na kufa papo hapo, kutokana na uzembe wa dereva mwingine. Watu wengine wameanguka ghafla na kufa bila kutarajia. Wengi wamelala wakiwa wazima na kufariki wakiwa usingizini, bila ugonjwa wowote. Vijana wadogo wamekufa, na kuwaacha babu zao wakiwa hai. Hakuna kanuni! Ndiyo maana Mungu anatuonya katika MITHALI 27:1 akisema, ”Usijisifu kwa ajili ya kesho, kwa maana hujui yatakayozaliwa na siku moja“. Hatujui yatakayotokea kwetu siku hii ya leo! Sasa basi, tukifa tunakwenda wapi? Kufa ndiyo mwisho wa mambo yote au kuna maisha baada ya kufa?


  Mpendwa msomaji, Neno la Mungu linatupa uhakika wa maisha baada ya kufa. Biblia inasema katika MATHAYO 17:1-3, ”…Yesu akawatwaa Petro na Yakobo, na Yohana nguguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani,…Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye.“ Kulingana na maandiko, na pia historia ya Biblia, Musa alikufa na kuzikwa miaka 1,700 kabla ya wakati wa tukio hili (KUMBUKUMBU LA TORATI 34:5-6). Eliya naye, alikuwa ametoweka duniani miaka ipatayo 1,000 kabla ya wakati wa tukio hili ( 2WAFALME 2:11). Hebu tafakari sasa kwa makini. Musa, aliyekufa na kuzikwa miaka 1,700 iliyopita anaonekana akiwa hai anazungumza. Eliya, aliyetoweka duniani miaka 1,000 iliyopita, yeye naye anazungumza hapa, akiwa hai. Kwa hakika kuna maisha baada ya kufa!


  Je, mtu anapokufa, huendelea kuishi tena huko kwa muda gani? Maisha ya mtu baada ya kufa, ni marefu sana kuliko maisha ya duniani. Musa alikufa akiwa na umri wa miaka 120 (KUMBUKUMBU LA TORATI 34:7), lakini wakati anazungumza na Yesu, Petro, Yakobo na Yohana; alikuwa tayari ameishi miaka 1,700 baada ya kufa, na hata sasa bado anaendelea kuishi. Baada ya kufa, mwanadamu huanza kuishi maisha marefu sana yanayoitwa maisha ya milele.


  Maisha ya milele, ni muda mrefu sana usio na mwisho. Ili upate kuelewa maisha ya milele ni muda mrefu kiasi gani, tafakari mifano ifuatayo: Umbali wa kutoka Dar-Es-Salaam hadi Kigoma kwa njia ya reli, ni karibu maili 800 au kilometa zaidi ya 1,200. Kama ingewezekana kwa jongoo kutembea na kufuata njia ya reli kutoka Dar-Es-Salaam hadi Kigoma na kurudi, na kufanya hivyo mara milioni moja; muda ambao jongoo huyo angetumia kufanya hivyo,ni sehemu ndogo sana ya maisha ya milele! Kama ingewezekana kwa mtoto mdogo kutumia kifuu cha nazi au kikombe cha chai kuchota maji kutoka katika bahari zote duniani na kuyamwaga nchi kavu; muda ambao mtoto huyo angetumia kukausha bahari zote, ni sehemu ndogo sana ya maisha ya milele! Kama mtu angeweza kusoma vitabu na magazeti ya lugha zote duniani, kila neno moja moja; muda ambao angetumia kumaliza kusoma vitabu na magazeti hayo, ni sehemu ndogo sana ya maisha ya milele!


  Duniani, kuna watu zaidi ya bilioni sita. Kama ingewezekana kwa mtu mmoja kuzungumza na kila mtu mkubwa na mdogo duniani kwa mazungumzo ya ana kwa ana, na akazungumza na kila mtu kwa saa moja; muda ambao angetumia mtu huyo kumaliza kuzungumza na watu wote duniani, ni sehemu ndogo sana ya maisha ya milele! Umbali kutoka hapa duniani hadi kwenye jua, ni maili zipatazo 93,000,000 au kilometa148,800,000. Kama ingewezekana kufunga kamba kutoka duniani hadi kwenye jua, na kobe akatembea juu ya kamba hiyo, kutoka duniani hadi kwenye jua na kurudi, na kufanya hivyo mara milioni moja; muda ambao kobe huyo angetumia kufanya hivyo, ni sehemu ndogo sana ya milele! Natumaini sasa umepata picha ya urefu wa maisha ya milele. Sasa basi, mtu anapokufa huishi maisha ya milele katika mateso ya moto wa milele au huishi mbinguni, kwenye raha isiyo na kifani.


