WanaJF,
Naomba kusahihishwa kama ntakuwa nimekosea, ninavyoamini mimi AMANI ndani ya Taifa letu imejengwa na Watawaliwa na si Watawala. Nasema hivyo kutokana na mambo mengi mabaya ikiwa ni pamoja na kukosekana umakini kwa watawala ambao wamewekwa madarakani lakini Watawaliwa (Watanzania ) tumekuwa wagumu wa kuhoji au kuandamana kudai haki kutendeka.
Mtakumbuka kejeli za viongozi wakuu mbalimbali ambazo zimewahi kutolewa na zingine zinaendelea kutolewa mfano: Kiongozi mmoja aliposhutumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka kwa kutumia ndege ya serikali kwenda nayo jimboni kwake kwa shughuli binafsi akawajibu wananchi kwa kejeli sasa nyinyi mlitaka niende na uongo ? Mwingine aliwahi kusema Ndege ya Rais lazima inunuliwe hata kama Watanzania mtakula nyasi, kibaya zaidi ndege ilinunuliwa na ikawa tena ni mbovu; katika hilo hatukuweza kuhoji tena, Mwingine aliwambia Wananchi kama hawawezi kulipa hela ya kivuko shs. 200 basi wawe wanapiga mbizi, zipo kauli nyingi za maudhi kutoka kwa viongozi tuliowapa dhamana ya kutuongoza. Amani ya nchi hii haijajengwa na watawala imejengwa na watawaliwa wenyewe kwa sababu ya uoga wa kuchukua maamuzi kwa watawaliwa
Uoga tulionao Watanzania tusipo badilika utatuletea hasara kubwa katika Taifa, hivi inakuwaje mambo makubwa yenye maslahi kwa Taifa kama vile mikataba tunayoingia na wawekezaji wa nje inakuwa siri ? Huduma muhimu za kibinadamu kama vile maji , afya , elimu zinakuwa ovyo lakini Watanzania hatuwezi kuhoji badala yake Wananchi wasiokuwa na uhakika hata wa kupata mlo kwa siku wanaombwa michango ya kuchangia elimu, afya nk. huku rasilimali za nchi yao zikiporwa kwa serikali kuingia mikataba yenye usiri ?
AMANI Iliyopo Tanzania haijawahi kujengwa na Watawala ila imejengwa na Watawaliwa wenyewe kwa sababu ya uoga wa kuhoji mambo dhidi ya watawala na kufanya maamuzi magumu kama vile kuandamana, kugomea baadhi ya mambo ili kuweza kusaidia kurekebisha mienendo ya watawala. Mawazo yangu naona pengine ni wakati muafaka wa kufikirisha akili zetu na tuanze kuwa na utamaduni wa kuhoji mambo na kulazimisha HAKI kutendeka, ikishindikana kuchukua hatua ya mabadiliko ya kiuongozi/Utawala