Mkulima, kama unafuatilia magazeti madai ya kosa la Anney haya hapa:
Mlemavu kortini kwa kumkashifu Kikwete
na Datus Bornface
MLEMAVU wa miguu, Anney Anney (50), mkazi wa Arusha Kilombelo, jana alipandishwa katika Mahakama ya Wilaya Ilala, jijini Dar es Salaam, akituhumiwa kumkashifu Rais Jakaya Kitwete.
Mwendesha Mashitaka, Mrakibu wa Polisi Niama Mwanga, alidai mbele ya Hakimu Samwel Maweda kuwa, mtuhumiwa alitenda kosa hilo Julai 23, mwaka huu, eneo la Ikulu jijini Dar es Salaam.
Alidai kuwa, siku ya tukio akiwa kwenye maeneo hayo ya Ikulu, mtuhumiwa alitoa ujumbe kupitia bango aliloliandaa ambao ungehatarisha uvunjifu wa amani kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwanga alidai kuwa, mtuhumiwa alitoa ujumbe wenye maneno Jakaya Kikwete, Ikulu ya Dar es Salaam, Nyerere alilinda ardhi yetu pia utu na uzalendo.
Alidai kwamba, maneno mengine ni Mwinyi aliua Azimio la Arusha, Mkapa aliuza mashirika yetu na nyumba za umma, wewe (Kitwete), unauza ardhi yetu kwa Wazungu na Waarabu pamoja na utu na utaifa wetu.
Aliendelea kudai kuwa, ujumbe huo pia ulisomeka kama, Udumu ujamaa na kujitegemea, lidumu Azimio la Arusha, zidumu fikra za Mwalimu Nyerere.
Mtuhumiwa alikana shitaka hilo na kurudishwa rumande kwa kushindwa kukidhi mahitaji ya dhamana kwani alitakiwa kuwa na wadhamini wawili.
Kesi hiyo ya aina yake, imeahirishwa hadi Agosti 10 na upelelezi bado haujakamilika.
Wakati huo huo, mfanyakazi wa ndani, Idd Hassan (19), mkazi wa Buguruni, jijini Dar es Salaam, jana alipandishwa kizimbani, akituhumiwa kwa kosa la kubaka mtoto mwenye umri wa miaka miwili (jina limeahifadhiwa).
Mwendesha Mashitaka, Inspekta wa Polisi Hamis Mhellya, alidai mbele ya Hakimu wa Wilaya, Afumwisye Kibona kwamba mtuhumiwa alitenda kosa hilo Julai 20, mwaka huu, eneo la Buguruni Malapa.