  Ni muhimu kufahamu kwamba mtu anapokufa na kuzikwa, roho yake haizikwi, bali mwili wake tu. Biblia inasema katika MHUBIRI 12:7 Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, nayo roho kumrudia Mungu Aliyeitoa.“ Ayubu alifahamu jambo hili, ndiyo maana anasema katika Ayubu 19:26- 27, ”Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, lakini pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu; nami nitamwona mimi nafsi yangu, na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine…“ Mtu anapokata roho, sekunde ileile roho yake inapotoka, roho ile huingia katika mwili mwingine. Biblia inasema katika 1 WAKORINTHO 15:40-44, ” Tena kuna miili ya mbinguni, na ya duniani;……Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko.“ Kufa, ni kumiminwa kwa roho kutoka katika mwili wa asili wa duniani na kuingizwa katika mwili wa roho. Ni kama mafuta yanavyoweza kumiminwa kutoka katika chombo kimoja hadi chombo kingine. Kwa msingi huu, Mtume Paulo anaeleza katika 2 TIMOTHEO 4:6, ”Kwa maana sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika.“


  Kumiminwa kwa roho ya mtu anayekufa na kuingizwa katika mwili mwingine, huambatana na mtu huyo kuikabili hukumu ya Mungu wakati huo huo. Hukumu ya Mungu haingojei! Biblia inasema katika WAEBRANIA 9:27, ”Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu.“ Hukumu ya Mungu kwa mtu, huamua mara moja mahali atakapoishi mtu huyo milele na milele. Mtu baada ya kufa, huishi katika moto wa milele (adhabu ya milele) au uzima wa milele mbinguni (MATHAYO 25:41,46). Katika LUKA23:43, Yesu Kristo alimwambia yule mhalifu msalabani, ”…Leo hivi utakuwa pamoja nami peponi.“ Katika LUKA16:19-24, pia tunasoma, …Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso… akalia, akasema,…ninateswa katika moto huu“. Unaona hapa! Tajiri huyu alikwenda kuishi maisha ya mateso ya moto wa milele mara tu baada ya kufa. Mtu mwenye dhambi, akifa tu, anakwenda kuanza maisha ya mateso ya moto; na mtu aliyekufa akiwa mbali na dhambi, anakwenda moja kwa moja kukaa na Kristo mbinguni milele na milele (WAFILIPI 1:21-23). Tusidanganyike kwamba kuna mahali pa katikati (toharani au Pugatori) ambapo mtu anakwenda na kungoja watu wa duniani wamwombee misa za wafu, na kutoa sadaka kwa Mungu, ili ampeleke mbinguni. Sadaka ya namna hii ni rushwa. Je kama mtu aliyekufa ni maskini na hana ndugu duniani mwenye uwezo wa kutoa sadaka baada ya kufa kwake, je mtu huyo atakwenda motoni kwa sababu ni maskini hana pesa? Biblia haisemi hivyo, bali inasema kwamba Mungu hapendelei nyuso za watu, wala hakubali rushwa ( KUMBUKUMBU LA TORATI 10:17).


  Siyo hilo tu, Biblia inatukataza kuwaombea watu waliokufa dhambini. Tunaweza tu kuwaombea
  wenye dhambi ambao bado wako hai. Kwa mfano, mwizi anapoiba, halafu akapigwa mawe mpaka akafa, dhambi yake ya wizi imekuwa ni dhambi iliyompa mauti, ni dhambi ya mauti. Kwa kuwa amekufa, hatuwezi tena kumwombea. Ila tu tungeweza tukamwombea kama angeiba na kunusurika kufa. Tutamwombea ili aache wizi na kupata uzima wa milele (1YOHANA 5:16). Tukumbuke wakati wote, baada ya kufa ni hukumu mara moja! Hatupaswi kuwaza jinsi
  tutakavyozikwa hapa duniani, bali tuwaze tutakwenda wapi kuishi milele baada ya kufa! Kuzikwa vizuri hakusaidii. Wakati miili yetu itakapokuwa inazikwa, roho zetu zitakuwa tayari zimemiminwa katika miili mingine ya roho, wala hatutayaona mazishi ya miili yetu duniani! Hata tukizikwa na maelfu haitusaidii. Tajiri katika LUKA 16, alizikwa na watu wengi wakiwemo matajiri wenzake, lakini hata hivyo alikwenda motoni.


  Kata shauri sasa, mpendwa msomaji. Je utakuwa wapi milele? Motoni au mbinguni? Mateso ya moto wa milele yanatisha, hata walioko motoni hawataki ndugu zao waliobaki duniani waende huko (LUKA 16:27-28; MARKO 9:43-48). Tufanyeje basi ili tuishi milele mbinguni? Jibu ni kwamba, tukiziungama dhambi zetu huku tukimaanisha kuziacha, tutaepuka mateso ya moto wa milele na kuokolewa! Kumbuka wakati uliokubalika wa wokovu ni sasa (MITHALI 28:13; LUKA 1:77; 2WAKORINTHO 6:2).


  Kama uko tayari kutubu dhambi zako sasa hivi na kuziacha, Yesu Kristo sasa hivi kwa miujiza mkubwa kwa njia ya imani tu, atakuwezesha kuzishinda dhambi na kuliandika jina lako katika wale watakaoishi milele mbinguni. Je, uko tayari kutubu dhambi zako sasa? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati :

  ”Mungu Baba, natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha kuanzia leo. Sitaki kabisa kuishi milele motoni. Nipe uwezo wa kushinda dhambi zangu kuanzia leo kwa Yesu Kristo Mwanao, na kuliandika jina langu katika orodha ya watu watakaoishi milele mbinguni. Asante kwa kunisikia na kuniokoa, katika Jina la Yesu Kristo. Amen.“

  Tayari sasa umeokoka. Ili uzidi kuukulia wokovu, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI.
   
 2. King Kong III

  King Kong III JF-Expert Member

  #2
  May 9, 2012
  Joined: Oct 15, 2010
  Messages: 25,153
  Likes Received: 2,402
  Trophy Points: 280
  I think I'm big meech,larry hoover,One Nation Under God,Allelujah!!!!!!
   
Loading...